*******
◇ Sehemu ya 19 ◇
Muda wa pumzi za kijana Baraka kutamba kwenye sayari ya dunia ulifikia tamati, alitulia tuli huku mkono wake mmoja ukiwa umeshikamana na mkono wa Mamy, uso wa Mamy tayari ulivimba kwa kilio cha kimyakimya , maumivu ambayo aliyasikia yalikua hayana mfano, alihangaika kumuamsha Baraka ambae tayari pumzi ilikata , aliamua kupeleka macho yake pembeni ili aubadilishe ukweli ila alikutana na kitu ambacho kilimshangaza .
Hakujali kabisa uwepo wa watu waliokua nyuma yake, ila alichokifanya yeye ni kutaka kuhakikisha kile ambacho amekiona, alijitahidi kuusogeza mkono wake hadi sehemu ambayo kulikua na stuli chakavu iliyoanguka huku madaftari mengi yakiwa pembeni pamoja na mapande ya viyoo , hapo ndio aligundua kua mshindo ambao waliusikia ulitokana na anachokiona , kwa umakini huku mikono yake ikitetema aliinyanyua karatasi ambayo ilikua juu ya madaftari huku vioo vidogo vidogo vikiwa juu yake, maandishi makubwa juu yaliyokolezewa wino wa rangi nyekundu yalisomeka BARUA KWA MAMA yalimstaajabisha, Mmh ...BARUA KWA MAMA ? Alijiuliza Mamy nafsini mwake.
Aliitazama vyema karatasi ile na kujihakikishia kua ule ulikua ni mwandiko wa kipenzi chake, hakuona vyema ujumbe ule kuusoma yeye ikiwa mlengwa alikuwepo, kwa hatua za kiuchovu alimsogelea bi.Sadifa ambae muda huo alijiinamia akilia, Mamy alichuchumaa na kumshika bega.
"Mama, nadhani haya ni mavuno ya kile ambacho tulikipanda na kukipalilia siku za nyuma, hatupaswi kulia kwa maana machozi hayana msaada tena , bila ya shaka huu ni ujumbe wako" Mamy alizungumza kwa hisia na upole , alimkabidhi mama Baraka karatasi ambayo hakuna ambae alijua kilichoandikwa , kwa mwendo wa maumivu na uchovu Mamy alijikokota na kutoka kwenye chumba kile.
Bi Sadifa alilia baada ya kuona maandishi makubwa juu ya karatasi ile, hata maneno ya Mamy yalimchoma kiasi ambacho alishindwa kuisoma na kubaki nayo mkononi, alimtazama Mamy ambae alikua anaishia kutoka nje, kwa muda ule hakuna aliyethubutu kumwambia chochote zaidi ya mamaake bi.Huba kumfuata nyuma.
Mume wa mwalimu Swami na yeye aliikimbia aibu , tokea watu walipoingia chumbani kwa Baraka yeye tayari alikula nyayo, ingawa mwalimu Swami alikua na maumivu ya kumfumania mumewe ila hayakufikia maumivu ya kifo cha mwanafunzi wake Baraka, aliumia kuona mtaji mkubwa ambao ungezalisha biashara yenye tija mbeleni umejifilisi , mwalimu Swami alimsogelea bi. Sadifa aliyekua akilia huku karatasi ikiwa mkononi mwake , Ndaze na Masha walikua pembeni wakichukua kila hatua za tukio .....kwao wao ilikua ni furaha kuona adui yao akiteseka.
"Sadifa , sifikirii kama unapaswa kumwaga machozi kiasi hiki, wewe muda huu unatakiwa ufurahi kwa vile hiki kiumbe hakitashuhudia maovu yako tena, najua kuwa hata ule uchungu wa kufiliwa na mtoto basi huna kabisa ila tu unajitafuta, Sadifa...hii laana haitakuacha salama, umepoteza taa ambayo ingekusaidia vyema kumurika siku za mbele, kwaheri" mwalimu Swami aliongea hayo huku machozi yakimtoka , hakuona sababu ya kubaki pale hivyo alitafuta njia mikono yake ikiishia kufuta machozi.
"Mpanda ovyo hula ovyo" hii ilikua ni kauli iliyotamkwa kwa dharau kutoka kwa Masha .
" Ulisahau kua dunia ni mti mkavu na kiumbe hupaswi kuuelemea hata kidogo , umelikoroga Sadifa jiandae kulinywa" Ndase na yeye hakua nyuma kutoa ya moyoni, alipomaliza alimshika mkono shogaake na wao wakatoka nje huku wakicheka.
Sadifa alilia kama mtoto baada ya kuona kila mtu aliondoka, alisikitika kuona akibaki pekee kwenye jambo zito kama hilo, kila alipotaka kumtazama kijana wake nafsi yake ilimsuta, aliishia kutazama barua ambayo ilikua mkononi mwake, nguvu za kusoma hakua nazo angewezaje ? alihisi kuwehuka hadi kufikia hatua ya kupiga kelele ambazo zilikwenda kuwashtua majirani.
Nadhani mnaijua vyema Jiulize kwa hekaheka yaani kelele moja tu ya bi .Sadifa ilikijaza chumba cha Baraka kwa umati wa watu , walioshika na kutikisha vichwa vyao kwa huzuni walikuwepo , hata wale ambao waliziba midomo yao kwa viganja vya mikono pia walijaa, haikushangaza wengine nyuso zao kuonekana kujaa nuru ya tabasamu, kila mmoja na namna yake alivyochukulia tukio lile .
Bi Mwinde aliusogelea mwili wa Baraka na kuustiri kwa kitenge chake ambacho alikifungua kichwani kwake , kile kisu ambacho kilizama tumboni hakuthubutu kukishika, baada ya hapo alimsogelea bi Sadifa ambae hadi muda huo hakuna aliyekwenda kumpa maneno ya faraja zaidi ya lawama, alimtazama kwa jicho kali huku ndita zikijengeka usoni mwake.
" Wapiganapo fahari wawili ziumiazo ni nyasi, Sadifa nilikwambia mapema kuhusu hili ila ulidharau, ona leo hii kilichotokea hata ulimwengu wenyewe unakucheka , unashindwa hata kumtazama eeeh? Nitamzika Baraka kwa vile nilimpokea wakati wa kuja duniani " bi Mwinde aliongea kwa uchungu na hasira huku akitoa simu kumpigia Mwenyekiti wa mtaa.
"Najua ulimwengu na vilivyomo vinanilaani ila ningefanya nini? Yote haya kayataka Mshirazi........" Bi Sadifa alitamani kujitetea ila aliishia njiani kwa kilio.
"Sadifa......Siku zote nakwambia ya kwamba kila mtu dunia hii huyaharibu maisha yake kwa mikonoye , hukutakiwa kabisa kumfikiria yule aliyekuangusha ila ulitakiwa uangalie nini ambacho alikuachia, Baraka umemkatisha ndoto zake, Baraka umemkosesha haki zake za msingi nyingi mno, Baraka umemuumiza na Baraka huyuhuyu umemuua kwa tabia zako" alilalamika bi Mwinde machozi yakimtoka.
"Niueni na mimi? Niue bi Mwinde? Kwanini lawama zote kwangu? Mnakijua alichonifanyia Mshirazi? Yeye ndie sababu ya yote haya.... " alilalamika bi Sadifa huku akilia kwa hasira.
"Sitakuua mimi Sadifa ila matendo yako ndio yataamua khatma ya maisha yako, hukupaswa kuyakumbatia na kuyaweka kifuani yale yaliyokuumiza badala yake ulitakiwa kuyashusha na kuyafukia kabisa, siku zote makosa ndio hutufunza mwananguu!!" Bi Mwinde alizidi kutoa lawama.
Bi. Sadifa alizidi kulia kama mtoto kutokana lawama za bi. Mwinde, ghafla simu ya bi Mwinde iliita na kumfanya atoke nje , bi .Sadifa aliitumianafasi hiyo kusota kwa tabu hadi alipoufikia mwili wa Baraka, hata kama ulifunikwa ila aliutazama kwa masikitiko na kuanza kuikunjua karatasi ambayo ilikua mikononi mwake, kishingo upande alianza kusoma maandishi ambayo yaliandikwa.
BARUA KWA MAMA.
Mama..
Wino na karatasi havitoshi kueleza yale machungu ninayohisi moyoni mwangu ila wacha nijaribu kuyaeleza kwa uchache , machozi yangu yaangukayo humu yatatosha kukuonyesha jinsi gani naumia kuandika haya, naelewa kua hukuwahi kunipenda tokea pale nilipoonyesha dalili za kuja duniani ila hukua na njia kwa vile Mungu mwenyewe kataka iwe.
Niliumia kuona watoto wenzangu wakiwa wenye furaha na wazazi wao, uliniachia kiulizo...kwanini isiwe mimi? Sio wewe mamaangu wala yule nisiyemtambua hadi kufa kwangu, yawezekana ungenikutanisha au kunieleza chochote kuhusu yeye basi ingepunguza robo ya kiu yangu, Mama....ingawa sioni ladha ya utamu kila nitamkapo jina hili ila sikuacha kukuita, watoto wenzangu wananidharau sababu ikiwa ni matendo yako kwangu na kwa jamii iliyokuzunguka.
Nilitamani niwe mbele yako nikuelezae haya ila hukuwahi kunipa hiyo nafasi, na hiyo nafasi ningeipata saa ngapi ikiwa masikio na mdomo wako vimezowea kunitamkia maneno makali yenye kuchoma, mama kama ni furaha basi leo unatakiwa kufurahi maana naondoka kwenye sayari hii, hukuwahi kunipa nafasi ya kua mtoto wako ila ulinifanya kua mtu baki ambae sikuwa na msaada wowote kwako, achilia msaada hata ile thamani ya utoto kwako pia sikuona kabisa.
Mama nakuachia ulimwengu wako, tamba uwezavyo , nimechoka kuwekwa lawamani, nimechoka kushuhudia matendo yako, nimechoka kudharauliwa na kutukanwa. Ukitaka nipumzike kwa amani waeleze wana Jiulize kilichokufanya ukawa na maisha haya.
Ikikupendeza pia ....mpe salamu zangu Mamy mwambie NAMPENDA ❤️........itaendeleaaaaaa
Naam hii ndio barua aliyoacha Baraka kwenda kwa mamaake, jee? Bi Sadifa atawaambia wana Jiulize kilichomfanya kuwa alivyo? Tukutane sehemu ya mwisho ya simulizi hii.
◇ Sehemu ya 20 ◇
Aliporudi tu aliamua kujifungia chumbani kwake na kulia kwa sauti, hata baba yake alimshangaa maana alimpita ukumbini bila kumsemesha chochote, kwa vile yeye alifika mwanzo kabla ya mamaake basi hakutaka kuzungumza na yeyote , dakika chache bi Huba na yeye alifika akiwa haihai hali ambayo ilizidi kumchanganya babaake Mamy, wote walikisogelea chumba cha binti yao na kuanza kugonga mlango bila mafanikio yoyote, ni sauti ya kilio pekee ndio walifanikiwa kuisikia.
"Kuna nini? Mbona siwaelewi!! Aliuliza babaake Mamy kwa hofu huku akimtazama mkewe aliyeonekana kuchanganyikiwa, hakupewa jibu lililoeleweka hali ambayo ilimzidishia wasiwasi.
Ilipita robo saa nzima chumba kikiwa kimya hata kilio kama kile cha awali hawakusikia, hofu juu ya binti yao iliongezeka , lakini kwa vile walikua pembeni ya mlango basi waliamua kugonga tena ila hakuna walichoambulia zaidi ya ukimya , juhudi na maneno mazuri yenye ushawishi ziligonga mwamba hadi kufikia uamuzi ya kuvunjwa mlango.
Sauti ya kilio kikali kutoka kwa mama mzazi ndio ilisikika, kwa mwendo wa haraka mikono ikiwa mdomoni alimfuata Mamy aliyekua chini huku mapovu yakimtoka mdomoni na kifungashio chenye picha ya panya kikiwa kando yake, muonekamo wake ulidhihirisha kua roho yake tayari iliachana na kiwiliwili, hakua na nguvu ya kulia tena zaidi ya kutulia tuli kama sanamu lililokosa mteja huku machozi yakimtiririka.
Baba wa Mamy alimtazama kwa uchungu bintie ambae hakuonyesha dalili za uhai, roho ilimuuma kuona mtoto wake wa pekee akipoteza uhai kwa namna ile, viulizo vingi vilikua kichwani mwake asijue nini kimemfika mwanawe, alimsogelea na kumkumbatia mkewe ili watiane ujasiri wa kukabiliana na kile ambacho wanakiona, hawakutamani iwe hata ndoto maana sio tukio zuri, alijaribu kumtazama na kumchunguza bintie kwa mara nyingine pengine kunaweza kua na mabadiliko ila alibahatika kuona karatasi ambayo bila shaka ilikua na ujumbe, taratibu aliichukua huku mikono ikitetema na jasho jembamba la vidole likimtoka.
KWENU WAZAZI...
Mnisamehe kwa hili licha ya kwamba litawaumiza, kama ndege wafananao hutua tawi moja basi naamini huu ni mti ambao tumeuchagua mimi na Baraka, yawezekana mti huu ukawa na kivuli kitakachotufanya tupumzike kwa amani, naamini pia tutakua na maisha bora zaidi ya haya tuliyoyaishi hapa, hata ndoto zetu naamini tutazitimiza kwa maana tulikua na imani sawa, siwezi kusoma bila uwepo wa Baraka na wala siwezi kupiga hatua yoyote pasipo na Baraka.
Najua kwamba mlinipenda sana wazazi wangu na kila ambacho nilikitaka mulinipa kwa wakati , ila hamkufanikiwa kunitendea jambo moja tu, hili jambo ndio limewapeleka mukanikosa leo hii, WAZAZI WANGU hamkuziheshimu hisia zangu wala hamkuwahi kulitilia maanani lile lililonitatiza....au ndio tunaishi kwenye dunia ya KILA MTU ABEBE MSALABA WAKE? Na ile zama ya MTOTO WA MWENZIO NI WAKO tukaifukia ardhini! Imeniumiza mno na moyo wangu haukuridhishwa na maamuzi ya Baraka na hii yote imetokana na jamii yetu jinsi inavyotuchukulia sisi watoto.
Kama kizuri kinaundwa basi naamini matendo ya mama Baraka yangebadilika, Kila kitu kina chimbuko lake hatukutakiwa kumhukumu hadi kizazi chake, hata wewe MAMA mwishoni ulidiriki kunivua imani uliyonivisha miaka mingi, uliwaamini wao kuliko mimi mwanao? Uliwasikiliza wao kuliko mimi? Unakijua alichokitaka mwalimu Mkandarasi kwangu? Mmmmh sina mengi nawaachia JIULIZE yenu iliyojaa uozo .
Mamy Baraka..... ❤️
"Mke wangu nilikwambia zamani kuhusu huyu mtoto ona sasa....tumempoteza kwa uzembe wako , kwanini mambo yote haya yanatokea unakua kimya? Ona sasa ...faida yake nini? huyu mwalimu Mkandarasi kafanya nini kwa binti yangu? Aliuliza baba wa Mamy kwa hasira.
Bi.Huba alibaki kulia asijue cha kujibu baada ya kuona hasira za wazi kwa mumewe, alitamani kusema kitu ila mdomo bado ulikua mzito mno, machozi ndio ambayo yalizungumza kile anachokisikia moyoni mwake, hata mumewe aligundua hilo ila hakua na cha kufanya.
***************
Kama hatua ndefu hutumika kufupisha mwendo basi Baraka na Mamy waliamua kuyafupisha maisha yao, familia ya Mamy ililazimika kuungana na familia ya Baraka lengo ikiwa ni kukienzi kile ambacho watoto wao walikiacha. Wote wawili walizikwa sehemu moja na kila ambae alifika msibani kwao basi hakuacha kuangusha chozi. Ilihuzunisha ila hakuwepo ambae angekua na uwezo wa kubadili ukweli.
Baada ya mazishi kumalizika Sadifa aliomba muda wa kuzungumza machache kabla ya watu kutawanyika, kila mmoja masikio yake aliyategesha kwa lengo la kutaka kusikia nini kitakachosemwa, hii aliifanya kwa lengo la kutimiza alichotakiwa kufanya na kijana wake.
"Najua nimewakosea wengi Jiulize hii, hata wale niliowaumiza na kuwavunja moyo ni wengi ila kamwe hamkunilipa ubaya , wote mumeungana na mimi kumstiri mwanangu, Nimejifunza kua ubaya haulipwi kwa ubaya japo kua sikulitilia maanani hapo mwanzo na haya ndio madhara yake, sikupaswa kumchukia na kumkomoa kijana wangu Baraka sababu ikiwa ni matendo ya uovu kwa babaake, alinitendea mengi Mshirazi......." aliongea Sadifa kwa upole na kusita kidogo kuacha machozi yaanguke, hata watu wa Jiulize walisimamisha masikio yao ili wasipitwe na neno.
"Nadhani wengi wenu hakuna asiyemjua Mshirazi, ingawa alikuja kama Mkandarasi wa soko kuu la Jiulize ila mapenzi kati yetu yaliingilia kazi yake, sikutazama alipotoka wala ukoo wake ila niliangalia uzuri na maokoto, mazima nilizama na kujiachia kwake, Mshirazi alinipa kila nilichotaka tena kwa wakati sahihi, Jiulize hii ndio ilimbadilisha Mshirazi wangu maana baada yamimi kuonekana nang'aa basi na wengine walitamani, badala ya kuwa wangu Mshirazi alikua pata sote, tuligombana kiasi ambacho ilipelekea kuachana, hakuniacha mtupu ila aniachia ....." kilio ndio kilisitisha simulizi ya bi.Sadifa na kufanya wengine wabaki wakimtazama.
" Siku ya mwanzo kujigundua kua ni mjamzito nilifurahi mno, nilifurahi baada ya kuona nakwenda kuongeza familia baada ya wazazi wangu kufariki, niliamini kua hii ni Baraka , hata sikumchukia Mshirazi maana nilikua nampenda sana hivyo niliamini kaniachia kumbukumbu tamu mbeleni, sikuamini mimi sikuamini........kumbe Mshirazi alianiachia gonjwa hatari , ugonjwa ambao ulikwenda kuibomoa furaha yangu na kuijenga chuki moyoni mwangu......" kilio chake kilichobeba kwikwi kilizidi kuwaumiza waliokua wanamsikiliza .
"Chuki yangu na Baraka ilianzia hapa, nilijaribu mara nyingi kuuharibu ujauzito wake ila uligoma , hata nilipomzaa nilitaka kumdhuru ila bi.Mwinde alimsogelea na kumkinga, ilipita mwezi sikuwa nimempa jina ila bi.Mwinde alimpatia jina la Baraka, Mshirazi kayaharibu maisha yangu,Jiulize ilinipeperushia furaha yangu kwanini na wao nisiwaumize? Nilijiapiza na nyinyi lazima muumie, nisameheni kwa kuwaenezea ugonjwa, hata ukaribu wa Mamy na Baraka sikuutaka kwa sababu niliona mwenyewe namna ambavyo Mamy alimpenda kwa dhati Baraka, nihukumuni ikiwa mnahisi kuna adhabu inanifaa" alimalizia bi Sadifa huku mtandio wake wote ukirowana machozi na kamasi.
Kila aliyejijua mumewe au mwanaume wake kaangukia mikononi mwa bi Sadifa basi alilia kwa uchungu, mwalimu Swami, Ndaze na wengine wengi walibaki wakigaragara chini na kumlaani vilivyo bi.Sadifa, walikua wanaamini kuwa kivyovyote vile na wao wameathirika, makaburini palikua hapatoshi, kumbe Mkandarasi alikiwa pembeni bwana! Hata yeye alijikuta akiumia maana aliwahi kutembea na bi.Sadifa bila kutumia kinga yoyote , mamaake Mamy alibahatika kumuona mwalimu Mkandarasi akiwa kwenye sura ya taharuki, kwa hasira alimsogelea na kuanza kumkunja huku akimtupia maneno.
"Mwalimu mpumbavu sana wewe!! Hivi unajua jamii na serikali yetu inakuaminii kiasi gani? Kwanini umeondoa vazi la heshima ambalo umevishwa, bila ya shaka hii simulizi ya Sadifa imekugusa eeeh!! Sijui umetembea na wanafunzi wangapi ila najua umeharibu sana....chuki yako kimahusiano ndio imesababisha nishindwe kuwa upande wa mwanangu...aaaaagggh" alilalamika na kulia mamaake Mamy huku bado akiwa kamshikilia shati mwalimu Mkandarasi na kumtikisa.
Hata baba mzazi wa Mamy alimsogelea na kuanza kumtupia lawama, alimtaka akiri hadharani makosa yake kabla hawajaamua kumuadhibu, Angefanya nini mwalimu wa watu? Aliweka bayana kila uovu alioufanya kwa wanafunzi wake, alikubali pia alikua mbioni kumvaa Mamy ambae alikua mgumu. Alikiri kila uovu na njia alizotumia kumuweka matatani Baraka, mwisho aliwataka wanafunzi wa kike wakachunguzwe afya zao ili wazijue hali zao, wanafunzi wengi ambao walihudhuria mazishi walilia baada ya kusikia hayo.
Kwa vile mwenyekiti akikuwepo basi alipiga simu polisi na mwalimu Mkandarasi akawekwa chini ya ulinzi. Kesi dhidi yake ilifunguliwa, ushahidi ulikusanywa kwa wanafunzi wengi ma kuhukumiwa kifungo cha maisha.
Kila siku zilivyosogea ndivyo hali ya bi.Sadifa ilizidi kudumaa, hakua na mpangilio mzuri wa kula wala kufanya chochote, kifo cha Mamy na Baraka kilimuumiza sana , mwisho wa siku mawazo yalimuandana na kuamua kujiua kwa kujichoma kisu na kuacha ujumbe ambao ulisomeka👇
KWENU WAZAZI:
NI JUKUMU LETU SOTE KUWALINDA NA KUWATUNZA WATOTO WETU, WANAPITIA MAMBO MENGI MAZITO WAKIWA SHULENI NA MITAANI, VITA KATI YA MAMA NA BABA AU FAMILIA VISIMHUKUMU MTOTO.TUWATUNZE MAANA WAO NDIO HAZINA YETU.
MWISHO..