Rutabanzibwa aikana IPTL
Asema hahusiki kutia saini mkataba wake
Na Njumai Ngota (Uhuru)
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji, Patrick Rutabanzibwa ameruka kimanga suala la kampuni ya umeme ya IPTL na kusema hahusiki na utiaji saini wa mkataba huo.
"Madai ya Dk. Willibrod Slaa na wenzake dhidi yangu ni ya uzushi mtupu. Ninakanusha vikali tuhuma zote... wakati mkataba huo unatiwa saini mimi nilikuwa kamshina na sio katibu mkuu kwa hiyo sihusiki," alisema.
Alifafanua kuwa wakati mkataba huo unatiwa saini Mei 26, mwaka 1995, alikuwa Kamshina wa Nishati na Madini hakuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Dk. Slaa na wenzake katika mkutano walioufanya viwanja vya Mwembeyanga, Temeke mjini Dar es Salaam, walimtuhumu Rutabanzibwa kuwa anahusika na ufisadi kutokana na kuwa Katibu Mkuu wa Nishati na Madini wakati mikataba waliyoita mibovu ya madini inasainiwa, hasa wa IPTL na kampuni ya Tangold.
Rutabanzibwa alisema wakati mkataba huo ukiwa mbioni kutiwa saini alipinga na kupendekeza ufanyiwe marekebisho jambo lililofanya gharama ya uendeshaji kupungua kwa asilimia 40.
Alisema Mei 11, mwaka 1997 ndipo alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Nishati na Madini.
"Matamshi ya Dk. Slaa na wenzake yamenishangaza, yamenisikitisha na yamenihuzunisha sana," alisema na kumtaka kiongozi huyo na wenzake wamuombe radhi kwa kumsafisha jina lake.
Rutabanzibwa alisema anatarajia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Dk. Slaa na wenzake kwani wamemchafulia jina lake.
Alisema ili atendewe haki na kulinda heshima yake inayotokana na kuutumikia umma wa Watanzania kwa uadilifu kwa miaka 28, anafikiria kuchukua hatua hiyo.
Rutabanzibwa alisema anashauriana na wanasheria wake na kuwa tuhuma hizo, sio suala la kukurupuka hovyo.
Alisema katika kumfikisha mahakamani Dk. Slaa, atafanya hivyo mapema iwezekanavyo ingawa hakuweka wazi ni lini.
Akieleza jinsi alivyozipokea tuhuma hizo, Rutabanzibwa alisema bado linamuumiza kichwa kwa kuwa anamfahamu Dk. Slaa tangu akiwa Padri na hadi sasa hawajawahi kukosana naye.
Alisema alikuwa katika wizara hiyo kwa miaka tisa, ambapo mikataba minne ilitiwa saini, ukiwemo wa Songosongo.
Katibu Mkuu huo alifafanua kuwa hakuna kitu kinachopitishwa bila ya kupitia Kamati ya Mawaziri na mambo yote makubwa yanayohusu nchi yanasimamiwa kwa mujibu wa sheria.
Kuhusu kampuni ya Tangold, Rutabanzibwa alisema yeye ni Mkurugenzi wa kampuni hiyo ya serikali inayosimamia hisa za serikali katika kampuni za madini.
Hata hivyo, hakufafanua kuhusu kuhusika kwake na tuhuma zinazotolewa na wapinzani dhidi ya kampuni hiyo.
Dk. Slaa aliongoza wenzake mbalimbali wa upinzani kutoa tuhuma dhidi ya baadhi ya viongozi na watu maarufu hapa nchini. Baadhi ya waliotuhumiwa wamejibu tuhuma hizo.
Miongoni mwao ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na Mbunge wa Musoma Mjini, Nimrod Mkono.
Mgonja na karamagi walisema watamfikisha Dk. Slaa, gazeti lililochapisha habari hizo na kampuni iliyohusika kuchapisha gazeti hilo mahakamani.
Mkono ambaye ni mmoja wa wabunge maarufu hapa nchini alipangu hoja mbalimbali zilizotolewa dhidi yake na kusema zote hazina ukweli.
Mkono hakuunga mkono wala kupinga suala la kuwapeleka mahakamani watu waliomhusisha na tuhuma hizo ambapo alisema hawana fedha za kumlipa, lakini bado anatafakari nini cha kufanya dhidi yao.