Mama yangu kaniumiza sikutegemea

Mama yangu kaniumiza sikutegemea

Mwachiluwi

JF-Expert Member
Joined
Mar 10, 2022
Posts
25,258
Reaction score
48,589
Tafsiri ya kitaalamu inaelezea malezi kuwa ni mchakato wa maandalizi ya mtoto utakaomwezesha kukua, kukubalika na kushiriki katika shughuli za kijamii na kiutamaduni kwa kumlinda, kumjamiisha na kumpatia mahitaji na huduma za msingi.

Iwapo malezi ni mchakato wa maandalizi ya mtoto basi shurti iwepo mipango toka kwa wazazi ili kufanikisha hili. Zama za kujipatia watoto na kuwaacha wakue zinajongea ukingoni. Sasa tunaishi katika wakati wa kuzaa na kulea. Kulea ni pamoja na kuwekeza katika mahitaji muhimu kama vile lishe bora, afya, elimu, ulinzi na hata maji safi na salama.

Mwenendo wa maisha ya wazazi hujumuisha maneno, matendo, tabia na desturi za wazazi wanazotumia katika kuendesha maisha yao ya kila siku katika familia zao na jamii inayowazunguka kwa ujumla. Mahusiano kati ya wazazi, mahusiano na majirani, ndugu, jamaa na marafiki na jinsi unavyowakarimu wageni, nk. Vyote hivi huathiri makuzi na tabia za watoto katika nyanja kuu mbili tofauti; athari chanya na athari hasi. Sote tunajua watoto kwa kiasi kikubwa hujifunza kutoka kwa wazazi wao. Wanachokiona anafanya mzazi, wao pia hufanya.

Hakuna ushuhuda mkuu kuliko kumuona mtu mwenye hadhi na sharafu akipigana na majaribu makubwa, wazazi wanapitia mambo mengi mno kuhakikisha watoto wao wanapata malezi wanayostahiki , wengi hujinyima ili watoto wao wapate licha ya hayo kumekuwa na wazazi ambao huyakimbia majukumu yao na kuwaacha watoto wakiteseka, hiyo hali huleta migogoro baina ya wazazi hao na huwaathiri watoto kiakili na kiafya kwa maana hubaki na maswali mengi kichwani mwao.

Karibu tuangalie kwa pamoja jinsi malezi ya watoto yanavyojenga na kubomo akili za watoto hao, njoo tuisome BARUA KWA MAMA ambayo imeandikwa na mtoto BARAKA, kwanini aandike barua? Ina ujumbe gani? Naam njoo tujumuike pamoja .

◇SEHEMU YA 1◇

Watoto ni kama vichipukizi kwenye bustani ambavyo vinahitaji kutunzwa kwa uangalifu kwa kuwa wao ni viongozi wa kesho na elimu ndiyo huleta mabadiliko yenye mafanikio kutoka utoto hadi utu uzima.Elimu ni muhimu katika kuunda na kukuza nguvu za kihisia na kiakili za mtoto, kumtayarisha kushinda vizuizi vyovyote katika njia yao ya mafanikio kwa kuzingatia hilo kila jamii ya leo imehakikisha watoto wanapewa elimu bila kujali maumbile yao na hali zao za maisha, shule zimesogezwa kwenye jamii zetu ili kila mtoto afaidike nayo.

Haki hiyo ya msingi iliwafikie watoto wa mtaa wa JIULIZE ambapo asilimia kubwa ya wazazi wa mtaa huo walionekana ni wale waliochakazwa na maisha , ndio maisha yaliwachakaza kwani tafuta yao ilikuwa ni kubwa kuliko pata yao, wengi wao walilala kwa kushukuru na walichokipata zaidi ya kile walichotarajia ni wachache mno ambao walijiweza kiuchumi, kiufupi JIULIZE ulikuwa ni mtaa wa walala hoi ndani ya jiji kubwa la TULEANE na ndio mtaa ambao ulikuwa na idadi kubwa ya watoto maana waliamini uzao wao ndio utajiri wao, nyumba zilizochakaa , mitaro iliyohatarisha afya zao na maji ya tabu yaliyokosa usalama ndio ilikuwa sehemu ya maisha ya maisha yao naam hiyo ndio JIULIZE mtaaa ambao mtoto Baraka alikuwa akiishi na mzazi wake wa kike aliyeitwa Sadifa

"Nakwambia usipomaliza kujaza maji ndani hamna kukusanya miguu yako kwenda shule...sasa endelea na ujinga wako maana tokea ulipoamka sujui unakiandika nini hapo " bi Sadifa ambae ni mama Baraka alimfokea mtoto wake huyo huku yeye akimaliza kuchoma vitumbua.

"Lakini mama hiii kazi ningefanya saa ngapi na jana tulilala giza, nilipotaka kwenda kwa kina Mamy ulinikataza unadhani ningefanya nini kama sio kuandika muda huu , halafu bado unataka nikachote na maji hivi huoni kama nitachelewa shul...."

"Eeeeh koma wewe kenge! Wa kusoma utakuwa wewe? Muone vile, yalinishinda mimi mamaako na ndio leo hii unaona hapa napika zangu maandazi na vitumbua" aliwaka bi Sadifa na kumfanya Baraka aufumbe mdomo wake, maana alimjua vizuri mamaake na hakupenda kumkwaza kamwe.

Taratibu Baraka alikusanya madaftari yake kuyaweka kwenye mkoba wake wa kitambaa ambao ulitoka kutolewa unga wa ngano siku za nyuma, aliinua ndoo zake mbili na kuanza safari ya kuelekea kisimani, njiani alikuwa ni mwenye mawazo mno huku akionekana kuchoshwa na vitendo vilivyokuwa vikiendelea kumnyima raha, roho ilimuuma kuona baadhi ya watoto wenziwe wakiwa na sare zao wakielekea shule huku yeye akielekea kisimani.

"Hivi mamaangu lini atakua muelewa? Tuseme haujui umuhimu wa elimu? Hemu ona maisha maisha yetu yalivyo kwanini asinitengezee mazingira ya kuwa mkombozi wake hapo baadae? Au tuseme yeye alisharidhika na maisha haya? Na leo nisipokuwa makini nitachelewa tena darasani hata hii kazi niliyoifanya nitakosa kuipeleka kwa mwalimu " Baraka alisema na nafsi yake huku akianza kukazanisha miguu.

" Samahani Bi Mwinde naomba zamu ya kwako nichote mimi maana bila ya hivyo nitachelewa shule" aliomba Baraka mara tu baada ya kumaliza kuwasalimia aliowakuta.

"Mmh imekuwa ni ada yenu eeeh! Mwambie mamaako mbinu zake tumezijua, haiwezekani yeye akae huko sisi tusote hapa na foleni ukija wewe upishwe....hapa leo hupishwi kila mtu ana haraka zake" aliyekua hakuombwa alijibu kwa sauti kubwa, huyu hakuwa mwengine bali ni bi.Kidubwa ambae mtaa mzima alijulikana na tabia yake ya kuwa na maneno mengi.

"Ndio hivo sasa, mamaake na yeye kazidi ujanja, sote hapa tuna watoto na wajukuu wanaosoma na tumewachagulia moja la kufanya, hapo leo uchelewe tu lakini hakuna ruhusa ya kupishwa na mtu" jirani mwengine aliyechoshwa na tabia hiyo na yeye alichangia mada.

Mpaka kufikia hapo Baraka aliona ugumu wa siku hiyo, ni kweli ilikuwa ni kawaida kila akifika pale kupishwa ili awahi shule ila kwa siku hiyo walio wengi walionekana kuchoshwa, mamaake hakuwahi kwenda kisimani na badala yake alimtegemea yeye, bi Mwinde ambae alimtegemea kumtetea siku hiyo mdomo wake haukuwa na jibu lolote kutokana na kauli alizozipokea kutoka kwa wenziwe, macho yake ya huruma yalimfikia bi Mwinde ambae alibaki njia panda asijue wapi kwa kuelekea.

"Kesho ndiyo mwisho wa kila kitu, kama kusoma ni matayarisho ya maisha basi wacha nikatayarishe ya kwangu, nitajua cha kufanya nikifika nyumbani bila ya maji " Baraka alijiwazia baada ya kukosa msaada.

Hakuwa na cha kusubiri zaidi ya kuchanganya hatua za miguu na kuitafuta njia ya kwao, aliuthamini sana muda alionao, kwake yeye elimu ndio alihisi itakwenda kubadilisha maisha ya kwao , aliamini kupitia elimu hiyohiyo atakwenda kuwakomboa wale waliokosa matumaini ya kusoma wakihofia kukosa ajira.

Pumzi kubwa aliishusha baada ya kuona mlango wa nyumba yao, aliuchunguza vizuri kabla ya kuingia na kugundua kuwa uliegeshwa na sio kufungwa , masikio yake mawili aliyoyategesha kusikiliza chochote kutoka ndani yalimpa jibu la ukimya ambao uliashiria hapakua na mtu yoyote, alifurahi kuona mamaake tayari alikwenda kwenye biashara zake .

"Heheeh hapa wacha ninunue kesi , najua hukumu yake itaniumiza mno ila wacha iwe hivyo" alijisemea Baraka huku akipenyeza ndoo zake zilizokosa maji na kubeba madaftari yake kisha safari ya shule ikaanza.

Mwendo wa kijeshi ndio alihisi utamfikisha haraka safari yake , njiani alipishana na baadhi ya wanafunzi ambao kiuhalisia walionekana ni wachelewaji maarufu, akisikitika kuona na yeye ni miongoni mwao ila angefanya nini?

Baada ya mwendo wa robo saa hatimae aliufikia uzio wa shule yao, uzio ambao ulijengewa na senyenge, geti kubwa la bati lenye kibao chenye maandishi yaliosomeka SHULE YA MSINGI SOMENI yalifikisha tamati ya safari yake, pumzi kubwa aliishusha akionekana kushukuru kuwa pale bila ya usumbufu wowote.

"Mungu wangu na leo nimechelewa tena , sikushiriki shughuli yeyote ya usafi ila nitawahi kuingia darasani" aliongea huku akiendelea na mwendo wake wa kijeshi .

Mlango wa mbao uliokuwa umechorwa namba 6B juu ndio ulikua ukomo wa kukaza kwake, kupitia madirisha yenye uwazi alifurahi kuona darasani hakukuwa na mwalimu, tabasamu zito lilimtoka mwanamke ambae alikuwa kasimama akionekana kusubiri kitu kwa muda mrefu, mwanamke huyo aifurahi mno baada ya kuona sura ya Baraka ikiwa mlangoni .

" B lete daftari lako la English haraka sana, ni muda sasa nimechelewesha kuyapeleka nikikusubiri wewe tu " aliongea mwanamke yule akiwa na rundo kubwa la madaftari mkononi mwake.

"Mamy , hivi nisingewahi ungefanya nini" alidadidisi Bakari huku akipekua mkoba wake na kumkabidhi.

"Ningekereka sana maana nimekuwa nikikuhimiza mno, ila B jiandae na bakora za mwalimu wa usafi maana na leo tena hukuonekana" Mamy aliongea hayo na kutokomea zake nje.......Itaendelea.

Ndio tumeanza hivyo!!!

Tupia like na comments yako hapo chini, muitiko wenu ndio mwendelezo wangu twende kazi!!

◇SEHEMU YA 2◇

"Mamy, hivi nisingewahi ungefanya nini" alidadidisi Bakari huku akipekua mkoba wake na kumkabidhi daftari la kiswahili.

"Ningekereka sana maana nimekuwa nikikuhimiza mno, ila B jiandae na bakora za mwalimu wa usafi maana na leo tena hukuonekana" Mamy aliongea hayo na kutokomea zake nje huku akimuacha Baraka akijigusa makalio yake.

Mamy ni binti ambae alizaliwa kwenye familia iliyojiweza kiuchumi, licha ya kwamba walikuwa wakiishi ndani ya mtaa wa JIULIZE ila changamoto za maisha walizimudu vyema , mamaake na Mamy alikuwa ni daktari huku babaake akiwa ni bosi mkuu wa kampuni kubwa ya uuzaji vifaa tiba katikati ya jiji la TULEANE mbali kidogo na mtaa wa Jiulize.

Licha ya kuwa walijiweza kiuchumi tofauti na wenzao , Mamy hakuwa mwenye majivuno , alimheshimu kila mmoja na kuishi nae kwenye daraja sawa , Mamy alijenga urafiki na Baraka tokea siku ya kwanza alipofika shuleni hapo wakati huo walikuwa darasa la 5 , kilichomvutia zaidi kutoka kwake ni ile nidhamu ya upole na utulivu awapo darasani, ufahamu katika masomo yake ndio ulimfanya azidi kupendeza kwake hata kama hakuwahi kushika nafasi ya kwanza darasani na hiyo ikitokana na kukosa baadhi ya vipindi na muda mzuri wa kujisomea .

"B.....hivi unajua kuwa kila siku huja na zawadi yake " Baraka alishtushwa na kauli ya Mamy mara tu baada ya kuketi kando yake.

"Hhhh ni wewe hivi umefika muda gani" alihoji Baraka akiwa hakufahamu hata akichoulizwa ingawa alisikia .

"Inaonekana ulikuwa mbali mno kimawazo hemu niambie nini shida B wangu " Mamy aliuliza huku sura yake ikijenga hofu .

"Mamy siku zote sitaacha kuwaza kuhusu maisha yangu maana bado najiona nina safari ndefu mno, changamoto ambazo zinanisumbua muda huu ndizo ambazo zinanifanya nisiache kuwaza , kuna mengi napaswa kuyaweka sawa na nina imani ipo siku nitayamaliza" Baraka alijibu kwa upole mno hadi Mamy huruma ilimuingia.

"Mama kuna siku alinambia ya kwamba "Wito wa maisha ni kuamini, kutumaini na kusonga mbele" hivyo kupitia hamasa hiyo nina imani utakamilisha yale unayotamani yakamilike" Baraka alipewa maneno ya kutia moyo huku akiwa kashikiliwa mikono yake.

"Naamini hilo Mamy na ndio maana kila nikiamka asubuhi basi namshukuru mungu kwa maana nipo hai, napumua na nina akili timamu ya kuweza kufikiria nini natakiwa kufanya ili kusonga mbele......" alijibu Baraka macho yake akiwa kayakaza usoni kwa Mamy.

"Ila ukumbuke kuwa maisha ya ndoto hayapatikani kwa kukaa na kuwaza tu, bali kwa kupigania unachoamini na lazima ndoto yako kutimia kama ukiwa na ujasiri wa kuifukuzia" Mamy alizidi kukazia na kuondoa mikono yake kwa Baraka.

"Tuachane na hayo Mamy , ulipofika ulinisemesha ila sikuwa nimekuelewa kamwe" Baraka alibadili mada.

"Nilikuuliza, hivi unajua kuwa kila siku huja na zawadi yake? Mamy alirudia tena kumuuliza huku akiwa makini kumsoma atajibiwa nini.

"Ahaa ndio naelewa hilo, ila hii zawadi ya leo sifikirii kama ina manufaa kwangu, nimewahi vipindi vya asubuhi ila hadi muda huu hakuna mwalimu aliyeingia jambo ambalo sio kawaida, nimeacha jukumu alilonipa mama ambalo bila ya shaka nikirudi sijajua namna ya kujitetea" ingawa Baraka alijibu kwa masikitiko ila hakuacha kumalizia na kicheko kilichoashiria alijihisi mjinga kwa kukaidi amri ya mamaake.

"Hujapoteza bado na hii ni zaidi ya zawadi kwako, hemu jiangalie jana tokea umerudi kutoka shule umesoma nini? Nilikwambia uje nyumbani ila hukutokea kabisa! Hapa shuleni sikuwa napata muda mzuri wa kujisomea na wewe zaidi ya muda wa mapumziko, Baraka ni wakati wetu huu wa kujisomea na kuwekana sawa pale ambapo hatukuwa tumeelewa na wewe ulipokosa vipindi , kutokuwepo kwa mwalimu darasani kusitufanye tukaona tumepoteza muda " Mamy alimuweka sawa Baraka baada ya kuona kama kapoteza muda na siku yake.

"Ni kweli uyasemayo ila namfikiria sana mamaangu na jinsi gani anavyochukia nisipotekeleza agizo lake, sipendi kumkwaza mamaangu ila kuna muda inanibidi"

"Kwani umemfanya nini mama? Mamy alihoji .

"Sikujaza maji ndani kwa ajili ya kuwahi shule, nilikuta foleni kubwa kisimani na hata nilipoomba hakuna ambae alitaka tabia yangu iliyojenga mazowea, Mamy toa kitabu tuanze kusoma mambo ya nyumbani hayawezi kumaliza kwa hapa"

"Wa kwanza kuomba msamaha ni jasiri na yule wa kwanza kusamehe na kusahau ni mwenye furaha zaidi" maneno hayo kutoka kwa Mamy yalimfanya Baraka atikise kichwa kama ishara ya kuyaelewa.

"Nitafanya hivyo ila hapo kwenye kusamehewa sifikirii , mimi mamaangu ana......." Baraka alisita baada ya kuona atavuka mipaka na hilo jambo hata Mamy aliligundua na kuamua kupotezea.

"B akili yako ihamishie hapa ili twende sawa , mitihani ya mwisho wa mwaka itakuja kuanza hapa kichwani mtakuwa hamna kitu badala ya matope hahahaaaaa" Mamy aliongea hayo huku akitoa kitabu cha Mathematics (hesabati ) na kumtaka Baraka aongoze mjadala kwa vile aliliwezea hilo somo.

"Na wewe kwa hesabu dduh!! huwezekani sijui unataka kuwa mhasibu wa dunia" alitania Baraka huku akijiweka sawa kumsomesha mtoto wa kike.

Kwa vile walimu walikua na kikao ofisini kwao basi kiongozi wa darasa ambae ni Mamy alitoa tangazo, kila mmoja alikuwa na uhuru wa kufanya anachotaka , wanafunzi wengine na wao walikwenda kujiunga kwenye meza ya akina Baraka huku wengine wakibaki na tabia zao za kufurahia kuweka zogo pale mwalimu akiwa hayupo darasani, wapo waliojisomea wenyewe masomo mengine na wengine waliamua kutoka kabisa nje ya darasa kwenda kuzurura.

*****************
Kama maisha ni kujaribu vitu mpaka upate kinachofanya kazi basi bi Sadifa alikuwa ni mmoja wao, hakuwa mtu wa kutegemea kazi moja imuingizie kipato, ingawa alikutana na changamoto nyingi ila hilo halikumfanya aache kufanya kazi kila iitwayo leo, kila asubuhi alijitahidi kuwahi kufika makutano makubwa ya soko kuu ambalo lilipatikana katika mtaa wao wa JIULIZE, biashara eneo hilo zilichangamka na watu walikuwa wengi mno kwa maana bidhaa nyingi zilipatikana.

Tayari beseni lake la vitumbua na maandazi lilikuwa jeupe, biashara ilikuwa nzuri mno kiupande wake kwa siku hiyo, meno yote yalikuwa wazi kuonyesha ni furaha kubwa kiasi gani alikuwa nayo, alianza kukunjakunja na kuwaaga wenziwe ambao bado biashara iliwadodea.

"Sio bure mimi nawaambia mtu kila siku anaondoka mwanzo yeye? Kuna mchezo anatuchezea huyu mwanamke" alianza kusema mmoja ya wale ambao walikuwa nae pamoja, mama huyo alikuwa na biashara inayofanana na bi Sadifa.

"Kuwa na mapenzi na kazi yako na hapo kila kitu kitajipanga vizuri katika mstari, akili yako ina nguvu kuliko unavyodhani hivyo unatakiwa kuijaza akili yako fikra chanya ili uone mafanikio, Sadifa sio mchawi na wala hamrogi mtu ila umakini wake na ubunifu ndio unamfanya amalize kazi mapema" Mama mwenye hekima zake alimtetea bi Sadifa.

"Unasema nini na wewe? Ina maana mpo shirika moja , hivi wewe umeona ubunifu gani pale? Ubunifu wa kucheka ovyo na waume za watu? Aagh tumemchoka!!! Mwengine na yeye alidakia.

"Munatakiwa mujiamini na muwe na imani juu ya uwezo wenu, bila kuamini uwezo wenu wenyewe kamwe hamuwezi kuwa na mafanikio"

"Aaagh tupishe sisi weeh na darasa lako bovu, hapa kesho akija tunampasulia ! haiwezekani yeye kila siku awe wa kwanza kuondoka, tuseme ndio anajua sana kupika? Halafu na sisi!! Aaah weeeh , hapana kwa kweli kesho akija lazima ameze kichambo, mtu mapema unakuja hapa kabla ya sote kufika kama sio kuroga kitu gani? Aliyeanza mada aliongea kwa jazba na kuwafanya wengine wafurahie na kucheka .

**********

"Leo nitampikia mapema yule mtoto , tena nitampikia vitamu maana nina furaha kubwa mno, lazima ale kuku leo mwanangu, tuna mwaka wa nne huu kazi yetu kula tembele tu na dagaa, kwanza sina hata mteja wa mchana ! " Sadifa aliongea hayo kwa mbwembwe zote beseni likiwa kichwani kukaribia nyumba ambayo walipangishwa.

Alifungua mlango wao wa bati na kuingia zake ndani, hatua ya mwanzo aliweka beseni chini na kukimbilia chooni kwa vile haja ndogo ilimbana, mshangao ulimkumba baada ya kumaliza haja na kuona ndoo zikiwa nyeupe bila ya maji , hasira za wazi zilianza kumvaa na kumfanya apoteze tabasamu lake alilolijenga muda mfupi uliopitia.

"Huyu mtoto mshenzi eeeh na atanitambua leo akirudi, kwa maana hakujaza maji hata sehemu moja? Sasa mimi nitanawa na nini? Heeeh nadhani kanisahau" alifoka maneno ambayo yalikwenda kupenya kwenye masikio ya Baraka aliyekuwa
 
"Huyu mtoto mshenzi eeeh na atanitambua leo akirudi , kwa maana hakujaza maji hata sehemu moja? Heeeh! nadhani kanisahau" alifoka maneno ambayo yalikwenda kupenya kwenye masikio ya Baraka aliyekuwa akikatiza nje ya dirisha la chooni kwao.

"Amchokoae nyoka awe tayari kutafunwa, kama tayari nimekaribia kichaka ya nini tena nikimbie na hapa ndio nyumbani......Aah liwalo na liwe"alijisemea Baraka kwenye nafsi yake huku akisikitika na maneno ya mamaake.

Baraka aliamua kwenda kujitosa kwenye bahari ambayo alitegesha nyavu zake tokea asubuhi, taratibu kwa hatua za uoga alianza kuusogelea mlango wa nyumba yao, maneno yasio na mipaka yaliyojaa matusi yaliendelea kumtoka bi sadifa dhidi ya kijana wake, Baraka alitikisa kichwa huku akianza kuvuta mlango wao wa bati.

"Ajabu iliyoje kwa mwanadamu kuwa bahili wa mali yake lakini si bahili wa wakati, ilhali wakati ndicho kitu cha kufanyiwa ubahili kuliko mali" maneno hayo yaliyoambatana na mguso wa bega yalikwenda kusitisha Baraka kuufungua mlango wa kuingia ndani kwao.

Baraka alitaka kuhakikisha kile ambacho alikisikia kwenye masikio yake, naam ubongo wake haukumdanganya kwenye kutafsiri sauti ile, ni Mamy ndie alikuwa pembeni yake tena akiwa kwenye mavazi ya shule kama yeye mwenyewe, mshangao wa kuwa pale ulimuandama huku aliyemshangaa akionekana kukosa tabasamu usoni.

"Mamy naomba uniache na urudi shule , siioni maana ya kuendelea kuwepo darasani ikiwa nafsi yangu haina amani kwa kile nilichokifanya, lengo la kusoma ni kuitafuta amani ya kweli, endapo kusoma hakuleti amani faida yake ni nini? Aliuliza Baraka huku mkono wake ukiwa umeshikiliwa na mtoto wa kike na mamaake akiwa bado anaendelea kumwaga mvua ya maneno.

"Aonae nyundo ni silaha basi kila tatizo huliona ni msumari, wewe ni mwanaume na unatakiwa usimame kama mwanaume, ikiwa leo hii huwezi kuitetea haki yako ya msingi unafikiri nani atasimama na wewe? Huruma na amani vinakunyima utulivu wa kuamua kilicho sahihi kwako kulingana na muda! Unafeli mno Baraka" Mamy alimtambia Baraka.

"Upo sahihi kabisa, ila unatakiwa kuwa na mipaka kwenye maamuzi yangu ambayo yananihusu mimi na familia yangu, mamaangu ni kila kitu kwangu na sitaki kabisa nimkwaze, hemu sikia maneno ambayo anayaongelea juu yangu........." Baraka aliongea kwa hasira na kumpa nafasi Mamy asikilize maneno kutoka kwa mamaake.

"Ujinga tu , mimi nateseka usiku na mchana kumhudumia yeye halafu anashindana na mimi? maisha yangu yamekuwa ya ovyo tokea alipoonyesha dalili za kuja dunian! Mimi Sadifa wa kuwa hivi? kumzaa kwenyewe ni bahati mbaya tu! Ataenda kula kwa babaake leo" bi Sadifa aliendelea kubwata asijue kama kijana wake yupo nje.

"Aupendae upinde huupenda na mshale wake Mamy, ona sasa! ingawa mamaangu ana maneno makali juu yangu ila hilo halijawahi kunifanya nimchukie wala kukataa agizo lake, wazazi wako wewe wanakutegemea na ndio maana wamekutengenezea misingi mizuri ya elimu, unawahi darasani, vitabu vya kusomea unavyo , muda mzuri unao, nini tena unataka? Hatuwezi kufanana kamwe Mamy, rudi darasani ukafate wazazi wako walichokuagiza " Baraka aliongea maneno hayo kwa uchungu mno hali iliyomfanya Mamy aanze kutiririsha mvua ya machozi.

"Maneno yako yananiumiza sana Baraka, uwepo wangu hapa ni bora kuliko kuwa darasani , naamini asiyefanya wema ni sawa na afanyaye ubaya Baraka , nitapata wapi amani ya kuendelea kusoma ikiwa ninaefungamana nae haupo! Kauli hizo zilimtoka Mamy machozi yakiwa shavuni mwake.

"Ila kumbuka mimi na wewe tumejuana ukubwani ! Hivi unapata wapi nguvu ya kunichagua tuambatane pamoja , Baraka mimi sio wa aina yako, wewe ni mtu mwengine mwenye maisha yako na mimi nina mfumo wangu wa maisha hivyo kumbuka hatuwezi kulingana kwenye mwendo" Baraka alijitahidi kumuelewesha Mamy bila kuyajali machozi yake.

"Daima nitakumbuka kilicho changu na kisicho changu, naamini kupitia hili sitapata shida maishani mwangu , leo hii nitasimama na wewe na kamwe sitarudi shule bila wewe, sote ni watoto wenye haki sawa bila kujali hali za kiuchumi" Mamy alikazia msimamo wake huku akitumia kiganja chake kujifuta machozi.

Baraka aliuona msimamo wa Mamy juu yake, aliligundua hilo kutokana na maneno na macho ya Mamy ambayo yalidhihirisha upendo uliopo moyoni mwake , Baraka alimjua fika Mamy kuwa hakuwa mtu wa kushindwa hasa pale anapoipigania haki ya mtu, mwisho wa siku aliona sio sahihi matatizo yake yakawa chanzo cha Mamy kukosa vipindi, alikumbuka masaa machache aliyomtoroka na kuja nyumbani kwao na yeye akamfata hukohuko, alimkumbuka na mamaake ambae aliendelea kusema maneno ya ovyo yaliyojaa matusi bila kituo, aliujua vyema mziki wake endapo atawakuta wawili hao pamoja.

" Nimeamini kuwa aogopae jua kali sio chifu, kwa vile niliyabomoa mapema sifikiriii kama napaswa kuyajenga jua likiwa linazama, twende tukasome adhabu yangu nitaikuta tukirudi" Baraka aliongea kijasiri na kumshika mkono Mamy wake kisha safari ya shule ikaanza.

********
Tayari jua liliaga na kuzikaribisha nyota zitawale kwenye anga lililotumika kuwafunika wana JIULIZE ndani ya jiji kuu la TULEANE, ulikuwa ni muda sahihi kwa wanadamu kuzituliza akili zao ambazo walizituma kutwa nzima , lakini wapo ambao usiku huu waliutumia kwa lengo la kwenda kujitafutia riziki kutokana na uhalisia wa kazi zao. Mmmm haya ndio maisha.

Ulikuwa ni muda sahihi kwa familia ya bi Huba na bwana Zahir kujipatia chakula cha usiku wakiwa na binti yao, ukimya ulitawala kwenye ukumbi ule ikiwa ni ishara za kukipatia adabu chakula chao, sauti za vijiko zikigonga sahani ndizo ambazo zilisikika, kwa hakika familia hii iliishi kimaadili mno, uvumilivu ulimshinda bi Huba baada ya kugundua kuwa binti yake hakuwa anakula zaidi ya kugongagonga kijiko kwenye sahani iliyojaa chakula.

"Mamy..... " aliita bi.Huba huku akimuangalia bintie ambae macho yake aliyagandisha kwenye sahani .

"Mamyy.....Mamyyyyy!!! Aliita tena baada ya kuona bado hakukua na muitiko, bi Huba alimgeuzia jicho mumewe ambae na yeye alikuwa makini kuusoma mchezo ule.

"Weeh Mamy si nakuita wewe! una matatizo gani lakini? Bi Huba aliuliza kwa sauti ya hofu huku akijaribu kumshika bega bintie ambae alishtuka.

"Barakaaa....!! Jina hilo lilimtoka Mamy aliposhtuliwa na mamaake.

"Baraka? Aliuliza bwana Zahir kwa mshangao baada ya kulisikia jina la kiume likitoka kinywani mwa bintie.

Macho ya viulizo yalitua kwa zamu kwenye uso wa bintie na mkewe bi Huba, akilini mwake hakukuwa na mtu aliyemfahamu kwa jina hilo na hata kwenye koo zote mbili jina hilo halikuwepo, uoga ulimvaa Mamy baada ya kuona sura ya babaake ikibadilika hata bi Huba aliligundua hilo.

"Nauliza Baraka ndio nani? Aliuliza kwa ukali bwana Zahir baada ya kuona swali lake lilikosa jibu hapo awali.

"Mama anamjua..." alijibu Mamy kwa uoga huku akimtazama mamaake kwa jicho la nitetee.

"Weeh usimtupie paka wa uso mamaako, nimekuuliza wewe Baraka ndio nani? Aliuliza tena bwana Zahir baada ya kuona anazungushwa na bintie.

"Sipendi ujinga utawale kwenye nyumba yangu! Hivi ndio mamaako anavyokulea nikiondoka eeeh...sasa utanitambua.......ITAENDELEAAAAAAA .

Naam mzee Zahir kachachuka mbele ya bintie baada ya kusikia jina Baraka, jee mamaake atasema nini? Hatma ya Baraka juu ya kosa lake bado hatujaijua, unahisi nini kinakwenda kutokea? Usikose sehemu ijayo maana ni ya moto.

◇SEHEMU YA 4◇

"Sipendi ujinga utawale kwenye nyumba yangu! Hivi ndio mamaako anavyokulea nikiondoka eeeh...sasa utanitambua.." aliwaka mzee Zahir huku akijiandaa kumpiga mtoto wake ila alichelewa maana tayari mkono wake ulizuiliwa na bi Huba.

"Mfanye mtoto wako aogope fimbo lakini asiogope mkono wako, Kumpiga au kumfinya mtoto wako kutamfanya mtoto aogope mikono yako ambayo kiuha
lisia ndio ya kumuhudumia" bi Huba alizungumza hayo kwa hisia huku akimvutia bintie akae nyuma yake.

Mamy alikuwa akilia tu , alimuogopa mno babaake maana alizijua hasira zake, alijuta kulitamka jina la Baraka mbele ya babaake ambae hakuwa anataka bintie ajenge mahusiano na wanaume wa ovyo mitaani, tayari aliliona furushi la lawama likimuangukia mamaake , hakutaka kuushuhudia ugomvi huo na haraka mno alihesabu hatua za haraka kuelekea usawa wa chumba chake na kujifungia akilia.

"Ulitaka nifanye nini Huba? Nimchekee ili mwisho wa siku tumwage machozi! Asipoadhibiwa huyu atazowea" alifoka mzee Zahir huku akitaka kumfuata bintie chumbani ila bi Huba alimzibia njia.

" Simaanishi hivo mume wangu ila endapo mtoto anakosea basi mjengee ujasiri wa kukukaribia kwa kujua kuwa mikono yako ni salama, lakini kama huwa unamwadhibu kwa mikono yako basi hatasikia wala kuona usalama mikononi mwako na mwisho wa siku atakuogopa hata kama hakuna fimbo mikononi mwako" maneno ya bi Huba kidogo yalituliza hasira za bwana Zahir.

"Ila sio kulisikia jina la kiume likitamkwa mbele yangu, tena eti mtoto anakosa hamu ya kula kwa sababu ya ujinga huu, nyinyi ndio mnaongoza kuwaharibu watoto" lawama kutoka kwa bwana Zahir zilihamia kwa mkewe.

"Tukiwa kama wazazi ni lazima tuelewe hisia za mtoto wetu katika maswala mbalimbali anayokutana nayo ili tuweze kumsaidia kihisia. Sisi tusiwe watu wa kwanza kuumiza hisia zake, bali tuwe watu wa kuzirejesha hisia zake katika hali yake ya kawaida. Tukijua mtoto wetu anajisikiaje basi tutaelewa nini cha kufanya" bi Huba alitoa darasa huru kwa mumewe ambae alionekana kutulia akisikilizia.

"Ila kweli binti yangu sikumzowea kuwa hivi kabisa inawezekana kuna kitu kinamsumbua" aliropoka bwana Zahir huku akionekana kutafakari kitu.

"Na hapo ndipo unapotakiwa umakini, sisi kama wazazi ni lazima tuzijue hisia za mtoto wetu na kisha tuwe karibu naye kwa upendo ili kumsaidia. Kuna wakati mtoto anajisikia mpweke lakini mzazi hajali kabisa, anajisikia duni, mnyonge na dhaifu awapo mbele za watoto wenzake lakini mzazi hajali kabisa na pengine ndiye anayesababisha mtoto wake ajisikie hivyo, bila shaka mtoto huyu hatakuwa na chembe ya ujasiri maishani mwake" alimalizia bi Huba na kumwangalia mumewe ambae alikua makini kumsikiliza.

"Nimekuelewa vyema mke wangu ila yote haya umeyajuaje?

"Baraka ni miongoni mwa watoto ambao wana sifa nilizotaja hapo juu" aliongea kwa ufupi mno bi Huba.

"Wewe umemjuwaje! Ina maana kweli unafahamu kinachoendelea kati yao? Bwana Zahir alionyesha hamu ya kutaka kujua yale asiyoyajua.

"Ndio. Namjua vyema kupitia Mamy, Baraka ni mtoto ambae kabebeshwa hatia isiyomuhusu, hatia ambayo sidhani kama itakwenda kuamua hatma njema ya maisha yake"

"Mmh kwanini iwe hivyo? Alizidi kudadisi bwana Zahir.

"Simlaumu Mamy kuwa kama alivyo saivi kwa sababu hapendi na anayachukia maisha anayoishi Baraka, yanamuumiza mno! Nafikiria namna ya kumsaidia kama ambavyo yeye mwenyewe Mamy kataka, Baraka ana safari kubwa ya maisha iliyokosa muongozaji, Baraka ni hodari mno shuleni ila huzuni , unyonge na hali duni ya maisha zimeficha uhodari wake" bi Huba machozi yalimtoka alipoongelea habari za Baraka.

"Nyamaza kulia mke wangu! Natamani kumjua Baraka zaidi , subiri nimfuate binti yangu nina imani hatonificha kitu" bwana Zahir aliongea hayo huku akipiga hatua mbele ila alizuiliwa tena na mkewe.

"Mbora ni yule awezaye kukaa pweke faraghani huku akitafakari yanayomkabili, muache mtoto mume wangu " maneno ya bi Huba yalimstaajabisha bwana Zahir.

"Nimuache ili iweje? Mtoto ulimuona alivyoondoka! Hatujui yupo kwenye hali gani mke wangu" aliongea bwana Zahir kwa hofu huku akimshangaa mkewe kumzuia.

"Hakuna aliyekosa furaha kwa kutojua nani anafikiri nini, bali wale waliokosa kujua wanafikiri nini akili mwao ndio wasio na furaha, nina imani na binti yangu hata kama analia ila najua ananiamini na ndio maana alitaka nikueleze kuhusu Baraka kwa hiyo hili tutamalizana mimi na yeye na msaada wako ukihitajika nitakwambia" bi Huba alimtoa hofu mumewe.

Mzee Zahir alikubali japo kishingo upande. Familia iliamua kuyavalia njuga maisha ya Baraka ili asiendelee kudidimia kwenye shimo la msongo wa mawazo, Mamy na yeye hasira zake zilimtuma alie hadi pale usingizi ulipoamua kumchukua.

*********
Siku zote mwenda tezi na omo kurejea ngamani ni lazima jirani, tayari ilikua ni majira ya saa mbili usiku, Baraka alionekana akinyatia kufungua mlango na kuingia ndani ya nyumba yao, mwangaza mdogo wa kibatari kilichokuwepo kwenye sebule yao ndogo ulimfanikisha aone pazia zito lililotumika kama stara ya chumba chake licha ya kuwa na viraka kila kona, taratibu alilivuta na kufanikiwa kulifungua ila alishtukia akikaribishwa na kofi zito lililotua shavuni mwake. Hata hakuwa amekaa vyema aliongezwa na ngumi iliyoweka makazi mgongoni mwake, uvumilivu ulimshinda na kutoa kilio cha uchungu.

"Aaah mama naumiaaaaa! Alilalamika Baraka huku akiugulia maumivu kwa kushika shavu na mkono mwengine mgongoni.

"Una maumivu kama niliyoyapata wakati wa kujifungua kwako! Mtoto huna aibu wala hubebeki kabisaa" bi Sadifa aliwaka huku akianza kumpiga tena.

Kipigo cha paka mwizi kilichosindikizwa kwa maneno makali kilimshukia Baraka. Usiku ule kwake haukuwa ni mapumziko bali ulikuwa ni wa mateso na maumivu , alivumilia mno kipigo cha mamaake ila mwisho wa siku alijiona atakufa mikononi kwa mamaake na kumuachia kesi ya mauaji, hakutaka hilo litokee na ndio maana alijichagulia kulala nje kwa siku hiyo.

"Na usirudi humu mbwa wee! Mtoto kama nimekuomba mzimuni, huna faida zaidi ya hasara tupu!! Ndio maana mnatupwa majalalani kwa kuhofia mambo kama haya, na usirudi utatafuta kwa kwenda kenge wewee" bi Sadifa alimsindikiza vyema Baraka aliekimbia kipigo.

Mbio zake Baraka ziliishia kwenye mti mkubwa wa muembe uliokuwa kama hatua thelasini kutoka nyumba ya kwao, aliamua kukaa hapo huku akiugulia maumivu yaliyomvaa mwilini mwake, machozi ndiyo yalikuwa rafiki kwa muda huo huku mbu waliojali maumivu yake wakimuimbia mashairi mazuri masikioni mwake ila hawakujua kama yalizidisha maumivu mwilini mwake.

"Aaagh!! kwanini Mungu ulinileta kwenye ulimwengu huu wenye majaribu kiasi hiki? Tuseme mamaangu hakusikia uchungu ule wanaosikia wazazi wengine wakati wa kujifungua ? Mbona mateso yamezidi juu yangu tokea siku ya kwanza kukaribishwa ulimwenguni? Nimemkosea nini mama? " Baraka alijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.

Viganja vyake vya mikono alivitumia kama ni mto wa kuegeshea kichwa chake, mwili wake aliamua kuuweka juu ya ardhi akiamini kwa siku ile ndio mkeka wake, mbu waliomsumbua aliwaacha wajipatie riziki yao kwa siku ile kwa maana mwili wake aliusadakia , usalama wa maisha yake aliukabidhisha kwa Mungu akiamini yeye ndie atamsitiri kama alivyokuwa tumboni kwa mamaake, taratibu usingizi uliokumbwa na huzuni ulioambatana na upweke ulimvaa Baraka .

Bi Sadifa yeye aliendelea kubwata, kamwe hakuujali usalama wa mtoto wake , ndio kwanza alianza kutafuta mabeseni yake ya unga wa maandazi na kuanza kuukanda.

"Yaani mimi niteseke mtu yeye afurahie maisha na wanawake wengine. Kuna mbegu nyengine kuzilea kazi wallahi...." kabla hajamalizia maneno yake alishtushwa na ugongaji wa mlango wake ambao tayari alifunga kwa ndani ili baraka asiingie.

"Nikiinuka hapa na nikigundua kama ni wewe Baraka basi nitakuua, tafadhali ondoka nakwambia na ulale kwa hao wanaokupa jeuri " alifoka bi Sadifa ila mgongaji hakuongea lolote zaidi ya kuendelea kugonga.

Bi Sadifa aliinuka na kigongo chake cha kusukumia maandazi, tayari alijiandaa kumkabili Baraka endapo angemkuta mlangoni, maneno mabaya juu ya kijana wake hakuacha kuyatamka hadi pale alipofanikiwa kuufungua mlango, macho yalimtoka baada ya kushuhudia sura ya..............ITAENDELEAAAAAAA

Nani huyo mlangoni kwa bi Sadifa ? Wazazi wa Mamy watamsaidia vipi Baraka. Usiku wa Baraka akiwa nje ya nyumba yao utakuwaje? Usikose sehemu ijayo maana mambo ni moto.
 
Jirani ukimaliza utanisimulia kwa voice WhatsApp 😹
Uwe live leo nakutolea kitu hapa weekend nilikuwa na adhabu so sikufanya kitu utangulizi
 

Attachments

  • IMG_0286.jpeg
    IMG_0286.jpeg
    850.5 KB · Views: 2
Back
Top Bottom