Historia ya Mikwaruzano ndani ya Kambi za CCM
Muktasari Chama kurejeshwa mikononi mwa CCM Asilia :
“Hakuna sababu ya kutoa shutuma hizo kwa sababu walioharibu ni CCM na anayetengeneza ni CCM,” alisema Kinana jana alipokuwa na Rais Magufuli mjini Muheza wakiwa njiani kwenda Tanga na kisha kuwahoji wananchi juu ya kile wanachokitaka nao kujibu ‘ndiyoo’ kisha akasema kinachotakiwa ni maendeleo na si kitu kingine
Kurejea kwa kada halisi wa chama
CCM ni chama cha kikada - hata kama sasa baadhi ya matendo na maneno ya wafuasi na viongozi wake hayatoi picha hiyo. Katika chapisho lake mashuhuri la What is to Done lililochapwa mwaka 1902, Vladmir Lenin - Baba wa Mapinduzi ya Urusi ya mwaka 1917, alieleza kuhusu umuhimu wa kuwa na chama cha kikada - cha kimapinduzi, kitakachokuwa na uwezo wa kulinda mapinduzi dhidi ya adui zake.
Mwanasiasa V.I Lenin alieleza kuhusu umuhimu wa kutengeneza wanachama maalumu - kadrovyy sostav (makada) - akitohoa kutoka neno la lugha ya Kifaransa Cadre, waliopikwa vyema kiitikadi na kijeshi. Kazi ya makada ilikuwa ni kuwa na uwezo wa kufanya siasa na wakati huohuo kuwa tayari kukilinda endapo kutatokea changamoto zinazohitaji mbinu za kijeshi.
Makada ni watu waliokuwa wakiaminika kwamba hata kama watabaki watano tu, wanaweza kukifufua chama na kukirejesha kilipokuwa.
Hiyo ndiyo sababu ya CCM - iliyoundwa kimapinduzi, kutengeneza wanachama waliopitia pia mafunzo ya kijeshi kama Jakaya Kikwete, Andrew Shija, Moses Nnauye, Yusuph Makamba, Edward Lowassa, Kinana na wengine. Katika muktadha huu, ni vigumu kuona ni kwa vipi Kinana angekataa kuitikia wito wa Mwenyekiti wake, Rais Samia, wa kutaka kukirejesha chama katika njia yake.
Novemba 2012, Kinana aliitwa tena na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wakati huo, Jakaya Kikwete, kuwa Katibu Mkuu katika wakati ambao chama tawala kilikuwa kinapitia mitihani mikali ndani na nje ya chama. Ndani ya chama, wafuasi wa Lowassa walianza kuonesha waziwazi kampeni za kutaka awe mrithi wa Kikwete kwenye urais na uenyekiti, wakati nje Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kilikuwa kimetoka kupata mafanikio makubwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Kinana alishika ukatibu mkuu baada ya jitihada za 'kukinyoosha' chama chini ya Katibu Mkuu, Wilson Mukama kuanzia April 2011 kutozaa matunda.
Ni Kinana aliyesifiwa kwa kufanikiwa kubadili upepo na kurejesha umaarufu wa CCM kiasi cha kupata ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 - ambapo John Magufuli alimshinda Lowassa aliyekuwa amehamia Chadema baada ya kuihama CCM. Lowassa sasa amerejea chama tawala.
Kinana, mbunge wa zamani wa Arusha Mjini ni kiongozi anayefahamika utendaji wake wa kazi na anayekifahamu chama vilivyo. Alipokuwa Katibu Mkuu wa CCM kati ya Novemba 2012 hadi Mei 2018 alipoomba kupumzika, ilikuwa ikifahamika kwamba hakuwa akichukua mshahara kutoka CCM kama ilivyokuwa kwa watumishi wengine wa chama. Ni kama vile alijitolea kufanya kazi za chama.
Askari, Mwanadiplomasia, MwanaBunge, Mwanasiasa na Mfanyabiashara
Kinana ni mtu mwenye kofia nyingi. Ni askari aliyepitia mafunzo ya kijeshi kufikia cheo cha Kanali. Ni mwanadiplomasia aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi.
Ni MwanaBunge aliyewahi kuwa mbunge na baadaye Spika wa Bunge la kwanza la Afrika Mashariki mwak 2001.
Ni mwanasiasa aliyewahi kushika vyeo vya kisiasa kama mbunge, waziri na Katibu Mkuu wa chama. Mtu wa mipango na mtekelezaji wa mikati, kwani aliongoza kampeni nne za urais kwa mafanikio; mwaka 1995 na 2000 akiwa Meneja wa Kampeni mgombea wa CCM Benjamin Mkapa, pia meneja wa kampeni wa Jakaya Kikwete mwaka 2010 kabla ya kusimamamia kampeni za Magufuli 2015 akiwa Katibu Mkuu.
Kadhalika ni mfanyabiashara aliyewahi kuwa kwenye bodi kadhaa za mashirika ya umma na sekta binafsi. Sifa yake kubwa ni kwamba anaweza kuvaa kofia yoyote kati ya hizo pale anapotaka au inapobidi.
Kofia zake hizo zimemfanya kuwa mmoja wa viongozi wenye wigo mpana wa marafiki ndani na nje ya nchi - kuanzia marais, wafanyabiashara maarufu, wanasiasa wa vyama tawala na upinzani na watu wa kawaida ambao wamekuwa muhimu kwake kwa kumwongezea maarifa na taarifa katika majukumu yake tofauti.
CCM Mpya, CCM ya zamani
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, niliandika uchambuzi kupitia BBC Swahili
Mwisho wa zama za 'kizazi cha zamani CCM' - BBC News Swahili, ambao niliueleza uchaguzi huo kama mwisho wa zama za kizazi cha akina Kinana ndani ya CCM.
Utawala wa Rais Magufuli ulikuwa na uhusiano usio na afya na waliokuwa wakijulikana kama wenye CCM - akina Kinana, na kuna wakati Katibu Mkuu huyo wa zamani na Yusuph Makamba walifikishwa katika Kamati ya Maadili ya chama kukiwa na tishio la kuwafukuza uanachama.
Kinana alipewa karipio na kuwekwa chini ya uangalizi kwa miezi 18. Makamba alisamehewa lakini Waziri wa Mambo ya nje wa zamani Benard Membe alifukuzwa uanachama. Baadaye Kinana na Membe walisamehewa.
Kurejea kwa Kinana kuna maana zaidi ya moja ndani ya CCM. Kwanza ni kurejea kwa mtu anayeweza kukirudisha chama katika misingi yake na kukizimua ikibidi - kazi aliyofunzwa kama kada, kuandaa kizazi kipya cha viongozi wajao wa chama hicho na kukitayarisha chama kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Mwaka 2020, CCM ilitumia zaidi nguvu za dola kushinda uchaguzi kuliko ushawishi kwa wapiga kura na inaonekana Rais Samia hataki kujirudia kwa siasa za namna hiyo.
Kulikuwepo tuhuma nyingi za viongozi wa vyama vya upinzani dhidi ya CCM kunufaika na nguvu za dola. Hata hivyo, viongozi wa CCM mara kadhaa walikanusha tuhuma hizo na kuwataka wanaodai kuonewa kufungua kesi mahakamani.
Uzoefu wa Kinana ni mtaji mkubwa kwa CCM. Katika historia ya vyama vingi nchini Tanzania; kuna chaguzi mbili zinazotajwa kuwa ngumu zaidi kwa CCM - ule wa mwaka 1995 dhidi ya NCCR Mageuzi ya Augustine Mrema na wa mwaka 2015.
Mtindo wa Kinana wa kufanya kazi ni CCM kutoionea haya serikali na kuwa msemaji wa kero za wananchi. Muda si mrefu, tutaanza kuona viongozi wa CCM wakiwa wasemaji wa kero za wananchi pengine kuliko hata vyama vya upinzani.
Pengine huu ni wakat iwa vyama vya upinzani kukaa chini na kuangalia kama mipango yao inaendana na mabadiliko haya ya 'upepo' ndani ya chama tawala.
Kinana alizaliwa Arusha Mei mwaka 1951. Alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mnamo mwaka 1972 na kulitumikia hadi mwaka 1992 alipostaafu.
Ni msomi wa shahada ya kwanza katika Sayansi ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Ljubljana katika iliyokuwa Yugoslavia na Shahada ya Uzamili katika Uongozi na Utawala aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani.
Katibu Mkuu huyu wa zamani wa CCM ni mtu asiyependa kuanika maisha yake binafsi na familia yake hadharani lakini inajulikana kuwa ana mke, Rahma, na watoto.
Makala toka BBC
Membe afukuzwa CCM, Kinana aonywa, Makamba asamehewa.
Kamati kuu ya Halmashauri kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi imemvua uanachama kada wake Bernad Membe huku ikitoa karipio kwa katibu mkuu mstaafu Abdulrahman Kinana na ikimsamehe katibu mkuu mwingine mstaafu Yusufu Makamba.
Katibu wa itikadi na uenezi wa halmashauri kuu ya chama hicho Humprey Polepole amesema uamuzi huo wa kamati kuu umefikiwa ikiwa ni utekelezaji wa katiba ya chama hicho kulingana na makosa ambayo makada hao watatu walituhumiwa kuyafanya.
Kinana apewa karipio, awekwa chini ya uangalizi miezi 18.