JamiiTalks
JF Advocacy Team
- Aug 7, 2018
- 706
- 1,230
UTANGULIZI
Baada ya Serikali kutangaza kuwa wanafunzi wa Kidato cha Sita watapaswa kurudi shule ili wakajiandae na mitihani yao ya mwisho inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Juni kuanzia Juni 29 mpaka Julai 19, nimeona kuja na mawazo ambayo yatatoa mwongozo kwa namna wanafunzi, walimu na wafanyakazi wa shule wataweza kuchukua tahadhari dhidi ya COVID – 19.
Ni wazi wazazi, walezi na jamii kwa ujumla imekumbwa na taharuki kubwa sana baada ya Serikali kutangaza maamuzi ya wanafunzi kurudi shule huku hali ya ugonjwa wa COVID-19 nchini ikiwa bado ni kizungumkuti. Kufungua Shule ni jambo zuri ila kuwalinda wanafunzi na maambukizi ni jambo kubwa zaidi.
Kwa upande wa Serikali imewatoa wasiwasi wazazi na walezi kuwa wasiwe na hofu kwa wanafunzi kuwa Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha wanafunzi wanakuwa salama wakiwa mazingira ya shuleni.
MAMBO AMBAYO SHULE INATAKIWA KUYAFANYA ILI KUHAKIKISHA USALAMA WA WANAFUNZI KWENYE MAZINGIRA YA SHULE
Kuwajenga wanafunzi Kisaikolojia: Hili ndilo suala la kwanza na muhimu kwa shule.
Wakuu wa shule wanatakiwa kuhakikisha wanawajenga wanafunzi kisaikolojia na kuwaondolea hofu ili waweze kuzingatia masomo na akili yao kuweza kurudi katika hali ya kawaida.
Tutambue shule hazina facility za kujifukiza wala madawa, lakini pia wanafunzi wanaathirika zaidi kisaikologia pale wanapobaini yupo chumba kimoja na mgonjwa.
Wahudumu wa Afya: Kila shule itatakiwa kuwa na mhudumu wa afya karibu kwa ajili ya kutatua changamoto za kiafya zitakazo jitokeza katika maeneo ya shule.
Shule za bweni zenye vituo vya afya watatakiwa kuwepo muda wote eneo la kazi. Pia ni wakati muafaka kwa shule kuwa na mawasiliano ya karibu na taasisi na wataalamu wa afya ili kupata huduma kwa urahisi pindi dharura itakapotokea.
Vituo vya kunawa mikono: Shule zinatakiwa kuweka miundombinu mingi ya wanafunzi kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni. Sehemu muhimu za kuweka miundombinu hiyo ni darasani, maabara,bwenini,bwalo la chakula nk , viweze kutumika na walemavu na sanitizer zinaweza kutumika
Mpangilio wa kukaa darasani na bwenini: Shule zitatakiwa kupangilia upya namna ambavyo wanafunzi wanakaa wakiwa madarasani, yaani kuongeza nafasi kati ya dawati hadi dawati. Pia kwakuwa vidato vingine vitakuwa bado havijafunguliwa hivyo ni vyema shule kuangalia namna ya kutumia madarasa mengi Zaidi ambayo sasa yako wazi.
Mikusanyiko ya Asubuhi: Shule zitatakiwa kuachana na mikusanyiko hii kwa kipindi hiki, kama kutakuwa na ulazima basi zipangilia upya namna ambavyo wanafunzi watasimama wakiwa assembly, yaani kuongeza nafasi kati ya mtu na mtu.
Huduma ya Chakula: Kuwe na mpangilio mpya wa namna ambavyo wanafunzi hususan wa bweni watapata huduma za chakula wakati wa mlo bila kusongamana
Kukabiliana na dharura za kiafya: Ni vyema shule kuimarisha utaratibu wa kukabiliana na dharura za kiafya, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa wanafunzi na wafanyakazi ambao wanakuwa wagonjwa shuleni au wenye dalili zinazotia shaka wanapatiwa huduma maalum.
Ni vyema shule zikaweka utaratibu bora wa kushughulika na yeyote anayeugua (ugonjwa wowote) kwa namna ambayo haitazua taharuki kwa wengine na kuwaathiri kisaikolojia.
Wanafunzi wenye dalili wapimwe kabla ya kwenda, walio na corona wasiende shule na watakaoonesha dalili wakiwa shule/chuo kituo cha afya cha karibu kijulishwe Kuchangia vifaa vya shule: Pamoja na wanafunzi kuhimizwa kutochangia vifaa wakiwa madarasani na maabara, hili linaweza kuwa gumu kidogo kutekelezeka miongoni mwao, hivyo ni vyema kukawekwa vituo maalum vya kunawa mikono ili angalau kufanya mashirikiano haya yasiwe ya hatari sana.
Udhibiti wa wageni: Ni vyema shule zikapunguza ama kusimamia kwa ukaribu sana maingiliano ya wanafunzi na wageni kutoka nje ya shule. Mfano, ni vyema kusimamia kwa karibu sana namna wanafunzi wanapokutana na wenzao kutoka shule nyingine katika midahalo, michezo nk.
Jumbe za Tahadhari: Ni vyema shule ikatumia namna ya kukumbusha wanafunzi kuchukua tahadhari kwa kuweka mabango yenye ishara na jumbe za kujikinga. Hivi vinaweza kuwekwa katika maeneo mbalimbali kama ville milango ya kuingilia shule, mabwenini, madarasani, mabwaloni, maabara nk.
Elimu ya Afya kwa Walimu: Shule zinapaswa kutumia wataalamu wa afya kutoa mafunzo kwa walimu kuhusu Covid-19 ili kuwaachia ujuzi ambao walimu hao wataendelea kuutoa kwa wanafunzi kila siku. Kunaweza pia kutengwa muda maalum ambapo wanafuzi watakuwa wakikumbushana (chini ya uongozi wa walimu) masuala mbalimbali yanayohusu kuzingatia hatua za kubaki salama dhidi ya Covid-19. Shule iandae programu maalumu na za mara kwa mara za njia za kujikinga ikiwemo uvaaji wa barakoa, unawaji mikono. Pia wanafunzi hususani wa shule wapewe onyo kuhusu matendo yanayoweza kuwaweka hatarini ikiwemo wizi wa barakoa
Kupima wanafunzi: Kwa shule zenye uwezo, kama inawezekana, ni vyema kufanya check-ups (mfano: kupima joto, ama kuangalia dalili) za kila baada ya muda fulani ila kujua hali ya kiafya ya wanafunzi wakati wote.
Lishe na Michezo: Ni vyema shule kuhimiza walimu na wanafunzi na kuwawezesha kula kwa afya, kufanya mazoezi na kupata wakati wa kutosha kupumzika.
MAMBO AMBAYO MWANAFUNZI WA BWENI ATATAKIWA KUZINGATIA ILI KUHAKIKISHA USALAMA WAKE AWAPO SHULENI
Kushirikiana vifaa: Ni vyema wanafunzi wa bweni wakajitahidi kutoshirikiana kutumia vifaa kama vile chanuo, mataulo, ndoo, sahani, vijiko, vikombe nk
Kushirikiana sehemu ya kulala: Wanafunzi wana tabia ya kupenda kulala zaidi ya mtu mmoja kwenye kitanda. Kwa wakati huu ni vyema kuacha kuchangia vitanda na mashuka. Kuacha kuchangia vitu hivyo kunaweza kuwaweka mbali na hatari ya kuambukizana endapo mmoja atakuwa tayari ameathirika.
Kunawa mikono: Kutokana na mazingira ya shule kuwa hatarishi kutokana na mwingiliano mkubwa, ni vyema wanafunzi kuchukua tahadhari na kunawa mara kwa mara kwa sabuni na maji tiririka
Mawasiliano: Ni vyema wanafunzi kuhakikisha wanawasiliana na uongozi wa shule au wao kwa wao pindi wanapohisi hali tofauti ya kiafya kwao wenyewe ama kwa wenzao.
Barakoa na Vitakasa Mikono: Ni vyema kila mwanafunzi akawa na barakoa za kutosha ambazo atavaa awapo kwenye mazingira yenye zaidi ya mtu mmoja. Pia Sanitizer kwa ajili ya kutakasa mikono endapo kutakuwa na uhaba wa maji tiririka.
Kusoma kwa makundi: Ni kawaida kwa wanafunzi kusoma kwa namna ya majadiliano ya zaidi ya mtu mmoja. Kwa wakati huu ni vyema wafunzi wakatengeneza makundi ya wanafunzi wachache ambayo wataweza kusoma kwa kujadiliano huku wakiwa wamepeana nafasi yakutosha baina yao
MAMBO AMBAYO MWANAFUNZI WA KUTWA ATATAKIWA KUZINGATIA ILI KUHAKIKISHA USALAMA
Usafiri: Kwa wanafunzi wanaotumia usafiri wa umma, ni vyema wakachukuwa tahadhari kwa kuvaa barakoa wakati wote. Kwa wenye uwezo, ni vyema kubeba sanitizer zao ili kujitakasa kila wanaposhika maeneo yanayoguswa na wengi wawapo kwenye daladala nk.
Pia wale wanaotumia mabasi ya shule, ni vyema nao kuzingatia uvaaji wa barakoa na kutumia vitakasa mikono wanapogusa sehemu ambayo inaguswa na wengi. Wasipande gari ambayo imejaa
Kutembea: Wanafunzi wanaoishi karibu na maeneo ya shule lakini huwa wanaona ni vyema kutumia usafiri wa umma, ni vyema kubadili mazoea na kutembea waendapo shuleni.
Hii itawasaidia kufanya mazoezi na kujiepusha kuwa kwenye mikusanyiko wakati wote.
Masomo ya ziada: Wanafunzi wa kutwa wanaosoma masomo ya ziada ni vyema kuchukua tahadhari muhimu kwa sababu wawapo huko hukutana na wanafunzi wengine ambao wametoka mazingira tofauti. Hivyo ni vyema kuwa na barakoa na vitakasa mikono.
Mikusanyiko isiyo na ulazima: Ni vyema kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima wawapo shule. Kama mikusanyiko sio ya kujenga kimasomo ni vyema kuachana nayo ili kujiweka mazingira salama. Mikusanyiko hukusanya wanafunzi ambao wametoka mazingira mbalimbali na kukutana shule kwa muda wote wa masomo hivyo ni hatari sana.
Nyongeza kwa Wanafunzi wa chuo
Kuepuka safari zisizo za msingi: Wanafunzi wa chuo wana uhuru wa kwenda popote hivyo ni muhimu wajitahidi kuzuia safari au mitoko isiyo ya lazima ili kudhibiti maambukizi
Kuongeza matumizi ya TEHAMA: 'Discussion' zifanyike kwa njia ya mtandao ili kuepuka maambukizi na kuzingatia 'social distancing'.
Manunuzi kwa njia za kimtandao: Pesa zinaweza kusambaza maambukizi ya COVID19 kutoka mtu mmoja hadi mwingine hivyo malipo kwa njia ya simu yanaweza zuia maambukizi.
Serikali ya wanafunzi inaweza kushauri uongozi wa vyuo uweke utaratibu mzuri wa malipo ya ada na usajili ili kuepusha wanafunzi kwenda benki
Pia, soma mwongozo wa Wizara ya Afya
JamiiTalks