Ndugu zangu, kanisa haliendeshwi hivyo kama mnavyodhani. Kanisa la KKKT kila Dayosisi ina Katiba yake na miongozo mbalimbali.
Huyu ndugu anayeleta tuhuma za viongozi wa kanisa kula fedha na kuwabambikia deni ni utovu wa nidhamu na ni kinyume na maandiko.
KKKT ni miongoni mwa madhehebu ya dini yenye utaratibu mzuri sana katika uendeshaji wa kanisa na usimamizi wa fedha za kanisa. Moja wapo ya njia bora wanayotumia ni kuweka wazi mapato na matumizi ya fedha kwa kusomwa Ibadani kila Jumapili na kuandaliwa taarifa ya mapato na matumizi ya kila robo mwaka, nusu mwaka na ya mwaka.
Lengo ni kuwapa nafasi washarika kujua mapato na matumizi ya fedha wanazotoa kama sadaka na michango mbalimbali. Pia masuala yote ya matumizi ya fedha yanafanyika chini ya usimamizi wa Kamati husika, mfano kama ni suala la ujenzi muhusika hapa ni Kamati ya ujenzi au miradi.
Kamati hizi zinaundwa na washarika wenyewe kupitia mabaraza ya wazee na mchungaji wao. Pia utaratibu ndio huo huo hadi ngazi ya Jimbo na Dayosisi.
Muhimu kuzingatia kuwa sharika, majimbo, Dayosisi na vituo vyake vyote hesabu zake ukaguliwa na wakaguzi wenye weledi na masuala ya fedha na uhasibu.
Mleta mada anasema wameelezwa juu ya deni bila ufafanuzi kuwa limetokana na nini. KKKT wana njia nyingi za kupokea maoni, ushauri, mapendekezo na ukosoaji ikiwemo mkutano mkuu wa mwaka kwa kila ngazi kuanzia Jumuiya hadi Dayosisi ambapo moja wapo ya kazi ya mkutano mkuu wa mwaka upitisha makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka unaofuata na kupitia taarifa za fedha na miradi za mwaka unaoisha. Pia wakuu wa sharika na vituo ukaribisha maoni na mapendekezo wakati wowote msharika anapokuwa na jambo la kushauri kwa kwenda moja kwa moja ofisini kwa kiongozi husika.
Mara nyingi utakuta mikutano mikuu ya mwaka msharika haudhurii hivyo anakosa fursa ya kujua mipango ya kanisa lake siku akiambiwa kuwa kuna mradi haukufanya vema na kupelekea kuzalisha labda deni au kuna mradi umekwama kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo wafadhili kuchelewa kuleta fedha nk, ndipo utaona msharika hasiyewajibika ipasavyo anakimbilia kwenye mitandao ya kijamii na kutuhumu viongozi wa kanisa kula fedha. Hii si sawa kwani kwanza inadhalilisha kanisa la Mungu na kuwavunja moyo viongozi wanaokesha usiku na mchana wakifikiria juu ya kuzijengea uwezo wa kiuchumi sharika na Dayosisi zao.
Pia haisaidii kuleta suluhu zaidi ya upotishaji.
Namshauri mleta mada aende ofisi husika awasilishe maoni yake yatafanyiwa kazi na atapata ufafanuzi wa kina wa nini kilitokea hadi deni hilo kuwepo.
Mungu awabariki sana.