Waziri Januari Makamba amesema hata kama hatumkubali Samia ni wetu
By
X dot com / JMakamba
January Yusuf Makamba,
Hakuna sababu ya kuongopa. Taarifa tulizotoa kwa umma zipo wazi kwamba safari ya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan nchini Korea ina sehemu mbili: sehemu ya kwanza, Rais wetu amealikwa na Rais wa Jamhuri ya Korea, yeye kama Rais wa Tanzania, kufanya ziara rasmi ya mahusiano ya nchi na nchi (bilateral) nchini Korea; sehemu ya pili, amealikwa pamoja na Marais wenzake wa Afrika kujumuika nao kuhudhuria Mkutano wa Korea-Africa Summit.
Nimeweka picha ya sehemu ya taarifa yangu kuonyesha kwamba tulisema ukweli.Sehemu ya kwanza ya ziara hii imefanyika tarehe 2 Juni 2024, ambapo Rais wetu alikaribishwa na Rais mwenzake Ikulu ya Korea kwa mazungumzo ya uhusiano kati ya nchi mbili, chakula cha heshima cha mchana, na kusaini mikataba, ukiwemo wa dola bilioni 2.5.
Hapa, tofauti na unavyotuhumu, hakukuwa na Rais wa nchi nyingine. Sehemu ya pili ya ziara itakuwa tarehe 4 - 5 Juni, ambapo Rais wetu amealikwa na wenzake wa Afrika kuhudhuria Mkutano wa Kwanza wa Marais wa Afrika na Korea.
Taarifa za Mkutano huu zipo mitandaoni. Katika mkutano huu, Rais wetu atahutubia kwenye Mkutano Mkuu wa Pamoja wa Ufunguzi (plenary) na pia atazungumza kwenye majopo mawili (panels): moja, kuhusu miundombinu na la pili kuhusu usalama wa chakula na madini. Rais wa Korea alionelea amualike Rais wetu kwa ziara yake mwenyewe katika kipindi hiki cha kuelekea Mkutano wa Korea-Africa Summit ili iwe rahisi kufanya mambo mawili katika safari moja: kufanya ziara ya mahusiano ya nchi na nchi na kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Korea na Afrika.
Ukisoma taarifa zetu ndivyo tulivyosema. Kwenye mahusiano ya Kimataifa mambo kama haya ni ya kawaida. Majuzi tu, hata sisi tulialika Marais kadhaa kwenye Sherehe za Kuadhimisha Miaka 60 ya Muungano tarehe 26 Aprili 2024, ikiwemo Rais wa Somalia. Siku iliyofuatia, 27 Aprili, Rais wa Somalia akafanya ziara ya kitaifa (State Visit) nchini na kupewa itifaki stahiki.Katika mipango ya ushirikiano wa Kimataifa, Tanzania ni moja kati ya nchi za Afrika zilizopewa kipaumbele na Korea.
Pia Tanzania ni moja kati ya nchi tatu ambazo Korea imeamua kufanya nazo makubaliano makubwa ya Ushirikiano wa Kiuchumi (Economic Partnership), ambapo leo, mbele ya Marais wawili katikaIkulu ya Korea, tumesaini hilo Tamko. Pia kwa Korea, Tanzania ni nchi ya pili kwa kupokea ODA kubwa zaidi, baada ya Misri.
Kumekuwa na manufaa makubwa katika ushirikiano na Korea. Kwa uchache sana, kuanzia mwaka huu tu pekee, manufaa yanayotarajiwa ni:- hospitali yote ya Muhimbili kujengwa upya kabisa na kuwa kubwa zaidi na ya kisasa zaidi na pia ujenzi wa Chuo Kikubwa Cha Kisasa cha Teknolojia kule Dodoma.
Katika Mkutano kati ya Rais wetu na Rais wa Korea, mambo mapya makubwa ya ushirikiano yameamuliwa ikiwemo ushirikiano mpya kwenye Uchumi wa Kidijitali, Kusambaza Elimu Kidijitali hadi Vijijini, Uchumi wa Bluu, Kuongeza Thamani kwenye Madini Nchini na Ujenzi wa Miundombinu.
Baada ya Korea-Africa Summit kunatarajiwa kutolewa Tamko la Pamoja la Ushirikiano Mpya kati ya Afrika na Korea. Leo Mawaziri wa Mambo ya Nje tumekaa na kupitia Tamko hilo kabla kikao cha Marais tarehe 4 Juni.Nimechukua ushauri wa Fatma Karume kwamba tuwe tunaelezea,hata kama ni kwa urefu kiasi gani, haya mambo ili kusaidia kuelimisha.