Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Zimepita siku 72 tangu kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu ilipoahirishwa, kwa muda usiojulikana baada ya upande wa Jamhuri kwenda Mahakama ya Rufaa kuomba mapitio ya kesi hiyo Februari 24, 2026.
Hatua hiyo ilikuja wakati usikiliwaji wa mashahidi upande wa Jamhuri ukiendelea, hata hivyo baadaye, mawakili wa Jamhuri waliomba ahirisho la muda tangu saa tano asubuhi na waliporudi saa 9 alasiri walisema wamewasilisha maombi Mahakama ya Rufaa wakitaka mapitio.
Akijibu taarifa hiyo mahakamani Lissu aliuomba upande wa Jamhuri kumkabidhi nakala ili aweze kujiandaa na shauri hilo la mapitio.
Lissu alieieleza mahakama kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 8(2D) cha sheria ya Mamlaka ya Rufaa kwamba hakiruhusu rufaa wala mapitio wala marejeo ya maamuzi ya mahakama ambayo hayamalizi shauri la msingi.
Alieleza kuwa anafahamu hilo limefanyika kwa lengo la kurefusha mashauri haya ili aendelee kukaa gerezani “Hilo lengo ni kupeleka huko huku yasimame ili huyu mbaya wao aendelee kukaa gerezani.
“Kwa vile wanalipeleka mahakama ya rufani nitawafuata huko huko na kwenda kuwashughulikia huko huko. Najua nitakaa gerezani lakini nitarudi hapa na tutakaporudi hapa tutaona jinsi ambavyo kesi yao ilikuwa imekufa” Lissu alisisitiza.
Tangu wakati huo, kesi ya Lissu imegeuka kuwa kitendawili kisicho na jibu, huku yakiibuka maswali kuhusu sababu za mahakama kuchelewesha rufaa ya Jamhuri ili kesi ya msingi iendelee.
Juhudi za kuupata upande wa Mahaka kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa, kwani licha Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa Mahakama, Gerald Julius Chami kutaka atumiwe maswali kuhusu suala hilo, Machi 19, 2026, maswali hayo hayakujibiwa hadi taarifa hii ilipoandikwa, zikiwa zimepita siku 50.
Hatua hiyo inakuja wakati Jaji Mkuu, George Masaju amekuwa akionya Mahakama kutumika kama eneo la kupaki kesi, akisema inasababisha Mahakama kupoteza heshima yake.
Akizungunza Aprili 9, 2026, katika ufunguzi wa wiki ya Usuluhishi Wiki ya Usuluhishi, inayofanyika katika Ukumbi wa PSSSF Golden Jubilee Tower jijini Dar es Salaam Jaji Mkuu Masaju alikemea vikali Mahakama kukaa na shauri kwa muda mrefu.
"Mahakama sio sehemu ya kupaki kesi," alisema.
Lissu aliyekamatwa Aprili 9, 2025 wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma na kusafirishwa hadi Dar es Salaam, ameshatuimiza mwaka na mwezi mmoja akiwa rumande katika Gereza la Ukonga.
Aprili 10, 2025 alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam aliposomewa mashitaka ya uhaini na kuchapisha taarifa za uongo.
Kesi hiyo ilihamia Mahakama Kuu Agosti 2025, ambako mpaka sasa inaendelea.
Mbali na kesi ya uhaini, Mkurugenzi wa Sheria wa CHADEMA, Gaston Garubindi amesema hata kuchapisha taarifa za uongo inayosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu nayo haiendelei kusikilizwa kwa sababu ambazo hazieleweki.
Mahakama inastahili lawama kuchelewa kesi ya Lissu?
Akizungumzia suala hilo, Wakili Edson Kilatu alisema, “Mahakama inastahili lawama kwa kesi hii ya Lissu, kwa sababu, Jaji Mkuu ndiye anayetunga kanuni za mahakama. Serikali imetimiza wajibu wake kwani Rais ameteua majaji wengi kiasi kwamba wanaweza kukaa hata vikao vinne kwa wakati mmoja na hiyo ni kazi ya Jaji Mkuu.
“Mahakama pia inapaswa kuangalia kesi muhimu na kuzipa kipaumbele, Kwa mfano mtu ana kesi ya mauaji au kesi ambayo hukumu yake ni kifo, unamweka rumande kwa muda mrefu, halafu baadaye unamhukumu kifo, lakini tayari ameshakaa gerezani muda mrefu.”
Alisema pia kuna shida kwenye mfumo wa mahakama kwa sababu kesi ikishapelekwa kwenye mahakama ya rufaa, hakuna kifungu cha sheria kinachoibana mahakama kwa kuweka muda maalum.
“Kwa hiyo mtu akitaka kuichelewesha kesi, anakata rufaa,” amesema.
Hata hivyo, alisema tofauti na Mahakama ya Rufani, kwenye Mahakama chini kuna muda maalum wa kesi kusikilizwa.
“Kesi za Mahakama ya rufaa zinasikilizwa kwa session na ni lazima kuwe na bajeti ya kuitisha jopo la majaji wakae na kuisikiliza. Kwa hiyo kama hakuna bajeti ndio basi mpaka ipatikane,” alisema.
Alizungumzia pia suala la mawakili kukata rufaa kwa jambo ambalo halina msingi na wala haliwezi kuibadilisha kesi ya msingi.
“Badala ya kusubiri kesi iishe mtu akate rufaa kwa kesi nzima, anakata rufaa kwa jambo dogo tu, kwa mfano mtu anakatia rufaa jina lililokosewa, haliwezi kubadilisha kesi ya msingi zaidi ya kupoteza muda tu,” alisema.
Alisema mambo yote yako ndani ya uwezo wa mahakama, inawezekana uyatatua na kesi zikaenda haraka.
Naye Wakili Fulgence Massawe akizungumzia suala hilo, alisema Mahakama ya Rufani inaweza kutumia busara zake kuharakisha kesi hiyo, lakini haibanwi na sheria.
“Hayo ni maombi tu ya kutaka tafsiri ya mahakama kuhusu kesi inayoendelea, kwa hiyo siamini kama itachukua muda mrefu, kwa sababu kwenye ile kesi ya mali za chama, mawakili wa Chadema waliomba marejeo kwa kutoridhishwa na mwenendo wa jaji anayeendesha (Jaji Hamidu Mwanga),” alisema.
Katika uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Rufani Aprili 15, ulimwondoa Jaji Mwanga kuendelea kusikilia kesi hiyo, huku pia ikiondoa zuio la Chadema kufanya kazi lililowekwa Juni 10, 2025.
Alipoulizwa kuhusu muda unaotakiwa kusikilizwa kwa mapitio hayo, Massawe alisema, “hiyo ni discretion ya mahakama yenyewe.”
Akizungumza katika mkutano mkuu wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) uliofanyika jijini Arusha, Rais wa chama hicho, Boniface Mwabukusi alisema, uendeshahi wa shauri la Tundu Lissu hauzingatii sheria.
“Tusiruhusu kiongozi mwenzetu aonewe, ule sio uendeshaji wa shauri wa aina ile. Shauri ambalo limeshaanza linasitishwa, kunakuwa na rufaa za ajabu katikati, watu wanaandika barua za malalamiko, mwennzetu yule ni mdhaifu mnamwona, mwaka mzima yuko ndani anazunguka na wote tuliona ukamataji ule, sisi sote ni wanasheria katika huu ukumbi.
“Mimi nilisema tunaelewa subjudice rule (kesi inayosubiri uamuzi wa mahakama), lakini usikamate mtu kwa kumwonea ukaniambia subjudice rule. Tundu Lissu sio mhaini, tunajua sote.
“Kama Tundu Lissu anatusumbua kisiasa, futa mfumo wa vyama vingi, kwa sababu kikibaki chama kimoja mtamwondoa kwenye chama chenu akose jukwaa,” alisema Mwabukusi.
Mkurugenzi wa Sheria CHADEMA, Gaston Garubindi
Operesheni ya CHADEMA
Kutokana na kutotabirika kwa muda maalum wa kesi hiyo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeandaa operesheni ya mikutano ya hadhara nchi nzima mwezi huu, ikiwa ni sehemu ya mikakati yake ya kisiasa na kijamii inayolenga kuhamasisha mabadiliko ya Katiba pamoja na kudai uhuru wa mwanasiasa Tundu Lissu.
Akisoma maazimio ya Kamati Kuu ya CHADEMA mbele ya waandishi wa habari Mei 2, 2026 Katibu mkuu wa chma hicho, John Mnyika alisema operesheni hiyo itajulikana kama Operesheni Katiba Mpya, Free Tundu Lissu, na itafanyika kwa awamu mbili, ikiwamo ya Kanda za Serengeti, Victoria na Kaskazini, na inatarajiwa kuanza wiki ya tatu ya mwezi Mei mwaka huu.