Dc mstaafu amshushia kipigo mkewe,amtishia kumtandika bastola.
Philomena Toima ambaye ni mke wa mkuu wa wilaya mstaafu wa wilaya mbalimbali nchini,Peter Toima amelazwa katika kituo cha afya cha Simanjiro kufuatia kipigo cha mmewe akiuguza majeraha mbalimbali mwilini mwake.
Chanzo cha kipigo hicho kinatokana na ugomvi uliozuka katika sherehe ya send off iliyofanyika katika kijiji cha Loborsoit wilayani Simanjiro mkoani Manyara hivi karibuni.
Hii si mara ya kwanza mwanamke huyo kupokea kipigo kutoka kwa mmewe kwani amekuwa akipigwa na kunyanyaswa mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kutishiwa bastola.
Mwaka jana mwanamke huyo alipigwa na kisha kulazwa hali iliyopelekea jeshi la polisi kumnyang’anya bastola Toima lakini hatahivyo alirejeshewa tena silaha hiyo Katika mazingira ya kutatanisha.
Akiongea na waandishi wa habari jana katika kituo hicho cha afya Philomena alieleza kwamba mara baada ya sherehe kumalizika akiwa ndani ya gari aliona gari ya mmewe ikimfukuza kwa nyuma na mara aliposimama mmewe alishuka na kisha kwenda katika mlango wa gari na kuanza kumtishia kwa bastola aufungue.
Philomena alieleza kwamba ghafla alipofungua mlango mmewe akiwa na mwanamke aliyetambulika kwa jina la Scolla Mollel ambaye ni hawara yake walianza kumshambulia kwa mateke kabla ya kuokolewa na wasamaria wema.
“Walianza kunipiga kwa mateke akiwa na yule hawara yake wakati huo ameshika bastola mkononi “alisimulia Philomena
Hatahivyo,alisisitiza kuwa kwa muda mrefu ndoa yake imekuwa na changamoto kutokana na mme wake kutokuwa mwaminifu baada ya kupata mwamamke nje ya ndoa aitwaye Scolla Mollel.
Philomena alidai kwamba mara kwa mara amekuwa akipingana na hatua ya mmewe kuchukua mali walizochuma pamoja na kisha kuzitumia hovyo na hawara yake.
“Mimi nimekuwa nikipinga sana yeye kuchukua mali tulizotafuta pamoja na kuzitawanya hovyo na hawara yake sisi tuna watoto wanne hizi ni mali za familia “alisisitiza Philomena
Philomena aliomba msaada kwa wanasheria pamoja na wanaharakati wamsaidie kwa kuwa amekuwa akinyanyaswa kijinsia na hata kutishiwa kifo na mmewe.
Mwisho.