Thursday, March 16, 2017
Ofisi ya CAG iwezeshwe itimize majukumu
Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Prof. Mussa Juma Assad
Kwa ufupi
- Ilielezwa kuwa ufinyu huo, siyo tu ulikuwa unakwamisha maofisa wa ofisi hiyo kusafiri kwenda kutekeleza majukumu yao kisheria, bali pia kushindwa kuwasaidia wafanyakazi katika masuala ya afya, hususani wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU).
By Mwananchi
Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imelalamikia ukata. Mara ya kwanza ilikuwa Mei mwaka jana ilipolalamika kuwa ilikuwa ikifanya kazi katika mazingira magumu kutokana na ufinyu wa bajeti.
Ilielezwa kuwa ufinyu huo, siyo tu ulikuwa unakwamisha maofisa wa ofisi hiyo kusafiri kwenda kutekeleza majukumu yao kisheria, bali pia kushindwa kuwasaidia wafanyakazi katika masuala ya afya, hususani wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU).
Wabunge walisikia kilio hicho. Hivyo, wakati wa mjadala wa bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2016/ 17 walipigania ofisi hiyo, ambayo ni jicho la Serikali katika usimamizi wa matumizi bora ya rasilimali za umma, iongezewe fedha ili itekeleza majukumu yake, hasa ikizingatiwa kuwa mikoa, wilaya, mashirika na maeneo mengine ya ukaguzi yameongezeka.
Ofisi ya CAG ndiyo hukagua matumizi ya hesabu za Serikali Kuu (wizara ya idara zake), Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (mikoa na wilaya zake), mashirika ya umma, wakala za Serikali na miradi ya maendeleo.
Mbali ya maeneo hayo ambayo yanafahamika, ofisi ya CAG pia huitwa kufanya ukaguzi maalumu mahali popote au ofisi yoyote ambayo inatiliwa shaka kuhusu matumizi ya fedha kama vile taasisi ya umma. Vilevile, ofisi ya CAG ndiyo hukagua matumizi ya fedha ya balozi zetu nchi za nje pamoja na ofisi za mashirika ya kimataifa yaliyoko chini ya Umoja wa Mataifa (UN) ambayo Tanzania iliingia mkataba kwa miaka sita kuanzia mwaka 2013.
CAG akifanya ukaguzi, kwanza hujiridhisha kama hayo ndiyo matumizi yaliyopangwa na pia hujiridhisha kuhusu thamani ya fedha katika miradi husika. Mwishoni mwa ukaguzi wake hutoa hati chafu au safi kulingana na namna alivyoona.
Lakini katika bajeti ya mwaka 2016/ 17 ilijitokeza hofu kwamba CAG asingeweza mwaka huu kufanya ukaguzi wa maana na ikiwa angefanikiwa asingefikia ofisi nyingi kama alivyokuwa akifanya miaka ya nyuma. Haikufahamika sababu ya kutengwa kiasi kidogo cha fedha kwa ofisi hiyo hasa ikizingatiwa bajeti ilikuwa ya Sh29.5 trilioni.
Katika kipindi hiki cha kuelekea kukamilisha mwaka wa fedha wa 2016/ 17 ofisi hiyo ya CAG imelalamika kwamba inashindwa kufanya kazi kufikia kiwango cha kitaifa na kimataifa, kama inavyotakiwa licha ya kuwa na watumishi wenye ari kwa sababu ya ufinyu wa fedha.
Pia, ofisi hiyo imesema inakabiliwa na madeni makubwa ya makandarasi ambao wanajenga majengo, likiwamo la Rukwa.
Waswahili wanasema kupanga ni kuchagua. Hatua yoyote ya kutoipa nguvu ofisi hii ambayo kwa miaka iliyopita ilisaidia kufichua uovu, wizi na ufisadi hadi Serikali ikachukua hatua dhidi ya maofisa au mikoa, itakuwa inachangia kurudisha nyuma juhudi zilizofikiwa.
Sote tunafahamu kwamba tangu CAG alipoanza kuwekwa hadharini ripoti ya ukaguzi wa hesabu mbalimbali, utunzaji mbovu wa hesabu umepungua, wizi na ubadhirifu umekwisha na ofisi nyingi zilizokaguliwa hupewa hati safi. Pia, imekuwa rahisi hata kugundua maeneo ambayo kuna kiwingu katika usimamizi wa miradi.
Tunaonya kadri ofisi hii itakavyokuwa inapunguziwa uwezo wake wa kukagua kutokana na kutengewa fedha kidogo ndivyo maofisa “wajanja” au wezi wa kutumia kalamu watakuwa wanarudi taratibu na kujiimarisha. Tunashauri ofisi hii iwezeshwe itimize majukumu yake.