Inaendelea....
MAKALA: SEHEMU YA TATU
Katika makala yetu ya sehemu ya pili tumeangalia mambo mbalimbali kama awamu za malipo ya kodi, viwango vya kodi kwa walipa wa aina tatu tofauti, ukokotoaji kwa walipa kodi kwa wanaoweka kumbukumbu lakini mauzo yao ni chini ya milioni 20 kwa mwaka na mengineyo mengi mazuri ya kutupa elimu zaidi.
Katika makala yetu hii sehemu ya tatu tuangalie masuala yafuatayo:
1. JE UTAFANYAJE KAMA UMEJIKADIRIA/UMEKADIRIWA MAKADIRIO MAKUBWA AU KIDOGO?
Unapoanza au unapoendelea kufanya biashara huwa na matumaini chanya ya biashara kuwa nzuri kwa mwaka husika. Hivyo hata makadirio unayokuwa umekadiriwa unakuwa na uhakika wa kuyalipa kwa awamu zote nne bila tatizo. Lakini kuna nyakati biashara inaweza kustawi sana au kusinyaa sana hadi inafikia hata gharama mbalimbali za kujiendesha biashara yenyewe kushindwa kulipwa au biashara imenawiri. Je utafanya nini kama
a) Umejikadiria kodi kidogo?
Iwapo utagundua kabla ya mwaka wa mapato kuisha, kuwa makadirio yako ya kodi ya awali ni pungufu ukilinganisha na hali halisi unaruhusiwa kisheria kufanya marekebisho yanayostahili ili kuepuka tatizo la kutozwa riba baadaye. riba hutokwa kutokana na viwango vilivyowekwa na Beki Kuu
b) Umejikadiria kodi kubwa?
Ikiwa ukadiriaji wa kodi unayostahili kulipwa ni kubwa kuliko uwezo wako, utaandika barua kwa kamishna wa kodi kutaarifu suala hili na sababu za msingi na kujaza fomu rejea ya makadirio ya kodi kwa kiwango ambacho unaona utaweza kulipa.
c) Malalamiko juu ya makadirio ya kodi
Mojawapo za haki ya Mlipakodi zilizoainishwa katika Mkataba wa Mlipa kodi (Taxpayer's Charter)
ni kupinga makadirio ya kodi iwapo anaamini sio sahihi. Fuata taratibu hizi kupinga makadirio ya Kodi (Rejea Sheria ya Usimamizi wa Kodi mwaka 2015):
1. Andika barua kwa kamishna ikielezea sababu za msingi zenye kuonyesha makosa yaliyofanywa ktk ukadiriaji
2. Barua ya kuoina makadirio ni lazima iwasilishwe ndani ya siku 30 toka tarehe ya makadirio ya kodi husika
3. Ili pingamizi la kodi likubalike mlipa kodi anatakiwa alipe 1/3 ya kodi yote kubwa uliyokadiriwa ndani ya siku 30 toka tarehe ya makadirio
Kamishna wa kodi atakutaarifu kupokea malalmiko yako na iwapo baada ya hukumu kutoka kama hujaridhika basi waweza kukata rufaa kwenye Baraza la Rufaa za Kodi au Mahakama Kuu ya Rufaa za Kodi kwa maamuzi ya mwisho
2. SHERIA YA KODI YA ONGEZEKO LA THAMANI (VAT 2014)
VAT ni kodi ya Mlaji inayotozwa na mfanyabiashara aliyesajiliwa kwa miujibu wa sheria kwenye mauzo ya bidhaa au huduma zinazostahili kutozwa VAT. Bidhaa zinazotozwa ni zile zinazozalishwa hapa nchini Tanzania Bara na kutoka nje ya Tanzania
a) Ngazi za utozwaji VAT
Utozwaji hufanywa ktk ngazi ya uzalishaji, uingizaji bidhaa au huduma kutoka nje, uuzaji wa jumla na reja reja mpaka bidhaa inapomfikia mlaji wa mwisho. Mlipaji wa VAT ni mlaji wa mwisho
b) Usajili wa VAT
Sifa hizi zinahusika
1. Awe mfanyabiashara alie na TIN
2. Mauzo yake yawe kuanzia au anatarajia mauzo kuwa zaidi ya mil 100 kwa mwaka
3. Biashara za huduma za kitaaluma kama vile wanasheria, wahandisi, na wahasibu walazaimika kusajili VAT pasipo kuangalia kiwango maalumu cha mauzo kwa mwaka
c) Ulipaji VAT
Ulipaji VAT hufanyika ndani ya siku 20 baada ya mwezi wa malipo husika ie kila tarehe 20 ya mwezi utajaza ritani na kuwasilisha kwa njia ya mtandao
d) Bidhaa zilizosamehewa VAT
kuna bidhaa na huduma zimesamehewa VAT kutokana na sababu mbalimbali za kijamii na kiuchimi zenye tija kwa Taifa.Bidhaa hizo ni kama vile vyakula ambavyo havijasindikwa mfano: mahindi, unga wa mahindi, ngani na unga wake, matunda yasiyosindikwa nk
Bidhaa nyinginezo ni pamoja na madawa ya binadamu yaliyotajwa na Wizara ya Afya, huduma za tiba kama meno na magonjwa mbalimbali, pia magazeti, majarida nk
Vilevi;e usafirishaji wa abiria kwa basi, ndege, treni isipokuwa usafiri wa Taxi, gari za kukodi, boti na ndege za kukodi, huduma za elimu, uuzaji au upangishaji nyumba za kuishi au ardhi nk
3.SHERIA YA USHURU WA STEMPU
Hutumika kuhalalisha miamala ikiwemo hati za kisheria au mikataba mbalimbali. Gharama yake ni 1% ya thamani ya mauzo au sihia kwa maswala ya hati ya kisheria na mikataba hutegemea na viwango maalum vilivyoainishwa kti sheria ya mwaka 1972 na kurejewa mwaka 2006
Muda wa kulipa ushuru wa stempu ni ndani ya siku 30 baada ya kusaini hati au mkataba.
4. KODI YA ZUIO
Utangulizi:
Kodi ya zuio ni kiasi cha kodi kinachozuiwa na mtu anapomlipa mtu mwingine kutokana na bidhaa zilizosambazwa au huduma iliyotolewa na mlipwaji. Mtu anayepokea au anayestahili kupokea malipo ambayo kwayo kodi ya mapato inatakiwa kuzuiwa ni mkatwaji wa kodi ilhali mtu anayepaswa kuzuia kodi ya mapato kutoka katika malipo yaliyofanyika kwa mkatwaji anajulikana kama Wakala wa kodi ya zuio.
Malipo yanayostahili kukatwa kodi ya zuio
Kodi ya zuio inatozwa katika malipo husika ikiwa ni pamoja na malipo yanayopaswa kujumuishwa katika kukokotoa mapato ya mwajiriwa yanayostahili kukatwa kutoka kwa mwajiriwa katika ajira, malipo ya mapato ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na magawio, riba, malipo ya maliasili, pango au mrabaha, malipo ya huduma na malipo ya mikataba na malipo ya bidhaa zilizosambazwa serikalini na kwenye taasisi zake.
Taarifa na Muda wa Kulipa Kodi Iliyozuiwa
- Kila wakala wa kodi ya zuio atalipa kwa Kamishna kodi ya zuio aliyozuia ndani ya siku 7 baada ya kila mwisho wa mwezi wa kalenda.
- Kila wakala wa kodi ya zuio atapeleka kwa Kamishna ndani ya siku 30 baada ya kipindi cha kila miezi sita ya kalenda taarifa katika fomu maalum iliyoandaliwa inayobainisha malipo yaliyofanywa na wakala katika kipindi husika cha zuio la kodi, jina na anwani ya mzuiwa, kodi ya mapato iliyozuiwa kutoka katika kila malipo yaliyozuiwa; na taarifa nyingine yoyote ambayo Kamishna ataelekeza.
Hati ya Kodi ya Zuio
Wakala wa kodi ya zuio ataandaa na kumtunuku mzuiwa hati ya kodi ya zuio ikionesha kiasi cha malipo alicholipwa mzuiwa na kodi ya mapato iliyozuiwa kutoka katika malipo hayo. Hati ya zuio itahusisha mwezi wa kalenda na itatolewa ndani ya siku 30 baada ya mwisho wa mwezi. Hata hivyo, kwa upande wa kodi inayozuiwa kutoka katika kodi ya ajira hati itahusisha sehemu ya mwaka wa kalenda katika kipindi ambacho mwajiriwa atakuwa amejiriwa na atahudumiwa ifikapo tarehe 30 ya Januari baada ya mwisho wa mwaka au, pale ambapo ajira yake imesitishwa na wakala wa zuio katika mwaka si zaidi ya siku 30 kutoka tarehe ambayo ajira ilisitishwa.
Aina za Kodi za Zuio
Sheria imegawanya kodi ya zuio katika aina kuu mbili, ambazo ni:-
- Kodi za Zuio za mwisho
- Kodi za Zuio zisizo za Mwisho
Kodi za Zuio za Mwisho ni kodi ambazo mzuiwa hawezi kudai punguzo lolote la kodi wakati wa kukokotoa kodi ya mapato inayolipwa kwa mwaka wa mapato.
Kodi za Zuio zisizo za Mwisho: ni kodi ambazo mzuiwa anastahili punguzo la kodi kiasi sawa na kodi inayochukuliwa kuwa imelipwa kwa mwaka wa mapato ambamo kiasi hicho kimekokotolewa.
MWISHO