Kizungumkuti kambi ya upinzani Mtikila sasa amwita Mbowe fisadi
Habari Zinazoshabihiana
Mbowe: Makamba hawezi kuua Upinzani 04.01.2007 [Soma]
Mzimu wa ufisadi waingia upinzani 15.03.2008 [Soma]
Dkt. Mvungi amcharukia Mchungaji Mtikila 17.10.2005 [Soma]
*Adai Mrema angeingia Ikulu angekuwa kiroja
*Wote wamjia juu na kudai anataka malumbano
Na Gladness Mboma
MWENYEKITI wa chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, amemhusisha Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Freeman Mbowe, na miongoni mwa mafisadi kwa kukopa fedha za walalahoi za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya Taifa (NSSF).
Mchungaji Mtikila alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) kuhusu ufisadi uliotokea Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
"Mwenyekiti wa CHADEMA amefanya kazi nzuri ya kizalendo ya kumhusisha Rais Kikwete na wizi wa zaidi ya sh. bilioni 8 za EPA zilizochotwa BoT na kampuni ya mawakili ya IMMA Advocates inayomhusu mwanawe Rais akawapa watuhumiwa uwaziri na ujaji wa Mahakama Kuu.
"Lakini CHADEMA wamefumbia macho kabisa uporaji wa zile sh. bilioni 84 za walalahoi NSSF/PSPF, ambazo ni nyingi mara kumi kuliko za EPA zinazohusu IMMA Advocates! Kumbe pesa za NSSF ambazo wenyewe wastaafu na wafanyakazi wenye nazo hawakopeshwi hata wakifiwa na wazazi wao, zinaliwa na akina Freeman Mbowe," alidai Mchungaji Mtikila.
Alidai kuwa maswali yanayojitokeza ni kwamba Bw. Mbowe alipataje mkopo huo NSSF ikiwa walalahoi wanachangia Mfuko huo lakini hawapewi hata wakifiwa na ndugu wa damu na kuhoji kama si kwa ufisadi ni nini?.
Mwenyekiti huyo alitaka kujua kama kweli Bw. Mbowe hakuwa na uwezo wa kulipa deni au ni tatizo lake tu la kimaadili na kwamba kama kweli ilitolewa amri ya kukamatwa na kuwekwa gerezani, lakini akafaulu kukwepa na jalada la Mahakama linapotezwa ili kukwamisha utekelezaji wa amri zilizomo dhidi yake na kudai kuwa huo ni ufisadi.
Alisema ufisadi una sura nyingi na zote ni hatari kwa Taifa na kwamba siasa za nguvu ya pesa na zenye misingi ya ukabila, ni ufisadi wa hatari kwa nchi.
Mchungaji Mtikila aliongeza kuwa wivu wa watu fulani kutaka wajulikane wao tu kwa kudhibiti kifisadi vyombo vya habari visiwape jukwaa wengine wanaowazidi nguvu kwa wito wao wa kweli kwa ajili ya ukombozi wa nchi ni ufisadi pia.
Alisema ufisadi ni pamoja na kulazimisha kuwazidi umaarufu mashujaa wa kisiasa kwa kuwatukana kwamba wanatumiwa ili kusudi wadharaulike, ili umma uwaandamie wao.
"Wanasiasa wa nguvu ya pesa hukubali kuhongwa mapesa hata na mabeberu wanaotafuta vibaraka katika nchi wanazotaka kuzitawala upya kiuchumi, ili wakishika madaraka wao waipore nchi yetu kwa ubia na hao wasaliti. Lakini huu ukahaba wa kisiasa na usaliti wenzetu hawaufichi, badala yake wanauonea fahari," alidai Mchungaji Mtikila.
Aliendelea kudai kuwa siasa safi ni ushindani wa ajenda na viwango vya uhanga kwa ajili ya ukombozi wa nchi na walalahoi na kwamba "hatuwezi kulaani ufisadi wa CCM wa kuwanunua wapinzani na kunyamazia CHADEMA wanapofanya vivyo hivyo, kwa sababu upendeleo ni ufisadi pia".
Alidai kuwa ikiwa chama kinapata ruzuku ya mamilioni ya fedha za umma kila mwezi, mbali na misaada ya mabeberu wanaowatumia kununua uhuru wa nchi, halafu kinashindwa kutumia kiasi kidogo cha fedha hizo kwa ajili ya kupata Tume huru ya Uchaguzi mahakamani, ikatengeneza Daftari la kweli la Kudumu la Wapiga kura ni ufisadi pia.
"Itakumbukwa daima, kuwa Bw. Mbowe pamoja na viongozi wa CUF walitumiwa kuhujumu maazimio ya Aprili 18, 2004 ya vyama vyote vya upinzani, ambayo yangekuwa yameleta ukombozi wa nchi yetu," alidai Mchungaji Mtikila.
Hata hivyo, alimpongeza Bw. Mbowe kwa ushujaa wa kupambana na 'magabachori' baada ya kichocheo kizuri cha Dkt. Wilbroad Slaa na Bw, Zitto Kabwe aliyemsakama Bw. Nazir Karamagi aliyekuwa waziri wa Nishati na Madini.
Alisema lakini ni lazima warudi katika Torati kupata viongozi safi wenye sifa alizoagiza Mungu na kuwataka wasisahau kwamba kwa ajili ya nchi, ni lazima wawepo wahanga na si wanasiasa wa nguvu ya fedha na kwamba wanahitajika wanasiasa wenye wito, maono, vipawa na uponyaji wa kifikra na si helikopta.
Mchungaji Mtikila alidai kwamba tangu awamu ya tatu ya utawala, nchi inateswa na pepo chafu la ufisadi, ambalo baada ya kuinyonya damu yote sasa linataka kuitia kiberiti nchi iishie mbali na kwamba lisipowahiwa, haliwezi kutolewa kwa ufisadi.
"Hata Mwenyenzi Mungu anatwambia katika Biblia Takatifu, kuwa pepo mchafu hawezi kumtoa pepo mwingine, isipokuwa kama ufalme huo umefitinika na tiba ya ufisadi na uporaji na kunajisiwa nchi, utauawa na uzalendo wa kweli na si mkono mwingine wa ufisadi kwa mlango wa nyuma.
Kwa vile vita ya kutokomeza ufisadi kwa sehemu inachangiwa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, tukishaitokomeza CCM na kuwafilisi na kuwatupa jela mafisadi wake kama watapona kupigwa risasi hadharani katika viwanja vya Jangwani, tunawatahadharisha wananchi kuwa macho, wasidanganyike na kujikuta wamekabidhi nchi kwa mafisadi ambao ni waporaji zaidi," alisema Mchungaji Mtikila.
Alisema kutokomeza ufisadi na kuokoa nchi ni pamoja na Watanzania kuwaogopa kama moto uteketezao, wanasiasa waliojitajirisha kwa uporaji wa benki kwa usanii katika hundi, achilia mbali biashara haramu za dawa za kulevya, ndipo wakaingia katika siasa za kifisadi za nguvu za fedha.
Mchungaji Mtikila pia alimshutumu vikali Mbunge wa Igunga, Bw. Rostam Aziz na kudai kuwa alikuwa ni Mungu wa nchi ambaye alikuwa hatishwi na mtu yeyote yule.
"Rostam alikuwa ni Mungu wa nchi hii, ni nani angeweza kutia neno kwake na kumtisha kwa lolote; yeye alikuwa ndiye mwenye amri pekee ndani ya nchi hii, yote hiyo ni kutokana na kuwekana madarakani kirafiki," alisema Mchungaji Mtikila.
"Serikali inasema kiasi cha fedha kilichoibwa Benki Kuu na mafisadi ni sh. bilioni 133, hiyo si kweli fedha halisi zilizochotwa ni sh. trilioni 4.3," alidai.
Mchungaji Mtikila alimlaumu pia Mbunge mmoja akidai kuwa aliingiza mchele mbovu nchini na kuugawa kwa Watanzania bila huruma.
"Ninasema kuwa Watanzania mjiandae kufa siku si zenu kutokana na mchele mbovu mliokula na unaoendelea kuingizwa," alidai Mchungaji huyo.
Alisema kazi ya mbunge huyo ni kuwasiliana na nchi zinazohifadhi mchele mbovu kwenye makontena na kisha kusafirishwa hadi Tanzania bila kuwa na huruma.
Mchungaji Mtikila alimwandama pia Mwenyekiti wa TLP, Bw. Augustino Mrema na kudai kuwa mwaka 1995 alipokuwa akigombea urais, wafuasi wote waliokuwa wakimuunga mkono walikuwa wa kwake na si wa Mrema.
"Mwaka 1995 Bw. Mrema alikuwa awe Rais, hebu niambie kama angeshinda, huko Ikulu kungekuwa na kiroja gani, wafuasi wote walikuwa wangu, Mungu akitaka niwe Rais kwa saa na dakika naweza kuwa Rais," alijigamba Mchungaji Mtikila.
Akizungumza kwa njia ya simu akijibu tuhuma zilizotolewa na Mchungaji Mtikila dhidi yake, Bw. Mbowe alionekana kushtushwa na kauli zilizotolewa.
"Sina ugomvi wowote na Mtikila na wala sipendi malumbano naye na sikumbuki kama nilishawahi kugombana na Mtikila, ninamshangaa sana kwa kauli zake," alisema Bw. Mbowe kwa mshangao.
Alisema habari aliyoitoa hivi karibuni kuhusu ufisadi ni kwa maslahi ya Watanzania na wala si yake. "Mambo yote nilieleza juzi katika vyombo vya habari ni ya kweli sikupindisha, sasa namshangaa Mtikila kutaka malumbano nami," alisema.
Akizungumzia fedha za NSSF, Bw. Mbowe alisistiza kuwa yeye ni mwanachama wa Mfuko huo kama walivyo wanachama wengine na kwamba ana haki ya kukopa na kukopeshwa kama ilivyo kwa wanachama wengine na kisha kurejesha mkopo huo.
"Nimefanya makosa kukopa NSSF jamani? Mbona kampuni nyingi zinakopa ikiwemo Serikali; mimi mwenyewe ninachangia wakiwamo wafanyakazi wangu sijachota fedha kienyeji, nimefuata taratibu zote, ninamwomba Mtikila akafanye uchunguzi juu ya mkopo huo ndipo anivamie, asijisemee tu bila uchunguzi,"alisema Bw. Mbowe.
Alisema haitakuwa busara kuendelea kulumbana na Mchungaji Mtikila kwa kuwa hana ugomvi wowote naye na kwamba alifuata taraibu zote kuchukua fedha hizo NSSF.
Kuhusu Bw. Mbowe na viongozi wa CUF kuhujumu maazimio ya Aprili 2004 ya vyama vyote vya Upinzani, alisema yeye hakumbuki kama kuna hujuma yoyote ambayo alikwishafanya ya kupingana na wapinzani wenzake.
"Chama changu kiko mstari wa mbele kutetea haki na maslahi ya wananchi na kukubaliana na ajenda zote zinazopitishwa na vyama vya upinzani kwa pamoja, ninashindwa kuelewa anachozungumza Mchungaji Mtikila, nilihujumu kitu gani?," alihoji Bw. Mbowe.
Naye Bw. Mrema akijibu tuhuma dhidi yake kwa njia ya simu kuhusu wafuasi wote waliokuwa wakimuunga mkono yeye wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 1995, alisema hana sababu ya kulumbana na Mchungaji Mtikila kwa kuwa tangu mwaka 1995 haelewani naye na kwamba hana sababu ya kuzua ugomvi na mtafaruku naye.
"Anaposema kuwa wafuasi wote walikuwa wake, Mungu pekee ndiye aliyekuwa na uwezo wa kunifanya mimi niwe Rais, urais sikuupata sasa kwa nini anaendeleza malumbano nami? Aendeleze malumbano na marais walioingia madarakani mimi aniache," alisema Bw. Mrema.
Alisema mambo ya uchaguzi yalikwishapita tangu mwaka 1995 kinachotakiwa sasa ni kila mtu kufuata mambo yake na wala si kuchunguzana na kumtaka achunguze mambo yaliyoko sasa ya Richmond na EPA na si ya kwake kwa sababu hayaisaidii jamii.
"Mimi namshangaa sana, anasema mimi ningeingia Ikulu ningekuwa kiroja kwa lipi, mimi nina historia safi bwana, katika kipindi nilichokaa madarakani miaka ya nyuma, niliweza kukamata ndege iliyokuwa na dhahabu na sh. milioni 175 za walalahoi na bado nitakumbukwa kwa mazuri niliyowafanyia Watanzania.
"Ninachoomba kila mtu afikirie maisha yake, Mtikila asitafute malumbano nami na wala sitaki malumbano naye na wala sina muda huo, kila mtu ajenge chama chake, huu si muda wa kutupiana madongo na kujengeana chuki," alisisitiza Bw. Mrema.