◇ Sehemu ya 13 ◇
Endeleaaaa..
Kwa vile tayari ilikuwa ni muda wa jioni ya saa kumi na moja basi alimshuhudia mamaake jikoni akiandaa chakula, alijisogeza na kutengeneza kikohozi cha uongo ila mamaake hakugeuka, alijua leo kazi anayo hata hivyo hakutaka kushindwa, alimsogelea karibu na kumkumbatia kwa nyuma.
" Mamaa , siku zote unasema yule ambae anahukumu bila ya kuusikiliza upande wa pili hata akitoa hukumu sahihi hawezi kuitwa hakimu" Mamy alianzisha mada huku bado akiwa mgongoni kwa mamaake aliyesimama.
"Ibadilikapo ngoma basi na mdundo hubadilika , kuna muda maamuzi huhitajika zaidi kuliko maelezo, Mamy hivi unajielewa kweli wewe mtoto ? unanitia aibu! babaako akiona hizi picha si utaleta balaa hapa ndani? juzi tu hapa uliponea chupuchupu na nikakutengezea mazingira mazuri hadi babaako alifurahi , unadhani akiona huu upuuzi itakuwaje? " aliongea bi Huba akiacha mchele uliokuwa kwenye ungo na kumgeukia bintie.
" Najua nimekosea mama ila vizuri ungenisikiliza, nipe nafasi basi Mamaangu" Mamy alideka.
"Unataka kusema nini? kwamba yule sio wewe? Mamy mimi ni mtu mzima na hayo yote nilipitia unataka kunidanganya nini? basi hilo kataa , Jee leo umerudi shule muda gani? " bi Huba aligeuza kibao.
" Nimerudi mapema kwa sababu nilikuwa sijisikii vizuri mama" aliamua kudanganya huku macho yakiwa chini .
" Nyote hamkua vizuri wewe na Baraka wako! Mamy unanidanganya mimi mamaako? najua kila kitu kuhusu wewe na hata mlipopishana kauli na Monah kisa huyo Baraka pia najua... "
"Heeh Monah " aliita kwa hasira.
"Habari ndio hiyo na hili halitaishia hapa , nikuone utoe miguu yako hapa kwenda kwao, kumtetea kote kule kumbe mna yenu? bi Huba alifoka na kumfanya Mamy aondoke kwa hasira kuelekea chumbani mwake.
********
Taratibu alijisogeza alipokua mamaake aliyekuwa akiandaa chakula cha usiku , alichukua matembele mawili na kuanza kumsaidia kuchambua , bi Sadifa alimuangalia kijana wake kwa jicho la huruma, alijua anayopitia ila hakuona msaada wowote wa kumsaidia maana ya kwake tu yalimuendesha.
"Mwanangu..... hivi ndio yale ya jana tu au kuna zaidi? maana shule umerudi mapema, umelala zako hadi muda huu unajilazimisha kutengeneza tembele! "
"Lakini mamaa, unadhani ni rahisi kuyatoa akilini yale yaniumizayo , kila siku huwa ni ngumu kwangu na afadhali yake ikiwa ni jana! "
"Utangoja hadi lini ili ufikie ubora wako na utasubiri hadi lini ili uamini kuitumia akili yako kufanya mambo yako? Baraka simama na kile unachokiamini na wala maneno ya watu yasikurejeshe nyuma"
" Ni kweli hayo usemayo mama, ila unadhani nitaendelea vipi na safari ikiwa tabia zako ndio zinanikwamish.... " kabla ya kumalizia kauli yake Baraka aliwashwa kibao kitakatifu.
" Umekua eeeh! hivi hujui kama hizi tabia zangu ndio zinakufanya uendelee kupumua, nakuhudumia kila kitu kwa hiihii tabia yangu, unadhani nitaishije bila kufanya hivi? babaako lini umemuona hapa akakuletea matumizi ni mimi mwenye tabia chafu ndio nakuhudumia kila kitu , weeeh mtoto na unyamaze usinitibue nadhani unanijua vizuri " Mama Baraka alikua mkali kupitiliza.
"Nipeleke basi huko kwa babaangu, mama unaniumizaaa! kwanini mimi tu kila siku aaaagh....." aliongea kwa hasira na kuniunuka pale kwa kasi ili aingie chumbani kwake ila kabla hajalifikia pazia lake ulisikika ugongwaji wa fujo kwenye mlango wao wa bati.
Walitazamana mtu na mamaake ila hilo kamwe halikubadili kilichoendelea nje, bi Sadifa alishusha mchuzi wa dagaa ambao ulikuwa unaelekea kukauka, alimpa ishara ya kuingia ndani Baraka wake na yeye bila ya ubishi alitii.
"Nani tena hawa jioni hii? mbona kama sidaiwi!" alijiuliza huku akiusogelea mlango wake.
Umati wa watu ulionekana mara tu baada ya kufungua mlango wake, chupa za maji zilimsalimu pale alipoelekeza uso wake kwa watu hao, alirowa tepetepe, akiwa anajifuta maji alivutwa dera ambalo wavutaji walilichana sehemu ya ziwa, hatimae mambo hadharani! aliwekwa mtu kati mithili ya kibakuli cha mchuzi kwenye sahani ya ugali, Kumekuchaaaaa!!!!
"Malaya mkubwa wewee! kazi kuiba waume za watu tuu! kama ni rahisi kwanini usitafute wa kwako ukaishi nae! mtaa mzima unatajika kuvunja ndoa za watu looh! sitokubali nakwambia kama mimi ndoa yangu imekufa basi nahakikisha na wewe leo unakufaa" huyo ni Ndaze ambae uso wake ulifura kwa hasira jumlisha na kipigo alichopewa asubuhi mbona alipendeza, maneno yake yaliwafanya wapambe wake wapige vigelegele vya kufurahia lile jambo.
Alijipanga kisawasawa bi Ndaze maana hapohapo aliamrisha wenye ngoma waamshe waliolala, watu walicheza , mauno hadharani yaani nyama na mifupa zilisurubika vibaya, huku ndio uswahilini bwana! mauno yalipelekwa pande zote za dunia, Sadifa alipatikana maana kila mmoja alimnyambua alivyojisikia , alizodolewa hiyo siku akazodoleka, alitulia kama sio yeye .
"Muone vilee, ukimuona na sura yake ya huruma kumbe fisadi kama yeye hakuna na leo hii nitakupiga kama ngoma nilipize ulichonifanyia sokoni mchawi mkubwa weeeeh" huyo alikua ni Masha ambae na yeye hadi muda huo uso wake haukua sawa.
" Na mimi leo ndio namalizia hasira zote kila siku mume wangu akirudi anadai kachoka haki yangu hanipi kumbe huyu malaya ndio anamroga na madawa yake na kummaliza nguvu zote " alidakia mwanamke mwengine ambae na yeye alikuwa miongoni mwa waliomzunguka.
Kila maneno yaliyotamkwa Baraka aliyasikia na kila alipomaliza kusema mmoja wao basi goma lingepigwa na mamake akapewa kipigo, roho ilimuuma na nafsi ilimtuma atoke nje akamsaidie mamaake, nafsi nyingine ilimtaka abaki ndani ili mamaake afunzwe adabu pengine ikawa sababu ya kubadilika ila alikumbuka kuwa ile haikua mara ya kwanza, hapohapo alibadili maamuzi baada ya kukumbuka kuwa yule ni mamaake hata awe na makosa gani bado atabaki kwenye nafasi yake, alijiambia yeye anapaswa kuwa mtetezi wa mamaake hivyo alitoka nje
Uzalendo ulimshinda baada ya kumuona mamaake akiwa chini akichezea kipondo, asilimia kubwa ya mwili wake ulikua wazi kutokana na nguo zake kuchanwa, kila mtu alimpiga alivyotaka yeye, ni yeye Sadifa siku hiyo hakujaribu kurusha hata ngumi moja, Baraka alifika hadi katikati ya umati ule, alipojaribu kuwavuta wanawake wale alijikuta akitupwa pembeni, ama kweli siku ya kufa nyani miti yote huteleza! Baraka alibaki akilia
Kwa mbali Baraka alimuona bi Mwinde akirejea shambani kwake na mzigo wa kuni kichwani, haraka alimkimbilia na kumuomba akamsaidie mamaake , bi. Mwinde aliwakimbilia wale wapiga ngoma na kuwataka wazime mziki, Baraka alichomoa kuni mbili refu na kukimbilia hadi alipo mamaake na kuanza kutembeza kipigo kwa wanawake wale waliaonza kujikuna na kuugulia maumivu, Baraka alihakikisha wote anawatembezea kipigo huku bi Mwinde akimvuta Sadifa na kumuingiza ndani mwake kwa ajili ya kwenda kumsitiri , haraka Baraka na yeye hakubakia maana alikijua kitakachofuata endapo atakamatwa.
"Washenzi wakubwa nyie, hii ni rasharasha tu mvua kamili ipo njiani" alifoka bi Masha.
"Na lazima hii nyumba tuichome motooo" bi Ndaze aliongea huku akipumua kwa kasi kutokana na hasira alizokua nazo jumlisha na kichapo alichoshusha.
"Na badoo! tulitaka tukuvue nguo zote hizo tuone ulichopewa wewe sisi tukanyimwa" mwengine nae hakua nyuma.
Mziki uliishia hapo na kila mmoja alitafuta njia ya kwao, Sadifa alikuwa hoi huku akipumua kwa shida mno, Baraka na yeye alibaki akilia huku akimkanda mamaake na kumfuta baadhi ya sehemu za mwili , kwa mwendo wa kunyata bi Mwinde alitoka nje lengo ni kwenda kutafuta dawa ili aje amsaidie bi Sadifa..... Itaendeleaaaaaa
Sadifa kachezea kipigo cha kufa mtu, hivi ni yeye kweli? Jee akipona ataacha tabia yake au ndio sikio la kufa? Ugumu na vizingiti vinazidi kuwekwa juu ya Mamy na Baraka jee unahisi nini
kinakwenda kutokea? see u next.
◇ Sehemu ya 14 ◇
Mawingu yaliyoashiria uangukaji wa matone ya mvua muda mfupi ujao yalitanda kwenye anga la ardhi ya Jiulize , bila ya shaka ilikuwa ni Ijumaa yenye baraka kwa wale ambao walikua na mazao yaliyohitaji maji shambani kwao, pia ilikua ni kero kwa wale wauza biashara zao soko kuu la Jiulize ndani ya Jiji kubwa la Tuleane, ndio hivyo kila mmoja alilia mamaake.
Tayari muda wa darasani uliwadia, wanafunzi walikua tayari kumsubiri mwalimu wao awape kile alichowaandalia asubuhi hiyo, Mamy hakuwa miongoni mwa wanafunzi wenye hamu ya kupokea chochote kutoka kwa walimu wake , shingo yake haikutulia kila muda alitazama nje, hata pale ilipombidi kusimama pia hakuacha maana alifika hadi mlangoni na shingo yake kuzama nje, hakuona kitu zaidi ya wingu zito lililotanda, alichoka kuona kile alichokitarajia hakukipata , alirudi mdogo mdogo huku mwili wake ukimnyong'onyea na kukaa kwenye kiti machozi yakianza kumtoka , saa ngapi asichekwe na wanadarasa, alizodolewa na kuzomewa pia hadi pale mwalimu wa kipindi alipoingia.
" Basi hadi shule kupewa jina la Someni ila watoto bado hamuoni? mwalimu kuchelewa kidogo tu ndio imekua sababu ya kila mtu kuleta simulizi za nyumbani kwao! sijui mtabadilika lini nyinyi watoto au ndio mna akili kama za wazazi wenu! alifoka mwalimu yule wa kike aliyejulikana kwa jina mwalimu Swami.
" Hakuna viumbe wenye kazi ngumu kama sisi walimu, yaani kulea akili ambayo haiendani na vinasaba vyako ni shida! Sasa mpige mtoto wa mtu hapa weeh unakuja kuletewa kigodoro nyumbani kwako umepumzika, toeni madaftari yenu ya sayansi msinitolee mimacho" alizidi kufoka mwalimu huku akitoa kitabu na kuweka mezani.
"Ehee...Kabla ya kuanza darasa letu, ningependa tujikumbushie tulichosoma siku ya Jumatatu bila ya kuangalia kwenye daftari, nitakaemuona anachungulia nitamramba fimbo, ehee Monah Jumatatu niliwafundisha nini? aliongea mwalimu Swami huku akimyooshea kidole Monah aliyekua mbeleni mstari wa kati.
"Hewa" alijibu bila ya uoga mara tu aliposimama.
"Nzuri sana , hivi unaweza kutupa na maana yake mtoto mzuri?
"Hewa ni mchanganyiko wa gesi tofauti zisizoonekana na zinazunguka katika anga"
"Mpigieni makofi jamani, yaani wanafunzi wote mngelikua hivi basi ningejivunia hili darasa " aliongea mwalimu yule na kelele za pongezi zikimshukia Monah aliyekaa kwa pozi, angalau tabasamu lilirudi kwa Mwalimu yule.
"Aanh Monah mchague rafiki yako kipenzi atutajie sifa za hewa" kauli ya mwalimu huyo ilimfanya Monah amuangalie Mamy aliyekua mbali kimawazo , alicheka kwenye nafsi yake na mwisho wa siku alikua tayari kumuumbua kipenzi chake.
"Mamy naomba ututajie sifa za hewa" Monah aliongea kwa sauti jambo ambalo liliwafanya wanafunzi wote kutupa macho yao alipokuwa Mamy wakisubiri jawabu.
Aliyeulizwa swali hakuwa darasani kiakili ingawa macho yake yalikuwa mbele, mwalimu Swami na wanafunzi wote walibaki wakimtazama bila ya kusema chochote, wale walioshindwa kuvumilia waliamua kucheka, mwalimu alichukia na kuwapa ishara ya kufumba midomo yao, taratibu alisogea hadi alipokua Mamy na kumshtua kwa bakora nzito iliyotua mwilini mwake.
"Aaagh.... mwalimuuuuu" Alilalamika Mamy kwa sauti ya uchungu.
"Unawaza nini wewee! ahaaa ni Baraka leo hayupo ndio kaondoka na akili zako" aliyasema hayo baada ya kugundua kuwa Baraka hakuwepo.
"Sio hivo mwalimu sijisikii vizuri tu , nahisi kichwa kinauma" alijitetea .
"Uongo ukizidi sana huondosha ladha ya uaminifu ulioupika siku nyingi , Ondosha matamanio kabisa kwa maana yule akitamaniye kitu na asikipate huingiwa na huzuni, Mamy bado upo safarini, na safari hii ili ufanikiwe basi unapaswa kujiepusha na yale yaliyo nje ya uwezo wako" Madam Swabi alishusha darasa kwa bibie Mamy aliyebaki mpole.
"Mwalimu najua unanitakia mema mwanafunzi wako ila ingependeza zaidi wema huo ungeugawa kwetu sote, Baraka na yeye ana haki kama sisi, matatizo ya familia yake isiwe chanzo cha kuonekana hafai" Mamy alifunguka.
"Hakuna ambae anataka mwanafunzi wake aanguke isipokua wazazi wenu wanarejesha nyuma, mama Baraka alishaonyeshwa nyota mara nyingi ila yeye hukiangalia kidole tu Jee! unadhani tutafika? Sisi ni kama mayai tu ila yule mama ni jiwe hivi unadhani yupo wa kushindana nae?
Mamy alibaki kimya, kiukweli hakuwa na cha kumtetelea B wake, alikiona kiza kinene mbele yake baada ya kuona hata walimu wameyakatia tamaa maisha ya Baraka licha ya uhodari aliokua nao , aligonga meza kwa hasira hadi mwalimu na wanafunzi walishangaa, kitendo hicho kilimfurahisha Monah maana hadi hapo tayari aliona nafasi ya Mamy ataichukua yeye, mwalimu nae hakufurahishwa na tukio hilo hivyo aliamua kuondoka na vitabu vyake huku darasa likiishia hapo.
"Yaani ujinga wa mtu mmoja unatukosesha kipindi kweli? hivi wewe Mamy unajikuta kama nani darasa hili! kwa mwendo wake wa madaha Monah alisema hayo huku akisogea alipo Mamy ila hakujibiwa kitu .
"Tumewachoka na Baraka wako ikiwezekana mutafute shule nyingine, kila siku walimu wanaingia na kutoka bila kusomesha kitu kisa mapenzi yenu nyinyi , yule mtoto wa malaya atakupa nini wewe? mwengine na yeye uvumilivu ulimshinda.
"Tuheshimiae Devo, sitaki tukosane hata kidogo, kama walimu kutokusomesha mimi sio sababu ila ni tabia zao wenyewe " Mamy uvumilivu na yeye ulimshinda.
"Wewe na huyo mpumbavu wako ndio sababu na kamwe huwezi kuliepuka hili? mwalimu gani angevumilia vitendo vyenu, ulikua mwema ila sasa hivi walimu watakuona wa ovyo na usipozingatia mwisho wa siku na wewe utapelekwa kwenye madanguro badala ya shul...... " kabla Monah hajamaliza maneno yake alishtukia kofi zito shavuni mwake.
Ngumi zilianza kurushwa darasani, walivutana nywele mpaka na sare kuchanika, Mamy siku hiyo alikuwa wa moto jumlisha na hasira alizotoka nazo kwao mbona alikiwasha, shangwe la wanafunzi lilikua kubwa wakifurahia mapigano yale, Monah chalii.... alirembelewa mbele ya darasa ikisha Mamy alimfuata hukuhuko na kusimama mbele yake.
"Si kila jicho lililofumba ukajua limelala, nilikuona mwenzangu kumbe ni mnafiki mkubwa, nimekuvumilia sana wewe ila bado unaendelea kuyachimba maisha yangu, hadi kwenye familia yangu umepakaza huu ufisadi ili ukusaidie nini? na hili kaseme basi! na bado ...... nitapambana hadi nijue mwisho wa Baraka" Mamy alimtambia Monah.
"Hujui ulitendalo Mamy ila nakuapia mwisho wa hii tabia yako ni majuto, utakufa kwa ukimwi siku sio nyingi, ile sio familia hata ya kuombea maji ya kunywa ila wewe unajifanya kuvamia mji yatakukuta, hii ndio Jiulize" Monah alitaka kuinuka kwa hasira ila aliwekwa chini.
"Najua sana ninachokifanya na wala sitajutia kwa litakalonikuta , maisha yangu hayakuhusu hivyo naomba kaa mbali kabisa"
"Maisha yako yananihusu maana huyo ambae unampapatikia basi mamaake kaivunja ndoa ya wazazi wangu, tumeanza kuishi bila baba hivyo na yeye ajiandae kuishi bila ya Elimu" kwa hasira na yeye Monah alijibu na kujipangusa vumbi kuelekea nje
Maneno ya Monah mwishoni yalimmaliza nguvu Mamy, alihisi dunia inazidi kumuelemea , kila likiondoka moja la pili linasogea, hadi kufika hapo tayari alikijua chanzo cha chuki kati yake na Monah.
"Na usichokijua jana mama Baraka alifungiwa mtaa na bi Ndaze (mama Monah) , alipigwa akapigika, alichambwa akachambika, alivuliwa nguo zote hadharani kiufupi alikomeshwa, na asipoacha hiyo tabia basi yule mama ni kiboko" mmoja wa wanafunzi wa kike alimsogelea Mamy na kumdadavulia kilichojiri.
Mamy alizidi kuchoka baada ya kusikia habari hizo, hakuona sababu ya kuendelea kubaki pale, kwa vile tayari aliyavulia nguo basi hakuona tabu kuyakoga, alibeba begi lake na safari ya kwa kina Baraka ikaanza, alijua kipenzi chake kilikua kwenye wakati mzito na vile wanaishi peke yao basi alitaka awe pembeni yake.
*******
Bi Sadifa alilala kwenye mkeka uliochakaa sebuleni kwake, kichwa chake kilikua mapajani mwa mtoto wake, bakuli dogo jekundu lililosheni maji yaliyochanganywa na majani yaliyosadikika kuwa ni dawa lilikuwa mikononi mwa Baraka, alijitahidi kumywesha mamaake ambae alionekana kukata tamaa .
"Mama jitahidi basi umalizee, hali yako kidogo inaridhisha tofauti na jana" alibembeleza Baraka akimtazama kwa umakini mamaake.
"Siwezi Baraka, mwili wote huu unaniuma, hata huu mdomo kuunyanyua siwezi nauhisi mzito mno" Alilalamika bi Sadifa.
"Lakini mama haya yote umeyataka wewe, kwanini hubadiliki? sio mara ya kwanza hii mamaangu, kama ndio kuna sababu inakufanya hivi kwanini huniweki wazi? Yaani mtaa mzima huu mamaangu tunanuka na tabia zako chafu, nimechokaa!! hadi natamani kuf...... "
"Barakaa........ " Itaendeleaaaaaa
Hatimae Baraka atema nyongo kwa mamaake ila kuna sauti iliyoita jina lake imemsitisha kuendelea , Monah na Mamy waanzisha bifu , nini kinakwenda kutokea kwenye simulizi hii ya kusisimua.