Yoyo Zhou
Senior Member
- Jun 16, 2020
- 126
- 215
Katika mwaka 2024, Afrika ilichukua nafasi kubwa kwenye ajenda ya maendeleo ya kimataifa, ikionesha uthabiti wa bara hilo na uhusiano wake wa kina na China na nchi za Dunia ya Kusini kwa ujumla katika medani ya kimataifa.
Kuanzia Mkutano wa 19 wa Wakuu wa Nchi Zisizofungamana na Upande wowote, hadi Mkutano wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) wa Beijing, Afrika imeonesha azma na uwezo wake wa kuungana na China na nchi nyingine za Kusini katika kufikia maendeleo ya pamoja na kutafuta usasa.
Mwezi Septemba, Mkutano wa kilele wa FOCAC wa Beijing uliashiria hatua nyingine muhimu ya kihistoria katika uhusiano kati ya China na Afrika na kwa Dunia pana ya Kusini. China na Afrika ziliapa kushikana mikono kutekeleza hatua 10 za ushirikiano ili kuendeleza usasa.
China ikiwa mwanachama wa Dunia ya Kusini, imekuwa ikihimiza mara kwa mara kuwepo kwa uchumi wa wazi duniani, na kuzisaidia nchi zinazoendelea, hasa mataifa ya Afrika na nchi zenye maendeleo duni, kushiriki kikamilifu katika ushirikiano wa kimataifa wa viwanda na kunufaika na utandawazi wa kiuchumi.
Mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Ufuatiliaji wa Sera na Utafiti cha Zambia, Sydney Mwamba, alisema katika mahojiano kuwa usasa wa China unatoa muongozo muhimu kwa nchi za Afrika, na mafanikio ya China katika kupunguza umaskini, maendeleo ya miundombinu na maendeleo ya teknolojia ni mifano ya kuigwa kwa nchi za Afrika katika kufikia maendeleo endelevu.
Anaamini Afrika inaweza kujifunza kutokana na safari ya China kutoka hali yake ya kabla ya usasa hadi hali yake ya sasa, ambayo imebadilisha nchi hiyo kutoka jamii ya kilimo na kuwa nchi yenye nguvu kubwa ya kiuchumi duniani. Safari hiyo ya China inatoa mafunzo muhimu kwa Afrika, ambayo inajitahidi kujiletea maendeleo kwa njia ya kisasa.
Bw. Mwamba pia alipongeza hatua 10 za ushirikiano zilizopendekezwa na China kwa ajili ya kuendeleza usasa kwa pamoja na Afrika, hususan hatua ya ushirikiano kwenye suala la muunganisho, ambayo inawiana na Ajenda ya 2063 ya Umoja wa Afrika na Eneo la Biashara Huria la Afrika.
Mwezi Julai mwaka 2024, Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kiliitisha kikao cha tatu cha Kamati yake Kuu ya 20, kikitoa mwongozo wa kuimarisha mageuzi ya kina ili kuendeleza usasa wa China, ambao unatoa mwongozo muhimu kwa mataifa ya Afrika hasa yale yanayotafuta maendeleo yao kwa njia za kisasa.
Ikumbukwe kuwa msaada wa China kwa Afrika, hasa katika maendeleo ya miundombinu, unachukua nafasi muhimu katika kuendeleza bara hilo kuwa la kisasa. Ndio maana China imelivalia njuga suala la kuipatia Afrika uwekezaji mkubwa unaohitajika katika miundombinu, kama vile barabara, reli na nishati, kufungua uwezo wake na kutoa nafasi za ajira, kulingana na malengo ya Ajenda ya 2063 ya Umoja wa Afrika.
Naye mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Afrika na China cha Sera na Ushauri nchini Ghana amesema ingawa uwekezaji wa miundombinu unatoka kwa washirika mbalimbali ili kuongeza juhudi za Afrika za kuziba pengo la miundombinu na kuimarisha usasa wake, msaada wa China unapita msaada wa washirika wengine wote.
“Hakuna nchi iliyokaribia kiasi na kiwango cha uwekezaji ambacho tumepokea kutoka China katika uwekezaji wa miundombinu katika miongo kadhaa iliyopita," alisema.