Makwa, Gatundu North, Kaunti ya Kiambu, imeingia tena kwenye mjadala wa pombe haramu baada ya mwanaume mmoja kuripotiwa kufariki baada ya kunywa pombe inayoshukiwa kuwa mbaya.
Lakini safari hii, si taarifa ya vifo pekee inayovuta hisia. Ni video ya kina mama wakilia kwa uchungu baada ya taarifa za vifo hivyo.
Video hii inaonyesha majonzi ya familia na jamii kwa jumla.
Kwa sasa, ni muhimu kutenganisha kile kilichoripotiwa na kile ambacho kimehakikishwa rasmi. Uchunguzi ndio utaamua iwapo pombe hiyo ilisababisha lakini ni ukweli usiopingika kuwa tukio hili linaingia kwenye simulizi kubwa ambalo tumekuwa tukiliona mara kwa mara mwaka huu, hasa katika maeneo ya Kiambu na sehemu nyingine za Mlima Kenya.
Tumekuwa tukiona taarifa za misako ya pombe haramu, bidhaa zikikamatwa, baa zikifungwa, washukiwa wakikamatwa, kisha baada ya muda, tunarudi tena kwenye habari za watu kulazwa au kupoteza maisha baada ya kunywa pombe.
Na hapo ndipo video hii ya Makwa inaleta picha tofauti.
Kwa sababu nyuma ya kila taarifa inayosema “watu wawili wamefariki” kuna familia zinazobaki na pengo, wazazi wanaolia, watoto wanaoondokewa na wazazi wao na jamii inayolazimika kushughulika na madhara yake.
Hivyo, mjadala hauishii kwenye “pombe haramu imeua tena.” Hapana! Swali kubwa ni:
Ikiwa tumekuwa tukiona misako na operesheni dhidi ya pombe haramu, kwa nini bado tunarudi kwenye matukio kama haya?
Je, tatizo ni utekelezaji wa sheria, upatikanaji wa pombe hizo, mfumo wa utoaji leseni, au kuna changamoto nyingine ndani ya jamii inayofanya biashara hii iendelee?
Makwa imetukumbusha kwamba nyuma ya takwimu za pombe haramu kuna watu halisi na familia halisi zinazolia. Hebu watazame tena kina mama hao wakilia kwa uchungu kisa pombe!