Mazungumzo ya ngazi ya juu ya uchumi na biashara kati ya China na Marekani yamefanyika hivi karibuni huko Geneva, na kupata matokeo muhimu. Hali ambayo inaonyesha kuwa baada ya mvutano mkali wa zaidi ya mwezi mmoja, nchi hizo mbili zimechakua njia ya mazungumzo kutatua maoni yao tofauti. Matokeo hayo si kama tu ni “kifungo cha kuanzisha upya uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Marekani, bali pia yataleta utulivu katika uchumi na biashara duniani.
Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mazungumzo hayo, China na Marekani zitaondoa ushuru wa ziada wa asilimia 91, Marekani itasitisha utekelezaji wa “Ushuru Sawa” wa asilimia 24 dhidi ya China, huku China pia ikisitisha utekelezaji wa ushuru wa asilimia 24 kwa bidhaa za Marekani kwa kulipiza kisasi. Taarifa hiyo imesema nchi hizo zote zimetambua umuhimu wa uhusiano wao wa kibiashara kwa uchumi wao na uchumi wa dunia nzima. Mwitikio chanya wa masoko ya hisa duniani unaonesha kuwa matokeo hayo yanaendana na maslahi ya nchi hizo mbili na maslahi ya pamoja ya dunia.
Hivi sasa, uchumi wa dunia unakabiliwa na changamoto kubwa. Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Shirika la Fedha la Kimataifa kuhusu uchumi wa dunia imepunguza makadirio ya ukuaji wa uchumi duniani mwaka 2025 hadi asilimia 2.8, kutoka asilimia 3.3 ya mwezi Januari mwaka huu. Wakati huohuo, Shirika la Biashara Duniani linatarajia kuwa biashara ya bidhaa duniani inaweza kushuka kwa asilimia 0.2 mwaka huu. Mapato ya kitaifa ya China na Marekani yanachangia zaidi ya theluthi moja ya jumla ya mapato ya kitaifa ya nchi zote duniani, na thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili inachangia karibu moja ya tano ya jumla ya biashara duniani.
Uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Marekani una umuhimu mkubwa kwa uchumi wa dunia. Wakati uchumi wa dunia unakabiliwa na changamoto mbalimbali, China na Marekani ambazo zinashika nafasi ya pili na kwanza duniani kwa ukubwa wa uchumi, kurejesha mazungumzo ni ishara chanya kwa jumuiya ya kimataifa.
Katika kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja uliopita, vita ya ushuru iliyoanzishwa na Marekani imeleta athari kubwa kwa China na Marekani, pamoja na dunia nzima. Vita hiyo imevuruga uthabiti wa mnyororo wa ugavi duniani, kudhoofisha utaratibu wa biashara ya kimataifa, na kuongeza hatari ya kudodora kwa uchumi wa dunia. Mashirika ya kimataifa yakiwemo Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki ya Dunia yameonya mara kwa mara kwamba vitendo vya kujilinda kibiashara ni moja ya vitisho vikubwa dhidi ya kuimarika kwa uchumi wa dunia. Mazungumzo hayo kati ya China na Marekani bila shaka yamepunguza hali mbaya ya uchumi wa dunia ulio katika njia panda.