Kwenye hii thread tutakuwa tuna share Mbinu za wizi za mafundi ujenzi ili kusaidia wale wanaotaka kujenga "wasipigwe ".
Wengi tumepigwa sana hadi kuzijua hizi mbinu.
Karibuni.
Fundi ujenzi asiye muaminifu atakuibia kupitia moja ya mbinu hizi, kutegemeana na umakini wa wewe unayejengewa nyumba.
1. Kuzidisha bei za vifaa - Hii hutokea kama wewe mwenye nyumba ni mgeni sana na masuala ya vifaa vya ujenzi na materials. Hapa bei zitaongezwa kiholela na utaibiwa kizembe kabisa.
Unawezaje kuepuka hili? Usiwe na papara, kabla hata ya kutafuta fundi jipe walau wiki moja ya kuuliza bei ya vitu kwenye maduka yaliyo karibu na site yako lakini pia pitia maduka makubwa kama yale ya Kariakoo - Mtaa wa Swahili, Kipata na mengineyo na ukiweza walau pitia pale Mwenge lakini pia maeneo ya Buguruni, Veterinary n.k
Kama ni mjanja unaweza kupita kwenye kurasa za mitandao za makampuni na wasambazaji wa vifaa vya ujenzi.
2. Kuzidisha idadi ya vifaa vinavyohitajika - Hapa nazungumzia ''materials'', hapa sasa kutegemeana na uzoefu wako wa masuala ya ujenzi, fundi atakutajia idadi kubwa ya materials zinazohitajika. Hapa atakuibia kwa namna mbili, moja kama utaenda kununua vifaa mwenyewe basi atavisubiri vifike eneo la ujenzi ili vile vinavyozidi akaviuze, njia ya pili kama ukimtuma yeye kwenda kununua basi hapo ataenda kununua idadi sahihi na hela ya vifaa alivyozidisha atabaki nayo kujipongeza kwa ujinga wako.
Hili unaweza kuepuka kwa kuwa na mtu mwenye utaalum wa mahesabu ya materials (Mkadiriaji Majenzi - QS) na usimamizi wa uhakika kwenye eneo lako la ujenzi.
3. Kuuza vifaa ulivyonunua - Hapa sasa kama amekukosa kwenye njia ya kwanza na ya pili.
Hapa fundi anaamua tu kwa makusudi kuuza ama kuchukua vifaa ulivyonunua kwa ajili ya ujenzi na kuuza. Hii hutokea sana kama eneo la ujenzi halina usimamizi kabisa. Hapa fundi umempelekea Gypsum board 50
sawasawa na hesabu na yeye anaamua tu kuchukua na kuuza Gypsum board 5. Hapa jioni unapokea simu kuwa kuna chumba hakijawekwa gypsum kwa kuwa zimeisha hivyo anakuomba kesho umpelekee gypsum boards 5 ili amalizie kazi.
Au kwa hesabu nyumba inahitaji ndoo tano za rangi, anaanza kazi huku anakwambia kuwa zinatosha, saa tisa , mchana anakutumia meseji kuwa upande wa nyuma hajapiga rangi kwa kuwa rangi imeisha hivyo umletee ndoo moja amalize kazi. Hiyo ndoo moja ameamua kuichukua na kuuza. Hii hufanywa sana wakati wa finishing; gypsum, tiles, rangi n.k
Unaweza kukabiliana na hili kwa kuwa na usimamizi wa uhakika kwenye eneo lako la ujenzi.
4. Kushirikiana na wauza vifaa vya Ujenzi - Hii hutokea fundi anapojua kabisa kuwa hautampa hela ya kwenda kununua vifaa na mtaongozana kwenda dukani kununua vifaa vya ujenzi. Atakachofanya ni kuwa na ushawishi wa kukuelekeza duka la kwenda kununua vifaa.
Hapa atampa taarifa mwenye duka kuwa kuna mteja namleta na hajui bei, hivyo kwenye bei ongeza hela ya juu. Ukifika dukani utashangaa kuona fundi wako anaunga mkono kila bei unayotajiwa lakini pia akisisitiza kuwa katika eneo hilo ni duka hilo ndio bidhaa zake ni bora zaidi.
Unanunua vifaa vya Milioni mbili na Laki tatu kumbe bei halisi ni Milioni Mbili kamili.
Njia ya kuepuka hili ni kuwa taarifa za bei kabla ya kwenda dukani na kutomshirikisha fundi kwenye wapi ukanunue vifaa vya ujenzi.
5. Kutumia mafundi wenzake kwenye kuzidisha bei - Hapa sasa una fundi wa ujenzi ambaye anajenga nyumba halafu umefika hatua fulani kwenye ujenzi unamuulizia kama anamfahamu fundi bomba (Plumber) au umeme (electrician). Hapa fundi akimleta huyo fundi bomba au fundi umeme ujue amashampanga azidishe bei ili na yeye apate chochote kitu.
Njia ya kuepuka hili ni kujua gharama za hizi kazi na kutomshikisha fundi wako kukutafutia mtaalamu wa haya mambo mengine.
6. Fundi kubaki na materials na vifaa vingine ambavyo ulinunua kwa ajili ya ujenzi - hapa sasa ndipo watu huwa wanawapa mafundi faida bila kujua. Unakuta unajenga nyumba na fundi anakwambia yanahitajika machepe, mbao za jukwaa, ndoo, mbao za kufungia column, beam , lintel na zile za slab. Unanunua vitu hivi kwa ajili ya nyumba yako. Lakini mwisho wa ujenzi hata wala hukumbuki kama kuna vitu ulinunua ili kurahisisha ujenzi wa nyumba yako. Fundi anatoka site akiwa na vitu vingi ambavyo sio mali yake ila wewe mwenye nyumba hujui kuwa zile ni mali zako.
Jinsi ya kuepuka hili ni kujua kuwa vifaa ulivyonunua wakati wa ujenzi ni mali yako na sio mali ya fundi.