NI NINI DHAMIRA YA MZEE KINANA, MAKAMBA NA GENGE LAO?
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa nafasi hii ili niweze kuzungumza na Watanzania wenzangu leo, hasa wanaCCM. Nimeamua kutumia uhuru huu wa kikatiba ibara ya 18 baada ya kuona habari mbali mbali kwenye vyombo vya habari ambazo ni za kifedhuli kwa Chama na Serikali yetu. Hatuwezi kukubali CCM na serikali kutunwa na Waliotufisha anakotutoa JPM.
Mwanzo ilitokea barua iliyosadikika imetoka kwa wazee wetu wastaafu yaani mzee Kinana na Mzee Makamba. Nimesema inasadikika kwa kuwa hawajajitokeza hadharani kukubali au kukanusha. Barua yenyewe iliandikwa kama wito au tamko ambalo lilielekezwa kwenye Baraza la wazee wa CCM linaloongozwa na Mzee Mwinyi kama Mwenyekiti na Mzee Pius MSEKWA kama Katibu wa Baraza hilo. Na kwenye tamko lao waliandika wakionyesha kukerwa na lugha za kudhalilisha zinazotolewa na Ndugu Musiba.
Makamba na MH Nape kwa mwendelezo wa mikakati hiyo hiyo Siku chache baadae zimetokea sauti zinazosadikika zilizodukuliwa. Mwanzo inaonyesha mzee Kinana akizungumza na Mh Nape na wakiwa kwenye mkakati huu ambao ninadhani ndio zao la barua hiyo.Baadae imetokea sauti ya Mh Ngereja na Mh Nape wakiwa kwenye mikakati hiyo ovu. Baada ya siku chache imetokea tena sauti ya Mh Makamba akizungumza na Mh January Makamba na baadae January anamuunganisha Mzee.
Kabla sijatoa kusudio langu la kukemea na kulaani uhaini huu ndani ya CCM, ninaomba tuunganishe dots kidogo. Barua au tamko linalosadikika kutolewa na hawa wazee kwenda kwa Katibu wa Baraza na baadae katibu wa Baraza kujibu ni kuwa mzee Msekwa kwenye barua yake anakiri alipokea barua ya Mzee Kinana na Mzee Makamba kutoka kwa Mh Nape. Kitendo cha Mh Nape kwenda kumpelekea mzee Msekwa barua nyumbani, kitendo hiki kinanifanya niamini hizi sauti hazijatengenezwa na ni sauti zao ambazo maudhui yao ni kujenga mpasuko ndani ya CCM.
Si jambo jema na la hekima sana kwetu vijana kuwakosoa, kuwasahihisha, kuwakemea na kuwakumbusha wazee wetu au viongozi wetu. Lakini ni wajibu wetu vijana wa kuhakikisha tunalilinda Taifa na tunalinda misingi ya CCM. Inapotokea mzee au kiongozi ambaye kwa makusudi anajaribu kutengeneza jaribio la kuhatarisha umoja huu, basi ni wajibu wetu vijana kuvaa uzalendo na kuwakosoa bila aibu wazee hawa ambao baada ya kula matunda ya umoja wa taifa hili sasa wanataka kuharibu misingi ya umoja huu.
Kitendo cha Ndg Kinana na Mzee Makamba kuandika barua ile kwenda kwa Mzee Msekwa ili kuonyesha hisia zao si dhambi, lakini kitendo cha kuandika na kusambaza kwenye mitandao kunaonyesha hawana nia njema. Tukipima actus reus na mens rea(nia) zao zilikuwa ni za hujuma na za kulibagaza Taifa. Ni wazee hawa waliotufundisha maadili ya Chama na kutufundisha namna ya kuyafuata, iweje walimu wa kanuni ndio wawe wa kwanza kuvunja? Nia yao ilikuwa nini? Kwa nini hawakwenda Lumumba kupeleka malalamiko yao?
Labda niwakumbushe tu kuwa wakati wa mzee Makamba ndicho kipindi ambacho mzee Lowasa alitukanwa sana na kufedheheshwa sana. Kipindi cha Kinana mzee Warioba alitukanwa na kupigwa na watu waliosadikika ni Wana CCM na hakuna hatua iliyochukuliwa. Kipindi cha Kinana wakati wa oparesheni vua gamba akiwa Mtwara, Ruvuma na Mbeya alisema kuna mawaziri mizigo na akasema bila kuwasema hadharani tutakuwa wanafiki. Sasa kama wao walitumia mfumo huu wa matusi kwenye kujivua gamba wanalalamika nini kwa ndg Musiba kwenye kujenga CCM mpya? CCM mpya haiwezi kujengwa bila kuwataja wezi, wahaini, na waliotumia hovyo mali za Chama.
Nyie ndio mliotudanganya kuwa CCM ni ya wakulima na wafanyakazi lakini kiuhalisia kipindi chenu CCM ilikuwa ni ya Wafanyabiashara, Wezi na Mafisadi. Mh Magufuli anajaribu kurudisha misingi haswaa ya CCM ili hata wakulima wa Ileje, Nkasi, Namtumbo, Nyakanazi, Ikungi n.k wale matunda ya CCM. Hatuwezi kuendelea kuwa na CCM ya utwana na ubwana mliyokuwa mnajaribu kutujengea. Muacheni Mwenyekiti anyoshe Nchi. Miaka mitatu na ushee ya uongozi wake tunaona vitu vinavyoonekana. Sasa hakuna mapapa ndani ya CCM, hata sis watoto watoto wa vijijini tumekuwa na nafasi ndani ya CCM.
Uhauri wangu kwa viongozi wakuu wa CCM, Ukisoma ile barua na ukisikiliza zile audio ni wazi hawa watu hawana nia njema na Taifa. Wakati tunapendekeza kuwapa adhabu kali ambayo itakuwa fundisho kwa wanaCCM wote wanatakiwa kujitokeza hadharani na kuliomba taifa msamaha kwa uhaini ndani ya CCM. Haiwezekani watu ambao ndio wametufikisha hapa kumuita Rais mshamba na anaogopa kurudi Da res salaam. Huu si upuuzi wa kuendelea kuulea. Tunapohitaji kurudisha Taifa kwenye misingi ya haki na usawa basi hatunahaja ya kumtazama mtu usoni. Mtu yeyote anayejaribu kukwamisha juhudi za Mh Rais si tu si mzalendo bali ni mtu anayetakiwa kutazamwa kwa jicho la tatu.
Mh Rais ni binadamu na si Mungu, hivyo wakati mwingine anaweza kukosea katika kuwatumikia Watanzania Zaidi ya milioni 50. Anaweza kukosea kwa kupotoshwa au kwa namna nyingine. Lakini kwa viongozi kama hao niliowataja hawawezi kutumia lugha kama hiyo kufikisha ujumbe kwa Mwenyekiti. Ili kulinda heshima ya Chama na serikali kama ambavyo Watanzania wengine wamekuwa wakitumbuliwa kwenye nafasi zao wakionyesha utovu wa nidhamu, ni wazi hawa watu wanaoonyesha dhahiri wanaajenda ya siri na huenda huko nyuma kuna ujanja walikuwa wanaufanya maofisini. Ni muda wa kuwachunguza na kupitia upya mafaili yao kama hawajauhusika kulihujumu Taifa wakiwa madarakani.
Wakati ninaandika haya ninajiuliza maswali mengi. Mwaka 2012 niliingia kwenye mkutano mkuu wa CCM uliofanyika Kizota. Yapo makundi yalijitokeza kuhamasisha MH KIKWETE apigiwe kura za hapana za Uwenyekiti. Mzee Makamba ndiye alisimama na kukemea tabia hiyo kwa ukali na kumuombea mh Kikwete kura. Kutokana na hotuba yake nzuri huku Mh Mkapa akiwa mwenyekiti wa mkutano wa uchaguzi ukumbi ulizizima na tukasimama kumpa fedha za shukurani mzee Makamba. Mkutano wa kumchagua Mh MAGUFULI ni mzee Makamba alipewa nafasi ya kushukuru baada ya Magufuli kupata kura nyingi. Aliongea maneno mengi mazuri, lakini mwisho alimalizia kwa kusema JK aliwabatiza kwa maji, HUYU ATAWABATIZA KWA MOTO. Hivi alitaka ubatizo hupo uwe wa matabaka au usawa? Kama ni wahi basi ni muda wa CCM kuwabatiza hawa wazee kwa ubatizo wa moto.
Barua yao iko wazi imewalenga viongozi wakuu wa CCM, Kwani angekuwa mtu mwingine analengwa kuwa anamkingia kifua Musiba basi barua ingeenda kwenye chama na isingepelekwa kwenye mitandao kuleta taharuki. Sisi Watanzania tuliozoea kula viazi na maziwa ya ng’ombe wa kienyeji hatuna shaka kabisa na Mh Rais. Tunaona ndege zinanunuliwa, barabara zinajengwa hata huku kwetu Ileje, vituo vya Afya, Elimu bure na shule zinaboreshwa, Meli zinanunuliwa, Viwanja vya ndege vinajengwa, safari za hovyo hovyo kwenda nje zinaisha, Utendaji maofisi umeongezeka mara dufu, makusanyo kwa mwezi yamepanda kutoka bilioni 8 hadi 1.3 trillion n.k unaanzaje kuzungumza Rais Mshamba? Huu ni upuuzi na tunaosoma historia ya nchi yetu ilikotoka na tunakoenda sasa hatuwezi kumwacha Mh Rais ambaye wazi ni mzalendo kufedheheshwa na watu waliokula Taifa bila kuwaonea wenzio huruma.
Chama imara huzaa serikali imara, na Chama dhaifu huzaa serikali dhaifu. Ili serikali ipone na Mh Rais aweze kufanya kazi zake vema hakutakiwi kuoneana aibu kwa mtu yeyote. Inawezekana wa mijini msielewe, sisi tulikulia vijijini tunajua shida zilizokuwepo huku. Rushwa ilitamaraki lakini kwa sasa hali hata ukienda hospitali unatibiwa haraka bila kuhonga honga honga.
Hili genge ni kubwa. Mwanzo nilikuwa ni mtu ambaye nilikuwa nikimpuuza ndg Musiba, na nitumie furusa hii kumuomba radhi sana hata kama njia alizotumia kufikisha ujumbe hazikuwa sahihi. Lakini baada ya kusoma barua na kuzisiliza clip ambazo inasemekanna ni za hawa Watu wakubwa ninaona ndg Musiba alikuwa sahihi mno. Ninawaomba Watanzania hasa WANACCM wenzangu ni muda mwafaka wa kumlinda Mh Rais na kuwapuuza hawa watu ambao hawana nia njema. CCM inawatu wengi.Waliondoka nab ado CCM ipo. Tunapotaka kuirudisha nchi tusiangalie sura hata kama mtu ni mkubwa kama mlima Kilimanjaro ashughulikiwe tu.
Ahsante
Elius W ndabila
Ibaba-Ileje