Mhe. Mwenyekiti gazeti la Mwananchi la tarehe 14 Aprili 2014 limeandika kuwa "Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu na Bunge), William Lukuvi ameanza kampeni kanisani kuwataka wananchi kupinga serikali tatu zilizopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, vinginevyo nchi itatawaliwa na jeshi kwa kuwa Serikali ya Muungano itashindwa kuwalipa mishahara wanajeshi."
Mhe. Lukuvi aliyasema haya katika Kanisa la Methodist, Jimbo la Dodoma alipokuwa mgeni rasmi akimwakilisha
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika ibada ya kumsimika Mchungaji Joseph Bundala kuwa askofu. Hoja kama hiyo pia ilizungumzwa na Rais Kikwete wakati akilihutubia bunge Maalum tarehe 21 Machi 2014.
Mhe. Mwenyekiti, Rasimu ya Katiba imeletwa na Tume ya Rais ili tuijadili na kuipitisha. Rasimu hii siyo ya CUF, siyo ya CHADEMA, siyo NCCR Mageuzi, siyo ya Wapemba. Ni Rasimu ya Tume ya Rais Kikwete.
Katika hotuba yake katika kanisa la Methodist Mhe. Lukuvi pia alisema "Serikali tatu zikipita ni wazi kuwa hata makanisa yatafungwa kwani nchi haiwezi kuwa na amani tena."
Lukuvi alisema Wazanzibari wanaotaka kuwa na nchi yao hawawezi kujitegemea, bali wanataka Serikali ili wapate nafasi ya kujitangaza kuwa ni nchi ya Kiislamu.
Baadaye alipotakiwa kufafanua kauli yake, Lukuvi alisema alichokizungumza kanisani hapo ni mawazo yake binafsi ambayo yanafanana na Watanzania wengi, akiwamo Rais Jakaya Kikwete.
Mhe. Mwenyekiti je lengo la serikali mbili ni kuwadhibiti Wazanzibari wasianzishe dola ya Kiislam kama alivyoeleza Mhe. Lukuvi? Baada ya hotuba ya Mhe. Lukuvi "Askofu Bundala alisema kanisani hapo kwamba ili kudumisha Muungano ni vyema Katiba ya Zanzibar ifutwe ili iwepo moja ya nchi moja ambayo inadumisha Muungano."
Mchakato wa kupata katiba mpya unapaswa kuwa wa maridhiano, Vipi Waziri anayemuwakilisha Waziri Mkuu anaenda kanisani na kusema Wazanzibari wanaotaka kuwa na nchi yao hawawezi kujitegemea, bali wanataka Serikali ili wapate nafasi ya kujitangaza kuwa ni nchi ya Kiislamu.
Kama hamuitaki Rasimu ya Katiba ya Tume ya Rais kwa nini mmetuleta hapa kwa gharama kubwa. Tunaambiwa Bunge limekarabatiwa kwa shilingi bilioni 8.2. Je ni utaratibu wa 10 percent uliohamasisha kutumia fedha nyingi huku serikali ikiamini kuwa Rasimu ya Katiba haifai kabisa.
Mjadala umekuwa wa matusi na siyo wa kujenga hoja. Kauli za kibaguzi zimetolewa dhidi ya Wapemba, dhidi ya Waarabu, dhidi ya Wahindi. Wajumbe wa Bunge Maalum wanashangilia kauli za kibaguzi. Tunaanza kupanda mbegu ya intarahamwe wa Tanzania. Kauli za kibaguzi ni kinyume cha maadili na tunu za Watanzania.
Kwa utaratibu wa kanuni 33 (7), Baada ya taarifa ya kamati namba moja hadi namba kumi na mbili kuwasilishwa, taarifa hizo zitajadiliwa kwa kipindi kisichozidi siku tatu. Baada ya mjadala kamati ya uandishi inapaswa kuanda vifungu vya sura hizo mbili ili vipigiwe kura na wajumbe wa pande mbili za muungano. Hilo halitafanyika.
Kufuatana na Ratiba, Bunge Maalum litaendelea hadi tarehe 25 Aprili bila kupiga kura na kufanya maamuzi ya vifungu vya sura hizi mbili kinyume na kanuni. Bunge linaahirishwa hadi Agosti bila kufanya maamuzi ili kuwapa nafasi CCM watafute theluthi mbili ya pande zote za Muungano kwa njia yeyote ile.
Tunaopigania katiba ya wananchi hatuwezi kubariki uchakachuaji wa maoni ya wananchi. Wakati umefika tuwaache CCM muendelee na vioja vyenu kwani hamtaki kuandika katiba inayotokana na mawazo ya wananchi badala yake mnahamasisha chuki dhidi ya Wapemba, Wahindi na Waarabu na kupandikiza uhasama wa kidini.