Mahakama ya Wilaya ya Iringa imemhukumu mfanyabiashara, Kaloli Mkusa kifungo cha miaka 30 jela na fidia ya shilingi milioni moja baada ya kumtia hatiani kwa kumbaka mama yake mzazi.
Hata hivyo mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 30 pamoja na baba yake Joseph Mkusa ambaye alimuwekea dhamana, wametoweka kusikojulikana ambapo hati ya kukamatwa kwao tayari imetolewa.
Imeelezwa mtuhumiwa alitenda kosa Julai 7, 2021, alikuwa akifanya biashara Mkoani Songwe, alirejea Iringa akafikia kwa baba yake ambaye anaishi nyumba tofauti na mama yake kutokana na kutalikiana.
Siku ya tukio mtuhumiwa alienda nyumbani kwa mama yake usiku na kuvunja mlango, akamtishia kwa panga mama yake kisha kumbaka.
Baada ya tukio hilo, mama mzazi alitoa taarifa na taratibu za kumkamata zikafanyika, inadaiwa alifanya hivyo kwa Imani za kishirikina kutokana na biashara zake kuyumba.
Hati ya kumkamata mtuhumiwa alitolewa Machi 9, 2022 lakini mtuhumiwa na baba yake hawajulikani walipo, kwa mujibu wa sheria mtuhumiwa ataanza kuitumikia adhabu hiyo mara baada ya kukamatwa.
Source: Azam TV