SURA AL JINN.
1. Kwa jina la Mwenyezi Mungu,
Mwingi wa rehema, Mwingi wa ukarimu.
2. Sema: Imefunuliwa kwangu ya
kuwa kundi la majinni walisikia wakasema: Hakika Tumesikia Qur'an ya ajabu,
3. Inaongoza kwenye uongofu, kwa
hiyo tumeiamini, wala hatutamshirikisha
yeyote na Mola wetu:
4. Na kwa hakika utukufu wa Mola
wetu umeinuka, Hakuchukua mke wala mwana:
5. Na kwa hakika mpumbavu miongoni mwetu alikuwa akisema maneno ya
upuuzi juu ya Mwenyezi Mungu;
6. Nasi tulikuwa tukidhani ya kuwa
watu na majinni hawatasema uwongo juu ya Mwenyezi Mungu
7. Na hakika kulikuwa na watu
miongoni mwa wanadamu wakijikinga kwa watu miongoni mwa majinni, hivyo wakawazidishia kiburi:
8. Na kwa hakika wao walidhani
kama mlivyodhani ninyi ya kuwa Mwenyezi Mungu Hatamtuma ye yote.
9. Nasi tuligusa mbingu tukaiona
imejaa walinzi wenye nguvu na nyota zing'aazo.
10. Na hakika tulikuwa tukikaa
humo katika baadhi ya makao ili kusikiliza; lakini atakayejitahidi kusikiliza sasa atakuta kimondo kikimvizia.
11. Nasi hatujui kama shari inatakiwa kwa wale wanaokaa ardhini au
Mola wao Anawatakia mwongozo.
12. Na hakika katika sisi wamo
wema na wengine katika sisi ni kinyume cha hayo: tulikuwa njia mbalimbali:
13. Nasi tulijua ya kuwa hatuwezi
kumdhoofisha Mwenyezi Mungu katika nchi wala hatuwezi kumponyoka kwa kukimbia:
14. Nasi tulipousikia mwongozo,
tukauamini, basi anayemwamini Mola wake hataogopa hasara wala ubaya:
15. Nasi wamo miongoni mwetu
waliosilimu na wamo miongoni mwetu wanaokengeuka; lakini aliyesilimu basi hao ndio hutafuta wema:
16. Waama wanaokengeuka basi
wamekuwa kuni za Jahanamu.
17. Na kama wangalishika kwa imara njia (iliyonyoka) Tungaliwanywesha
maji kwa wingi,
18. Ili Tuwajaribu kwa hayo. Na
anayepuuza kumkumbuka Mola wake Atamsukuma kwenye adhabu ngumu:
19. Na kwa hakika misikiti yote ni
ya Mwenyezi Mungu, basi msimwombe mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu.
20. Na hakika Mtumishi wa Mwenyezi Mungu aliposimama kumwomba
walikuwa karibu kumwangukia (wamwangamize).
21. Sema: Ninamwomba Mola
wangu tu wala simshirikishi na ye yote.
22. Sema: Kwa hakika mimi similiki
kwa ajili yenu dhara wala heri.
23. Sema: Bila shaka hapana ye yote
awezaye kunilinda na Mwenyezi Mungu, wala sitapata makao ya salama ila Kwake Yeye tu:
24. Ila kwa kufikisha (ujumbe)
utokao kwa Mwenyezi Mungu na risala Zake; na atakayemwasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, basi bila shaka atapata moto wa Jahanamu, watakaa humo muda mrefu.
25. Hata watakapoyaona wanayoahidiwa, ndipo watajua ni nani msaidizi dhaifu na mwenye idadi ndogo
26. Sema: Sijui kama yako karibu
mliyoahidiwa au Mola wangu Atayawekea muda mrefu:
27. Yu Mjuzi wa yasiyoonekana, na
Hampi ye yote uwezo wa kiutawala juu ya milki Yake ya mambo yasiyoonekana.
28. Isipokuwa yule Anayemchagua
kuwa Mtume Wake. Na mbele yake na nyuma yake hutembea malaika kama walinzi.
29. Ili Ajulishe ya kuwa wamekwisha fikisha risala za Mola wao; na
Ameyazunguka waliyo nayo na Amehesabu idadi ya kila kitu