Ndugu watanzania wenzangu, salaam.
Imekuwa kama sehemu ya utamaduni kutokumpa mtu sifa zake njema angali hai bali ni rahisi sana kuona yale mabaya au tusiyoyapenda. Mtu huyohuyo anapokufa ndio sasa utasikia mema yake lukuki mengine hata hukuwahi kuyasikia.
Awali ya yote, napenda kukumbusha japo ninajua tunafahamu ya kuwa Magufuli kwa mama yake yeye ni mtoto, yaani John, yeye ni mume wa Janet, baba wa akina Jesca na ndugu zake, mjomba, baba mkubwa/mdogo, rafiki na mtanzania kama nilivyo mimi na wewe.
Tukumbuke kuwa Magufuli hajawa malaika ba kamwe hatakuwa malaika. Magufuli sio mtakatifu na wala hajaingia kwenye mchakato wa kuwa mwenye heri. John is just a man.
Ninatambua kuwa unapokuwa Rais kuna sifa za ziada zinazotarajiwa kwako lakini pamoja nazo bado hazikuondolei ule uasili wa ubinadamu wako.
Rais John Magufuli anao udhaifu wake kama mwanadamu lakini tupime zaidi uimara wake hasa kwenye taasisi hiyo ya urais na pale tunapoona madhaifu, basi tumkosoe kistaarabu.
Rais Magufuli amejitahidi mno na nadhani amewashinda marais wote waliomtangulia kwa kigezo cha mambo aliyoyafanya kimaendeleo katika kipindi hiki cha miaka mitano.
Kwanza amekuza sana makusanyo ya Kodi. Udhaifu katika makusanyo ya kodi kilikuwa kilio cha wengi hasa wapinzani. Ameongeza kasi kwenye ujenzi wa barabara na madaraja. Serikali ya awamu ya tano imenunua meli na vivuko vipya.
Kwenye Kilimo mikopo inatolewa kwa wakulima, anapambana na watu wa Kati wanaowadhulumu wakulima. Njaa sasa imekuwa historia nchini kwetu. Nidhamu imeimarika sana serikalini hivyo kuboresha huduma. Rushwa imedhibitiwa kwa kiwango kizuri.
Tumeongeza ndege na kufufua shirika la ndege. Mgawo wa umeme umebaki kuwa historia. Umeme umesambazwa maeneo mbalimbali ya nchi mpaka vijijini. Maji yameendelea kusambazwa.
Elimu bila malipo ambayo imeongeza udahili. Shule zote kongwe zimekarabatiwa kwa kiwango kizuri na kurejesha kiwango chake cha awali. Shule za umma sasa zinaanza kurudi kwenye kumi bora. Zahanati na hospitali nyingi zimejengwa, bajetibya dawa imeongezwa sana. Sera yetu ya mambo ya nje imehuishwa na kuwa inaingalia Tanzania kwanza.
Mambo ni mengi na takwimu zipo. Ukiangalia vizuri utaona Rais Magufuli amegusa kila nyanja na hii ndio maana tumeingia kwenye uchumi wa kati. Ukiwa na jicho la kuangalia baya ni lipi kwenye kila jema basi huwezi kuona kazi kubwa iliyofanyika.
Rai yangu ni kuwa Rais Magufuli ni mchapakazi na mtu mkweli. Tumuunge Mkono kwa kufanya kazi kwa bidii. Kwa wapinzani, ninawashauri wajikite zaidi kwenye kuojenga nchi badala ya kuikwamisha. Mambo yakiharibika, haharibikiwi Magufuli peke yake, tunaharibikiwa watanzania.
Magufuli amekuwa Rais wa mfano, tumuunge mkono kwa vitendo na kuhakikisha tunampa kura tarehe 28.10.2020 ili atupaishe zaidi kama nchi.
Mungu mbariki Rais Magufuli
Mungu ubariki uchaguzi mkuu wa tarehe 28.10.2020
Mungu ibariki Tanzania
Amani Msumari
Tanga