Mfanyabiashara wa madini aliyetambuliwa kwa jina la Festo Marwa (55) na mtoto wake John Marwa wameuawa kikatili kwa kupigwa kichwani na kitu kizito chenye ncha kali.
Marwa na mwanawe ambao ni wakazi wa Kunduchi jijini Dar es Salaam, wamekutwa na umauti wakiwa katika kitongoji cha Mkerema Kijiji cha Lilondo, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma.
Akitoa taarifa ya mauaji hayo jana Jumatano Agosti 30, 2023, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, ACP Marco Chilyaakati amesema John (mtoto) amekutwa na jeraha kubwa kichwani na uchunguzi wa awali unaonyesha kapigwa na kitu kizito chenye ncha kali kilichosababisha ubongo kutoka nje.
“Baada ya mauaji hayo, wauaji hao waliichukua miili yao na kuiweka kwenye gari la Marwa ambalo ni Jeep kisha wakalisukuma gari hilo hadi kwenye korongo,” alidai kamanda huyo.
Amedai lengo la kulisukumia gari hilo korongoni ni kutaka ionekane kuwa walipata ajali.
Hata hivyo, Kamanda Chilyaakati amesema makachelo walipolikagua gari hilo halikuwa limepata ajali.
“Baada ya kufanya utafiti tumefanikiwa kumkamata dereva aliyekuwa akiliendesha lile gari aliyetuambia kuwa baada ya tukio wenzake walimsindikiza hadi kituo cha mafuta kusudi aende polisi akatoe taarifa kwamba kapata ajali,” alidai kamanda Chilyaakati.
Amedai ili kupoteza ushahidi, dereva huyo alipigwa na kitu chenye ncha kali mguuni ili naye aonekana kapata majeraha kwenye ajali hiyo ya kutengeneza.
Anadai baada ya kumhoji alimtaja mtuhumiwa mwingine ambaye naye ametiwa mbaroni akihusishwa na tukio hilo.
View attachment 2734691