Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye (pichani), amesema serikali imeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kudhibiti na kupambana na vitendo vya mauaji vinavyofanywa dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) na hivyo kusababisha kukithiri.
Akizungumza jijini Mwanza juzi wakati wa uzinduzi wa albamu ya watoto ya Kanisa la EAGT Lumala mpya, Sumaye alisema vitendo vya baadhi ya watu kuwanyakua watoto wenye ulemavu wa ngozi na kuwaua, vinasikitisha, kwani vinakiuka haki za binadamu.
Alisema serikali kutochukua hatua mwafaka dhidi ya vitendo hivyo, kunalisababishia taifa aibu, hasa pale inapoonekana baadhi ya wahusika kutumia viungo vya albino kutafuta madaraka au utajiri.
Hivyo, aliishauri serikali na vyombo vya usalama kuchukua hatua zaidi ili kukabiliana na vitendo hivyo.
"Haiwezi kuingia akilini eti viungo vya binadamu, hasa albino vinasaidia kupata umaarufu wa uongozi ama madaraka. Kama ni hivyo, kwanini usitumie kiungo chako ili ufaidike na utajiri huo," alisema Sumaye.
Alisema fedha zinazotolewa na baadhi ya watu katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu zinatokana na ubadhirifu wa mali za umma na kuwatahadharisha viongozi wanaosimamia michakato ya uchaguzi kutenda haki kwa wagombea na wapigakura ili kuepukana na machafuko kama yanavyotokea kwa baadhi ya nchi barani Afrika
Awali, Mchungaji wa Kanisa hilo, Daniel Kulola, alisema wamekuwa wakiwalea watoto katika matunzo ya kumtukuza Mungu ili kupeukana na matendo maovu.
Chanzo:Nipashe