Vita vinaingia mwezi wa tano. Wapalestina wa Gaza wamepiga makelele sana na hawakupata msaada wanaostahiki. Sasa ni mayowe tu kutoka kila eneo mfano wa yale mayowe ya watu waliovamiwa na majambazi wenye silaha usiku.
Mayowe sasa hivi yanatokea Rafaha mpakani na Misri. Upande wa nyuma kuna makuta yenye seng'enge na mbele yao na juu ni majeshi ya Israel yanayojiandaa kuvamia na kuvuruga eneo lote kwa kisingizio cha kuwamaliza Hamas na hata mateka hawawataji tena.
Eneo hilo kwa sasa lina watu takriban milioni moja na laki 3 zaidi ya nusu ya watu wa Gaza kabla ya vita.Watu hao wamesongamana kwenye mahema na wachache kwenye nyumba za ndugu zao ambazo zimegeuka kama vyumba vya mahabusu kutokana na msongamano.
Jamal Abu Tour kwenye eneo hilo ameiambia CNN katika kujifariji na kuwa na tamaa ya kupata msaada kuwa wanaomba Allah awasaide ili majeshi ya Israel yasitekeleze nia yao hiyo kwani hawana tena sehemu ya kukimbilia.
Mzee huyo akaendelea kusema kuwa hawataki warudi jiji la Gaza au Khan Younis na El Nuseirat kwani wamesikia wenzao huko wanakula majani na kunywa maji machafu.
Mahmoud Khalil Amer ambaye alikimbizwa kutoka kamba ya El Shati kaskazini ya Gaza na ambaye kwa sasa amejenga hema pembezoni pa makubiri eneo hilo Rafah,amesema kwa kweli kwa sasa hawana maisha.Waliokufa wanaweza kuwa ni bora kuliko wao.
Wakati mayowe ya watu wa Gaza yakiwa ya hali ya juu watu waliotarajiwa kuwasikia na kuwasaidia karibu wote ndio wamekuwa kimya zaidi kuliko mwanzoni mwa vita.Wale wanaoinua sauti baada ya kusikia mayowe hayo wanatoa matamko kama ya walevi.
Raisi Erdogan wa Uturuki karibuni alimlinganisha Netanyahu na Hitler.Wakati hukumu ya ICJ haikumshtua Netanyahu kauli kama hiyo ya Erdogan haina maana yoyote na ni kama ameridhia aendelee na analolifanya wakati angeweza kumzuia.
Ofisi ya raisi Mahmoud Abbbas wa mamlaka ya Palestina ukingo wa magharibi imesema wakati umefika kwa kila mmoja kutekeleza majukumu yake kuhakikisha janga kubwa zaidi halitokei na kuliingiza eneo lote kwenye vita visivyokwisha...
Tangu vita vianze ofisi hiyo haijaona janga tu na kauli ya ofisi hiyo mbona ni nyepesi kuliko uwezo wao wa kuzuia janga.
Katika hali ya kutosikilizwa mayowe yao ni vyema kwamba watu wa Gaza eneo la Rafaha wamejua ni wapi pa kupeleka kilio chao, kwa Allah muweza wa kila jambo, kwani huyo pekee ndiye mwenye uwezo wa kuwakinga na balaa kama alivyofanya kwa nabii Mussa a.s mbele ya Fir'aun na jeshi lake.