mHAMAS-shaji
Member
- May 31, 2024
- 63
- 177
- Thread starter
- #81
MAISHA YA DEPO
SEASON-2
EPISODE 19
Alituambia kuwa inafika kipindi unachoka mpaka unakosa hamu ya tendo yaani mwanamke anaweza akawa mtupu na usifanye wala kumtamani ukamuona ni kama msela mwenzio.
Afande alitutahadharisha kuwa tujitahidi mno kipindi hicho hata mtu akidoji asiwe peke yake kwani unapodoji ukaenda kulala unaweza kulala kwa muda mrefu na ukiamka unajikuta una njaa ya kwenda.
Alitusimulia kuwa kipindi wao wako kozi kuna mwenzao alidoji peke yake walimtafuta wiki nzima bila mafanikio.
Siku moja walimkuta shambani akiwa amelala walipomuamsha hakuweza kufumbua mdomo, kuongea wala kutembea mana hata walipomsimamisha alikuwa akitetemeka na kuanguka kutokana na njaa kali aliyokuwa nao.
Tulimpinga sana afande kwenye swala la kuchoka mpaka kutotamani kufanya tendo pendwa mimi nilikuwa kinara wa hilo sikukubaliana naye.
Ilifika hatua tukawekeana viapo maana aliniambia kuwa kuna kipindi walidoji na MADAWILI kadhaa sasa kuna doja mmoja alikuwa anawachezea wale MADAWILI na hawajawahi kugundua mpaka kozi inaisha.
Nilimwambia kama huyo mwenzao aliweza kufanya hivyo basi siyo kweli na kama ni kweli basi itakuwa hao wengine wanashida ya nguvu za kiume, afande Elisha aliniahidi kunitafuta wakati huo utakapofika.
Tulipomalizana na kipengele hicho tulirejea zetu kikosini na afande Elisha ndiye aliyekuwa akiliongoza bogi hilo.
“Afande Elisha: Ewii
Sisi: Ewaaah
Afande Elisha: Ewii
Sisi: Ewaaah
Afande Elisha: Ewii
Sisi: Ewaaah
Afande Elisha: Ee Shaa, Shangazi
Sisi: Usikate shanga
Afande Elisha: Zuu zungusha
Sisi: Zungusha nyonga
Afande Elisha: Aii mama nilikuwa sijui
Sisi: Nikipata demu mauno mpaka asubuhi”.
Tulifika salama MAHANGANI na kuyafanya tuliyostahili kuyafanya ila hali ya hewa kidogokidogo ikawa inaanza kubadilika.
Ukafika muda wa msosi tukaenda zetu kuwakilisha kwa MZABUNI na hatimaye tukaelekea KOMBANIA ambako nilikutana na mazagazaga yangu kutoka kwa mtoto Linda nikayapokea na kuyapeleka HANGANI.
Ilipofika mishale ya saa tatu iliporomoka mvua kama ya buku na mdogo wake ilibidi tutolewe sehemu ile iliyokuwa wazi na kupelekwa kwenye bwalo la chakula walilokuwa wakilitumia maafande wa JKT.
Tuliwakuta Service Man hao wa JKT wakiwa wanaangalia tamthilia za azamtv hivyo ni kama tulienda kuwaharibia kwani iliwabidi waamke kwenye viti nao wasimame na viti kuviweka sehemu moja kwa kuvibananisha ili kusudi ipatikane nafasi ya kutosha.
Usiku huu haukuwa usiku wa kuimba wala kusifu ila ule usemi wa “Burudani kwa wote” ndiyo uliokuwa ukitanua mbawa zake kwa usiku huo.
Ilifika saa nne muda muafaka wa tamthilia pendwa ya Sultan ambayo iliwafanya watu kutokujali kama kuna mvua ilikuwa ikinyesha walikuwa wakiongezeka.
Alikuwa akionekana mama wa himaya Bi Hulem Sultana akiwa na chawa wake aliyemjaza nyota za kutosha wakiwa kwenye mipango ya kumpelekea pumzi ya moto Waziri mkuu aliyefahamika kwa jina la Ibrahim Pasha.
Kilikatika kipande cha kwanza kati ya vile vitatu kilipofika cha pili walikuja maafande wa zamu yaani afande Jamali aliyeongozana na afande Mpemba aliyekuwa na kifimbo chake mkononi kama cha afande Pastima.
Ilibidi runinga izimwe ili tuendelee na zoezi la lokoo lililochukua muda mrefu kutokana na kukosea kuhesabu maana tulikuwa hatusikilizani vizuri kutokana na makelele ya mvua na hata hivyo eneo lilikuwa ni dogo na tulikuwa wengi mno.
Hesabu zilipokaa sawa tuliruhusiwa na kwenda zetu MAHANGANI, asubuhi yake hakukuwa na mvua hivyo tuliendelea na ratiba nyingine.
Kipindi zinaendelea ratiba hizo nilipata kuuona umuhimu wa rainboot maana udongo wa sehemu ile haufai kabisa ulikuwa ukiteleza mno hata hivyo kulikuwa na nyakati nyingi za kukimbia hali iliyopelekea wengi wetu kwenda kuhiji Maka bila pasi na gharama yoyote ile.
Kwa kweli ardhi ya kikosi ilikuwa haitamaniki kabisa kuitazama maana kila sehemu ilikuwa imekanyagwakanyagwa utadhani watu walikuwa wakitengeneza udongo wa kufyatulia tofali za matope ama kujengea nyumba za ukuta wa udongo.
Ulipofika mchana mvua ikanyesha tena zaidi ya ile ya usiku hali iliyopelekea kupewa UTAWALA maana hakukuwa na kazi ingeweza kufanyika.
Tulifurahi na tukawa tunaomba iwe inanyesha mara kwa mara ili tusiwe tunafanya kazi kumbe tulikuwa tunajidanganya bila kujua wenyewe wana wimbo wao usemao “Haiwezekani kamanda maji kupanda mlima".
Kauli hiyo ilikuwa ikimaanisha kuwa kisichowezekana jeshini ni maji kupandisha kwenye mlima pekee na kama unakumbuka aliwahi kutuambia Afande Rashidi kuwa jeshini ni sehemu pekee ambayo kipara kinanyolewa hawa mabwana si ajabu wakatuaminisha kuwa inawezekana kabisa kuideki bahari😅.
Mvua hiyo iliyokuwa ikinyesha kwa heshima ilikuwa ikipungua na kukata kabisa ila ilikuwa tukifika KOMBANIA tu mawingu yalikuwa yakigongana na kumwaga cheche hivyo watu wakawa wanawapongeza babu zao kwa kazi wanayofanya.
Ustadhati Rehema alionekana kupata tabu na hali hiyo maana nguo zake zilikuwa zikikusanya tope la kutosha mbaya zaidi kuna kipindi tukiwa kwenye bwalo tulitakiwa kukaa chini hali iliyopelekea kukalia matope yaliyotokana na kukanyaga kwa viatu vyetu.
Asubuhi ya siku iliyofuata kulikucha shwari tukakimbia MABIO na kufanya usafi na kwenda zetu KOMBANIA tukaelekea zetu kwenye FATIKI ila tuliporudi tulijazana dukani kwa ajili ya kununua rainboot.
Siku hii hatukumkuta yule afande mnoko Koplo Jose ila tuliwakuta vijana wao wa JKT.
Wapo waliopata ila sisi wengine hatukufanikiwa maana ziliisha hivyo walichukua hela zetu na kutuambia tufuate baadaye mana waliendaa kufungasha kwa kawaida ilikuwa ni vigumu mno kuondoka dukani hapo bila ya kuacha hela.
Yaani ilikuwa ukienda ukakosa unachohitaji utawaachia hela tu labda uende ukaulizie kitu ambacho hawafungashagi ama kitu cha bei ndogo kama vile pipi ama biskuti hapo utanusurika ila si kwa bidhaa za msimu kama hizo.
Usiku ulipofika tukiwa KOMBANIA kuna dada mmoja alinifuata akiniomba nimsaidie kutoroka kikosini hapo maana alikuwa ameshapachoka.
Alikuwa ni Winifrida ambaye kama unakumbuka ile siku nawasili kikosini tukiwa maingate tunaandikisha PARTICULARS aliletwa dada mmoja na gari akisindikizwa na familia yake.
Kwanza nilimshangaa kwanini kanishirikisha jambo hilo lakini pia nilimuuliza ningewezaje wakati sikuwahi kufanya hivyo lakini niliogopa tusipofanikiwa huenda yakanikuta makubwa.
Aliniambia kuwa kwa anavyoniona ana uhakika kazi hiyo naiweza ila hata kama siwezi basi nimsaidie hata kwa mawazo.
Kwa kweli lilikuwa jambo gumu kwangu hivyo nilijaribu kumshauri asitishe na nilivyoona anang’ang’ania ilibidi nimwambie amtafute mtu mwingine. ,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,
**************Itaendelea……….…………...
MAISHA YA DEPO
SEASON-2
EPISODE 20
Hatukumaliza mazungumzo hayo vizuri kwani afande Ashiru alikuwepo hapo kwa ajili ya lokoo hivyo nilishukuru ujio wake kwani uliniepusha na balaa hilo.
Tuliruhusiwa na kwenda zetu kulala ila nilipitia dukani kuulizia buti zangu nikakuta wamefunga hivyo nikanyoosha zangu HANGANI ambako nilichelewa kupata usingizi nikiliwaza swala hilo la mwanadada Wini.
Asubuhi kulikucha vizuri ingawaje ni kwa fujo na makelele kutoka kwa wazee wa mauzauza na baaada ya usafi tulienda zetu KOMBANIA.
Tukiwa tunasubiri muda wa FATIKI ufike ilisikika sauti moja ikisema “Nakuja sasa, nakuja” watu wote tuliangua vicheko.
Alikuwa ni mwamba kabisa wa kuitwa Mtalibani tulicheka kwakuwa tulijua shoo yake, mzee huyo hajawahi kupoa akiwa kazini.
Kama kawaida aliagiza ndoo zake tano za vifusi na kama ilivyo siku zote alilisimamia zoezi hilo yeye mwenyewe.
Kazi hiyo haikuwa ya kitoto kwani vifusi vyote tulivyoviweka awali vilikwenda na maji hivyo kama vijana wa China Civil (CCECC) tuliingia mzigoni chini ya mkandarasi Mzee Mtalibani.
Mzee huyo alikuwa akisisitiza vindoo vijazwe na yule aliyeleta nusu alimrudisha ama alimwaga bila kumhesabia kwa wale wenye bahati aliwaambia waunganishe na aandikwe mmoja.
Alipoona tunalegalega alitutia biti na kutuambia kuwa watakaokwenda kula mchana ni wale watakao kuwa wamelifikia lengo la kupeleka vindoo vitano.
Ilikuwa ni kivumbi na jasho siku hiyo niliwaona wengi wakihanya mfano mzuri ulikuwa ni Linda, Wini pamoja na Ustadhati Rehema niliwahurumia mno.😰
Ustadhati yeye ule upekee wake ulimsaidia na baadaye Mtalibani alimpa kitengo akituelekeza ni wapi tumimine vifusi hivyo.
Chakumshukuru muumba mbingu na ardhi ni kuwa leo hii katika wale makarani mmoja wao alikuwa ni mwanangu Amosi tuliyesoma naye ila yeye alikipiga CBG hivyo tukawa tunafanya uhuni mmoja hivi pamoja na Linda.
Kifupi ni kuwa nilipeleka ndoo tatu pekee ila alinijazia zote tano isipokuwa alikuwa akitumia akili moja hivi.
Amos hakutujazia hizo ndoo tano ilihali wengine wana mbili isipokuwa pale watu haswa wale kutoka kanda ya ziwa (sijawataja wasukuma😜) walipokuwa na ndoo mbilimbili mimi na Linda tulipeleka mojamoja ila yeye alitiki mara mbili kwa kila mmoja.
Safari nyingine tulimsaidia Wini ambaye aliandika jina kwa karani mwingine hivyo ikawa vigumu kucheza mchezo huo, ilikuwa nikibeba moja wao wanabeba ujazo wanaowezana nao wa nusunusu halafu tukikaribia kwa Mtalibani wanachangia anatoka mmoja kama kibati vile.
Awali nilikuwa nikimkwepa Wini ila aliponiona alijisogeza kwangu ikanishindwa kumkwepa tena hata hivyo nilimhurumia kipindi akihangaika safari yake ya kwanza.
Mchana wake tukiwa KOMBANIA jamaa niliyempa simu yangu akanichajie alinirejeshea baada ya siku mbili kupita akanipanga nimuongeze jero maana huko wanakochajisha bei imepanda eti kwasababu ya uwepo wetu.
Nilimkubalia ila nilimwambia kuwa ningempatia jioni maana kwa muda huo sikutembea na hela hivyo nikachukua namba yake na kumuahidi kumtafuta baadaye.
Mtalibani alikuja tena kwa awamu nyingine ila wakati huu lengo lilikuwa ni ndoo nne tulizama mzigoni na kulisongesha na isivyo bahati awamu hii Amosi hakuwepo kwenye ukarani.
Awamu hii Mtalibani alibadilisha wasaidizi wake wote isipokuwa Rehema ambaye wakati huu alionesha mabadiliko kwa kutokuja na juba.
Ustadhati alivaa suruali ya track (Mashaallah kwa mbali majaliwa tuliweza kuyaona😋) na tisheti kichwani akava kikofia chake tushindwe kuona kichwa chake nafikiri mataabiko ya mvua na matope ndiyo yalimpelekea kufanya hivyo.
Mabadiliko hayo hayakuharibu mifumo kwani mwanangu Baraka alipewa kitengo hicho hivyo mambo yaliendelea kuwa kitonga kama kawaida maana katika ndoo kumi na mbili zilizohitajika kutoka kwangu, Linda na Wini tulienda safari tatu ambazo ni sawa na ndoo sita.
Katika ndoo sita hizo tatu zilikuwa ni za kwangu na tatu nyingine ni za wale mabinti ambao waliunganisha nusunusu zao na kupata tatu kamili.
Uhuni mwingine uliokuwa ukiendelea ni kuwa watu walikuwa wanatikiwa halafu wanazuga wanamwaga kisha wanarudi na udongo wao ambao wanazugazuga nao katikati hapo (hawafiki kule unakochimbwa) na baadaye wanapeleka tena.
Kwa aliyekuwa masta wa hili ilimtosha safari moja tu kuzigeuza kuwa nne kikubwa SIFA WEPESI.
Kazi hiyo iliyokuwa na pilikapilika za hapa na pale ilifanyika mpaka ulipofika muda wa marejeo nasi tukarudi zetu MAHANGANI kuendelea na ratiba nyingine.
Kabla ya kufanya chochote nilipitia dukani kuulizia buti zangu licha ya kuwa tope lilikuwepo baadhi ya maeneo korofi ambalo sio swala swala ni kwamba nilikwishawapa maokoto ya jasho langu ambalo huwa sikubali liende bure.
Nilipofika dukani nilimkuta Koplo na aliponiona hali ikawa vilevile kwa kuwa aligundua najua sasa kukunja ngumi basi tabu ikawa palepale ila mwisho wa hadithi nilipewa buti zangu japo nilizipata kwa MASIMANGO😰 ya kiwango cha standard gauge.
Ilibidi nisubiri mpaka muda wa kula ndiyo aliniruhusu kuaondoka ingawaje alinipooza kwa juisi na biskuti kwakweli alikuwa akinichukulia poa sana😪.
Asubuhi yake ilikuwa ni siku ya Jumatatu tuliamka na kuendelea na ratiba kama zilivyokuwa zikitaka, tulienda kufanya usafi karibu na yalipo maskani ya mkuu wa kikosi ambapo mpaka kufikia wakati huo hatukuwahi kumuona.
Mara nyingi tulikuwa tukimuona makamu wake Matroni Neema aliyekuwepo kikosini wakati wote hivyo kwa upande wetu yeye ndiye tuliyemtambua kama mkuu wa kikosi.
Tukiwa tunarudi kufanya usafi njiani nilimuona Matroni Anna aliyeandikisha PARTICULARS zangu ile siku nafika ikabidi nisimame kusalimiana naye.
Nilisalimiana naye kupiga stori nikijifanya namjua na niliwahi kuonana naye mahali ila lengo halikuwa hilo kikubwa nilimuuliza kutaka kujua alichokua akikimaanisha siku ile kule main gate.
Kifupi nilitaka kujua maana ya msamiati Katerero licha ya kwamba nilijua ni jina la sehemu kule kwa kina Nshomile ila ilionekana kuwa na maana yao ya tofauti iliyowafanya wacheke.
Alitabasamu😊 na kuniambia “Aah we MZALENDO hembu niache nitafute baadaye mkiruhusiwa kwenda kulala ntakwambia”.
Nikamuuliza “Ntakuona wapi sasa hiyo saa tano wakati utakuwa ushalala zako HANGANI” akanijibu “Nitakuwa bwaloni naangalia zangu tv nalalaga saa saba eti”.
Kwa majibu hayo tu ilinibidi nifungue vitabu vyangu na maandiko mbalimbali yanayoelezea maswala ya uwekezaji katika mahaba nilipoyapitia nikagundua uwekezaji umelipa nikajisemea kumoyo “mtoto kanasa”💪🏿.
Nilijua itakuwa ni vigumu kumpata muda huo nilitaka nichukue namba yake ila simu niliiacha HANGANI kibaya zaidi nayeye yake hakuwa nayo.
Mdogomdogo niliondoka kuelekea HANGANI kwani tayari wenzangu walikwisha niacha mbali.
Nilipita njia iliyokuwa inatokea UWANJA WA DAMU ambao ulikuwa karibu na jengo la kuhifadhia silaha lililofahamika kama AMALA.
Niliwakuta askari wa jeshi la wananchi maarufu kama BAKABAKA wakiwa kwenye PAREDI la makabidhino ya silaha ambayo kwa siku ya jumatatu ilifahamika kama MASTER PARADE sasa bwana nikataka kujichanganya kitu kimoja. ,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,
*************Itaendelea……………………....