kwa nn hawa wafaransa wanapenda kutuchezea ?
hivi lini haya mataifa makubwa yataweka heshima kwa waafrika?
Ufaransa yamgeuka Bacar
2008-03-29 09:13:54
Na SAINT DENIS DE LA REUNION, France
Baada ya kutimuliwa na vikosi vya Umoja wa Afrika (AU) kisiwani Anjouan Jumanne iliyopita, kiongozi aliyejitangazia Urais kimabavu, Kanali Mohamed Bacar huenda akatimuliwa katika kisiwa cha Reunion kinachomilikiwa na Ufaransa ambako alipewa hifadhi ya muda, limeandika Shirika la Habari la Uingereza Reuters jana.
Baadhi ya maofisa wa Serikali ya Ufaransa walithibitisha jana kwamba serikali hiyo ilikuwa ikifikiria kumfukuza nchini mwake kiongozi huyo ambaye anasakwa kwa udi na uvumba na serikali ya Comoro kujibu tuhuma za uhaini na uasi.
Comoro juzi iliiomba Ufaransa ambayo ndiyo inatuhumiwa kumkimbizia Kanali Bacar kwenye kisiwa cha Reunion akitokea Mayotte imrejeshe ili aweze kufikishwa mbele ya sheria.
Mwendesha Mashtaka Mkuu kisiwani Reunion, Francois Muguet jana alisema kwamba bado hajapata taarifa zozote za kibali cha kimataifa kinachoruhusu kumtia mbaroni Kanali Bacar kutoka serikali ya Comoro.
Muguet alisema kwamba Kanali Bacar anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo kisiwani Reunion kwa tuhuma za kuingia visivyo halali katika ardhi ya Ufaransa akiwa na silaha.
Baadhi ya vyanzo vya habari vilisema kwamba kuna uwezekano mkubwa mahakama ikampa adhabu ya kumfukuza kisiwani humo kutokana na tuhuma hizo.
Hata hivyo, mwendesha mashtaka huyo alisema kwamba hukumu ya kesi yake inaweza kucheleshwa kwa siku 10 hadi 15 endapo Kanali Bacar ataiomba mahakama impe muda wa kuandaa wanasheria watakaomtetea.
Mwanasheria Muguet alisema kiutaratibu hawezi kusaini amri yoyote wakati bado hapajatolewa maamuzi ya kumpa hifadhi za kisiasa au kumfukuza Reunion.
Kanali Bacar akiwa ameambatana na askari wake 22 alikimbilia katika kisiwa cha Ufaransa cha Mayotte kabla ya kutoroshwa na ndege ya kijeshi ya Ufaransa hadi Reunion.
Kufuatia hifadhi aliyoipata kwa muda kisiwani Mayotte, wananchi wa Comoro jana waliandamana hadi katika Ubalozi wa Ufaransa mjini Moroni wakiishinikiza nchi hiyo kumrejesha Kanali Bacar.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Yves Jego alisema jana kwamba japokuwa nchi yake inafikiria ombi la kumpa Kanali Bacar hifadhi, upo pia uwezekano wa kumfukuza.
``Kimsingi (yeye na wenzake) wanastahili kurejeshwa Comoro,`` Waziri Jego aliwaambia waandishi wa habari.
SOURCE: Nipashe