Makamu wa Rais wa Tanzania Dk. Philip Mpango amesema kuwa hali ya Ushoga nchini Tanzania sasa imefikia pabaya na kutaka Jamii Kubadilika na Kuimarisha Maadili ya Mtanzania.
Taarifa: Gazeti la Nipashe la Leo.
Mama na Wewe sasa sema Kitu tu!!!
====
Mpango: Hali mbaya mmomonyoko maadili
MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, amesema hali ya mmomonyoko wa maadili, inazidi kuwa mbaya huku akikemea ndoa za jinsia moja.
Kutokana na hali hiyo, amewasisitiza wazazi kuwalea watoto wao katika maadili ya Kitanzania pamoja na kuongeza umakini katika maudhui yanayoonyeshwa kwenye televisheni.
Dk. Mpango amesema kwa sasa kumekuwapo na mmomonyoko wa maadili, ikiwamo ndoa za jinsia moja na kuwataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kukemea vikali, ili kuondokana na taifa lisilofaa kwa vizazi vya sasa na baadaye.
Alisema hayo jana wakati akizungumza na waumini wa kijiji cha Kasumo mkoani Kigoma baada ya kushiriki ibada ya kawaida ya katikati ya wiki katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani lililoko kijijini hapo.
Makamu wa Rais aliwataka wazazi na walezi kuwalea watoto kwa kuzingatia maadili ya kitanzania pamoja na kuongeza umakini katika maudhui yanayooneshwa katika televisheni.
“Paroko hili ni zito, gumu kweli. Maadili ya nchi yetu yameporomoka sana. Hayo masanamu uliyokuwa ukituhubiria yamejaa, yamekuwa mengi kupindukia na mengine hata kuyasema ni ngumu. Mimi niliyezaliwa katika kijiji hiki naogopa, ndoa za wanaume wawili, ndoa za wanawake wawili mliziona wapi? Hata wanyama hawafanyi hivyo,” alisema.
“Kwa hiyo nawasihini sana, najua nyumbani kuna televisheni, mchague watoto, vijana wanaangalia nini, vinginevyo tutakuwa na taifa la ajabu kabisa,” alisisitiza.
Ibada hiyo ilihudhuriwa pia na mke wake, Mama Mbonimpaye Mpango na kuongozwa na Paroko wa Parokia hiyo, Padre Joseph Mashaka.
CHANZO: Nipashe