"Hapa Kazi tu", ndio msemo unaotawala sasa katika eneo la siasa. Siku chache zilizopita msemo wa 'mabadilikooo' Lowasaaa, Lowassaa mabadilikoo' ndio ulitamba. Wakati huo vijana, wazee na watoto walitamani mabadiliko aliyotangaza Mh. Edward Ngoyai Lowassa. Lowassa aliwajengea wafuasi wake Imani kubwa hasa pale alipowaambia wampigie kura kwa wingi na suala la kumtangaza mshindi tumuachie yeye. Wananchi wakampigia kura kwa wingi na hadi leo, suala la kutangaza mshindi wamemuachia Lowassa.
Vyovyote vile, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni John Pombe Magufuli. Anaweza asiwe mioyoni mwa raia wengi zaidi, nikiwemo mimi, lakini ndio Rais. Tukitaka kujadili mambo Makubwa ya Taifa letu, hakuna budi kumtambua Magufuli kwamba ndiye Rais, kwa sasa.
Rais Magufuli ameanza kazi kwa staili ya JK alipoingia mwaka 2005. Magufuli amekuwa akivamia taisisi nyeti za umma, kukagua, kujionea hali halisi, kutoa maagizo na pengine kujifunza. Ni vema na haki kuona tuna Kiongozi anayeonesha kuyajali majukumu ya wengine kiasi cha kufanya ziara za kustukiza kwa lengo la kuona uhalisia wa mambo. Kama Magufuli angekuwa anatoa taarifa za ziara zake, labda pangefanyika maandalizi yanayoweza kuziba sura halisi ya utoaji huduma katika taasisi husika.
Wapo wanaobeza, kukejeli na kupuuza na hata kuita ziara hizi kuwa ni maigizo tu au Nguvu ya soda tu. Wengine wanasema hayo kwa sababu wao wannamini hivyo kutokana na sababu zao wanazoona kuwa ni za msingi, na wengine wanatamani iwe hivyo ili Magufuli akishindwa wajigambe mbele ya 'wapinzani' wao wa kisiasa. Watu hawa hawajui kuwa kushindwa kwa Magufuli ni kushindwa kwa Taifa. Na Taifa ni letu wote, kwa hiyo na sisi sote tutakuwa tumeshindwa.
Mimi binafsi naziona ziara za ghafla za Magufuli kama michezo ya mtoto mdogo anayejifunza kutembea. Mtoto mdogo anapocheza ni ishara ya maendeleo mazuri kiafya. Ni ishara kuwa mtoto hana tatizo. Ni matumaini. Hutokea hata mzazi kushikwa na wasiwasi mtoto wake anapoacha kucheza na wenzake, na hali ilkizidi humpeleka kituo cha afya.
Magufuli anacheza, na hiyo ni ishara nzuri kwa mtoto. Na hapo ndipo inapokuja hamu ya kutaka kuona maendeleo chanya ya Rais wangu Magufuli. Atakapoanza kutembea, atembelee maeneo haya.
1. MADAWA YA KULEVYA
Jeshi la wananchi la Tanzania JWTZ, lina wanajeshi wapatao 30,000 na kuongeza au kupunguza kidogo (around 30,000). Takwimu za vijana walioathirika kwa madawa ya kulevya ni around 700,000 (laki saba) kwa mwaka 2013. Kwa hiyo ukichukua 700,000 ? 30,000 = 23 (aprox).
Hii ni sawa na kusema ukichukua vijana waliathiriwa na madawa ya kulevya unapata ndani yake majeshi 23 ya Tanzania (kwa idadi ya watu). Hili ni kundi ambalo kwa kiasi kikubwa halizalishi, halilipi kodi, ni tegemezi na wengi wao ni wahalifu ingawa uhalifu zaidi ni matokeo ya uathirika wao.
Vijana ni nguvu kazi ya taifa, ndio nguzo ya taifa. Nguzo hii ikiliwa na mchwa taifa litaanguka.
Kwa hiyo kila mtanzania atapenda zaidi kuona Mh. Magufuli anapigana vita kufa kupona dhidi ya madawa ya kulevya ili kuokoa afya za vijana wetu kabla hajawatembelea kwa kushtukiza huko mahospitalini.
Wananchi wangependa kuona madawa ya kulevya yanakamatwa, na kuchomwa moto ili kudiscourage biashara hii ya kuhuisha. Na zaidi amuombe JK majina aliyodai kuwa nayo (kama haukuwa mkwara) ili aanze nayo.
Angalizo: Kila mtu anaweza kuwa mwathirika wa madawa ya kulevya.
2. UJANGILI
Sasa hivi Kilo moja ya meno ya Tembo ina thamani ya Tsh. 200,000. Siku chache zilizopita tumeambiwa Tanzania iliizuia Malawi kuteketeza Meno na pembe za Ndovu zilizokamatwa nchini huko zikitokea Tz. Ripoti zaidi kuhusu ujangili huo hazileti furaha kwa wazalendo.
Al Jazeera wameiita Tanzania 'Point of extinction'. Kwa maana eneo la kuondoa uhai Duniani, au eneo la maangamizi, wakiakisi hali ya ujangili katika Tanzania inayoonesha kuwa Tembo wamepungua kutoka 109,051 mwaka 2009 na kufikia 43,330 mwaka 2014.
Tembo 85181 wameuawa kwa kipindi cha miaka 5. Sawa na tembo 17,016 kila mwaka. Maana yake kwa tembo 43,330 waliobaki ukigawa kwa 17,016 ni sawa na miaka chini ya mi3, tembo watakuwa wamekwisha ikiwa hali haitadhibitiwa. Hiyo ni kwa Tembo tu. Magufuli aguse na hapo.
3. UFISADI
Escrow, Epa, Richmond, Meremeta, Mabilioni ya Uswis, Ufisadi katika uchaguzi, na madudu mengine kibao. Magufuli akitaka kujenga imani kwa wananchi asiache kushughulikia mafisadi kama alivyoahidi. Lakini akiendelea ku'deal' na wanataaluma (mf. Madaktari Muhimbili) lakini akaacha wanasiasa wafanye wanavyotaka, wafanyakazi watapoteza imani naye. Na hapo kazi zitafanyika siku akivamia maofisini na siku mbili tatu baadae halafu 'business as usual'. Itapendeza kama atagusa na Mafisadi.
4. MIKATABA YA MADINI, MAFUTA NA GESI
Tumeshuhudia ugeni mkubwa nchini petu mara baada ya ugunduzi wa mafuta na gesi. Lakini hata sasa watanzania wana wasiwasi kuhusu mikataba 35 ya siri iliyofanywa na Rais wa awamu ya nne na wageni wake Rais Obama wa Marekani na Xi Ji Ping wa China.
Magufuli atakapoacha michezo ya ziara za kustukiza, tungependa aweke mikataba hii wazi, kisha wananchi washuhudie, na kama kuna harufu ya maslahi binafsi ya viongozi waliotia saini mikataba hiyo kwa siri, hatua mahususi zichukuliwe.
Tumeonewa sana kwenye Madini. Wamiliki wa migodi hii sio tu ni watu Matajiri bali pia ni watu wenye ushawishi mkubwa kwenye serikali za mataifa yalipoasisiwa makampuni hayo. Magufuli atapata sifa akituokoa na dhuluma hii iliyofanywa kwa miaka mingi. Haina maana 'neno hapa kazi tu' halafu rasilimali zetu zinakombwa kwa ridhaa yetu wenyewe. Badala ya hapa kazi tu inakuwa 'Hapa ubwege tu'.
5. KATIBA MPYA
Katiba yenye tija, tumaini jipya na mwanzo mpya wa Utanzania tunaotamani. Inafahamika wazi kuwa Magufuli ni miongoni mwa wanaCCM waliouteka na kuubaka mchakato wa katiba mpya. Mh. Sitta akajiandikia kijitabu chake akakiita 'katiba pendekezwa' huku akishadidiwa na wanaCCM, wakapiga makelele ndani ya bunge letu 'tukufu' kama mazuzu waliokosa kunywa dawa siku hiyo. Magufuli alikuwa miongoni mwao.
Sasa Mh. Rais Magufuli ana nafasi ya kuwa huru na kuacha kufuata mihemko ya siasa za vyama kwenye jambo la msingi ka Katiba. Pindi apatapo wasaa, aurejeshe mchakato wa katiba mpya ili kurudisha matumaini yaliyopotezwa. Na hili halihitaji kuvamia wizara ya katiba na sheria.
Maeneo ya msingi ni mengi na muda wa miaka mitano ni mchache sana. Naomba itokee kuwa 'drama' hizi za Mh. Rais iwe mwanzo wa safari ya kuelekea huko nilipoeleza. Haitapendeza kama lengo la hizi 'drama' ni kutafuta kukubalika tu halafu business as usual (cheap popularity).
Pia, ifahamike kuwa kutekeleza mambo hayo ni kama kuingia vitani. Kwa hiyo Mh. Rais Magufuli anapaswa kuwa mtu anayehitaji msaada katika vita hii kuliko mtu mwengine yeyote. Kwa hiyo itakuwa vizuri zaidi endapo 'drama' hizi za ziara za kustukiza zikawa mbinu za kutafuta 'kupendwa na wananchi' na hivyo kupata support kubwa pale atakapoanzisha hiyo vita.
Au kama sivyo, basi ni vema Mh. Rais Magufuri akawa na malengo ya msingi kuliko maeneo niliyogusia. Kumbe sasa endapo hatagusia hayo atagusa wapi? Mh. Rais Utakapomaliza Michezo yako, Naomba uguse na hayo.
Asante.
0713933736