MwanaHalisi
Rostam Aziz, Mbunge wa Igunga, anamiliki makampuni mengi ambamo jina lake halionekani, MwanaHalisi limegundua. Hata pale anapokiri hadharani kuwa anamiliki kampuni fulani, bado kampuni hiyo haina jina lake kamili linavyofahamika katika kumbukumbu za Bunge.
Rostam anatajwa kumiliki makampuni 10 yaliyoanzishwa jijini Dar-es-Salaam kwa nyakati tofauti, lakini jina lake linaonekana katika kampuni moja tu, kwa mujibu wa fomu za Wakala wa Usajili wa Makampuni na Leseni za Biashara (BRELA).
Kampuni ambako jina lake linatajwa ni African Trade Development (T) Limited (ATDL) ambako pia limeongezewa jina jingine "sakarri" kwenye safu ya majina ya ukoo, ambalo hata hivyo halifahamiki kwa wengi.
Katika ATDL, orodha ya waanzilishi wenye hisa inaonesha kuna Rostam watano (5) huku jina la "Rostam" likiwa ama limekosewa au limebadilishwa herufi kadhaa au wahusiwa wakia na ubini tofauti.
Hata katika ununuzi wa magazeti ya Rai, Mtanzania, The African, Dimba, Bingwa na "chuo" cha Uandishi wa Habari – MAMET, kutoka kampuni ya Habari Corporation Limited (HCL), hakuna jina lake.
MwanaHalisi linaweza kuripoti kwua magaeti hayo yaliuzwa kwa kampuni inayoitwa Isenegeja Limited ya Dar-es-Salaam ambako jina la Rostam halionekani. Aidha, ni Rostam Aziz aliyekiri mbele ya waandishi wa habari, 3 Mei mwaka huu katika hoteli ya Kilimanjaro Kempinski, kuwa anamiliki magazeti hayo kupitia kampuni ya hiyo, gaeti lake la Rai liripoti kuwa "inasadikika kwamba Rai linamilikiwa na Rostam".
Kwa mujibu wa barua ya Katibu wa Bodi ya Wakurugenzi ya HCL Shaaban Kanuwa ya 30 Aprili mwaka huu, bado wamiliki wa sasa wa magazeti hayo hawajayalipia. Barua hiyo inayoandikwa kwa Isenegeja Company Limited, kupitia New Habari (2006) Limited (NHL), ambayo Rostam Aziz anadai kumiliki, inasema MAMET na magazeti ya Dimba na Bingwa, bado hayajalipiwa.
Kanua anasema katika barua hiyo kwamba wakurugenzi wa HCL wanapendeka zilipwe mara moja Sh 100 milioni ambazo walikubaliana wakati wa ununuzi wa kampuni hiyo. Wakati huo huo, Kanuwa anaelekeza kuwa iwapo Isenegeja haijawa tayari au imeshindwa kulipia magazeti mawili ya Dimba na Bingwa na MAMET , basi iache kuvitumia kwa maana ya kuchapisha na kuendesha chuo.
Habari Corporation iliuzwa miaka mitatu iliyopita. Haijafahamika magazeti ya Rai, Mtanzania, na The African yaliuzwa kwa kiasi gani. Lakini barua ya bodi ya HCL inasema gharama ya magazeti ambayo hayajlipiwa ilikuwa kama ifuatavyo: Dimba Sh. 40 milioni, Bingwa Sh. 30 milioni, na Chuo Sh. 10 milioni na ilitaka kiasi hicho kilipwe ifikapo 29 Mei mwaka huu.
MwanaHalisi haikuweza kufahamu majengo ya HCL yaliuzwa kwa kiasi gani. Kanua alipoulizwa iwepo Isenegeja wamekwishalipa alisema swali hilo aulizwe mwenyekiti wa bodi, Jenerali Ulimwengu ambaye imefahamika yuko nje ya nchi na hakuweza kufikiwa.
Uchunguzi wa gazeti hili haukuweza kubaini faili la NHL ambako ulitegemea kukuta jina la Rostam Aziz aliyesema anamiliki kampuni hiyo ya magazeti yake. Lakini miezi miwili iliyopita, kulikuwa na andihi kwenye mtandao wa jamiiforums lililokuwa linaenda kwa Rostam Aziz kumtahadharisha kuwa alikuwa anaendesha kampuni ya NHL bila kusajiliwa na bila mwelekeo.
Andishi lililosainiwa kwa jina la moja la Salva, halikujulikana iwapo lilikuwa linatoka kwa mmoja wa wakurugenzi wa HCL na ambaye sasa ni Mkurugenzi wa mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu.
Mwandishi alikuwa anaonya juu ya kutozingatia sheria za nchi, kushindwa kuendesha kampuni kwa misingi bora ya menejiment ambako kulikuwa kunaelekea "kuua kampuni".
Haijafahamika uhusiano wa NHL na Isenegeja, na uhusiano wa Rostam na makampuni yote mawili - NHL na Isenegeja. Waanzilishi na Wamiliki wa Isenega ni Hassani Haidari na Gulam Abdurasul wote wa anwani za Dar-es-Salaam.
Katika umiliki wa kampuni ya African Trade Development (T) Limited (ATDL) ndiko kuna vimbwanga vya majina yanayohusiana na Rostam.
Majina yaliyotumika kusajili kampuni hiyo ni Rostom A. Sakarri, Rostam Sakarri, Rustom Aziz Sakarri, Rustam Sakarri na Rustam Sakaari. Wahusika wengine wa kampuni hii waliojiandikisha BRELA ni Gulam Abdurasul Chakaar, Bahram Abdurasul Chakaar na Abdulkadir Mehrab.
Rostam hakupatikana kuthibitisha iwapo Rustam, Rustom. Rostom na Rostam Sakarri yalikuwa majina yake, kulikuwa na jina lake au yalikuwa ya ndugu zake wa karibu. Simu yake ilijibu wakati wote kuwa haipatikani.
Kwenye muhtasari wa kikao cha kampuni ya ATDL cha 17 Machi, 1993, kuna saini mbili za Rustam Chakaari (mkurugenzi) na Bahram A. Chakaar (Mwenyekiti). Kubalika badilika kwa tahajia (spelling) za jina la Rostam na mwingiliano wa majina ya ukoo, ni mambo ambayo yanaacha kitendawili kigumu kutegua.
Kwa mfano, siyo rahisi kujua iwapo majina haya yameparanganyishwa kwa makusudi: Rustam Sakarri na Rustam Sakaari. Mwanasheria aliyezungumza na na MwanaHalisi kuhusu utata huu amesema ni vigumu kumhusisha Rostam na majina hayo matano iwapo kunazuka matatizo ya kisheria kwenye kampuni hizo.
Amesema akihusishwa ataweza "kuruka kiunzi" na kudai hahusiki kwa kuwa nchi nzima na labda vyeti vyak, kama anavyo vinaonesha anafahamika kwa jina la Rostam Abdulrasul Aziz. Mwanasheria huyo alisema labda mtu wa aina hiyo anaweza kunaswa kwa kutumia ushahidi wa kimazingira.
Makampuni yanayotajwa kumilikiwa na Rostam lakini jina lake halionekani BRELA ni pamoja na Africa Tanneries Limited, Tanzania Leather Industries Limited na Wembere Hunting Safaris Limited. Mengine ambako jina lake halionekani ni Tanzania Packages Manufactures Limited na Caspian Construction Limited ambayo anwani zake zilikuwa zinatumiwa kampuni ya tata ya kufua umeme ya Dowans.
Gazeti hili lina orodha ya makampuni ambayo yanadaiwa kuwa ya Rostam, wale wote waliotajwa kuwa waanzilishi na baadhi ya ofisi za makampuni haya ambako inadaiwa alikuwa anakwenda binafsi kuhimiza utendaji au kufuatilia malipo.
Madai ya Rostam kumiliki kampuni zisizo na majina yake yalianza kujitokeza lilipozuka sakata la yeye kuhusishwa na kampuni kadhaa enye kashfa ikiwemo ya Dowans na Kagoda. Rostam mwenyewe alikiri kuwa na uhusiano na Dowans, lakini akadai hamiliki kampuni hiyo isipokuwa anuani na barua pepe za kampuni yake ya Caspian Construction zilikuwa zinatumiwa na kampuni hiyo ya Dowans.
Jina la Rostam linatajwa katika umiliki wa kampuni tata ya Kagoda. Wakili wa Mahakama Kuu, Byidinka Michael Sanze amenukuliwa katika hati ya kiapo, akisema kuwa Rostam ndiye aliyemtaka kushuhudia hati za mikataba ya Kagoda.
Kampuni ya Kagoda ilichota zaidi ya Tsh. 40 bilioni katika akaunti ya Madeni ya Nje, ndani ya Benki Kuu ya Tanzania.
Swali la Wiki:
Mnajuaje mtu anayeitwa Rostam Aziz ndiye Rostam Aziz? is he an impostor?