Kama kuna sheria ama kanuni mbaya zenye kuendekeza ubinafsi na kujipendelea kwa wabunge wetu na kwa upande mwingine kuwapendelea ndugu, rafiki, jamaa na hata nyumba ndogo zao ni sheria ya viti maalum kwa wanawake na pili, sheria ya wabunge kulipana posho za vikao.
Chukulia ni fedha kiasi gani inatumika kuwagharamia wabunge 121 ambao hawakutokana na kura ya moja kwa moja na mwananchi ambaye tunaamini ndiye bunge hili liko kwa ajili yake.
Jenga hisia pia kwamba kuna vijana wa kike wa umri wa miaka 24 ambaye hajawahi kukifanyia lolote chama anateuliwa kuwa mbunge wa viti maalum kwa sababu tu ni ndugu wa m/kiti wa chama wa mkoa au kwa sababu tu ni hawala wa kiongozi fulani wa juu wa Chama, wakati huo huo wanaachwa akina mama wenye sifa waliovipigania, kuvitetea na kuvijenga vyama miaka na miaka.
Malalamiko ya wanachama wa vyama vya CCM na CDM baada ya uteuzi wa wabunge wanawake wa viti maalum, umedhihirisha kuwepo kwa upendeleo ama kukosekana kwa utaratibu maalum wa vyama kuwapata wabunge hao.
La pili, ninalomwomba mhe Rais alifute wakati wa utawala wake ni ulipanaji wa posho za vikao wanazolipana kila siku wanapokaa kwenye vikao vyao vya bunge wakati wanalipwa mshahara kutokana na hilo.
Ni gharama sana kuwalipa wabunge zaidi ya 390 posho ya sh. 300,000 kila siku na bado wakimaliza miaka mitano unawaaga na kiinua mgongo cha sh 230,000,000 kila mmoja. Huu kama zi ufisadi wa wazi ni nini?