Juzi niliposoma habari kwamba wahariri nchini mwetu wanakutana kujadili rushwa, wakiongozwa na TAMWA, nilitamani kushiriki mjadala huo(bila kualikwa), lakini isingewezekana kwa kuwa niko mbali. Kwa sababu hiyo, niliamua kumwandikia Mkurugenzi wa TAMWA, Ananilea Nkya, ujumbe ambao angeufikisha kwa wanahabari wenzangu. Kumbe, wakati naandika, wahariri walikuwa wameshamaliza kikao chao na kurejea makwao. Hata hivyo, Nkya ameunakili na kuutuma ujumbe wangu kwa wahariri wote katika email zao, akiwataka wautazame na ikibidi waupe uzito unaostahili katika vyombo vyao, ili kukoleza mjadala wao wa juzi juu ya ufisadi. Nimeona vema niwashirikishe nilichoandika. Ni hiki hapa chini:
Dada Nkya na wapambanaji wote wa TAMWA,
Salaam.
Nasoma sana habari za nyumbani. Nawapongeza kwa mapambano makali mnayoshiriki katika ukombozi wa taifa letu. Kufanya kazi mnayofanya sasa, katika sheria dhalimu kadhaa tulizonazo, ni ujasiri unaopaswa kupongezwa.
Leo nimesoma kwenye vyombo vya habari kwamba mtakutana na wahariri wapato 50 kujadili ufisadi. Hili nalo ni tukio lenye uzito wake. Nawapongeza pia kwa kuandaa mjadala huo, na nawatakia mafanikio mema. Sijaalikwa, na sababu zinaeleweka, lakini nipo nanyi kiroho na kiakili katika mkutano huo.
Kwa sababu hiyo, naona bora niandike mawili niliyonayo, ambayo ni mchango wangu katika kufanikisha mjadala huo.
1. Wahariri dhaifu
Ni vema mjadala huu utumike pia kuwakumbusha wahariri wenyewe kwamba miongoni mwao wamo mafisadi. Hakuna haja ya kutajana majina hapa, lakini inajulikana kwamba baadhi ya wahariri
wamekuwa mafisadi ama kwa sababu ya tamaa au kwa kutumiwa bila kujua. Bahati mbaya, jamii iliyotuzunguka inatujua na inatusema kichini chini, inatudharau na itafika mahali itatupuuza au
kutuadhibu. Bahati mbaya, hata baadhi ya 'wanaotutumia' wakishafanikisha malengo yao, au mambo yakiharibika, wanatudharau na kutusema vibaya. Wanadhani kwamba kwa sababu wao waliweza kututumia tukatumika, ndiyo tabia yetu, hivyo tunaweza kutumiwa na wengine dhidi yao kwa njia hiyo hiyo. Hawatuamini.
Tusikubali kufika huko. Habari zilizonifikia ni kwamba kuna magazeti kadhaa hapo nchini yanaongozwa na wahariri 'dhaifu' ambao wamelainishwa na mmoja wa vinara wa mtandao - Rostam Azizi - kiasi kwamba wako tayari kuacha kuandika habari zinazoigusa serikali hata kama zina maslahi ya kitaifa, wako tayari kupotosha habari au kufifisha mapambano ya kifikra yanayoendelea ili kutumikia maslahi yao. Sina haja ya kuyataja hapa. Mnayajua, na wahariri hao wanaosubiri serikali 'iwafikirie' wanafahamika.
Tutumie fursa hii kukumbushana hilo, uhariri wa kizazi hiki umekuwa kama uongozi wa sasa wa CCM; kwamba tusipojisafisha sisi wenyewe, mjadala huu dhidi ya ufisadi hautakuwa na maana.
2. Haja ya uasi
Amri za Mungu zinatufundisha kuwatii wakubwa na wenye mamlaka. Lakini zinatufundisha pia kwamba hatuna sababu ya kuwatii watakapotutaka tuzivunje amri hizo. Tuna haki ya kuasi amri zao kwa ajili ya maslahi makubwa zaidi. Kwa msingi huo huo, wahariri tunapaswa kuzitupia macho sheria dhalimu tunazozitumikia na zinazosimamia taaluma yetu. Zipo nyingi, na 'mama yao' ni Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976. Tumekuwa tunapiga kelele ziondolewe au zirekebishwe. Serikali imekaa kimya.
Serikali hii ilipotaka kuonyesha uhodari, ikaibuka na muswada dhalimu zaidi wenye jina zuri na malengo mabaya, ambao tuliupinga na kufanikiwa kuusitisha 'kwa muda.' Serikali yetu haina dhamira ya kuwatumia wananchi kama inavyosema; ndiyo maana haiondoi sheria mbovu wala haizirekebishi, lakini inazidi kutunga sheria dhalimu nyingine tunazoripoti. Nasikia hata sasa wanapeleka muswada wa sheria mpya ya uchochezi.
Hiki ni kitanzi ambacho waathirika wa kwanza ni sisi tunaojipendekeza kwa serikali hiyo hiyo. Kumbuka, ni majuzi tu serikali hiyo hiyo (kwa kutumua Bunge letu) imetunga sheria ya TAKUKURU ambayo ni dhaifu kama iliyokuwapo.
Tufanye nini? Wahariri tunapaswa kuwa chachu ya mabadiliko ya kitaifa. Tunapaswa kusimama upande wa wanyonge wa Tanzania. Tunapaswa kuwa jasiri na kusimamia ukweli, uhuru na uhai wa taifa hata kama itabidi tutoe sadaka ya maslahi yetu na maisha yetu. Napendekeza wahariri tuanzishe uasi mtakatifu dhidi ya sheria dhalimu. Hata kama sheria hizi hazitaondoka leo, tukiendelea kuziasi tutazipunguza nguvu na hatimaye itakuwa rahisi kuwashawishi watawala kuzifuta.
Mshikamano tuliouonyesha dhidi ya Omar Mapuri, ulikuwa sehemu ya uasi wetu dhidi ya sheria dhalimu ya magereza - maana ni kweli waandishi waliopigwa walivunja sheriai hiyo! Hivyo, Mapuri
alikuwa sahihi lakini alikuwa anatetea sheria ya kihuni. Kazi iliyofanywa na gazeti la MwanaHALISI wiki iliyopita kuwataja watuhumiwa wa ufisadi ni uasi mtakatifu dhidi ya sheria hizi za kikoloni. Laiti magazeti yote nchini yangeandika hivyo na kushitakiwa, ungekuwa mwanzo mpya wa mageuzi ya
maana. Kingekuwa kishindo kikuu kama kilicholetwa na maandamano ya wafanyakazi na wananchi waliompokea Zitto Kabwe, au hata wanaowazomea viongozi mikutanoni wanapohisi wamehadaiwa.
Hatuwezi kujikomboa kwa kujikomba. Wahariri wakijikabidhi kwa watawala kwa sababu ya safari, mishiko na ahadi za kuteuliwa; wakizitii sheria dhalimu na kuwanyima wananchi kile wanachostahili kwa sababu tu ya kuenzi mawazo ya kikoloni, hata wakikaa na kujadili ufisadi kwa wiki nzima, stori za ufisadi zitafia kwenye madawati yao, isipokuwa kama zitakuwa zile ambazo baadhi yetu wanaziita 'zinazowahusu wale wanaopigwa vita na wanamtandao.'
Bila ujasiri na uasi huu, mjadala kuhusu ufisadi utapungua makali. Maana tutakuwa watu wa maneno yasiyo vitendo, na tutakosa dhamira halisi na mamlaka ya kuwasema mafisadi au watuhumiwa wa ufisadi. Nasi tutakuwa waigizaji na wasanii kama hao tunaowaandikia. Kimsingi, tutakuwa watumwa wanaotumia kalamu zetu kutetea uhuru wa wengine bila kufikiria ukombozi wetu wenyewe.
Dhamana tuliyobeba kwa nyadhifa zetu ni kubwa. Inaweza kulitosa au kulibomoa taifa. Tujikomboe kutoka kwenye minyororo ya ufisadi, ili mjadala wetu juu ya ufisadi uweze kuwa na maana. Tuuondoe uandishi kwenye 'ukarani' uwe zana ya uchambuzi, harakati na mapambano ya kuleta haki, usawa, heshima na tunu zote walizopigania waasisi wa uhuru wa Tanzania. Woga na uzembe viwekwe pembeni, tuvae uzalendo, tutimize wajibu wetu.
Naamini tuna wahariri makini. Naamini walio dhaifu wa dhamiri na tabia ni wachache. Ndiyo maana nina imani kubwa na mkutano wenu huo na mjadala utakaotokana nao. Yawezekana huu ni mwanzo wa matengenezo mapya ya wahariri na taaluma ya uandishi wa habari; na mwendelezo wa vita kali dhidi ya ufisadi. Nawatakia mafanikio.
Kwa unyenyekevu mkubwa,
Ndugu yenu,
Ansbert Ngurumo