Sehemu ya Tatu
Baada ya kupata majibu ya kukatisha tamaa kutoka kwa wazazi wa Upendo, niliamua kutoendelea kuwapa taarifa kuhusu maendeleo ya Upendo. Nilibaki kuwa faraja kubwa kwake pamoja na mtoto wetu. Tuliishi kwa furaha na upendo mkubwa sana. Wakati mwingine tulikuwa tukitoa machozi tukikumbuka nyakati ngumu zilizopita.
Katika mwaka wangu wa mwisho wa masomo, nilimuomba Upendo afunge safari kuelekea nyumbani kwetu ili nipate nafasi ya kupambana na kumaliza mwaka wa mwisho salama maana ulikuwa na programs nyingi sana. Mpenzi wangu Upendo alikubali na wazazi wangu walikuwa na shauku kubwa ya kumuona. Wakati akiwa safarini, niliwasiliana na rafiki yangu ambae alikuwa akiishi Dodoma akifanya kazi. Rafiki yangu huyu tulisoma pamoja na kiukweli alikuwa kama ndugu. Mpenda dini sana. Katika kipindi chote ambacho nilimfahamu hakuwahi kuwa kwenye mahusiano na binti yoyote. Nilimueleza kuhusu mpenzi wangu kurudi nyumbani.
Rafiki yangu aliniomba Upendo wangu apite nyumbani kwake amsalimie kabla ya kuelekea nyumbani kwa wazazi wangu, Mwanza. Ilinilazimu nimtaarifu mama yangu kwamba Upendo angechelewa maana anapita Dodoma kwa rafiki yangu Charles kumsalimia. Mama alishtuka kisha akaniuliza kama Charles Ana nyumba nyingine ya Upendo kufikia. Nilimuuliza Charles akanijibu kwamba nisiwe na shaka nyumba ipo na mimi sikuwa na wasiwasi juu ya Charles. Baada ya majadiliano hayo, nilimpigia simu Upendo akiwa safarini na kumuelekeza ateremke Dodoma kumsalimia shemeji yake.
Alifika salama na kupokelewa na Charles. Baada ya siku tatu, nilimpgia simu Upendo nikimuelekeza aelekee mwanza. Baadae kidogo rafiki yangu Charles akanipigia simu akinisihi Upendo asielekee Mwanza kwamba angekwenda kuwasumbua wazazi tu na hali ngumu iliyopo nyumbani. Tuliongea mengi na kisha nikamuuliza Upendo kama alikuwa huru kuendelea kukaa pale. Alinijibu kwamba hapakuwa na shida.
Ajabu ni kwamba, siku ile usiku nilikuwa naota Upendo akiwa anafanya mapenzi na rafiki yangu. Nilifadhaika mno. Asubuhi nikampigia simu kumuuliza kama alikuwa salama, akanijibu kwamba hapakuwepo na shida. Ndoto ile iliendelea kwa siku tatu mfululizo. Niliumia sana. Nikawa mtu mwenye mawazo sana chuoni. Nilijipa moyo na kuendelea na masomo. Baada ya kumaliza chuo, nilikuwa na barua mkononi nikihitajika kwenda kufanya kazi singida katika kampuni fulani. Niliomba udhuru wa siku kadhaa kwenda kumufuata mke wangu. Nilisafiri hadi Dodoma na kufika kwa rafiki yangu. Upendo alifurahi sana kuniona laikini alikuwa mwenye mashaka. Rafiki yangu pia hakuwa na ule uchangamfu nilio uzoea. Baada ya mazungumzo mafupi, nilikaa na Upendo kwa mazungumzo. Nikamueleza kuhusu ile ndoto. Nikamkumbusha mambo mengi tuliopitia katika maisha. Kisha nikamuomba anieleze ukweli na akanithibitishia kwamba, rafiki yangu alikuwa akimuingilia kwa nguvu usiku wa manane na kweli mlango ule haukuwa unafungwa.
Sikumhoji Upendo mambo mengi. Nikajua mimi ndie mwenye makosa. Nikamuomba tuondoke pamoja na mtoto wetu. Rafiki yangu Charles, aliomba kuondoka nasi pia ili akaone tunapoishi. Tulisafiri na kufika Singida. Nikaoneshwa nyumba ya kuishi. Ilikuwa na kila kitu. Muda wote huo nilikuwa na mawazo sana. Sikuwa sawa. Niliwaza ni kwanini Upendo afanye vile. Niliingia chumbani kwenye ile nyumba. Nikatoka nikaingia jikoni. Nikaona kisu kikiwa kwenye beseni. Kipya kabisa. Akili ilinitima kwamba nilipaswa kumumaliza Charles. Nilikibeba kisu nikaelekea sebuleni alipokuwa amekaa Upendo na Charles. Nilitetemeka nikaangusha kile kisu.
Wakati huo, nilikuwa sijamueleza Charles chochote kuhusu alichokifanya kwa Upendo. Baada ya tukio lile, Upendo alilia sana. Akainama akanishika miguu na kuniomba msamaha. Niliongea na Charles kwa uchungu sana na kuamua kusitisha urafiki wetu tangu siku ile. Charles aliondoka kurudi Dodoma.
Itaendelea,,,