Wild Flower
JF-Expert Member
- Jul 20, 2023
- 977
- 1,966
Migogoro ya ardhi imeelezwa kuwa inaweza kupunguzwa kwa kuimarisha mfumo wa kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi mapema kabla hazijafikishwa mahakamani. Hayo yameelezwa jana Jumatano Februari 25, 2026 na Mbunge wa Arusha Mjini, ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda wakati akizungumza na wakuu wa idara wa jiji hilo, ambapo amesisitiza umuhimu wa viongozi wa halmashauri kuanzisha utaratibu wa ziara za kata kwa kata kwa ajili ya kushughulikia migogoro ya wananchi.
Makonda amesema badala ya kusubiri wananchi wafike ofisini, viongozi wanaweza kupanga ratiba maalumu ya kwenda kwenye kata na kukutana na wananchi wenye migogoro kwa kushirikiana na watendaji wa kata, madiwani pamoja na wataalamu wa mipango miji na ardhi. Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza migogoro inayoenda mahakamani, ambayo husababisha wananchi kuingia gharama kubwa na kuchangia mlundikano wa kesi katika mfumo wa mahakama.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha na kuwezesha mabaraza ya ardhi ya kata ili yawe na uwezo wa kuwasaidia wananchi kutatua changamoto zao kwa wakati, huku akieleza kuwa ushirikiano wa wataalamu wa sekta husika ni muhimu katika kuhakikisha kunakuwa na suluhisho la kudumu.