JUZI Rais Jakaya Kikwete alizindua awamu ya pili ya Mpango wa Mendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES-II) wenye lengo la kuboresha mazingira ya utoaji elimu hiyo.
Huu ni mwendelezo wa awamu ya kwanza ya MMES iliyoanza rasmi 2006 baada ya Serikali ya Awamu ya Nne kuingia madarakani. Katika hatua hiyo ilianzishwa kampeni nzito ya kufungua shule za sekondari za kata nchi nzima.
Lengo MMES-II utakaotekelezwa kuanzia 2011 hadi 2015 ni kuboresha elimu ya sayansi, mazingira ya kufundishia, kuboresha makazi ya walimu sambamba na kujenga maabara katika shule za sekondari za Serikali nchini.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Serikali, mpango huo utatekelezwa kwa msaada wa Benki ya Dunia (WB) ambayo imekubali kutoa dola za Marekani 150 milioni na tayari imetoa dola 49 milioni, huku Benki ya Maendeleo Afrika (ADB) ikiwa imekubali kusaidia mpango huo.
Hata hivyo mpango huu umezinduliwa wakati mfumo wa elimu nchini ukiendelea kudorora kutokana na mazingira ya kufundishia kuendelea kuporomoka kwa sababu ya kukosekana kwa walimu wa kutosha katika shule nyingi za sekondari na hasa za kata.
Ukweli ni kwamba, hali halisi inaonyesha kuwa shule nyingi za sekondari za kata hazina walimu. Baadhi ya sekondari za kata zina mwalimu mmoja ambaye ndiyo mkuu wa shule na mwenye jukumu la kufundisha madarasa yote, sawa tu na hali ilivyo katika shule nyingi za msingi za vijijini.
Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba kutokana na kukosekana kwa walimu, shule nyingi za kata zinaajiri walimu bila kuzingatia sifa, maadamu mtu kamaliza kidato cha sita ili kuziba pengo.
Si hivyo tu licha ya tatizo hilo la walimu kuwa kubwa, mwaka huu Serikali imetangaza kuwa kati ya walimu 17,684 walohitimu na kufauliu katika vyou mbalimbali vya elimu nchini, 9,226 tu ndiyo wamepata ajira na kati hao 187 wanakwenda kufundisha vyuo vya elimu. Hii inaonyesha kuwa bado kuna tatizo kubwa katika kuboresha sekta hii muhimu kwa maendeleo ya taifa letu.
Kwa ujumla, tunapongeza mipango ya Serikali katika kubioresha elimu, lakini tuna mashaka na utekelezaji wake ambao unaonyesha wazi kuwa unafanyika kisiasa zaidi badala ya kufanywa kisayansi.
Kwa mfano, katika awamu ya kwanza ya MMES tuliona nguvu kubwa iliyotumika kuhamasisha na kuwalazimisha wananchi kujenga shule za kata na kabla hazikamilika na kufanyika maandalizi mazuri ya kutoa elimu inayolingana na hadhi ya sekondari, shule zilifunguliwa kila mahali hivyo kushusha hadhi na kiwango cha elimu hiyo.
Ni kweli watoto wengi wamefika sekondari, lakini hali halisi inaonyesha kuwa wengi wa watoto waliopelekwa katika sekondari za kata hawajaeleimika, kwani miongoni mwao wanashindwa kusoma, ukiachia mbali masomo ya sayansi ambayo kwao ni sawa na usiki wa kiza.
Swali letu ni kwamba, kama Serikali imeshindwa kutoa ajira kwa walimu zaidi ya 7,000 waliohitimu na kufaulu mwaka jana wakati hitaji lipo, tutafanikiwaje kuboresha elimu na kutekeleza MMES-II?
Ni nguvu kiasi gani imepangwa kutumika kuhakikisha kuwa ajira za walimu zinapatikana na malengo ya kuboresha elimu yanafanikiwa?
Kulingana na uhitaji wa walimu unaolikabili taifa wakati huu, hatukutarajia walimu watashindwa kupata ajira, tulidhani walimu wote wangepangiwa kazi huku serikali ikendelea kutafuta walimu wapya.
Lakini kwa hali hii ni kwamba, hata watakaohitimu hawana uhakika wa ajira sawa tu na sekta nyingine ambazo hazina ajira.
Inakuwaje ajira ikosekane katika sekta ya elimu ambayo ina nafasi za kazi na walimu wanahitajika sana?
Inaonekana Serikali haikujipanga ipasavyo kuhakikisha kuwa walimu wote watakaohitimu wanapata kazi ingawa ilitumia fedha nyingi kuwapa elimu na kutangaza kuwa wote watapata kazi!
Hii ni changamoto kwa Rais Kikwete kwamba mafanikio ya MMES-II ni yumkini kama mfumo wa utekelezaji hatuabadilishwa.
Ikumbukwe kuwa elimu ni taaluma haihitaji siasa.