Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba
Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema ataviandikia vyama vingine vya upinzani barua rasmi, kuviomba visisimamishe wagombea urais, badala yake vimuunge mkono yeye katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu.
Profesa Lipumba alisema hayo wakati akiwashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CUF, kwa kumpitisha kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho katika uchaguzi huo Alisema anakusudia kuwasilisha maombi hayo kwa vile haoni kama kuna mtu katika vyama hivyo mwenye uwezo wa kukabiliana na mgombea wa kiti hicho kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, kulingana na hali ya kisiasa ilivyo nchini.
Profesa Lipumba aligombea urais katika uchaguzi wa mwaka 1995, 2000 na 2005 na kushindwa huku baadhi ya watu wakivitaka vyama vya siasa kusimamisha mgombea mmoja, lakini viongozi wa upinzani mara zote kushindwa kukubaliana.
Profesa Lipumba ambaye alipitishwa kwa kupata asilimia 99.7 ya kura zote zilizopigwa, alisema iwapo chama chake kitafanikiwa kushinda katika uchaguzi huo, miongoni mwa mambo makuu yatakayotekelezwa, ni pamoja na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Jana CUF walitangaza kwamba Lipumba alikuwa amepata ushindi wa asilimia 98.97, lakini baadaye usiku wakasema kulikuwa na makosa katika ukokotoaji hivyo kubainika kwamba alikuwa amepata asilimia 99.7.
Kadhalika, chama hicho kilisema kuwa ukokotoaji wa ushindi wa Maalim Seif nao ulikuwa umekosewa kuwa asilimia 96.38 badala ya asilimia 98.88.
Alisema pia, ataboresha elimu kufikia viwango vya kimataifa na atahakikisha mafisadi wote wanashughulikiwa ipasavyo.
"Naamini kwa uwezo nilionao, ninaweza kutatua matatizo ya nchi hii, na nina hakika ya kupata tuzo ya utawala bora," alisema Profesa Lipumba na kushangiliwa na karibu ukumbi mzima wa mkutano huo.
CHANZO: NIPASHE
Mimi binafsi yangu Nakubaliana na wewe waweza kushindana na CCM. Je Mnasemaje Wakuu wenzangu wa J.F?