Makampuni ya kutengeneza magari ya China sasa yanaongeza juhudi za kuingia katika soko la magari la Afrika, yakilenga magari ya umeme na magari mseto ya bei nafuu, katika wakati ambao dunia imegubikwa na siasa za kijiografia na kuongezeana ushuru bila sababu, na kuzuia ufikiaji wa masoko ya Magharibi.
Labda hujawahi kusikia kuhusu chapa za magari kama vile Haval au Chery, lakini ukitembelea Magharibi na kusini mwa Afrika, basi utazoea haraka kuona magari haya ya Kichina.
Chapa zinazoongoza za China kama vile BYD, Chery Auto, na Great Wall Motor zinapanua shughuli zake katika nchi za Afrika, na kuonekana kama njia ya kimkakati ya kulifikia bara pana la Afrika.
Nchini Zimbabwe na Nigeria, chapa kama vile Great Wall Motors, BYD, na Geely zinazindua magari mapya ya SUV na magari ya umeme mfululizo. Nchini Afrika Kusini nako gari la Haval H6 SUV ni miongoni mwa magari matano yanayouzwa zaidi.
Na sasa neema hii ya kustawisha nchi kupitia kuwekeza kwenye utengenezaji wa magari ya umeme na magari mseto ya bei nafuu pia imeifikia Tanzania. Kampuni maarufu ya China HARMONY Auto, imezindua rasmi biashara yake nchini Tanzania ikiwa kama sehemu ya juhudi za kuunga mkono mipango ya serikali katika kutumia nishati safi na kuleta usafiri rafiki kwa mazingira kote Afrika.
HARMONY Auto inapanga kuanzisha chapa ya Build Your Dreams, ama kwa kifupi inajulikana kama BYD, ili kuondoa kero ya usafiri rafiki kwa mazingira katika nchi hiyo, jambo ambalo linatarajiwa kuboresha kwa kiasi kikubwa hali ya usafiri ya wakazi nchini humo.
Baada ya miaka thelathini katika sekta hii, na baada ya kuanza kama mtengenezaji wa betri, BYD imekua moja ya chapa zinazopendwa zaidi duniani, ama tunaweza kusema kwamba kwa sasa imekuwa ikiongoza duniani kwa utengenezaji wa magari ya nishati mpya na teknolojia ya kijani.
Uzuri wa magari ya BYD yanayotumia umeme tu ni kwamba pia huja na chaji zake zinazobebeka, iwapo wamiliki wa magari watahitaji kusafiri umbali mrefu, basi hawahitaji kutumia hata shilingi moja kwa ajili ya mafuta. Kwa mfano, BYD Seal inaweza kuwafanya wamiliki wasafiri kwa umbali wa kilomita 500 kwa betri iliyochajiwa na kujaa kabisa. Na BYD Dolphin inaweza kusafiri hadi kilomita 400 kwa betri iliyochajiwa na kujaa kabisa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi mbele ya wanahabari, mwakilishi wa mauzo wa kampuni hiyo Khatib Hussein, alifafanua kwa undani sifa za kiufundi za gari la BYD Shark 6, ambapo mojawapo ni kwamba hata kama mafuta yameisha, betri inaweza kuendelea kutumika baada ya kuichaji. Gari hii inaweza kusafiri kwa zaidi ya kilomita 100 ikitumia umeme tu baada ya betri kuchajiwa kwa saa mbili.
Hii ni habari njema hasa kwa nchi kama Tanzania ambayo mara kwa mara imekuwa ikishuhudia bei ya mafuta ikipaa na kupelekea hata kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali za vyakula.
Kampuni hiyo tayari ina matawi manne kote Afrika ikiwemo Afrika Kusini, Msumbiji, Kenya, na sasa Tanzania. Pia inapanga kuanzisha kiwanda cha kutengeneza magari nchini Afrika Kusini na kituo cha kuunganisha magari nchini Tanzania ili kukidhi masharti ya uendeshaji wa ndani na kuchangia ukuaji wa sekta ya magari ya umeme kote Afrika.
Kwa sasa, magari yanayouzwa na kampuni hiyo yamewekwa katika mfumo wa lugha ya Kiingereza, lakini hilo sio tatizo kwani sasa kampuni ya HARMONY Auto ina mpango wa kuanzisha mfumo wa Kiswahili unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Makampuni ya China sio tu yamekuwa maarufu kwa kuwekeza na kupeleka teknolojia ya magari ya nishati safi, bali pia mabasi, skuta, na hata baiskeli za magurudumu matatu zilizotengenezwa na makampuni ya China zinazidi kukita mizizi barani Afrika, na kuifanya China kuwa ya kwanza kwa magari ya umeme ya kila muundo.
Jambo la kuzingatia ni kwamba kama chapa za magari za China zinaweza kuimarika barani Afrika, kimsingi zinaweza kufanikiwa popote pale duniani. Kwa sababu soko jipya la magari barani Afrika ni gumu sana kuliingia.