Kigogo mwingine ambana Slaa
Stella Nyemenohi
HabariLeo; Thursday,September 27, 2007
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, jana alikuwa kiongozi wa pili kujitokeza na kutangaza kuwa anatarajia kufungua kesi dhidi ya Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa (Chadema) kwa kumpaka matope kwa kumwita fisadi.
Uamuzi wa Mgonja umekuja siku moja baada ya Waziri wa Nishati ya Madini, Nazir Karamagi kuwaambia waandishi wa habari kuwa atamfungulia kesi Dk. Slaa sanjari na gazeti la MwanaHalisi na Kiwanda cha Printech kwa kuchapisha habari zenye kumchafua jina lake.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mgonja alisema tuhuma zilizotolewa dhidi yake na Dk. Slaa ni suala la ushindani wa siasa ambalo ni pigo kubwa katika maisha yake na kwamba zimemwathiri kwa kumvunjia hadhi katika utumishi wake. "Tuhuma zimeniathiri. Hadhi yangu ni ya juu, hili ni pigo kubwa. Nimekaa katika sekta ya umma kwa miaka 33 sijawahi kupata kashfa. Bahati mbaya mimi siyo mwanasiasa, siwezi majukwaa," alisema Mgonja.
Akisisitiza kuwa uamuzi wa kumshtaki mwanasiasa huyo hautokani na shinikizo lolote. Mgonja alisema hakuweza kuchukua uamuzi huo mapema kwa kuwa alikuwa hajapata vielelezo muhimu vya kumwezesha kufanya hivyo.
Ingawa hakutaja siku ya kufungua kesi hiyo, Mgonja ambaye alisema anaifungua binafsi na siyo kwa wadhifa wake, alisema, "hatufuati maneno ya mabalozi. Kila mtu ana uhuru wake. Kama ningepata vielelezo mapema, ningeshazungumza mapema. Hivi sasa ninavyo na wanasheria wangu wako tayari."
Mgonja alisema itakapofika wakati wa kuzungumzia tuhuma hizo kama Katibu Mkuu, serikali ndiyo itakuwa katika nafasi ya kutoa tamko. Hata hivyo, aliwaambia waandishi wa habari kuwa kwa upande wa uhusiano wa wafadhili, hususan katika utoaji wa misaada, tuhuma hizo za Dk. Slaa hazijaonyesha kuleta athari kwa kuwa hazina ukweli ndani yake.
Katika kujibu maswali ya waandishi, ingawa hakuelezea undani wa kile anachokwenda kudai mahakamani, alielezea kushangazwa kwake na tuhuma hizo kuelekezwa kwake ingawa wamepita makatibu wakuu mbalimbali katika wizara hiyo bila kurushiwa kashfa kama hizo. Alipohojiwa kuhusu mali anazomiliki, alisema, "namiliki mali kidogo sana".
Aliwaambia waandishi kuwa alishajaza fomu zinazoelezea mali zake na kuwashauri anayehitaji aende katika ofisi husika afuate utaratibu apewe taarifa hizo. Uamuzi wa Mgonja wa kumfungulia kesi, unatokana na kile alichosema kuwa ni matamshi ya Dk. Slaa aliyoyatoa Septemba 15, katika viwanja vya Mwembeyanga, wilayani Temeke kwa kumtuhumu hadharani kuwa ameshiriki katika vitendo vya ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma. Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, vile vile Dk. Slaa alirudia kutoa shutuma hizo katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Arusha Septemba 17.
Alisema gazeti la MwanaHalisi limekuwa likisambaza habari hizo za shutuma wakati huo huo Kiwanda cha Printech kinahusika kutokana na kuzichapisha. Katika hatua nyingine, ushirikiano wa vyama vya upinzani umetoa tamko lao kuhusiana na majibu ya serikali na watendaji wake kuhusu orodha ya wanaodai ni mafisadi kwa kugawa mkataba unaodaiwa ni wa uchimbaji madini Buzwagi.
Naibu Katibu Mkuu Chadema, Victor Kimesera alisema wameamua kuanika wazi kwa umma kupitia vyombo vya habari mkataba huo wanaodai ni wa uchimbaji wa madini ya Buzwagi kutoa nafasi kwa umma kujadili yaliyomo pamoja na mchakato uliosababisha mkataba huo.
"Tuko huru kuusambaza mkataba huu pande zote za Tanzania, ingawa ni maalumu kwa serikali kwa kuwa haukuwa na muhuri wa siri, kwa hiyo uko wazi kwa kila mtu kuuona," alisema na kuwakabidhi waandishi wa habari nakala ya mkataba huo jana.