Kumekuwa na Madai ya kwamba matumizi ya mboga za majani aina ya chainizi yamekua na madhara katika ufanisi wa tendo la ndoa kwa wanaume. Kuna ukweli gani katika hilo suala?
Naomba nijibiwe kitaalam niweze kuelewa.
Naomba nijibiwe kitaalam niweze kuelewa.
- Tunachokijua
- Chainizi hupatikana kwenye familia kubwa ya mboga za majani inayofahamika kwa jina la Brassica. Mfano wa mboga zingine zilizopo kwenye familia hii ni Kabichi (Cabbage) na Brokoli (Broccoli).
Asili ya Mboga hii ni nchi ya China ilikoanza kutumika Zaidi ya miaka 1500 iliyopita.
Bara la Amerika ya Kaskazini limeanza kulima mboga hii kwa zaidi ya miaka 100. Taarifa nyingi za kiuchunguzi na tafiti zinaonesha kuwa mboga hii kwa sasa imesambaa sehemu nyingi duniani, Tanzania ikiwemo.
Viambato na Kemikali zake
Kwa mujibu wa USDA, Mboga hii huwa na nishati, maji, protini, wanga, nyuzilishe, madini chuma, calcium, magnesium, phosphorus, selenium, potassium, sodium, zinc, copper na manganese.
Ni chanzo kizuri cha folate, vitamini C, viondoa sumu vya beta carotene pamoja na vitamin E.
Faida zake kiafya
Mjumuisho wa virutubisho vinavyopatikana kwenye Chainizi huwa na faida kubwa kwa afya ya binadamu. Kwa ujumla wake, mboga hii hufanya mambo yafuatayo-
- Kutoa kinga dhidi ya aina mbalimbali za Saratani hasa ile ya utumbo mpana
- Huzuia uvimbe (Inflammation)
- Hupunguza nafasi ya kuugua magonjwa ya mfumo wa damu na moyo
- Huimarisha afya ya mifupa
- Huboresha afya ya macho
- Huongeza uwezo wa kinga za mwili katika kupambana na magonjwa
- Ni nzuri kwa afya mama mjamzito katika kuongeza damu na kumkinga mtoto asipatwe na changamoto za kimaumbile, hasa tatizo la kuzaliwa na mgongo wazi
JamiiForums imefuatilia hoja hii kwa kuzungumza na wataalamu wa lishe na kugundua kuwa haina ukweli.
Chainizi haina kemikali sumu zinazoathiri ufanisi wa mwanamme kwenye kushiriki tendo la ndoa, pia hakuna tafiti za kiafya zinazoelezea madhara haya kwa binadamu.
Kwa kuwa msingi wa hoja za kisayansi hasa upande wa tiba huboreshwa, kupingwa na kuthibitishwa kwa tafiti, madai yanayohusisha mboga hii na upungufu wa nguvu za kiume hayabaki kuwa uzushi.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Afya ya Marekani (NHI), upungufu wa nguvu za kiume husababishwa na uwepo wa magonjwa sugu mwilini Pamoja na changamoto zingine zinazohusisha saikolijia, mfumo wa kati wa fahamu, homoni za mwili, mtindo wa Maisha Pamoja na matumizi ya baadhi ya dawa.