Mama yangu kaniumiza sikutegemea

Mama yangu kaniumiza sikutegemea

*******

◇SEHEMU YA 5◇

Bi Sadifa aliinuka na kigongo chake cha kusukumia maandazi, tayari alijiandaa kumkabili Baraka endapo angemkuta mlangoni, maneno mabaya juu ya kijana wake hakuacha kuyatamka hadi pale alipofanikiwa kuufungua mlango, macho yalimtoka baada ya kushuhudia sura ya bi.Mwinde ikiwa mbele yake, macho yalimtoka na sura ya kuchukiwa akiijenga mbele ya mgeni wake.

"Ehee kilichokuleta usiku wote huu ni nini kama sio uchawi? Halafu unapenda sana kufatilia maisha yangu eeh" Aliuliza Sadifa akiwa na kifimbo chake mkononi.

"Mmh! pumzi zinakuhadaa mno kiasi ya kwamba unasahau tulivyoishi ila hicho sio kilichonileta, Nimekuja tena tuongee kuhusu Baraka , ipo siku utampoteza mtoto wako kwa uzembe wako mwenyewe, mikono sio kazi yake hiyo na hasa kwa mzazi" bi Mwinde aliamua kufunguka na kulifunika neno la uchawi ambalo lilimuumiza moyoni mwake.

"Heheehhee kwa hiyo unaniadhibu kwa wema wako? sijawahi kusikia kama mikono ina kazi maalumu, eti hemu niambie kumbe mikono hii ifanye nini kwa Baraka " aliuliza Sadifa kwa dharau huku akicheka na kuikagua mikono yake.

"Unakosea sana kuitumia mikono kumuadhibu mtoto, mikono kazi yake ni kuonyesha upendo kwa kumkumbatia, kumshika , kumzawadia na kumfuta machozi pale ambapo anaumia" bi Mwinde alishusha darasa .

"Nisikilize bi .Mwinde hizo zilikuwa ni zama zenu , zama hizi akili za watoto wetu unadhani zinajengwa hivo? Nitampiga na nitamwambia chochote ninachojisikia kama nilimbeba miezi tisa tumboni mwangu, eti afanye kosa nianze kumbembeleza labda sio Sadifa mimi" alitamba huku akiwa na kigongo chake mkononi.

" Ulimwengu haujawahi kubadilika ila walimwengu wenyewe ndio tumebadilika, kupiga kelele kamwe hakufanyi kazi inapokuja nidhamu ya mtoto wako , badala ya kumpigia kelele mtoto wako mfanye ajitegemee mwenyewe kuwa ni sawa kufanya makosa lakini pia ni muhimu kujifunza kutoka kwake na kuwa mtu bora.Watoto hawana hatia kabisa na wanaweza kufinyangwa kwa urahisi jinsi unavyotaka wawe, badala ya kuwakemea, ni bora kuelezea tofauti kati ya tabia nzuri na mbaya kwa njia ya adabu..." bi Mwinde alizidi kutoa elimu .

"Nitatumia mikono yangu na mdomo wangu kumuadhibu mwanangu, sitaki kupangiwa namna ya kulea, kama unamuonea huruma nenda kamfuate umlee wewe" bi Sadifa alizidi kuchachamaa na msimamo wake.

"Mdomo ungekua kisu tayari ungelikata moyo wake, unamuumiza kiakili mtoto na ipo siku utajutia unayoyafanya na kutamani siku zirudi nyuma ili ufanye haya niliyokwambia" bi.Mwinde aliongea hayo na kuondoka huku akimuacha Sadifa mlangoni .

"Umasikini ni mama wa jinai na ndie ambae amenikokota huku nilipo, nina hasira na dunia kama vile dunia inajali baasi, maisha yangu ni yangu hivyo nitaishi kwenye mifumo yangu , baasi " aliongea kwa hasira na kuufunga mlango wake.

Alifanya kazi zake za kuandaa vitafunwa vyake hadi alipomaliza ilikuwa tayari ni saa 5 za usiku, vilibaki vitumbua ambavyo angewahi kuvichoma mapema alfajiri ili wateja wake wavipate vya moto, moyo wa huruma ulimuingia alipogundua kuwa tayari usiku ulikuwa mkubwa na kijana wake hakuonekana kurudi, alimhofia mtoto wake na wahuni wa mtaani walioshindikana, mbu waliousumbua mtaa ule na wadudu wadogo wakali pia walimjia akilini mwake.

"Baraka kwanini umekuja kwenye maisha yangu? unanipa wakati mgumu mno na unanifanya nifanye mambo ambayo wengi yanawashangaza" aliongea hayo huku akianza kutoka zake nje kwenda kumtafuta mtoto wake.

Hatua zake chache zilizosaidiwa na mwanga hafifu wa simu yake ndogo zilifanikisha kuuona mwili ambao ulilala chini ya mti wa muembe ukiwa kwenye sare za shule , mlalaji alionekana kulala fofofo ila hakuacha kujipiga mbu waliokua wanausumbua mwili wake, alitia huruma hali iliyomfanya bi Sadifa ashindwe kuzuia hisia zake na kuanza kumuamsha kwa kutumia mikono yake.

Alishtuka mno na kwa uoga Baraka alifikicha macho yake ili kuona ni nani ambae aliamua kumtoa kwenye bahari ya usingizi , sura ya mamaake ilikuwa mbele yake, uoga ulioambatana na hofu ulimvaa na kuanza kurudi nyuma kwa kutumia makalio na mikono yake.

"Mamaa usiniue mamaa!!! Alilalama baraka maneno yaliyokwenda kuumiza moyo wa mamaake.

"Sina lengo hilo mwanangu! Usiniogope! Baraka mwanangu nisamehe mimi kwa kukuleta kwenye dunia ambayo unajuta kuiona......" bi Sadifa aliamua kumtoa hofu mtoto wake ila bado haikumfanya amuamini mamaake.

"Mamaaaa!!!! Aliita Baraka kwa upole na uoga machozi yakimtoka.

"Naam mwanangu " muitiko huo uliambatana na kumbatio zito hali iliyomfanya Baraka azidishe kilio.

"NAKUPENDA sana mama, nakuahidi kuwa mtoto bora kwako, nisamehe mamaangu kwa kushindwa kukufanya ujivunie uwepo wangu, usijute kunizaa mama! Maneno hayo ya Baraka yalikwenda kuibua machozi ambayo bi Sadifa aliyarundika muda mrefu.

"Nimeamini kuwa yai haliwezi kushindana na jiwe, moyo wa upendo juu yako bado ninao mwanangu! Twende nyumbani ukalale baba" bi Sadifa aliyasema hayo huku akimuinua Baraka na kuelekea usawa wa nyumba yao.

Kabla ya kulala Baraka alilalamika njaa ambayo ni muda mrefu ilimsumbua, bila hiyana na kwa mapenzi yote alipatiwa maandazi manne ambayo tayari yalikuwa yamechomwa, dakika tano zilimtosha kumaliza kula huku maji pekee yakimsaidia kusukuma maandazi hayo tumboni mwake, akiwa anamalizia kula na kutoa vyombo alimuona mamaake akiwa kavalia mavazi ambayo yaliachia sehemu kubwa ya mwili wake .

"Mamaaa!!!! " aliita Baraka kwa mshangao huku akijaribu kuyafumba macho yake.

"Najua unachotaka kukisema ila naomba kwa muda huu usiruhusu neno lolote ambalo litakwenda kuuvunja upendo wangu kwako" bi Sadifa aliongea huku akianza kufunga nyuzi za viatu vyake vyenye ncha ndefu.

Baraka aliondoa viganja vyake usoni na kumuangalia mamaake jinsi anavyohangaika kujiweka sawa, kazi hiyo iliyofanyika usiku mkubwa hakuwa anaipenda ila angefanya nini? Alijuwa fika mamaake anakwenda kuuza mwili ili wapate pesa za kujikimu kimaisha jambo ambalo lilizidi kumuumiza kama mtoto.

"Baraka mimi naondoka kama kawaida nikirudi saa 10 uwahi kunifungulia mlango , na usisahau majukumu yako ya asubuhi , nenda kisimani mapema ili uwahi na kazi nyengine hapa nyumbani , ukirejea makosa mara hii sitokuangalia usoni" maneno hayo yalimtoka Sadifa wakati akifunga mlango wa chumba chake na kuondoka mbele ya Baraka ambae hakuacha kusikitika kwenye moyo.

Hiyo ndio ilikuwa biashara yake nyengine ukiachilia ile ambayo hufanya mapema sokoni, bi Sadifa alikuwa akijiuza kwenye baa maarufu katikati ya mtaa wa JIULIZE, uzuri wake ndio ulimfanya apokee order nyingi za kutoa huduma ya kimwili kutoka kwa mmiliki wa baa hiyo, hakuwa yule wa kuweka mwili wake pembeni ya barabara kuwasaka wateja ila kwa upande wake wateja ndio walimtafuta hiyo yote ni kutokana na umbo lake matata ambalo angekuwa mazingira ya kinyumbani basi lingefichwa na umasikini , huduma alizotoa zilikuwa za kufa mtu kwa maana aliumiliki vyema uwanja uliotumiwa kuchezwa mechi ya watu wawili bila ya mashabiki...ITAENDELEAAAAAAA

Naam hii ndio BARUA KWA MAMA, Baraka arejeshwa nyumbani ila tabia za mamaake zinazidi kumuumiza kichwa, Sadifa huyu Sadifa unadhani kipi kilimpeleka kwenye biashara hiyo au tuseme ndio hii sababu ya UMASIKINI. Mhhh! sijui ila kwa yote hayo basi usikose sehemu ijayo ambayo naamini itakwenda kukufunza vya kutosha.

◇ SEHEMU YA 6 ◇

Nuru ya jua ndio ilitawala jijini TULEANE, hata katika ule mji mdogo wa JIULIZE ndani ya soko kuu hali ilikuwa ni ileile, kila mtu alichakarika kuitafuta shilingi ambayo itakwenda kukidhi au kupunguza idadi ya mahitaji yake kwa siku hiyo, naam soko lilichangamka na wale wasakatonge ndio walikua mbioni .

"Yaani suku hizi biashara imekuwa ngumu hata sijui kwanini? Au ndio walaji wanaandaliwa na wake zao majumbani mwao wakitoka? Mmoja ya wamama wauza vyakula alianzisha mada.

"Wake zao wapi wakati ndio sisi tupo hapa! Hapa kuna mtu anatuchezea mchezo mchafu ila za mwizi arobaini" alidakia mama mwengine ambae alionyeshwa kuchoshwa na mwenendo mbaya wa biashara yao.

"Tena hiyo arobaini yenyewe ni leo! Sadifa tumekuchoka shogaa!! Umezidi kutuharibia biashara zetu, kwa usalama wako tu uhame kijiwe hikiii" alifoka mwengine ambae sura yake ilionyesha hakuwa na amani hata kidogo, huyu aliitwa Masha, wenziwe walimuunga mkono kwa vicheko .

"Mmh! siwaelewi Masha mnaposema nawaharibia biashara zenu, eti nihame pia kijiweni kwenu? Aliwatazama kwa zamu na kuuliza tena Sadifa maana alionekana kuachwa mbali.

"Eeh! kwani tusichokijua kipi kuhusu wewe? Sadifa wewe malaya na kubwa zaidi umeushika uchawi kwenye mikono yako" Masha alijibu maneno yaliyokwenda kumshangaza Sadifa.

"Eeeee! Masha ndio maneno gani hayo? Mbona jana tuliyaongea na yaliisha" aliongea mama mtu mzma ambae alionekana kuwa na busara zake.

"Yaliisha kwako wewe bi Kizuri ila sio sisi! Tunaumia tukirudi majumbani kwetu masinia na mabeseni yakiwa yametudodea, familia zinatusubiri tuzihudumie kupitia biashara hii eti leo unasema tunyamaze sio Masha mimi, Sadifa tumekuchokaaaa" maneno yaliyojaa maumivu na uchovu yalitoka kinywani kwa Masha.

"Kama mlikua hamjui basi nawaambia kua changamoto huibua fursa , hapa sihami, ingawa mumenikera ila atakaye kujiepusha na yamkerayo hahitaji kuhama huhitaji kuwa mtu mwengine, tutabanana hapa hapa" Sadifa aliongea kwa kujiamini na kuwafanya wenzie wamkodolee macho.

"Nakwambia hapa utahama, kama sio kwa hiari ni kwa lazima lakini utahama usituharibie biashara zetu , tulikuwa vizuri hapa na tulikupokea kwa mikono miwili leo unatugeuka !" Masha aliendelea kusimamia mkakati wake .

"Wasio na hekima hulaumu watu, wenye hekima kidogo hujilaumu nafsi zao, wenye hekima kamili lawama ni upuuzi mtupu, hivyo wacha tuone kati yangu na nyinyi nani mshindi? Mlidhani nilikuja kushangaa mji hapa!! " Sadifa na yeye hakuwa nyuma kuwajibu kwa namna mwenyewe alivyohisi anapaswa kuwajibu.

Naam huo ndio ulikuwa mwanzo mpya wa ugomvi kati ya Sadifa na wafanya biashara wenziwe, ingawa kweli alitumia mwili wake kama kitega uchumi ila hakuwahi kuifanya biashara hiyo hadharani, neno uchawi lilimuumiza kwenye nafsi yake maana hakuwahi hata kuufikiria kuufanya kwenye maisha yake, hapo ndio inakuja maana kamili ya mtenda akitendewa hujihisi kaonewa.

******************
Waliosema siku hazifanani basi walikuwa sahihi kabisa, Baraka alikuwa ni mmoja wa waliokwenda kuthibitisha ukweli wa kauli hiyo kwa kufanikiwa kufika shule mapema tena bila ya usumbufu wowote kutoka kwa mamaake, wengi aliosoma nao pamoja walimshangaa maana haikuwa kawaida yake.

"Baraka hivi ni wewe kweli ama naota? Aliuliza Mamy kwa bashasha kubwa huku akijizuia kumkumbatia ila ilishindikana.

"Mamy unafanya nini sasa mbele ya wanafunzi wote hawa, tusitafute matatizo..." alilalamika Baraka na kumtoa mwilini mwake huku wanafunzi wenzao wakiwa shuhuda wa tukio lile, ingawa waliwazowea ila ya leo ilikuwa kiboko.

"Hisia B wangu, siwezi kamwe kujizuia kwako, mmh imekuwaje leo kuwahi hivi? Tukifika darasani nina imani utanieleza " Mamy aliongea kwa bashasha na kuanza kupiga hatua kuelekea darasani kuweka begi lake.

Kanuni ya kimaumbile humuelekeza kila kiumbe aliyepo duniani kupigania nafasi yake, wanafunzi wengi walikua na shauku ya kujua ni kipi walimu wao walikiandaa kwa ajili ya kesho yao, naam ulikuwa ni muda sahihi kwa wana darasa kupewa kile ambacho walikifuata, mwalimu mwenye dhamana ya kusomesha somo la Uraia alikuwa mbele na bakora yake huku akiwa na madaftari mengi mkononi.

Ni yeye mwalimu Mkandarasi, ambae aliogopwa na kila mwanafunzi katika shule ya SOMENI, tabia ya kuogopwa imekuja baada ya kujiweka kuwa mtu wa kutopenda matani na kutojenga ukaribu na wanafunzi wake, alijua vyema kuitumia fimbo wakati akijaribu kuiweka kwenye mwili wa wanafunzi hao kwa ajili ya kutoa funzo.

"Kama unajijua hukufanya kazi yangu naomba pita mbele" aliongea huku akimuangalia Baraka ambae alikuwa mwenye tabasamu zito siku hiyo.

Baada ya kusikia sauti hiyo sura ya tabasamu ilihama na kuingia kwenye huzuni iliyomzowea , minong’ono baina yao ilisikika huku walio wengi wakimuangalia Baraka ambae hakua na namna zaidi ya kutoka mbele akiambatana na wanafunzi wasiopungua watano, Mamy uso wa huruma ulimvaa na kukosa ujasiri wa kuendelea kuangalia mbele alipokuwa B wake.

"Samahani mwalimu nilichelewa kufika darasani ila kazi niliandika na daftari hili hapa" alijitetea Baraka huku akionyesha daftari kwa mwalimu yule ambae alionekana hakua akionyesha walau tabasamu.

"Unachelewa eeeh! Kwanini unakua mtukutu wewe? Ufahamu unao ila kusoma hutaki eeh! Ulijua shule ya babaako hii? Nyoosha mikono mbele" aliwaka mwalimu yule huku akianza kumtandika bakora zisizopungua 5 .

Maumivu aliyoyasikia hayakua sawa na yale yaliopo moyoni mwake, maumivu ya bakora hakuyasikia kwa muda ule ila aliumia kuona akipewa sifa mbaya shuleni hapo , mbaya zaidi anatajiwa mtu ambae hakuwahi kusikia hata historia yake kiufupi , alijilaumu kuja duniani huku akijiuliza kwanini hakuna ambae anamsikiliza? maamuzi aliyoona yanafaa kwa mude ule ni kutoka nje ya darasa.

"Si mnajionea ujinga wenu, wazazi wenu wamewaleta hapa kusoma nyinyi mnakuja kufanya uhuni mnategemea nini kiwasaidie baadae, wazazi wenu wanawasafishia njia ya kupita ila nyinyi bado mnataka kubaki nyuma hivi mtafika kweli? Baraka ni kijana hodari ila mpumbavu kama yeye hakun......" kabla ya mwalimu kumaliza kauli yake alishtushwa na fujo za ugongwaji wa meza ya mwanafunzi wake.

"Inatosha!! Inatosha!! Inatosha mwalimu" hiyo ilikuwa ni sauti ya Mamy iliyoambatana na kilio ndani yake.

Macho ya darasa zima yalituwa kwenye sura nzuri iliyoharibiwa na machozi, midomo ya wanafunzi ilizibwa na mikono yao wakimshangaa Mamy huku wakimuangalia na mwalimu wao, Mamy alikuwa kwenye maumivu makali zaidi ya yale ya kidonda kilichowekea ndimu , chumvi na pilipili, roho ilimuuma kuona kipenzi chake kinaongelewa vibaya, tena mbaya zaidi akihusishwa na mzazi wake ambae hakuwahi hata kuambiwa wapi anapatikana, hakujua ni ujasiri gani ulimpata wa kuweza kufanya hayo mbele ya mwalimu aliyeogopwa na wanafunzi wengi.

"Inatosha mwalimu, kwanini unasema maneno yote hayo? Unatufanya tukuone ni adui kuliko rafiki kwetu! Unasahau kama wewe ni mlezi wa pili tukiwa mbali na nyumbani? Kwanini hutufurahii wanafunzi wako? Alilalamika Mamy kwa sauti yenye utii iliyojaa majonzi.

"Ehee binti kwa hiyo ulitaka niwachekee endapo mtaendelea na hii tabia mbovu eeh! halafu serikali itulaumu mukipata matokeo mabovu" kwa sura yake ya kuchukia mwalimu Mkandarasi alirejesha kibao kwa bibie Mamy.

"Ni dhahiri kuwa hakuna mwalimu anaefurahia nidhamu mbaya kwa mwanafunzi wake ila kumbuka darasa hujengwa na mahusiano bora ili katika ufundishaji kuwepo na matokeo mazuri, siku zote darasa lenye chuki, visasi, dharau na ugomvi kamwe haliwezi kutoa matokeo bora yenye kukuza taaluma yetu " Mamy alijibu kwa kujiamini maneno ambayo yalimgusa mwalimu na kumfanya akose la kusema.

"Mnatusema vibaya mno walimu, tunakua na uoga hata wa kueleza yale yanayotusibu, hii ni sehemu ya pili kati ya zile tatu ambazo zinatufunza maisha , ikiwa wazazi na jamii wanashindwa mnadhani watoto kimbilio letu ni wapi kama sio hapa? Mnatuumiza mno na mwisho wa siku haya mnayotuonyesha ndio tutaendeleza siku zijazo" Mamy alihitimisha maneno yake na kuamua kukusanya hatua zake kutokomea nje huku akiwaacha wanafunzi wenziwe na mwalimu wao mdomo wazi.

Aliijua sehemu ambayo Baraka hukimbilia akiwa ametoka kuvurugwa, kwa mwendo wake uliotambulisha uharaka aliokuwa nao alifanikiwa kufika kwenye mti mkubwa uliokuwa sehemu ya vyoo vya wanaume, alichokiwaza kilikuwa sahihi kwa maana alimkuta Baraka kajiinamia, moyo wake ulimuuma na nafsi ilisononeka , kumbatio lililojaa upendo lilimfikia Baraka, japo ilikuwa ni nyuma ya mgongo wake ila aliutambua uwepo wa Mamy kutokana na harufu yake bali pia ni yeye pekee ambae anaweza kufanya hivyo .

"Tafadhali Mamy naomba nafasi ya kuwa pekee muda huu " sauti nzito ya Baraka iliyoonyesha uhitaji ilisikika vyema kwenye ngoma za sikio za bibie Mamy.

"Hakuna kito king’aracho bila ya kusuguliwa kadhalika hakuna mtu aliyeongoka bila ya majaribu Barakaa, hivi unayajua madhara ya upweke au unaomba tu" maneno hayo yaliyojaa hasira yalishushwa kwa kijana Baraka huku msemaji akisogea mbele yake.

"Najua vyema kama kipimo cha dhahabu ni moto na kipimo cha mwanadamu ni shida, Mamy nahitaji kuwa peke yangu muda huu naomba uondoke" kwa sauti ya mkazo Baraka ali

"Jee rafiki ni nani?........Kwa sauti yake ya upole Mamy alidadisi macho yake yakiwa usoni kwa Baraka.........ITAENDELEAAAAAAA
Tumsaidie Baraka kujibu swali. Mwalimu Mkandarasi kapewa dozi yake jee! Unafikiri hatua gani atachukua, msimamo wa mama Baraka (Sadifa ) utafikia wapi? Tukutane sehemu ijayo.
 
◇ Sehemu ya 7 ◇

"Najua vyema kama kipimo cha dhahabu ni moto na kipimo cha mwanadamu ni shida, Mamy nahitaji kuwa peke yangu muda huu naomba uondoke" kwa sauti ya mkazo Baraka alisisitiza.

"Jee rafiki ni nani? Kwa sauti yake ya upole Mamy alidadisi macho yake yakiwa usoni kwa Baraka ambae alionekana ni mwenye hasira.

"Rafiki ni mtu ambaye unamwamini kwenye maisha yako ya kila siku, rafiki ndiye anayeweza kukusaidia au kuacha kukusaidia maana yeye ndiye mwenye kujua siri zako, hivyo rafiki pia anaweza akawa ndiye adui wako...."

"Unamaanisha hata mimi naweza kuwa adui kwako? Kabla Baraka hajamaliza maelezo yake Mamy alitupia swali.

"Adui hana sura Mamy wala alama yoyote usoni mwake na ndio maana ukiwa na rafiki hutakiwi kumshirikisha kila jambo, hichi kitu mama huniambia mara nyingi " Mamy alijibiwa majibu ambayo yalikwenda kuusononesha moyo wake.

"Hata mimi mama aliwahi kunambia kuwa "Rafiki wa kweli hukumbatiwa kwa mikono miwili" na ndio maana sina shaka juu yako, ni kweli rafiki mnafiki hana sura ila fahamu kama anakupenda basi hakuna kitakachomuweka mbali na wewe, lakini kama hakupendi hakuna kinachoweza kumfanya abaki kwako,mimi sio rafiki tu kwako bali nataka unifanye niwe mwanamke wa ......"

"Mamy nakuomba usimalize kile ambacho unajaribu kunieleza, ni kweli wewe ni rafiki wa kweli ila hukuwahi kuufikia upweke niliokua nao" safari hii Baraka aliamua kupotezea kile ambacho kilikua kinataka kuchukua nafasi ingawa kilimshtua.

"Kwanini upweke na sio mimi? Mamy aliuliza kwa mshangao.

"Upweke ni rafiki wa kweli kwangu, haujawahi kuniacha, hata ninapojaribu kujiondoa huwa na mimi kila wakati, ingawa leo upweke wangu umejaribu kunitabasamu ila umekwenda kuharibu kila kitu, ona machozi yangu Mamy jinsi yanavyoshindwa kuzuilika" maneno hayo yaliyosindikizwa na machozi yalimtoka Baraka.

Moyo na ubongo wa Mamy vilipiga kelele kwa wakati mmoja na hatimae vilikubali kuungana na Baraka kuelekea kwenye upweke, miguu ilikosa nguvu na kumfanya Mamy akae chini bila ya kujali uchafukaji wa nguo yake, alikosa cha kumwambia Baraka kiasi ambacho alijikokota na kumkumbatia kwa mara nyingine, hisia za upendo baina yao ndio ziliwatuma wafanye vile, walihisi kufanya vile kungewapunguzia machungu wanayopitia.

"Nakupenda Baraka na ndio maana kila hatua unayopiga nahakikisha nakua nyuma yako, sitojali nitakumbana na hatari ya aina gani ilimradi tu nuru ya tabasamu imurike usoni mwako, usijaribu kujiweka kwenye huzuni Baraka maana ni kisima ambacho ndani yake unazama zaidi na zaidi " kwa sauti yake laini maneno yaliyojaa hisia za upendo yalitoka kinywani kwake.

"Mmmh! Upendo upi ambao anauzungumzia? Kwani upendo ndio huondoa huzuni? " ingawa Baraka alijua anajiuliza kwenye nafsi yake ila kumbe sauti ilipenya kwenye masikio ya aliyekua kifuani mwake.

"Upendo ni hisia zinazopingana zaidi ya tunazoweza kuhisi , upendo unatufanya tujisikie furaha kabisa na kutabasamu zaidi kwani huzuni ghafla huvamia kwenye upendo na kuunda bahari ya machozi, hivyo basi unapohisi upendo kwa mtu basi ifanye furaha yake kama yako kwa maana maumivu yanaweza yakawa sehemu yake kama na wewe utamkosesha upendo huo......NAKUPENDA SANA BARAKA.." Mamy aliamua kufunguka akiwa mikononi kwa Baraka, hakuweza kuzuia hisia ikiwa anaamini wa kuzishikilia yupo mbele yake, tena aliongea hayo akiwa kwenye tabasamu zito ambalo halikuonekana na mlengwa .

Mshtuko wa maneno hayo ulimfanya Baraka ajitoe mwilini kwa binti mrembo, hakuamini kile alichosikia licha ya kwamba alijiuliza kwenye nafsi yake na alikihisi kwa muda mrefu kutokana na matendo, macho ya mshangao yalimtoka ila aliyemshangaa aliishia kutabasamu, alitamani kutamka neno ila alishindwa maana midomo yake ilikua mizito na mwisho wa siku kidole cha bibie kiliishia mdomoni kwa Baraka kumsisitiza kuwa hapaswi kuongea chochote , uwanja ulikuwa wake.

"Nakupenda Baraka na wala sio mgeni kwa hichi nilichoeleza, ingawa hii sio siku ambayo nilipanga kukwambia haya ila nahisi kuchelewa kwangu kutakupoteza, vitendo vyangu kwako ni ishara tosha ya kauli yangu hii, nipo tayari kwa lolote mbele yetu na nitahakikisha unakua Baraka mpya, Mapenzi yangu kw....." Mamy alisitisha kile anachokiongea baada ya kushtushwa kelele za pongezi.

Macho yaliwatoka baada ya kumshuhudia mwalimu Mkandarasi pembeni yao akiwa na fimbo ndefu huku hasira zikijidhihirisha usoni mwake, hofu na uoga vilimuandama Baraka akijua balaa litakalowakuta, sheria za shule walizikiuka, muonekano wao ulikua na utata maana walikua zaidi ya ngozi na nyama, lakini pia maneno ambayo yalikuwa yakitamkwa na Mamy jee! Walibaki wakitazamana.

"Mapenzi! Mnaijua hadithi ya Mapenzi? Mapenzi ni biashara mbaya inayotisha inayofanywa na wapumbavu, itawavunja moyo na kuwaacha mkivuja damu, hivi mnadhani mtakua mumepata nini mwishoni? Bila ya shaka ni kumbukumbu chache tu ambazo mtashindwa kuziondoa, Inasikitisha mno kuona wazazi wenu wakipoteza nguvu na mali kuwekeza kwenye elimu ila nyinyi mnawazadia upumbavu huu , mlipaswa muwepo darasani mjiandae na mitihani yenu ya mwisho ila mumeishia kushikana ovyo mafichoni si ndio ...hahaaaaa..." mwalimu Mkandarasi aliongea hayo huku akiwatazama kwa tabasamu ambalo halikumaanisha furaha.

"Lakini mwalim......" alijaribu kujitetea Baraka ila alinyamazishwa na fimbo moja ya mgongo, Mamy ilimuuma kama ni yeye aliyepigwa, alichukia mno .

"Hakuna cha mwalimu hapa! Wewe ndie umemtia kiburi huyu binti kiasi ambacho anafanya anachojisikia, na hiki ndicho ambacho kilimfanya leo anitolee maneno mabaya mbele ya wengine eeh! Sasa mtalipia kwa hili na ushahidi wa hili tukio nipo nao kwenye kiganja changu" mwalimu Mkandarasi aliongea hayo huku akiwaonyesha simu janja iliyokuwa mikononi mwake.

"Mwalimu nakuomba nipo chini ya miguu yako hili jambo liishie hapa...hakuna nilichokifanya cha ubaya kwa binti huyu " kwa sauti iliyokaribisha kilio Baraka alipiga magoti mbele ya mwalimu yule ambae hakuonyesha nia ya kuwasamehe.

"Sio kibaya eeeh,,,, kwa hiyo kukumbatiana chochoroni ni jambo jema si ndio.....sina msamaha kwa hili mtanikuta ofisini" mwalimu Mkandarasi aliyasema hayo huku akianza kupiga hatua akimuacha Baraka mdomo wazi.

"Unaona Mamy ulichokifanya! Naonekana mimi ndio nakuharibu, Unazidi kuniingiza matatizoni kila kukicha, nipunguzie mamaa, hili halijamaliza linakuja jengine, Nitamwambia nini mama? Alilalamika Baraka macho yake yakiwa mekundu kuashiria hasira alizonazo.

"Huu sio muda wa kulaumiana , unadhani naanzaje kuzituliza hisia zangu nikuonapo kwenye huzuni? Kichwa cha mtu jasiri hujaa majaribu amini na hili litapita Baraka mbona unakua muoga? Kwani katuona tunabusiana si tulikumbatiana tu! Unachoogopa nini sasa" aliongea Mamy kwa kujiamini huku akimtazama Baraka ambae bado alikuwa chini kapiga magoti.

"Unafikiri hili litaishia mikononi kwa mwalimu Mkandarasi, litaenda kwa mwalimu mkuu na mwisho tutaitwa na wazazi wetu, Mamaangu atakuja? Wazazi wako watanionaje Mamy? Ehee halafu umefanya tukio gani darasani? Alimazia kwa kumtupia swali.

"Nilikua natetea kile ambacho kilikua hakipo sawa, haiwezekani mwalimu ashindwe kumsikiliza mwanafunzi pale anapojaribu kujitetea, wanatufunza nini? Baadae tuwe kama wao tushindwe kusimamia familia zetu? Kwa hili nitasimama popote kulitetea, ni lazima watujengee upendo , upendo ambao utajengeka mioyoni mwetu leo na siku zijazo , au nimefanya kosa pia?" Mamy alitupia swali mwishoni mwa ila hakujibiwa kitu.

Baraka alijiinua bila kumwambia chochote binti yule na safari ya kuelekea ofisini kwa mwalimu Mkandarasi iliwadia, Mamy hilo halikumshangaza maana alijua kipindi ambacho Baraka alikua akipitia, kwa mwendo wake wa madaha na yeye alianza kumfuata.......ITAENDELEAAAAAAA
Tupia like na comments yako hapo chini, muitiko wenu ndio mwendelezo wa simulizi hii.

◇ SEHEMU YA 8 ◇

Misosi point ulikuwa ni mgahawa uliopatikana katikati ya mtaa wa Jiulize mbali kidogo na soko kuu, mgahawa huo ulichangamka kutokana na idadi kubwa ya wateja ambao walifika kujipatia huduma muhimu ya chakula, pembeni ya mgahawa huo kulikuwa na bar ambayo ilijumuisha na vyumba vya kulala wageni , naam kwenye hio bar nje kabisa walionekana wanawake wawili ambao walikuwa kwenye majadiliano .

"Una uhakika ni mume wangu? aliuliza mwanamke ambae alikua akikaza kilemba chake kichwani huku akiwa na wasiwasi.

"Nikudanganye ili nipate nini? hemu twende huku tukamfundishe adabu maana kazowea sana kuiba waume za watu" mpelekaji aliongea huku akimvuta mkono mwenye mume hadi sehemu ambayo wateja hukaa.

"Yuko wapi mbona simuoni? Sitaki matani kabisa na mume wangu unajua " mwenye mume alikuja juu baada ya kuona alichokifata hajakiona zaidi ya kuzubaa .

"Hivi mimi Masha nishawahi kukudanganya? kwa macho yangu haya mawili niliwaona Sadifa na mumeo wakiingia humu na tangu hapo nimekupigia simu basi macho yangu yote yalikua kwao" Masha aliongea huku macho yake yakiangaza pande zote za bar ile.

"Tafadhalini wapendwa, hii ni sehemu ya biashara tunaomba utulivu, kama mumefata huduma basi fateni utaratibu na sio kuleta kelele munasumbua wateja wengine..." muhudumu wa bar hiyo aliwafata baada ya kusikia kelele za malumbano.

"Hahaaa huduma zipi hizo? za kukaribisha uzinzi na kuharibu ndoa za watu? hahaaa jiheshimu wewe kaka na ukae pembeni maana hii ngoma hakuna mchezo ukufaao" Mwenye mume alikuja juu na kuwafanya wateja wote wabaki wakimuangalia.

"Nawaheshimu sana dada zangu, kama mumekuja na lengo jingine basi naomba mutoke nje kabla sijawaitia walinzi" muhudumu na yeye alitetea kibarua chake.

"Hahaaa unachekesha sana wewee! nadhani hunijui vizuri wewe , ukisikia Masha mikiki ndio mimi! Jiulize yote hii hakuna asiyeniju......" kabla ya kumalizia kauli yake alifanikiwa kuiona sura ambayo alikuwa akiitafuta ikija usawa wa sehemu ya mapokezi.

"Ndaze mumeo yule pale...." aliongea Masha kwa sauti ndogo ambayo ilimfanya mwenye mume ageuke haraka.

Muhudumu akiwa anafanya utaratibu wa kuwaita walinzi alishtukia kuachwa peke yake, alipopeleka macho yake pembeni alishuhudia mzee wa makamo akitiwa ngumi na kukunjwa vyema shingoni na mwanamke mwenye kilemba kikubwa kichwani .

"Utanieleza huyo mgoni mwenzio yupo wapi? hapa ndio Minarani eeh..! Kwangu ulikosa nini mzee wewe!! nikupe nini wewe mwanaume uridhike? Kwa sauti yenye hasira Ndaze aliuliza na kuanza kumvuta mumewe kuelekea usawa wa vyumba.

"Weeh mwanamke niache na urudi nyumbani kabla sijakufumua! alilalamika mzee yule ambae alikuwa kibanoni huku Masha akikoromeana na walinzi pamoja na wahudumu wa bar ile.

"Siwezi kurudi leo, kila siku nakukatalia hizi tabia ila leo nakomaa hapahapa nijihakikishie na nimuone huyo mwenye kukufaya ushindwe kukaa angalau dakika mbili na familia yako, nataka kuujua ukweli wa hayaaa" alifoka Ndaze huku akikifunga kitenge ambacho kilianza kuvuka kiunoni kwake .

"Atafutaye ukweli huutafuta kwa heshima ndipo ushindi wa kuusaka kwake utabaki nae daima na sio kuzunguka na wambea wa mitaani namna hii" hayo ni maneno yaliyomtoka mzee yule na kumfanya Masha azidishe hasira zake kwa mzee yule.

"Wewe ni roho iliyobeba mzoga na hakuna asiyejua hili mtaani kwetu? kila baya unalo wewe yaani tabia zote chafu umezibebea na sio leo tu kukuona hii bar...."alifoka Masha jina la mmbea lilimchoma.

Aidha Mungu anaweza kuondoa maovu ama hawezi, au pengine anaweza lakini hataki, lolote liwalo liko katika matakwa yake.Naam hakika Mungu kwa siku hiyo alikuwa upande wa Sadifa kwa maana akiwa hana hili wala lile aliamua kutoka nje baada ya kuona bwana wake anachelewa kurudi, macho yalimtoka baada ya kumshuhudia Masha na Ndaze wakizozana na wahudumu pamoja na walinzi huku mzee mzima akiwekwa kati, alijibana kwenye uchochoro mdogo usawa wa chumba alichotoka.

"Mmh kimenuka leo , wacha nikakusanye vitu vyangu! Mimi ndio maana kufanya biashara mida hii sipendi" Sadifa alijisemea na kuchomoka kuelekea chumbani ambapo alibeba kila kilichomuhusu , hakukomea hapo alipekua pochi ya yule mzee na kutoa hela kiasi ili kufidia muda wake, baada ya hapo aliamua kupitia mlango wa nyuma wa bar ile ambayo hakuwa mgeni nayo.

"Nimechoka na hii ndoa , kila siku vituko wewe tu na leo utanipa talaka yangu, bakia na malaya zako..." Ndaze alisema maneno hayo huku akiwa chini na machozi yakimtoka baada ya mumewe kugoma kabisa kumpeleka chumba alichokodi.

Mzee yule aliombwa aondoke na mke wake sehemu ile kwani kuendelea kubaki pale kungeharibu biashara yao, mzee yule aliomba radhi kwa uongozi na kumtaka mke wake ainuke wakayaongee nyumbani.

"Weeh mzee unajizima data eeh! tunamtaka Sadifa hapa na sio kuturejesha nyumbani , nimewaona kwa macho yangu mumefuatana kama kumbikumbi tena saiv....." kabla hajamaliza kauli yake Masha alistushwa na kofi zito lililotuwa shavuni mwake.

Kofi hilo lilimfanya aone nyota nyingi hali ya kuwa bado ilikuwa mchana, alitupia macho chini kuhakikisha kama kweli meno yake yalianguka ama laah ila alikutana na sura ya Ndaze iliyokumbwa na mshangao, Masha alijihakikishia kuwa meno yake yote yapo sawa baada ya kufanya hesabu kwa kutumia ulimi wake, hapo sasa aliamua kuvaa sura ya hasira dhidi ya mzee yule, umbea ulimponza ila angefanya nini na alitaka kumkomesha Sadifa.

"Umegusa pabaya wewe mzee na kwa hili nakuapia tutakula sahani moja na umalaya wako ipo siku yatakutokea puani "aliongea Masha maneno machache huku akiondoka sura ikiwa imechafukwa na hasira .

Mzee yule nae hakuona sababu ya kubaki pale , aliamua kuondoka zake bila kwenda kumuangalia Sadifa wala kumchukua mkewe huku akiwa na hasira nyingi mno, alipitia mapokezi na kuwaomba msamaha kisha akawapa maelekezo ya chumba alichokodi na kutokomea ambapo na mkewe alifuata.

********
Tayari giza liliivamia anga ya mtaa wa Jiulize ndani ya jiji kubwa la Tuleane , familia nyingi zilikua ndani zikiwa zimeweka miili yao kwenye vitanda kwa wale waliojaaliwa navyo, pia ni wachache ambao walibaki sebuleni kuangalia sinema au habari mbali mbali zilizoukumba ulimwengu, kijana Baraka na yeye tayari alijiweka kwenye kigodoro chake ambacho kilionekana kuchoka huku mamaake akimalisia kuandaa biashara zake.

Kibatari kwa siku hiyo kilishiba mafuta ya taa kiasi ambacho alipata nafasi nzuri ya kupitia masomo yake , akiwa anapekua mkoba wake wa madaftari kutafuta somo lake pendwa la hesabati alichukia baada ya kushika daftari la Kishwahili , aliliangalia kama vile alikua mgeni nalo.

"Najua kama hii ni lugha mama na nilikua nalipenda hili somo kupita maelezo, ila mwalimu Mkandarasi umeanza kunijengea chuki na hili somo" alijisemea Baraka kwa sauti ya chini huku akiliweka pembeni.

Taratibu akili yake aliihamishia shuleni na kukumbuka maneno mazito aliyopewa na mwalimu Mkandarasi wakati wakiwa ofisini........Itaendeleaaaaaa.
 
*********
◇ Sehemu ya 9 ◇

Taratibu akili yake aliihamishia shuleni na kukumbuka maneno mazito aliyopewa na mwalimu Mkandarasi wakati wakiwa ofisini kabla ya Mamy kuingia, hakujua kwanini mwalimu huyo alitaka iwe hivo hata kama alihisi kitu hakutaka kukiingiza akilini na kwa vile alitaka kusoma kwa amani basi aliamua kubaki upande ambao aliwekwa.

Ama kweli ng'ombe wa masikini hazai maana licha ya kwamba siku hiyo kibatari kilijaa mafuta ila matukio yaliyojitokeza kutwa nzima yalimnyima uhuru wa kujisomea na mwisho wa siku alibaki kutafuna kalamu yake na macho yakiwa pembezoni mwa ukuta uliobanduka rangi, alijilaumu kwanini anapitia yote hayo.

Mama wa Baraka baada ya kumalizia kuandaa vitafunwa na kujiandaa kwa ajili ya kuelekea kwenye mahangaiko yake ya usiku taratibu alilisogelea pazia la kijana wake akiamini muda huo angemkuta akijisomea, mawazo yake siku hiyo hayakua sahihi, Baraka aliubadilisha mfumo angesomaje na akili yake inawaza mengine, kwa kiasi fulani alisikitika kumuona kijana wake akiwa mwenye dimbwi kubwa la mawazo, alimsogelea na kuchuchumaa pembeni yake , alivyoona kijana wake bado yupo mbali kihisia aliamua kumshika bega kitendo ambacho kilionekana kumshtua mno Baraka.

"Mwanangu..... unatakiwa uyazowee haya matatizo na uyachukulie kama ni mafuta kwenye msafara wako, haya ndio maisha yetu na mimi ndie mamaaako na hizi ndio kazi zangu! sasa ukikaa na kujiinamia hivyo basi utashindwa kufanya kitu , maneno ya binadamu kamwe yasikunyime uhuru wa kufanya kile ambacho unakiona ni sahihi kwako....PAMBANA!! bi Sadifa alimtoa hofu Baraka ambae alibaki kumuangalia usoni mamaake kama kuna kitu alitaka kumuuliza.

"Nimeshajikubalisha kuwa wewe ni Mamaangu na wala sijawahi kujutia hilo , Mama.... kinachoniuma zaidi ni namna ambavyo watu wanakuzungumza, Naumia!! Kwanini wanakusema vibaya? leo hii tu nimesikia umetoka kufum......" alisita kuendelea kuongea Baraka baada ya kuona anavuka mipaka.

"Ehee unataka kusema nini! Kila unachokisikia kuhusu mimi basi elewa wewe hakikuhusu, ni bora kukaa kimya na kuonekana kama mpumbavu kuliko kufungua kinywa chako , kama unapata kula na unalala vizuri wasiwasi wako nini? Heeh usinitibue.....na uwahi kuzima taa usinimalizie mafuta, ni wiki nzima hayo na tafuta yake ndio hii ambayo inakupa mawazo" Sadifa alimfokea Baraka huku akiinuka pembeni yake.

"Ingawa wewe hujali ila yananiathiri mno, mtaani nachekwa na hata shuleni nafikiriwa vyengine yote ikiwa ni vile unavyonilea, mama ... mimi ndio wa kubadili maisha yetu ila na wewe unatakiwa uwepo pembeni yangu kwenye mabadiliko haya, leo hii ukiwa na matukio hayo unahisi amani ya moyo naitolea wapi ? " alilalama Baraka akiwa kapewa mgongo na mamaake.

"Mmh! maisha yangu kamwe huwezi kuyabadilisha ikiwa mimi mwenyewe nimeshindwa kuyabadilisha, zima taa ulale usinimalizie mafuta " alifoka Sadifa akitokomea nje .

"Mtu hata badili maisha yake kama hakuanza na kubadiri fikira zake, muda wako unakikomo, kamwe usipoteze kwa kujaribu kuishi maisha ya mtu mwingine'' hiyo ni kauli ambayo ilipenya sawasawa kwenye masikio ya Baraka na bi Sadifa baada tu ya kuweka mguu nje.

Baraka aliamua kuchungulia kupitia dirisha dogo la chumbani kwake, hakufanikiwa kuiona sura ya aliyetamka maneno yale ila sauti haikuwa ngeni kwenye masikio yake, ni yeye Bi Mwenda , bibi ambae alikuwa mstari wa mbele kwenye maisha yao , licha ya kwamba hakuweza kuona nje ila hilo halikumfanya ahame sehemu ile.

''Ni wewe tena bi Mwinde, hivi huchoki? Maisha huchanua na kusinyaa kutokana na ujarisi wa mtu husika, maisha yangu ni yangu bi Mwinde na wala hayamuathiri yeyote kati yenu, siishi kwa kumkomoa mtu ila naishi kutokana na mfumo wangu nilioutengenezewa" Sadifa aliongea kwa hasira mbele ya bi Mwinde.

"Maisha yako eeeh! hahaaaa unajidanganya Sadifaa! unapojikwaa kwenye mlango uliofungwa basi ujuwe mlango mwingine utafunguliwa kwetu. Kwa bahati mbaya, unaangalia mlango uliofungwa kwa muda mrefu hivi kwamba huuoni ule ulio wazi kwetu, Baraka ni zao lako kwanini umuumize na uliyopitia huko nyuma? mtunze na umlee ili awe mkombozi kwako baadae " bi Mwinde alianza kutoa darasa kama kawaida yake.

" Bi . Mwinde , nadhani unayajua fika niliyopitia huko nyuma, sitaki kuyakumbuka maana ndio chanzo cha mimi kuonekana mbaya leo hii, haya ndio maisha niliyoyachagua hivyo naomba uniache, siwezi kuanza upya kamwe" Sadifa aliyasema hayo huku akijiweka sawa wigi lake.

"Mtu hawezi kuandika ukurasa mpya maishani mwake ikiwa anaendelea kusoma na kusoma tena za zamani, Ikiwa Mshirazi alikusaliti basi hata iwe ni ngumu vipi kumbuka kuwa hatima iliondolewa tu kwa huyo mtu ila sio maishani mwako, yaliyopita yanaweza kuwa mazito sana kubebwa nawe kila mahali na ndio maana unabaki kujidhalilisha kila siku Sadifa, Wakati mwingine ni muhimu kusahau juu yake kwa ajili ya siku zako zijazo" bi Mwinde alizidi kusisitiza maneno ambayo yalimshtua Baraka baada ya kusikia jina ambalo sio geni kwenye masikio yake.

"Nakuheshimu bi Mwinde hivyo sitotaka nikuvunjie heshima, ingawa ulinisaidia sana ila maisha yangu hayakuhusu, niache na mwanangu na naomba hilo jina nisilisikie tena " kwa sauti yenye hasira Sadifa alimwambia bi Mwinde na kuondoka eneo lile haraka.

Baraka alishusha pumzi ndefu, alijawa na shauku ya kutaka kumfahamu huyo Mshirazi ni nani? alitamani kumjua na kumuuliza mengi , aliona msada pekee ni bi Mwinde hivyo aliamua haraka kutoka nje ili amuwahi kabla ya kuondoka.

Bi Mwinde alishtuka sana kumuona Baraka usiku mkubwa akitoka nje , macho yao yalipokutana kila mmoja alijua yamebeba viulizo, naam bi Mwinde tayari alijua kuwa Baraka alikisikia kila walichoongea ila hata na yeye Baraka aligundua kuwa bi Mwinde hakua tayari kuulizwa chochote na ndio maana alijifanya kumshika mkono kama njia ya kumfariji.

"Ili kuwa na furaha, unahitaji kujikwamua na yote ambayo ni ya kupita kiasi, kuachana na vitu visivyo vya lazima, malumbano yasiyo ya lazima na muhimu zaidi kuyatoa mawazo yasiyo ya lazima, Ujasiri wa kweli tu ni kuwa wewe mwenyewe Baraka " bi Mwinde aliongea taratibu kisha kumuachia Baraka na kupiga hatua kuelekea kibandani kwake ambapo ni hatua kumi tu kutoka hapo.

Maneno hayo yenye maana kubwa yalizunguka kichwani mwake, licha ya kwamba umri wake ni mdogo ila kilichokusudiwa alikifahamu, baada ya kumsindikiza kwa macho hatimae alifanikiwa kumfikisha bi Mwinde mlangoni kwake, hata na yeye hakuona umuhimu wa kubaki sehemu ile , hatimae kama kawaida yake alirudi malaloni kwake huku lengo lake la kusoma likiisha baada ya kibatari kukizima, ndio alibaki kuwa mlinzi wa nyumba.
************

Kwenye kijiwe chake cha biashara ya kuuza vyakula ajenda ilikua ni jina lake zikifuatiwa na tabia zake, spika wa kikao hicho ni yule yule ambae kiswahili chao hakipo sawa, ni yeye Masha hakuwa mwengine, ingawa walikuwa pamoja ila ungefanikiwa kupita ungesema aliyejadiliwa alikuwa mita mia kwa jinsi alivyokua kimya, sijui tuseme hakutaka vurugu au muda huo masikio aliyapa likizo? mmmh! hilo jibu alilijua mwenyewe Sadifa .

"Jambo kuu katika ulimwengu huu sio mahali tunaposimama, lakini ni mwelekeo gani tunahamia na kwa hali hii kama tutaendelea kunyamaza basi magonjwa yatatumaliza majumbani kwetu " Masha ambae ni spika wa bunge hilo aliendelea kutetea hoja yake huku wenziwe wakitilia mkazo

Biashara iliendelea huku vijembe vikizidi kutupwa kwa Sadifa, walijisahau kuwa waliyemtupia hakuwa mtu wa kujali zaidi aliona kama ni kama fursa kwake maana wateja wote walimfuata yeye ambae alibaki kimya , hilo jambo liliwakera zaidi maana baada ya saa moja tu basi beseni la Sadifa halikuwa na vitafunwa vyovyote.

"Mmmh ! kweli uchawi upo mimi si niliwaambia oneni sasa... " Masha aliongea huku akiacha beseni lake na kumfuata Sadifa ambae alikuwa akiinua beseni na kumuaga jirani yake bi Kizuri.

Baada ya kuona hakujibiwa kitu zaidi Sadifa alikuwa anajiandaa kupiga hatua, ghafla alimkwaa na kusababisha Sadifa awe chini na beseni lake kuangukia pembeni, hasira zilizotunzwa muda mrefu zilichomoka kutoka kwenye ghala lake, alimuangalia Masha kwa jicho baya mno, wale wenzake walibaki kucheka na kumpigia makofi kwamba alifanya kazi nzuri.

"Matumizi mazuri ya wakati hufanya wakati kuwa wa maana zaidi, ingelikuwa mna jitihada kwenye biashara zenu basi kwa hakika saivi mngeacha kufanya hiki mnachokifanya na mngejilaumu kwanini siku zote hizo hamkuwahi kufanya hivyo, nina mengi mno ya kufanya hivyo sitopenda kupoteza muda wangu hapa" Sadifa aliongea kwa hasira huku akijipangusa vumbi na kuokota beseni lake.

"Hahaaaa!!!! muone vilee, kwa kazi gani labda unayowahi kama sio umalaya, na ukute unakopwa maana naona maisha yako ni yaleyale" Masha alitiririka majibu ambayo yalikwenda kuibua minong'ono kwa wale ambao hawakua wakizijua tabia za Sadifa, hiyo hali Masha na wenziwe iliwafurahisha ila upande wa bibie Sadifa uso ulimvimba kwa hasira..... Itaendeleaaaaaa.

Sadifa na Masha mambo ni moto, Mwalimu Mkandarasi kamwambia nini Baraka? see u next episode.

Tupia like na comment yako hapo chini muitiko wenu ndio mwendelezo wa simulizi hii

◇ SEHEMU YA 10 ◇

"Hahaaaa!!!! muone vile, kwa kazi gani labda unayowahi kama sio umalaya, na ukute unakopwa maana naona maisha yako ni yaleyale" Masha alitiririka majibu ambayo yalikwenda kuibua minong'ono kwa wale ambao hawakua wakizijua tabia za Sadifa, hiyo hali Masha na wenziwe iliwafurahisha ila upande wa bibie Sadifa uso ulimvimba kwa hasira.

Pesa zake alizifunga vyema nchani mwa tenge lake, beseni lake alilirushia alipokuwa bi Kizuri akiamini ni sehemu salama, jicho pekee ndio ambalo lilidhihirisha kilichomo moyoni mwake , aliamua kumfundisha adabu Masha ili siku nyingine auheshimu ukimya wake, kwa kasi ya ajabu na wepesi wake wa mwili alimvaa Masha na kuanza kumshushushia kipigo hadi kumuangusha, mmmh! hatimae Masha chini Sadifa juu.

Masha hakutaka kuonekana mzembe hivyo nae alianza kujitetea kwa kurusha ovyo mikono ila nafasi ya kuinuka hakuipata , pumzi zilimsumbua kutokana na mwili wa Sadifa kuwa juu yake, kilemba cha mia tano tayari kilivuliwa na kutupwa pembeni huku kipilipili chote kilikuwa hadharani, hawakuamini macho yao hivyo hakuna aliyejizuia kucheka , alijua kuitumia nafasi Sadifa maana alikivuta kipilipili hicho hadi alipochoka, kwani kuna ambae alithubutu kuwaamulia na walitaka kumuona mbabe? huko ndio uswahilini eeh!!

Uvumilivu uliwashinda wapambe wake Masha, waliona wazi watamkosa mwenzao na kesi itakuja waangukia, walianza kumvuta Sadifa aliyekuwa akirusha ngumi mithili ya aliyechanganyikiwa, walifanikiwa na kumtupia pembeni! Masha alikohoa mfululizo na kutema damu zilizovuja kwenye meno yake , bila ya shaka hata meno mawili yaling'oka ukisaidia na kibao alichokula jana yake.

"Waacheni bwanaaa kwani nani aliwatuma? ilooo Masha ilooo Masha" walilalamika watazamaji huku wakimzomea Masha.

Baada ya kutupwa pembeni Sadifa alijiinua huku akihema , alimsogelea bi Kizuri ambae alitabasamu kama ishara ya kumpongeza na kumkabidhi beseni lake, kwa mwendo wake wa madaha alimsogelea Masha aliyekuwa chini akipangushwa vumbi na wapambe wenziwe.

"Haina maana kutafuta mafanikio kwa wivu, ukiona kazi yangu inalipa basi nifuate nikupe mbinu" Sadifa aliongea maneno ambayo hakuna aliyemjibu kwa muda ule wote walimheshimu, chezea kipondo weweeh!

************

Tayari ulikuwa ni muda pendwa kwa wanafunzi wengi, muda wa misosi!! wale waliopewa pesa majumbani kwao waliwakimbilia wauza biashara waliopatikana kwenye muembe mkubwa ndani ya shule hiyo, wapo ambao walibaki madarasani wakila kwa macho kutokana na kutopewa chochote na wazazi wao pia walikuwepo ambao walishiba kabisa nyumbani kwao bila ya kuwasahau akina Baraka ambao walifungashiwa vitumbua ama maandazi mikobani mwao.

"B wangu , mbona leo unanikwepa mno? tokea tumefika hutaki hata kuongea na mimi? aliuliza Mamy mara tu baada ya kumfikia Baraka aliyebaki darasani akitafuna andazi lake.

"Mamy kila kitu huwa na mwanzo na hii hali naomba iwe endelevu" alijibu bila kumwangalia usoni.

"Unamaanisha nini? kwa sauti yake yenye mashaka Mamy aliuliza huku akimsoma Baraka aliyekuwa bize kutafuna andazi lake.

"Sitaki mazowea" Baraka alijibu kwa ufupi , ingawa ni maneno mawili ila uzito wake ulikwenda kuvunja moyo wa bibie Mamy.

"Leo hii!" kwa mshangao Mamy aliuliza tena.
"Leo, Kesho , siku zijazo na milele kabisa " Baraka alitilia mkazo.
"Kwanini!" hofu ilizidi kumtawala Mamy.
"Mamy maswali yako hayatabadilisha chochote zaidi ya kuona muda wangu unaupoteza na kuendelea kubaki hapa basi ni kuvunja makubaliano haya, SITAKI UKARIBU NA WEWE" Baraka aliamua kuinuka kabisa alipoongea maneno hayo.

"Nimekukosea Baraka eeeh" kwa sauti iliyoashiria kilio Mamy aliuliza.

"Kosa kubwa ni kujaribu kurekebisha kosa la mtu mwingine na hiki ndio kimekuponza , kaa mbali na mimi"

"Siwezi kuwa mbali na wewe kamwe na wala haitatokea hiyo siku, niambie nani yupo nyuma ya hili" machozi ya uchungu yalisindikiza maneno ya Mamy.

"Usiogope mabadiliko kwani mara nyingi hufanyika haswa wakati ambao huhitajika"

"Kwanini iwe leo? mbona makubaliano yetu sio haya Baraka !! Usiahidi ikiwa huna uhakika kuwa utatimiza ahadi hiyo, kwa sababu maumivu ambayo unasababisha kwa mtu mwingine yatakurudia mapema au baadaye."

"Kati ya maovu mawili, siku zote mimi huchagua moja ambalo sijawahi kujaribu hapo awali, sikuitegemea hii siku ila adhabu yake nipo tayari kuipokea ikiwa nafsi yangu itakua na amani, ipo siku utanielewa Mamy" aliongea kwa ujasiri maneno hayo kuelekea nje akiwa na mkoba wake wa madaftari .

Mamy alibaki na mkono wake ukielea hewani, alijaribu kutaka kumzuia ila alishindwa, alitamani kusema neno ila viungo vilivyohusika vilimgomea, ganzi ya ghafla iliikumba miguu yake na kushindwa hata kupiga hatua kuelekea mbele, alihisi darasa likimuelemea na kumsaliti kwa kushindwa kumzuia Baraka wake, hasira zake za uchungu zilimtuma agonge meza kwa fujo hadi alipokuja kuzuiliwa.

"Mamy umechanganyikiwa? achana na Baraka atakupoteza!! anakuringia kisa uhodari wake? Umesahau kuwa akili bila ya maarifa ni mzigo? Hana tofauti kabisa na watoto wa mitaani kwa tabia zak..... " aliyekwenda kwa lengo la kumbembeleza yalimtoka maneno hadi alipozibwa mdomo wake.

"Monah..... naomba usimuongelee hivo B wangu, hayupo kama unavyofikiria, mimi ndie mwenye makosa nitamfuata ili nipate msamaha wake" Mamy alisema hayo huku akijifuta machozi.

"Ndio unizibe mdomo! mmmh Umerogwa wewe sio bure! fanya kilichokuleta na usijiingize kabisa kwenye hayo mambo, wazazi wako wakijua kuhusu hili jee? haya nenda ukakutane na huyo mamaake mwenye tabia za ajabu" kwa hasira Monah alijibu.

"Jambo muhimu zaidi katika maisha haya ni kusikia kile ambacho hakijasemwa, kama nimeamua kuvuna boga basi jua nipo tayari kubeba na ua lake , Monah hivi unadhani mimi ndio nitakua wa kwanza kuzindua kitu kinachoitwa mapenzi? au kupenda kwangu mimi ndio kutaushangaza ulimwengu?"

USISAHAU LIKE NA COMMENTS YAKO HAPO CHINI, MUITIKO WENU NDIO MWENDELEZO WA SIMULIZI HII

"Mmmh hata kama ila sio kwa Baraka, kwani hakuna wanaume wegine? "

"Ni yeye huyohuyo usiemtaka na wala sitampenda mwingine, nina malengo nae makubwa na kuyatimiza peke yangu siwezi" Mamy alisisitiza msimamo wake.

" Ukithubutu kuinua mguu hizi habari nitazifiisha kwenu na kwa mwalimu Mkandarasi " Monah alimtishia Mamy aliyeanza kupiga hatua.

"Sijawahi kujutia maamuzi yangu na nikiamua sirudi nyuma, simuogopi yeyote ni heshima tu ndio nawatunuku" Mamy alijibu kwa jeuri na kukusanya madaftari yake na safari yake ikianza huku akimwacha Monah na wanafunzi wachache midomo wazi..... Itaendeleaaaaaa.

Kumekuchaaaaa!!!!! Masha kipigo kimemuingia jee atakoma tabia yake? Sadifa wa moto leo, maamuzi ya Baraka yametokana na nini? Mamy safarini kuelekea kwa kina Baraka jee! nini kitatokea? usikose sehemu ijayo.
 
*********
◇ Sehemu ya 11 ◇

USISAHAU LIKE NA COMMENTS YAKO HAPO CHINI MUITIKO WENU NDIO MWENDELEZO WA SIMULIZI HII.

Minong'ono iliyoashiria ugomvi ilisikika nje ya nyumba ambayo ilikuwa na hadhi ya kawaida, sauti ya mwanamke iliizidi ya kiume na kuwafanya wambea wa mtaa wa Jiulize watege masikio yao, naam hiyo ndio Jiulize mtaa wenye wambea wake , walijikusanya ili jioni wakapate cha kusema vibarazani mwao.

"Sasa leo tutakula nini kama hutaki nitoke humu ndani" mzee wa makamo alianza kujishusha mbele ya mkewe ambae alishikilia kitasa cha mlango wa kutokea nje ya chumba chao.

"Tutakula upepo! mwanaume huna aibu hata kidogo , wewe wa kutembea na Sadifa kweli? kila mwanaume anajilia lengo lako nini kwetu? utuue na magonjwa!! " alifoka mwanamke huyo akionekana kuchukizwa vibaya

" Ndaze mke wangu haya si tumeshayaongea tokea jana usiku ! kwani hayajaisha tu? "

"Kirahisi rahisi tu yaishe, wanaume hamuambiliki hata kidogo kwani leo ni mara ya kwanza kuongea haya? Au unataka nikupigie tarumbet....." kabla hajamaliza kauli yake alishtukia kofi zito likitua shavuni mwake.

Uvumilivu wa kutupiwa maneno ulimshinda , aliamua kusimama kwenye nafasi yake, hasira zake zilijionyesha wazi kwenye uso wake, alimsukuma pembeni mkewe ambae alikuwa akiugulia maumivu, alipojaribu kufungua mlango wa chumba chao ili atoke nje alikumbana na kizingiti, mlango ulikomewa.

"Naomba funguo kaba sijakufumua, unaleta ujinga na kazi! tokea alfajiri nakubembeleza hadi jua limesogea katikati ya dunia"

"Sikupi na uniue kabisa, sioni faida ya wewe kwenda kazini ikiwa familia yako tunafikia kulala njaa eti maisha magumu kumbe unawanufaisha wengine!!

"Ndaze nitakuumiza!! nipe funguo nakwambia! kwa ukali aliongea hayo na kumkaribia alipo.

"Sikupi na kama unaniua niue! kheri nikaishi na funza kaburini kuliko kuishi na malay..... " Kofi jingine zito lilimnyamazisha kwa mara nyingine.

Hakuwa na nguvu tena ya kujitetetea zaidi ya kubaki akisubiri rehema ya Mungu, hakukubali kamwe kuutoa kwa urahisi ufunguo ambao aliuficha mapema asubuhi , aliamua liwalo na liwe ila funguo haitatoka.

"Mwanamke mpumbavu kabisa wewee funguo ipo wapii? uhakikishe nikifukuzwa kazi leo na wewe utarudi kwenu" mzee yule baada ya kuchoka kushusha kipigo kilichokosa majibu ya funguo ilipo alibaki kubwata huku akimuangalia mkewe kwa hasira.

"Ndoa thabiti ndio msingi wa jamii endelevu na ishara ya ustawi wa kizazi kijacho, kama hii haina nyenzo hata moja ya kueleweka nisubiri kufanya nini? nipe talaka yangu niondoke na wanangu" kwa sauti ya kilio iliyosheheni hasira Ndaze alijibu huku akijiinua na kwenda kuanza kukusanya vitu vyake.

Mzee yule na yeye kwa vile alimkaribisha sheteni basi alifata kile alichoelekezwa na shetani wake, alichukua karatasi na kalamu juu ya meza na kuanza kumuandikia talaka mkewe , baada ya kukusanya nguo chache kwa mwendo wake uliojaa maumivu alisimama mbele ya mumewe aliyeshika karatasi na kumtazama kwa hasira .

"Ulimwengu ni wa kuchosha kwa watu wenye kuchosha kama wewe, kupitia hili naamini kuwa njia zetu za maisha huwa zinatofautiana na mtu ulienae, wewe umetimiza jukumu lako maishani mwangu na ndio maana hukujali lolote kwa familia yako, nina imani atakaeshika nafasi hii katika maisha yako atakufundisha kitu kingine ambacho hukuwahi kufunzwa na mimi hapo awali, mizigo yangu na wanangu nitawafuata jioni" Ndaze aliongea kwa uchungu na kuivuta karatasi ile kisha akasogea mlangoni akaufungua na kutokomea zake nje huku mumewe akimkodolea macho.

"Usikubali nakwambia! haiwezekani Sadifa akuvunjie ndoa yako uliyoijenga kwa jitihada zote, kwani yeye ni nani Jiulize hii? Au ni sukari kila mwanaume awe sisimizi kwake? mmoja wa wanawake alisema hayo kwa sauti kubwa iliyopenya vyema kwenye masikio ya bi Ndaze aliyevimba uso kwa kipigo ila wala hakumjibu kitu maana alimuona ni mbea tu aliyekua akijizimua.

"Eeeh masikini kumbe umeumizwa namna hiyo! eeeh wanaume wabaya" alidakia mwengine.

**************

Kichwa kiliuma kutokana na kilio cha muda mrefu, macho aliyaona mazito kiasi ambacho alianza kuyafumba ila alishindwa kuzuia mvua ya machozi, angegawana na nani maumivu yake kama sio upweke aliokuwa nao! kama masihara usingizi ulimchukuwa.

Akiwa kwenye usingizi mzito alihisi mtu akimsogelea karibu yake, alimshika bega na kumwita kwa sauti ya chini mno, sauti ya mtu huyo ilipotafsiriwa kwenye ubongo wake aliitambua vyema kiasi ambacho ilimshtua, alitamani kumshika na kumvua kinyago alichovaa usoni ila mkono wake ulikumbwa na ganzi huku mwili wake ukishindwa kumpa mashirikiano .

"Nimehangaika sana kuwa karibu yako hatimae leo hii nimefanikiwa , nitahakikisha furaha haikufikii endapo utakaidi agizo hilii.." aliongea mtu huyo kwa sauti yake nzito.

Alipojaribu kutaka kuuliza alifikaje pale alishindwa hali iliyomfanya aanze kulia, aliushangaa mwili wake kwa kuonyesha udhaifu, aliulaani kwa usaliti huo, kitendo hicho kilimfurahisha aliyepo mbele yake kwa kucheka kicheko kikubwa, hakuishia hapo tu wakati huu yule mtu alimkokota Mamy hadi jikoni kwao , alitamani kuita mama ila sauti haikutoka.

Mamy alishtuka kumuona mtu ambae mwili wake umejaa majeraha kila kona, kilimchomshangaza ni mavazi ambayo hakuwa mageni nayo na ni muda mfupi tu aliyatia machoni, kama ni kidonda alihisi kusuguliwa ndimu moyoni mwake maana dalili za uhai hazikuwepo kabisa.

"Hahaaaa ....... Mamy mimi ni mtu mzuri sana ikiwa utakubaliana na matakwa yangu na pia ni mtu mbaya sana ikiwa utakwenda kinyume na maagizo yangu, nadhani unajua nini nataka kwako hivyo tu naomba unipe mbele ya huyu mdudu wako anaesubiria sekunde chache ahame ulimwengu huu" aliongea mtu yule kisu kikiwa mkononi mwake huku mkono mwingine ukianza kutalii kwenye mwili wa Mamy.

"Tuna dakika kumi tu kufanya kitendo hiki zaidi ya hapo nammaliza kabisa, uhai wake upo mikononi mwako"

Mvua ya machozi ilimuanda.ma Mamy, alitamani kufanya kitu ila mwili ulimkataa hadi mwenyewe alijishangaa siku hiyo alikuwaje, alipomtazama aliyefungwa alikosa cha kuamua maana na yeye hakuwa na cha kujitetea , kwa maana mwili wake ulionyeshea dalili ndogo ya kuendelea kupumua, Mamy alifumba macho akisubiri kupokea adhabu yoyote lakini sio kutekeleza alichoagizwa, aliona ni bora kufa ili amfuate aliye mbele yake.

Dakika tisa zilipita mwanaume yule akiwa makini kumuangalia Mamy jinsi alivyofumba macho, uzuri wake ulimchanganya na kumfaya hasira zimpande kwa kuona jinsi anavyodharaulika mbele ya mtoto yule, zilipobaki sekunde chache alimsogelea Mamy na kumshika hali iliyopelekea mshtuko kwa mguswaji.

"Una sekunde kumi za maamuzi, bila ya hivyo huyu mbwa wako nammaliza mbele yako na mimi nitatekeleza ninachotaka" aliongea kwa ukali mtu yule ingawa Mamy hakuonekana kujali.

Mwanaume yule alihamia kwa kijana mdogo aliyekua mbele yake hali ikiwa dhoofu mno, alianza kukiweka kisu kwenye shingo huku akianza kuhesabu sekunde akianzia kumi kushuka chini, Mamy hilo jambo lilimuumiza na kushindwa kuvumilia , alitamani kupiga kelele ila ilishindikana maana sauti yake ilipotea, alilia kama mtoto masikini, damu zilianza kutoka shingoni kwa kijana yule ambae uhai wake ulitegemea utekelezaji wa agizo alilopewa.

"Barakaaaa!!! Tafadhali usimuue B wangu, nipo tayari kwa lolote " Hatimae sauti yake ilitoka huku akiwa kafumba macho yake, alishangaa kupokea kofi zito lililotua shavuni kwakwe.

"Mamaaa! mara tu baada ya kufumbua macho aliita kwa hofu na maumivu huku akianza kukagua mazingira aliyokuwepo.

"Mamaa! Baraka wangu yupo wapi? aliuliza tena ila hakujibiwa kitu zaidi ya kuongezwa kofi jingine .

Ingawa alikua kwenye maumivu ila kofi la pili lilimtoa kwenye wenge la usingizi, alijigundua kuwa alikuwa kwenye ndoto, alipomtazama mamake bado sura ambayo siku zote hubeba tabasamu leo hii ilikuwa tofauti mno, Mamy hilo lilimpa hofu akiunganisha na makofi ambayo bado yalimpa maumivu , alishangaa siku hiyo mamaake alivyokuwa, mamaake aliendelea kumuangalia kwa hasira.

" Mamaa.. kwani kuna nini mbona sielewi?
"Nyamaza weeh mpumbavu! hivi kwanini unalazimisha nitumie mikono yangu kukuadhibu? malipo ya malezi yangu unataka nijutie mbeleni!! Mamy unaniabisha, ina maana haya ni matokeo ya kukuamini?" kwa sauti ya masikitiko iliyosheheni hasira bi Huba alisema hayo huku akimtikisa mtoto wake.

"Lakini Mamaa mbona sikuelewi, unanipiga tu bila kosa umekuwaje? Mamy alisikitika maneno ambayo yalikwenda kuzidisha hasira za mamaake.

"Nakuonea eeh! umekua mamaa, na hii pia nakuonea....." aliongea kwa hasira bi Huba huku akijipekua kwenye mfuko wa dera na kutoa simu kubwa ya kisasa (smartphone)........... Itaendeleaaaaaa

Kwenye simu kuna nini? Ndoto ya Mamy ina maana gani? Ndoa ya Ndaze imevunjika sababu ni Sadifa, Jee nini kitafuata?


◇ SEHEMU YA 12 ◇

"Lakini Mamaa mbona sikuelewi, unanipiga tu bila kosa umekuwaje? Mamy alisikitika maneno ambayo yalikwenda kuzidisha hasira za mamaake.

"Nakuonea eeh! umekua mamaa, na hili pia nakuonea....." aliongea kwa hasira bi Huba huku akijipekua kwenye mfuko wa dera na kutoa simu kubwa ya kisasa (smartphone).

Macho yake yalibaki yakitazama chini kwa kile alichokishuhudia, hakuwa na ujasiri wa kumuangalia hata mamaake , alimlaani mwalimu Mkandarasi, alimchukia kuliko neno lenyewe ila angefanya nini na ushahidi upo mbele yake , aliona kiasi gani anamburuza Baraka kwenye matatizo jambo ambalo hakutaka litokee ukiangalia bado wana ugomvi.

"Mamaa.." aliita Mamy kwa upole.

"Eeehe una nini chengine cha kunambia, sio wewe huyu! kumbe huyu Baraka ndio anakufanyia hivi ndio maan.... "
" Lakini Mamaa...."

"Kelele mpumbavu mmoja weeh! hivi sisi wajinga eeh? tunakuamini na tulikua tayari kukusaidia ila leo unatulipa haya"

"Lakini mama ungenisikiliza... "

"Huna cha kujitetea kwenye hili na kila kitu kipo wazi! sitalifumbia macho hili jambo, na kuanzia leo nisikusikie kuhusu huyu mpuuzi" bi Huba alisema hayo na kutokomea nje ya chumba cha bintie huku akimuacha Mamy kitandani.

Machozi yalimtoka, moyo ulimuuma, tayari aliona njia za kumsaidia Baraka zinakwenda kujifunga muda sio mrefu, aliona kila dalili za kua mbali na Baraka, alimlaani moyoni mwalimu Mkandarasi kwa tabia zake chafu.

"Ina maana yeye ndio kafikia huku baada ya kuona mipango yake ya kuwa na mimi imefeli? alijiuliza huku akianza kuvuta kumbukumbu siku waliyoitwa ofisini yeye na Baraka.

ILIKUA HIVI........

Kila Baraka alipoweka hatua basi na ya Mamy ilifuata, hakujali kabisa kama mwenzake alichukia mno ila yeye alijisikia fahari kutembea pamoja na Baraka, wanafunzi wote wakiokutana nao njiani waliwatazama kwa mishangao, hata walimu nao waliwasikitika , hatimae ofisini waliingia pamoja jambo ambalo lilimkasirisha tena mwalimu Mkandarasi.

"Kwa hiyo bado mnaendelea kithibitisha kile nilichokiona si ndio? mwalimu Mkandarasi alianza kufoka jambo lilimfanya Baraka amuangalie Mamy kwa jicho la unaniponza.

"Kwani mwalimu si umesema tukufuate! Shida ipo wapi wakati sote kosa letu ni moja " Mamy alijibu haada ya kuona Baraka yupo kimya.

"Yaani wewe ndio unamtetea huyu mjinga! atakuharibia na mwisho wake utakua na hasara tup...... "

"Lakini mwalimu mbona mimi sij....." Baraka alijaribu kujitetea ila alinyamazishwa na sauti ya ukali kutoka kwa Mwalimu wake.

"Kelele ngedere weweeh.. toka na usubiri hapo nje , akitoka huyu utaingia wewe" Kauli hiyo ilikwenda kuwashangaza wote , walitazamana na Baraka bila ya ubishi alianza kutoka na kuwaacha.

"Wewe binti una kiburi mno, ulikuja hapa ukiwa na adabu zako ila siku hizi umechachuka, Baraka anakupotosha na usipokua makini utapotea na wewe pia" aliongea mwalimu Mkandarasi akiwa kwenye kiti chake huku Mamy yeye alisimama vilevile.

"Bila kiburi hutamshinda shetani, lakini kiburi dhidi ya shetani unakishinda kwa hekima,mwalimu ni kweli nimefanya makosa ila haya yametokana na wewe mwenyewe! kila mtu dunia hii ana kiburi ila hukionyesha pale ambapo panastahili, nachukia mno kuona walimu wengi mnamuandama Baraka kwa maneno mabay......"

"Kumbe ulitakaje? "

" Ehee...... sisi sote ni watoto na tumeletwa hapa kwa lengo la kupewa elimu, elimu hii isiwe ya vitabuni tu bali hata namna ya kuishi na watu, mnapaswa kutuuliza changamoto zetu hasa pale mnapoona mwendo wetu umebadilika, hakuna aliye upande wa Baraka ndio maana nimeamua mimi kua kwake" aliongea Mamy kwa uchungu huku machozi yakianza kumtoka .

"Ndio ukaribu wako ukakufanya ufikie hatua hii? ndio sheria ya shule inataka hivi? wewe mtetezi eeh.... umetumwa kutufundisha kazi si ndio, sasa kuna mawili hapa.... " mwalimu Mkandarasi alisita ili amsikilize Mamy atasema nini ila alibaki kimya.

"Hizi picha zipo mikononi mwangu na hakuna ambae nitamweleza akawa upande wa kwenu, sasa basi chagua mawili kati ya haya...... KUWA NA MIMI KIMAPENZI au KESI IFIKE UONGOZI WA JUU" maneno hayo ya mwalimu Mkandarasi yalikwenda kumshtua Mamy aliyeweka umakini kumsikiliza .

"Unasemaje....!

"Nadhani umesikia vizuri na ndio maana umerudia kutaka uhakika, Mamy wewe ni Binti mrembo mno kwanini unasumbuka na Baraka? atakupa nini? njoo kwangu mtoto mzuri eeeh... "aliongea maneno hayo huku akisimama na kumsogelea.

Jicho la chuki lilimuangukia mwalimu yule, Mamy alichafukwa baada ya kusikia kauli zile, haikua kauli ngeni kuisikia kwa Mwalimu yule ila ilimuuma kuona inapakatishwa na Baraka, alijiandaa kutoka nje bila kutoa jibu ila mkono wake ulidakwa .

"Athari za hasira ni kubwa zaidi kuliko sababu zake, usipotumia akili utampoteza Baraka kwa maana hii kesi ikifika juu sifikirii kama yule mamaake anaweza kufika hapa, na huo ndio utakua mwisho wake... kubali uwe wangu Mamy nitakupa kila kitu na hii itabaki kuwa siri kwetu "

"Hata ukifunga milango ya makosa yote basi juwa ukweli utaachwa na ipo siku utajifichua, sipo tayari kabisa na huo upuuzi wako, fanya lolote" Mamy aliongea kwa ujasiri na kujitoa mikononi mwa mwalimu yule kisha akaondoka zake .

Nje alikutana na kijana Baraka aliyekua kwenye dimbwi la mawazo , kichwani mwake sio moja wala mbili iliyokaa, alishtuliwa na mkono mlaini uliotua usoni mwake sehemu ya shavu.

"Mtu husimama, hasimamishwi! Baraka... wakati mwingine ni bora utu na utulivu kuviweka mfukoni ili ufanikiwe"Mamy aliongea kwa fumbo na kuondoka zake, wakati huo alichafukwa na hakutaka stori kabisa .

Baraka alibaki kujikuna tu asijuwe alichoambiwa, alijua bila shaka ndani kulichimbika , alimuelewa vizuri Mamy jinsi asivyopenda kushindwa, haraka alizichanganya hatua zake baada ya kusikia purukushani za mwalimu Mkandarasi akipiga meza ovyo ofisini mwake.

Ni kama alijitafutia adhabu maana mara tu alipoingia alishtukia kofi zito likitua shavuni mwake, alipotaka kujitetea aliamrishwa kulala chini, hakuwa na mana alifanya kile alichoambiwa huku machozi yakimtoka, fimbo zisizo na idadi zilimshukia, alipigwa akapigika hadi mwalimu alipotosheka, Baraka hakupiga kelele hata moja maana tayari alijua kosa lake , hivyo alihofia kujaza watu na mwisho wa siku kesi ikawa kubwa kwao.

"Nisikilize wewe mtoto wa malaya uliyekosa malezi, kama mamaako ndio kakufundisha hii tabia basi baki nayo mitaani, sitaki ukaribu wowote na Mamy na endapo nikiwaona basi huo utakua ndio mwisho wako wa kujisomea shule hii... " maneno ya mwalimu Mkandarasi yalikwenda kuzidisha maumivu kwenye moyo wa Baraka, hakupenda mamaake kuhushishwa kwenye tabia zake ila angefanya nini na kweli?

"Sawa Mwalimu ingawa nipo na makosa ila hukutakiwa kumhusisha Mamaangu, mimi nitakua mbali na Mamy na wala sitomkaribia na asante kwa adhabu maana nimetambua kuwa wajibu wangu mkuu ni kuwa na nidhamu na kuirekebisha silka yangu nikiwa shuleni " Baraka alisema hayo huku akijifuta mavumbi na machozi yaliyogoma kutokutiririka mashavuni mwake.

"Ewalaaa ...... na mwisho usisahau kuwa Mamy haendani na wewe hata kidogo, utampa nini? hem toka nje" maneno hayo yalimzidisha hasira Baraka na kutoka ofisini humo machozi yakiwa bado yamemuandama.

"Nimeukosea nini ulimwengu? kwanini mama ulinizaa? ona sasa tabia zako napewa mimi au ndio mtoto wa nyoka hawi mjusi! aagh mamaaaa!!! naapa kukaa mbali na Mamy ili nitimize ndoto zangu, natakiwa kusimama mwenyewe kama ambavyo Mamy kasema" Baraka alisema na nafsi yake huku akielekea usawa wa vyoo .

Mamy alimfuata hukuhuko kumuuliza ilikuwaje ila hakuambulia kitu zaidi ya Baraka kuomba aachwe peke yake, Mamy alibembeleza sana ila alishindwa kumtoa Baraka chooni mwisho wa siku aliamua kuondoka na kurudi darasani.
USISAHAU KUWEKA LIKE NA COMMENTS YAKO HAPO CHINI, MUITIKO WENU NDIO MWENDELEZO WA SIMULIZI HII.
Na huo ndio uikuwa mwisho wa kumbukizi ya Mamy, alikumbuka alichoambiwa na Mwalimu Mkandarasi, alizingatia na ndoto aliyoota alijumlisha na matendo yaliyoonyeshwa na Baraka shuleni hadi kufikia hatua ya kuondoka kabla ya muda, alishusha pumzi ndefu na mwisho aliamua kumfuata mamaake ili ajitetee...... Itaendeleaaaaaa

Walimu hao!!! Hiki ndicho kilitokea kumbe? uamuzi wa Baraka ni sahihi? Jee Mamy atasikilizwa na mamaake? usikose sehemu ijayo....
 
◇ Sehemu ya 13 ◇

Endeleaaaa..

Kwa vile tayari ilikuwa ni muda wa jioni ya saa kumi na moja basi alimshuhudia mamaake jikoni akiandaa chakula, alijisogeza na kutengeneza kikohozi cha uongo ila mamaake hakugeuka, alijua leo kazi anayo hata hivyo hakutaka kushindwa, alimsogelea karibu na kumkumbatia kwa nyuma.

" Mamaa , siku zote unasema yule ambae anahukumu bila ya kuusikiliza upande wa pili hata akitoa hukumu sahihi hawezi kuitwa hakimu" Mamy alianzisha mada huku bado akiwa mgongoni kwa mamaake aliyesimama.

"Ibadilikapo ngoma basi na mdundo hubadilika , kuna muda maamuzi huhitajika zaidi kuliko maelezo, Mamy hivi unajielewa kweli wewe mtoto ? unanitia aibu! babaako akiona hizi picha si utaleta balaa hapa ndani? juzi tu hapa uliponea chupuchupu na nikakutengezea mazingira mazuri hadi babaako alifurahi , unadhani akiona huu upuuzi itakuwaje? " aliongea bi Huba akiacha mchele uliokuwa kwenye ungo na kumgeukia bintie.

" Najua nimekosea mama ila vizuri ungenisikiliza, nipe nafasi basi Mamaangu" Mamy alideka.

"Unataka kusema nini? kwamba yule sio wewe? Mamy mimi ni mtu mzima na hayo yote nilipitia unataka kunidanganya nini? basi hilo kataa , Jee leo umerudi shule muda gani? " bi Huba aligeuza kibao.

" Nimerudi mapema kwa sababu nilikuwa sijisikii vizuri mama" aliamua kudanganya huku macho yakiwa chini .

" Nyote hamkua vizuri wewe na Baraka wako! Mamy unanidanganya mimi mamaako? najua kila kitu kuhusu wewe na hata mlipopishana kauli na Monah kisa huyo Baraka pia najua... "

"Heeh Monah " aliita kwa hasira.

"Habari ndio hiyo na hili halitaishia hapa , nikuone utoe miguu yako hapa kwenda kwao, kumtetea kote kule kumbe mna yenu? bi Huba alifoka na kumfanya Mamy aondoke kwa hasira kuelekea chumbani mwake.

********

Taratibu alijisogeza alipokua mamaake aliyekuwa akiandaa chakula cha usiku , alichukua matembele mawili na kuanza kumsaidia kuchambua , bi Sadifa alimuangalia kijana wake kwa jicho la huruma, alijua anayopitia ila hakuona msaada wowote wa kumsaidia maana ya kwake tu yalimuendesha.

"Mwanangu..... hivi ndio yale ya jana tu au kuna zaidi? maana shule umerudi mapema, umelala zako hadi muda huu unajilazimisha kutengeneza tembele! "

"Lakini mamaa, unadhani ni rahisi kuyatoa akilini yale yaniumizayo , kila siku huwa ni ngumu kwangu na afadhali yake ikiwa ni jana! "

"Utangoja hadi lini ili ufikie ubora wako na utasubiri hadi lini ili uamini kuitumia akili yako kufanya mambo yako? Baraka simama na kile unachokiamini na wala maneno ya watu yasikurejeshe nyuma"

" Ni kweli hayo usemayo mama, ila unadhani nitaendelea vipi na safari ikiwa tabia zako ndio zinanikwamish.... " kabla ya kumalizia kauli yake Baraka aliwashwa kibao kitakatifu.

" Umekua eeeh! hivi hujui kama hizi tabia zangu ndio zinakufanya uendelee kupumua, nakuhudumia kila kitu kwa hiihii tabia yangu, unadhani nitaishije bila kufanya hivi? babaako lini umemuona hapa akakuletea matumizi ni mimi mwenye tabia chafu ndio nakuhudumia kila kitu , weeeh mtoto na unyamaze usinitibue nadhani unanijua vizuri " Mama Baraka alikua mkali kupitiliza.

"Nipeleke basi huko kwa babaangu, mama unaniumizaaa! kwanini mimi tu kila siku aaaagh....." aliongea kwa hasira na kuniunuka pale kwa kasi ili aingie chumbani kwake ila kabla hajalifikia pazia lake ulisikika ugongwaji wa fujo kwenye mlango wao wa bati.

Walitazamana mtu na mamaake ila hilo kamwe halikubadili kilichoendelea nje, bi Sadifa alishusha mchuzi wa dagaa ambao ulikuwa unaelekea kukauka, alimpa ishara ya kuingia ndani Baraka wake na yeye bila ya ubishi alitii.

"Nani tena hawa jioni hii? mbona kama sidaiwi!" alijiuliza huku akiusogelea mlango wake.

Umati wa watu ulionekana mara tu baada ya kufungua mlango wake, chupa za maji zilimsalimu pale alipoelekeza uso wake kwa watu hao, alirowa tepetepe, akiwa anajifuta maji alivutwa dera ambalo wavutaji walilichana sehemu ya ziwa, hatimae mambo hadharani! aliwekwa mtu kati mithili ya kibakuli cha mchuzi kwenye sahani ya ugali, Kumekuchaaaaa!!!!

"Malaya mkubwa wewee! kazi kuiba waume za watu tuu! kama ni rahisi kwanini usitafute wa kwako ukaishi nae! mtaa mzima unatajika kuvunja ndoa za watu looh! sitokubali nakwambia kama mimi ndoa yangu imekufa basi nahakikisha na wewe leo unakufaa" huyo ni Ndaze ambae uso wake ulifura kwa hasira jumlisha na kipigo alichopewa asubuhi mbona alipendeza, maneno yake yaliwafanya wapambe wake wapige vigelegele vya kufurahia lile jambo.

Alijipanga kisawasawa bi Ndaze maana hapohapo aliamrisha wenye ngoma waamshe waliolala, watu walicheza , mauno hadharani yaani nyama na mifupa zilisurubika vibaya, huku ndio uswahilini bwana! mauno yalipelekwa pande zote za dunia, Sadifa alipatikana maana kila mmoja alimnyambua alivyojisikia , alizodolewa hiyo siku akazodoleka, alitulia kama sio yeye .

"Muone vilee, ukimuona na sura yake ya huruma kumbe fisadi kama yeye hakuna na leo hii nitakupiga kama ngoma nilipize ulichonifanyia sokoni mchawi mkubwa weeeeh" huyo alikua ni Masha ambae na yeye hadi muda huo uso wake haukua sawa.

" Na mimi leo ndio namalizia hasira zote kila siku mume wangu akirudi anadai kachoka haki yangu hanipi kumbe huyu malaya ndio anamroga na madawa yake na kummaliza nguvu zote " alidakia mwanamke mwengine ambae na yeye alikuwa miongoni mwa waliomzunguka.

Kila maneno yaliyotamkwa Baraka aliyasikia na kila alipomaliza kusema mmoja wao basi goma lingepigwa na mamake akapewa kipigo, roho ilimuuma na nafsi ilimtuma atoke nje akamsaidie mamaake, nafsi nyingine ilimtaka abaki ndani ili mamaake afunzwe adabu pengine ikawa sababu ya kubadilika ila alikumbuka kuwa ile haikua mara ya kwanza, hapohapo alibadili maamuzi baada ya kukumbuka kuwa yule ni mamaake hata awe na makosa gani bado atabaki kwenye nafasi yake, alijiambia yeye anapaswa kuwa mtetezi wa mamaake hivyo alitoka nje

Uzalendo ulimshinda baada ya kumuona mamaake akiwa chini akichezea kipondo, asilimia kubwa ya mwili wake ulikua wazi kutokana na nguo zake kuchanwa, kila mtu alimpiga alivyotaka yeye, ni yeye Sadifa siku hiyo hakujaribu kurusha hata ngumi moja, Baraka alifika hadi katikati ya umati ule, alipojaribu kuwavuta wanawake wale alijikuta akitupwa pembeni, ama kweli siku ya kufa nyani miti yote huteleza! Baraka alibaki akilia

Kwa mbali Baraka alimuona bi Mwinde akirejea shambani kwake na mzigo wa kuni kichwani, haraka alimkimbilia na kumuomba akamsaidie mamaake , bi. Mwinde aliwakimbilia wale wapiga ngoma na kuwataka wazime mziki, Baraka alichomoa kuni mbili refu na kukimbilia hadi alipo mamaake na kuanza kutembeza kipigo kwa wanawake wale waliaonza kujikuna na kuugulia maumivu, Baraka alihakikisha wote anawatembezea kipigo huku bi Mwinde akimvuta Sadifa na kumuingiza ndani mwake kwa ajili ya kwenda kumsitiri , haraka Baraka na yeye hakubakia maana alikijua kitakachofuata endapo atakamatwa.

"Washenzi wakubwa nyie, hii ni rasharasha tu mvua kamili ipo njiani" alifoka bi Masha.

"Na lazima hii nyumba tuichome motooo" bi Ndaze aliongea huku akipumua kwa kasi kutokana na hasira alizokua nazo jumlisha na kichapo alichoshusha.

"Na badoo! tulitaka tukuvue nguo zote hizo tuone ulichopewa wewe sisi tukanyimwa" mwengine nae hakua nyuma.

Mziki uliishia hapo na kila mmoja alitafuta njia ya kwao, Sadifa alikuwa hoi huku akipumua kwa shida mno, Baraka na yeye alibaki akilia huku akimkanda mamaake na kumfuta baadhi ya sehemu za mwili , kwa mwendo wa kunyata bi Mwinde alitoka nje lengo ni kwenda kutafuta dawa ili aje amsaidie bi Sadifa..... Itaendeleaaaaaa

Sadifa kachezea kipigo cha kufa mtu, hivi ni yeye kweli? Jee akipona ataacha tabia yake au ndio sikio la kufa? Ugumu na vizingiti vinazidi kuwekwa juu ya Mamy na Baraka jee unahisi nini
kinakwenda kutokea? see u next.

◇ Sehemu ya 14 ◇

Mawingu yaliyoashiria uangukaji wa matone ya mvua muda mfupi ujao yalitanda kwenye anga la ardhi ya Jiulize , bila ya shaka ilikuwa ni Ijumaa yenye baraka kwa wale ambao walikua na mazao yaliyohitaji maji shambani kwao, pia ilikua ni kero kwa wale wauza biashara zao soko kuu la Jiulize ndani ya Jiji kubwa la Tuleane, ndio hivyo kila mmoja alilia mamaake.

Tayari muda wa darasani uliwadia, wanafunzi walikua tayari kumsubiri mwalimu wao awape kile alichowaandalia asubuhi hiyo, Mamy hakuwa miongoni mwa wanafunzi wenye hamu ya kupokea chochote kutoka kwa walimu wake , shingo yake haikutulia kila muda alitazama nje, hata pale ilipombidi kusimama pia hakuacha maana alifika hadi mlangoni na shingo yake kuzama nje, hakuona kitu zaidi ya wingu zito lililotanda, alichoka kuona kile alichokitarajia hakukipata , alirudi mdogo mdogo huku mwili wake ukimnyong'onyea na kukaa kwenye kiti machozi yakianza kumtoka , saa ngapi asichekwe na wanadarasa, alizodolewa na kuzomewa pia hadi pale mwalimu wa kipindi alipoingia.

" Basi hadi shule kupewa jina la Someni ila watoto bado hamuoni? mwalimu kuchelewa kidogo tu ndio imekua sababu ya kila mtu kuleta simulizi za nyumbani kwao! sijui mtabadilika lini nyinyi watoto au ndio mna akili kama za wazazi wenu! alifoka mwalimu yule wa kike aliyejulikana kwa jina mwalimu Swami.

" Hakuna viumbe wenye kazi ngumu kama sisi walimu, yaani kulea akili ambayo haiendani na vinasaba vyako ni shida! Sasa mpige mtoto wa mtu hapa weeh unakuja kuletewa kigodoro nyumbani kwako umepumzika, toeni madaftari yenu ya sayansi msinitolee mimacho" alizidi kufoka mwalimu huku akitoa kitabu na kuweka mezani.

"Ehee...Kabla ya kuanza darasa letu, ningependa tujikumbushie tulichosoma siku ya Jumatatu bila ya kuangalia kwenye daftari, nitakaemuona anachungulia nitamramba fimbo, ehee Monah Jumatatu niliwafundisha nini? aliongea mwalimu Swami huku akimyooshea kidole Monah aliyekua mbeleni mstari wa kati.

"Hewa" alijibu bila ya uoga mara tu aliposimama.

"Nzuri sana , hivi unaweza kutupa na maana yake mtoto mzuri?

"Hewa ni mchanganyiko wa gesi tofauti zisizoonekana na zinazunguka katika anga"

"Mpigieni makofi jamani, yaani wanafunzi wote mngelikua hivi basi ningejivunia hili darasa " aliongea mwalimu yule na kelele za pongezi zikimshukia Monah aliyekaa kwa pozi, angalau tabasamu lilirudi kwa Mwalimu yule.

"Aanh Monah mchague rafiki yako kipenzi atutajie sifa za hewa" kauli ya mwalimu huyo ilimfanya Monah amuangalie Mamy aliyekua mbali kimawazo , alicheka kwenye nafsi yake na mwisho wa siku alikua tayari kumuumbua kipenzi chake.

"Mamy naomba ututajie sifa za hewa" Monah aliongea kwa sauti jambo ambalo liliwafanya wanafunzi wote kutupa macho yao alipokuwa Mamy wakisubiri jawabu.

Aliyeulizwa swali hakuwa darasani kiakili ingawa macho yake yalikuwa mbele, mwalimu Swami na wanafunzi wote walibaki wakimtazama bila ya kusema chochote, wale walioshindwa kuvumilia waliamua kucheka, mwalimu alichukia na kuwapa ishara ya kufumba midomo yao, taratibu alisogea hadi alipokua Mamy na kumshtua kwa bakora nzito iliyotua mwilini mwake.

"Aaagh.... mwalimuuuuu" Alilalamika Mamy kwa sauti ya uchungu.

"Unawaza nini wewee! ahaaa ni Baraka leo hayupo ndio kaondoka na akili zako" aliyasema hayo baada ya kugundua kuwa Baraka hakuwepo.

"Sio hivo mwalimu sijisikii vizuri tu , nahisi kichwa kinauma" alijitetea .

"Uongo ukizidi sana huondosha ladha ya uaminifu ulioupika siku nyingi , Ondosha matamanio kabisa kwa maana yule akitamaniye kitu na asikipate huingiwa na huzuni, Mamy bado upo safarini, na safari hii ili ufanikiwe basi unapaswa kujiepusha na yale yaliyo nje ya uwezo wako" Madam Swabi alishusha darasa kwa bibie Mamy aliyebaki mpole.

"Mwalimu najua unanitakia mema mwanafunzi wako ila ingependeza zaidi wema huo ungeugawa kwetu sote, Baraka na yeye ana haki kama sisi, matatizo ya familia yake isiwe chanzo cha kuonekana hafai" Mamy alifunguka.

"Hakuna ambae anataka mwanafunzi wake aanguke isipokua wazazi wenu wanarejesha nyuma, mama Baraka alishaonyeshwa nyota mara nyingi ila yeye hukiangalia kidole tu Jee! unadhani tutafika? Sisi ni kama mayai tu ila yule mama ni jiwe hivi unadhani yupo wa kushindana nae?

Mamy alibaki kimya, kiukweli hakuwa na cha kumtetelea B wake, alikiona kiza kinene mbele yake baada ya kuona hata walimu wameyakatia tamaa maisha ya Baraka licha ya uhodari aliokua nao , aligonga meza kwa hasira hadi mwalimu na wanafunzi walishangaa, kitendo hicho kilimfurahisha Monah maana hadi hapo tayari aliona nafasi ya Mamy ataichukua yeye, mwalimu nae hakufurahishwa na tukio hilo hivyo aliamua kuondoka na vitabu vyake huku darasa likiishia hapo.

"Yaani ujinga wa mtu mmoja unatukosesha kipindi kweli? hivi wewe Mamy unajikuta kama nani darasa hili! kwa mwendo wake wa madaha Monah alisema hayo huku akisogea alipo Mamy ila hakujibiwa kitu .

"Tumewachoka na Baraka wako ikiwezekana mutafute shule nyingine, kila siku walimu wanaingia na kutoka bila kusomesha kitu kisa mapenzi yenu nyinyi , yule mtoto wa malaya atakupa nini wewe? mwengine na yeye uvumilivu ulimshinda.

"Tuheshimiae Devo, sitaki tukosane hata kidogo, kama walimu kutokusomesha mimi sio sababu ila ni tabia zao wenyewe " Mamy uvumilivu na yeye ulimshinda.

"Wewe na huyo mpumbavu wako ndio sababu na kamwe huwezi kuliepuka hili? mwalimu gani angevumilia vitendo vyenu, ulikua mwema ila sasa hivi walimu watakuona wa ovyo na usipozingatia mwisho wa siku na wewe utapelekwa kwenye madanguro badala ya shul...... " kabla Monah hajamaliza maneno yake alishtukia kofi zito shavuni mwake.

Ngumi zilianza kurushwa darasani, walivutana nywele mpaka na sare kuchanika, Mamy siku hiyo alikuwa wa moto jumlisha na hasira alizotoka nazo kwao mbona alikiwasha, shangwe la wanafunzi lilikua kubwa wakifurahia mapigano yale, Monah chalii.... alirembelewa mbele ya darasa ikisha Mamy alimfuata hukuhuko na kusimama mbele yake.

"Si kila jicho lililofumba ukajua limelala, nilikuona mwenzangu kumbe ni mnafiki mkubwa, nimekuvumilia sana wewe ila bado unaendelea kuyachimba maisha yangu, hadi kwenye familia yangu umepakaza huu ufisadi ili ukusaidie nini? na hili kaseme basi! na bado ...... nitapambana hadi nijue mwisho wa Baraka" Mamy alimtambia Monah.

"Hujui ulitendalo Mamy ila nakuapia mwisho wa hii tabia yako ni majuto, utakufa kwa ukimwi siku sio nyingi, ile sio familia hata ya kuombea maji ya kunywa ila wewe unajifanya kuvamia mji yatakukuta, hii ndio Jiulize" Monah alitaka kuinuka kwa hasira ila aliwekwa chini.

"Najua sana ninachokifanya na wala sitajutia kwa litakalonikuta , maisha yangu hayakuhusu hivyo naomba kaa mbali kabisa"

"Maisha yako yananihusu maana huyo ambae unampapatikia basi mamaake kaivunja ndoa ya wazazi wangu, tumeanza kuishi bila baba hivyo na yeye ajiandae kuishi bila ya Elimu" kwa hasira na yeye Monah alijibu na kujipangusa vumbi kuelekea nje

Maneno ya Monah mwishoni yalimmaliza nguvu Mamy, alihisi dunia inazidi kumuelemea , kila likiondoka moja la pili linasogea, hadi kufika hapo tayari alikijua chanzo cha chuki kati yake na Monah.

"Na usichokijua jana mama Baraka alifungiwa mtaa na bi Ndaze (mama Monah) , alipigwa akapigika, alichambwa akachambika, alivuliwa nguo zote hadharani kiufupi alikomeshwa, na asipoacha hiyo tabia basi yule mama ni kiboko" mmoja wa wanafunzi wa kike alimsogelea Mamy na kumdadavulia kilichojiri.

Mamy alizidi kuchoka baada ya kusikia habari hizo, hakuona sababu ya kuendelea kubaki pale, kwa vile tayari aliyavulia nguo basi hakuona tabu kuyakoga, alibeba begi lake na safari ya kwa kina Baraka ikaanza, alijua kipenzi chake kilikua kwenye wakati mzito na vile wanaishi peke yao basi alitaka awe pembeni yake.

*******
Bi Sadifa alilala kwenye mkeka uliochakaa sebuleni kwake, kichwa chake kilikua mapajani mwa mtoto wake, bakuli dogo jekundu lililosheni maji yaliyochanganywa na majani yaliyosadikika kuwa ni dawa lilikuwa mikononi mwa Baraka, alijitahidi kumywesha mamaake ambae alionekana kukata tamaa .

"Mama jitahidi basi umalizee, hali yako kidogo inaridhisha tofauti na jana" alibembeleza Baraka akimtazama kwa umakini mamaake.

"Siwezi Baraka, mwili wote huu unaniuma, hata huu mdomo kuunyanyua siwezi nauhisi mzito mno" Alilalamika bi Sadifa.

"Lakini mama haya yote umeyataka wewe, kwanini hubadiliki? sio mara ya kwanza hii mamaangu, kama ndio kuna sababu inakufanya hivi kwanini huniweki wazi? Yaani mtaa mzima huu mamaangu tunanuka na tabia zako chafu, nimechokaa!! hadi natamani kuf...... "

"Barakaa........ " Itaendeleaaaaaa

Hatimae Baraka atema nyongo kwa mamaake ila kuna sauti iliyoita jina lake imemsitisha kuendelea , Monah na Mamy waanzisha bifu , nini kinakwenda kutokea kwenye simulizi hii ya kusisimua.
 
Back
Top Bottom