Malezi - Sheria ya Mtoto inasemaje kuhusu picha za watoto mitandaoni?

Malezi - Sheria ya Mtoto inasemaje kuhusu picha za watoto mitandaoni?

Sema Tanzania

JF-Expert Member
Joined
May 18, 2016
Posts
251
Reaction score
466
Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inatamka wazi kwamba 'Mtu hatachapisha, kutengeneza, kuonyesha au kuagiza kuchapishwa, kuendeshwa au kuonyeshwa picha au taswira ya mtoto au mtoto aliyefariki, inayoonyesha ukatili au katika pozi za ngono.'

Ama kwa kujua au bila kujua, jamii hukiuka sheria hii mara nyingi kwa kusambaza picha za watoto katika taswira zisizo nzuri. Picha za ajali, mtoto akikata mauno, vifo na kadhalika. Hizi zinadhalilisha watoto, familia zao, kuwaathiri kisaikolojia na kudhoofisha ukuaji na maendeleo yao

Wahalifu katika kupiga na kusambaza picha za watoto mitandaoni ni jamii nzima. Watu wengi hufurahia kupata picha hizi na huwa wenye mshawawsha kuzisambaza kwenye makundi mbalimbali mitandaoni. Namna hii picha hizi husambazwa kwa mamilioni ya watu walioko kwenye mitandao kote ulimwenguni

Kundi jingine la wahalifu ni wamiliki wa vibanda vya filamu mtaani, maarufu kama ‘vibanda umiza’. Hawa wanaonesha filamu za aina zote bila kujali umri wa wateja wao. Watoto wadogo wanaruhusiwa kuingia kuona filamu za ngono alimuradi wanazo pesa za kiingilio. Tunapendekeza kuwa iwapo vibanda hivi vimeruhusiwa, basi ni vyema serikali za mitaa ziweze kudhibiti aina za filamu watoto wanazooneshwa vibandani ili kulinda maadili ya taifa la kesho na kuokoa nguvu kazi itakayojenga nchi

Ingawa mzazi huwezi kuwa kila mahala alipo mwanao. Ukosefu wa umakini wa kujua watoto wanacheza wapi, wanacheza na nani, wanatazama na kusikiliza vitu gani inaweza kuwa sababu kubwa ya watoto kuranda huku na kule kujifunza tabia zisizofaa kama hizi za kuingia vibanda umiza, nk. Pamoja na mzazi kuhakikisha anajua watoto wanapocheza na wanacheza na nani, vilevile, yakupasa kuhakikisha anatoa muongozo wa namna ya kuwalea watoto kwa mtu yeyote anayekaa na watoto pindi uwapo kazini

Vilevile Sheria ya Mtoto inakataza mtu kumtumia mtoto katika maonyesho ya harusi, maonyesho ya mitindo ya nguo au maonyesho mengine yoyote yanayofanana na hayo wakati wa usiku. Hili tunakuachia, vipi linafuatwa na washereheshaji nchini? Vipi kuhusu wanaotumia picha za watoto kuonyesha dhiki ili kupata fedha toka kwa wafadhili? Sheria pia imeweka angalizo katika hili kuwa kumhusisha mtoto aliye katika mazingira magumu kwa ajili ya kuombaomba au kwa ajili ya faida binafsi ni kosa

Tunapohitimisha, tuwaase wazazi na walezi kuwa wanao mchango mkubwa sana kuwafanya watoto wawe watu makini ukubwani. Hivyo wanao wajibu adimu kuwapatia watoto wao malezi yanayostahili, kama wasemavyo, ‘Samaki mkunje angali mbichi’. Namna mtoto anavyolelewa leo ina mchango mkubwa tu katika vile atakavyokuwa baadae ukubwani. Hakuna ajali katika malezi. Ukianda mchicha unavuna huohuo mchicha

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook, Instagram na JamiiForums: Sema Tanzania; Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org
 
Back
Top Bottom