Wakati wa uwekwaji wa Wakfu kwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Iringa Askofu Romanus Mihali, Kanisa Katoliki nchini katika salamu zake kwaniaba ya Maaskofu wa Kanisa hilo Makamu wa Rais wa TEC, Eusebius Nzigilwa amesisitiza umuhimu wa kusikilizwa kwa sauti na vilio vya watu wanaotaka mabadiliko ya sheria za uchaguzi ili kuwa na uchaguzi huru na wa haki.
“Tunaomba kauli hizi nzuri za kututia moyo za viongozi wetu zionekane kwa vitendo katika hatua zote za uchaguzi, kwani baadhi ya matukio tuliyoyashuhudia kwenye jamii yetu hayaoneshi watendaji au wasimamizi wa sheria wanatekeleza kile kinachoahidiwa na viongozi wetu,” amesema.
Kupata matukio na taarifa zote kwa kila mkoa kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025 ingia hapa: Special Thread: Mijadala na Matukio ya Uchaguzi Mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
Huku waamini wakimsikiliza kwa utulivu, Askofu Nzigilwa amesema: “Kinachoahidiwa hakiendani na kile kinachotendeka. Ndugu mgeni rasmi (Dk Biteko, Naibu Waziri Mkuu) kwa muda mrefu kumekuwa na sauti zinazotaka Katiba na sheria zinazosimamia uchaguzi wetu zifanyiwe marekebisho ama maboresho ili ziendane na hali ya demokrasia ya vyama vingi.”
“Inavyoonekana ni kuwa wanaonufaika na upungufu wa sheria za sasa hawana haraka ya kufanya maboresho hayo, na wale wanaojiona wanaathirika na upungufu huo ndio wanapaza sauti kutaka mabadiliko ya Katiba na sheria.”
“Wito wetu sisi maaskofu kwa mamlaka zinazohusika ni kuwa sauti na vilio vya watu wanaotaka mabadiliko hayo zisikilizwe na zisipuuzwe,” amesema Nzingilwa ambaye ni Askofu wa Jimbo la Mpanda.
Akihitimisha salamu za Maaskofu amesema:“Tunaomba maboresho stahiki kwenye mifumo ya uchaguzi yafanyike ili kuruhusu ufanyike kwa uhuru na wa haki katika nchi yetu, vinginevyo chaguzi zetu zitaendelea kugubikwa na dosari nyingi kama zilivyoshuhudia kwenye chaguzi za hivi karibuni.”
Akigusia suala la uchaguzi kama lilivyozungumzwa na maaskofu, Dk Biteko amesema: “Kama mlivyoahidi na mimi nitakwenda kumwambia Rais ahadi ya kanisa kuendelea kuliombea Taifa ili uchaguzi umalizike kwa amani.”
Dk Biteko amesema: “Ujumbe alioutoa Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu, jamani Askofu akisema jambo hajibiwi.” Kauli hiyo iliibua shangwe kisha Dk Biteko akasema: “Hapana ni amina, baba nimepokea. Lakini jambo moja ambalo nina amini ni Rais wetu anatamani Watanzania tuwe kitu kimoja.”