Mzee Muhammed Baramia alikuwa memba wa Chama cha Umma na alihusika katika kesi ya mauwaji ya marehemu Mzee Abeid Amani Karume. Hivi sasa ni memba wa Chama cha Wananchi (CUF) na ni Imamu wa Msikiti.
Halikuwa jaribio la kwanza. La 1972 tulipanga tangu 1968. Madhumuni khasa ilikuwa kukamata serikali ya Zanzibar. 1968 tulijiona kidogo. Sababu ni tuliona kuna mabadiliko
against [dhidi] yetu. Upepo ulikwisha anza kutugeukia. Karume kaifanyia hii nchi kama moja kwa moja yake, hasikilizi mtu, anafanya anavotaka. Mwisho wake ilikuwa baada ya wale kina Hanga, kina Twala, kina Saleh Saadalla, nani…, sasa alikuwa anamtaka Babu. Ndo akasema hasa, "lipo Hizbu kubwa huko Dar es Salaam, tunalitaka hapa." Kwenye mkutano wa hadhara.
Kweli Babu alikuwa Katibu Mkuu wa Hizbu na ndo maana Karume akasema "Hizbu kubwa." Sasa anaanza kumtia hewani, kumuandama. Anamtaka yeye kwa kuwa aje au atavunja muungano. Alimwambia Nyerere hivo. Akiogopa kwa sababu wataalamu wote yeye hawataki. Kina Twala, kina Hanga…Yeye na Sefu Bakari kuwa waendeshe nchi wanavotaka, wafanye wanavotaka, hivo ndo ilivokuwa. Baada ya kutangaza hivo sisi tukaitana, hapa Zanzibar na Dar es Salaam, mikutano ilikuwa mingi. Hata mie nafsi yangu nilimwambia Sefu Bakari "mbona upepo unatubadilikia?" Akanyamaza kimya. Nilimkumbusha wakati wa
interrogation [kuhojiwa]. Umesahau? Manake alinihujumu "hata wewe, wewe ulikuwa Afro-Shirazi na ghasia?" Nkamwambia "mmetugeukia."
Tukaendelea mpaka tuka-panga mipango. Kila nkiwatia kwenye
line hawaingii, kina Natepe, kina nani, lakini Sefu Bakari sikuweza hata kujaribu kwa sababu alikuwa
pro-Karume [akimuunga mkono] bila ya kiasi, Ali Mahfoudh alikuwa
pro-Karume, akisikia chochote vilevile hatari. Wengi katika Baraza la Mapinduzi walikuwa
pro-Karume. Hata Khamis Abdalla Ameir, Ali Sultani, tuliwaogopa. Badawi [Quallatein] baada ya kuhujumiwa Pemba, yeye alikuwa Waziri Mdogo, kahujumiwa na Karume, akageuka. Akabadilika akawa pamoja na sisi.
Babu akitushtakia sisi kuhusu Khamis Abdalla Ameir. Ilikuwa linakuja jambo mbele ya Baraza la Mapinduzi dhidi ya Babu, basi Khamis akinyamaza kimya na wala hakuripoti kwa Babu kwa kuwa iko hivi hivi hivi. [Saidi] Bavuai ndo alokuwa anamwambia Babu, mambo yako hivi hivi hivi. Ukisemwa hivi hivi hivi.
Basi tukenda tukafanya mkutano mpaka karibu ya mwisho tena sasa tayari mambo lakini sasa sie watu wenyewe kidogo. Mimi nafsi yangu nimewaambia Hizbu, nimewaambia wale walokuwa
Mobile Force wale, Afro-Shirazi nnowaweza wale, nimewaambia. Madhumuni ilikuwa tupinduwe kijeshi. Ikafeli kwa sababu walewale tulowaambia waje, kina [Amour] Dugheshi, kina nani, wote wamefanya woga. Ila yeye Babu ndo amesema kaja mpaka pwani hapo, akarudi. Kina Tahir Ali, wamepanda boti hasa waje. Walipopanda wakaona mambo yameshavuja wakarudi. Mambo hayo lini. Alkhamisi tuliwaambia watu wote waje, tuliagana
Youth Tournament inakuja hiyo, kwa kuwa na nyie kabisa, Alkhamisi tuwe tayari. Lakini alokuja mmoja tu. Hashil Seif. Bas.
Ndo baada ya kuona tumefeli ndo akapanda Cariboo bado hajajulikana, akarudi Dar es Salaam akakamatiwa hukohuko. Na wengine wengi wamekuja lakini tulikataa kuwataja majina.
Babu ilikuwa aongoze ile
coup d'état [mapinduzi ya kijeshi]. Viongozi wangelikamatwa, akamatwe Karume akatangaze kwenye
radio, aseme kuwa ameshindwa, na nini. Tulikuwa tuna wenzetu ndani ya jeshi. Walipoona tumefeli wakapinda wote. Sasa wakajifanya wao
shrewd against [mahodari dhidi] yetu. Hao wanajeshi waliofanyiwa kampeni na Ahmada, Humudi,
etc (na kadhalika)
Sisi tumepanga wiki moja ya kule
store [ghala] ya silaha ni yetu sisi, na wiki moja yao wao, Afro-Shirazi. Wale walioko zamuni, wote wale wetu sisi. Kina Sindano, hao walokufa. Na wiki ya pili wanakuwa wao. Sasa sisi tulianza tangu Jumatatu kutowa silaha. Zikakaa kwa Humudi, kiasi mia, silaha mbalimbali, bastola, bunduki,
machine gun. Aliziweka kwake. Humudi alimtowa mkewe akenda zake Dar es Salaam, ukumbi mzima zikawekwa silaha. Tungeweka kwa Ahmada ingelikuwa hatari. Niliwaambia tukiziweka kwa Ahmada na yeye
Captain in charge wa mambo ya silaha atasachiwa. Na kweli, walishughulika juu ya Ahmada hawakumgusa Humudi. Mpaka saa tisa za jioni silaha hazijajulikana ziko wapi.
Mpaka saa kumi. Mpaka magharibi sisi tunaripuwa hazijajulikana zile silaha ziko wapi. Siku ile walipokamata wale ma-ASP ilipojulikana silaha zimeshaibiwa siku ya Ijumaa, manake wiki nzima zimekaa, siku ya Ijumaa zilipohisabiwa hakuna, kina Ali Mahfoudh wakataka kutupiga
curfew ile Ijumaa usiku, sisi tukasema hatuwahi.
Humudi ndo alipata ripoti hiyo saa nne asubuhi ndo akatuletea. Kuwa tukamatwe sote siku ileile ijumaa. Saa tisa tumekutana kwa Humudi ndo tukaamuwa. Hapo alikuweko Miraji, Chwaya, Harakati, Humudi, Ahmada, kina Falahy walikuwa chumba cha pili, hawajajuwa tunazungumza nini. Ishajulikana, hapana njia isipokuwa tumpige Karume na Sefu. Kwa sababu wale hawakuja, tutafeli, kina Amari Kuku, Ali Mshamgama, wogawoga, hawakuja kwenye mkutano saa tisa. Wote hawakuja. Potelea mbali. Wale wengine, khasa Saidi [Sindano] alokamata
store silaha alikwishasema "tumeshakufa."
Kwa sababu Sindano keshakimbia tangu saa nne ilipojulikana, anatafutwa. Sasa watu wetu tena wakaanza khofu. Kupatikana gari ndo Harakati akenda kuazima kwa Khamis Abdalla Ameir, manake ndo dereva wake. Nna safari yangu nataka kwenda. Sasa Khamis hajuwi anataka gari kwa sababu gani. Hajui, kampa, haya nenda. Chwaya kachukuwa gari ya
People's Bank yeye ndo dhamana.
Tena kina Ahmada wakaingia katika gari ya Chwaya, pamoja na…Gari ya Khamisi, Harakati, Saidi alouliwa Vuga. Na Rashid Falahy akaingia palepale Makao Makuu [ya Afro-Shirazi]. Sasa kumi na moja unusu tuseme wametoka, kumi na mbili wameshafika pale, wakaripuwa. Gari ya Chwaya, rangi ya bluu bluu ilitokea Malindi, ya manjano, ya Khamis, ina kipande cha MBM (Memba wa Baraza la Mapinduzi) kimeandikwa, ikapitia njia ya
Majestic Cinema.
Iliamuliwa kuwa tumuuwe Karume, tusimuuwe Thabit Kombo. Tumtishe tu basi. Kwa sababu kuweka mgawanyiko, iweko ubaguzi, Karume na Kombo. Wote tungewaweza ati pale lakini tumefanya makusudi tuweze kubaguwa. Afro na Shirazi labda italeta mgongano. Manake Karume ndo "Afro", yule Thabit Kombo "Shirazi."
Soma zaidi:
Source: Kitabu: Kwakeri Mkoloni, Kwaheri Uhuru
Mlango wa Kumi na Saba: Hayeshi Majuto Yao | Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!