Matumizi ya vibao vya plastiki kukatia nyama mabuchani: Je, tunalishwa chembechembe za plastiki bila kujua?

Matumizi ya vibao vya plastiki kukatia nyama mabuchani: Je, tunalishwa chembechembe za plastiki bila kujua?

N'yadikwa

JF-Expert Member
Joined
Aug 10, 2014
Posts
8,308
Reaction score
12,812
Kuna jambo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likinitatiza kuhusu namna nyama inavyokatwa katika mabucha yetu na maeneo mbalimbali ya biashara ya nyama.

Matumizi ya vibao vikubwa vya plastiki kukatia nyama kwa kutumia visu, mapanga na hata mashoka yanaweza kuwa yanahatarisha usalama wa chakula tunachokula.

Nimekuwa nikiwashuhudia wauzaji wa nyama wakikatakata nyama juu ya vibao hivi vya plastiki, ambavyo kadiri vinavyoendelea kutumika huonyesha mikwaruzo, michubuko na sehemu zilizomenyeka kutokana na makali ya vifaa vinavyotumika kukatia nyama.

Mara kadhaa nimewauliza baadhi ya wauzaji kwa nini hawatumii vibao vya mbao kama ilivyokuwa zamani. Majibu yao yamekuwa kwamba mamlaka zinazohusika na afya na usalama wa chakula zinawataka au zinapendekeza watumie vibao vya plastiki badala ya mbao.

Hapa ndipo ninapoona kuna haja ya mjadala wa kitaalamu na mapitio ya utaratibu huu.

Kwa uelewa wangu, kila panga, shoka au kisu kinapogonga kibao cha plastiki kwa nguvu, kuna uwezekano wa chembechembe ndogo za plastiki kumenyeka na kuchanganyika na nyama inayokatwa.

Chembechembe hizo zinaweza kubaki kwenye minofu ya nyama, kisha kuingia kwenye chakula tunachopika, kuchemsha au kuchoma.

Tafiti mbalimbali zimeibua maswali kuhusu uwepo wa microplastics katika chakula na athari zake zinazowezekana kwa afya ya binadamu.

Mfano: Microplastics - A Silent Threat and How to Fight It - One More Tree Foundation - Microscopic plastic particles

Ingawa bado hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwamba chembechembe za plastiki zinazotokana na vibao vya kukatia nyama husababisha saratani moja kwa moja, suala hili halipaswi kupuuzwa.

Hoja yangu ni kwamba hatupaswi kuangalia usafi wa kibao pekee, bali pia uimara wake na uwezekano wa kuachia chembechembe zinazoweza kuchanganyika na chakula.

Ninaamini matumizi ya vibao vya mbao ngumu, vinavyofaa kwa matumizi ya chakula, vilivyotengenezwa vizuri na kusafishwa ipasavyo, yanapaswa kuruhusiwa kama mbadala wa plastiki.

Mbao nazo zinahitaji utunzaji makini ili kuzuia uchafuzi wa bakteria, lakini hazipaswi kupigwa marufuku kwa dhana tu kwamba plastiki ni salama zaidi.

Ninapendekeza mambo yafuatayo:

1. Mamlaka zinazohusika na afya na usalama wa chakula zifanye tathmini ya matumizi ya vibao vya plastiki vinavyotumika kukatia nyama kwa mapanga na mashoka.

2. Vibao vya plastiki visitumike kabisa. Au vitumike vyenye material yasiyo na athari kwa afya.

3. Wauzaji wa nyama waruhusiwe kutumia vibao vya mbao ngumu vinavyokidhi viwango vya usalama wa chakula, badala ya kulazimishwa kutumia plastiki pekee.

4. Mamlaka zitoe ufafanuzi wa kitaalamu kuhusu aina za vibao vinavyofaa kwa shughuli za kukatia nyama, hasa pale vinapotumika vifaa vizito vyenye makali.

5. Utafiti ufanyike kubaini kiwango cha chembechembe za plastiki kinachoweza kuingia kwenye nyama kutokana na matumizi ya vibao hivi katika mazingira halisi ya mabucha yetu.

Nimalizie kwa kuuliza:

Je, wataalamu wa afya ya jamii, usalama wa chakula na udhibiti wa viwango wanaweza kutueleza kama kweli matumizi ya vibao vya plastiki ni salama zaidi kuliko mbao, hasa pale nyama inapokatwa kwa mapanga na mashoka?

Na je, kuna sababu za msingi za kisayansi za kuwazuia wauzaji kutumia vibao vya mbao vinavyotunzwa katika hali nzuri ya usafi?

Kwa maoni yangu, ni wakati wa kuangalia upya suala hili kama TBS walivyoangazia athari za matumizi ya vigodoro kufutia vikaango vya chapati masokoni.

Usalama wa chakula haupaswi kupimwa kwa urahisi wa kusafisha vifaa pekee, bali pia kwa hatari zinazoweza kutokana na vifaa hivyo kuchakaa na kuachia chembechembe hatarishi kwenye chakula.

Binafsi nikikutana buchani na hilo bao la plastiki huwa sinunui nyama tena!
 
Back
Top Bottom