Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Hawa Mchafu amedai baadhi ya wanaume wa Tanzania wanatumia nguvu kubwa kujadili habari za timu za Simba na Yanga zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, kuliko hata kujadili afya zao.
Hawa amesema kama nguvu hiyo ingetumika kujadili masuala ya afya ikiwemo kupima Ukimwi, huenda vita dhidi ya ugonjwa huo ingekuwa nyepesi.
Mbunge huyo ametoa kauli hiyo leo Jumanne Mei 11, 2021 bungeni mjini Dodoma wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya mwaka 2021/22.
Amesema wanaume wakikutana maeneo yote wanazungumzia timu hizo zenye upinzani wa jadi nchini badala ya kujadili masuala mengine ya msingi zikiwemo afya zao.
"Wanaume wa Tanzania wanatumia muda mwingi kujadili Usimba na Uyanga, hawapimi virusi vya Ukimwi na hawataki kupima, hivi ingetumika muda huo kuzungumza masuala ya kupima afya zao si tungeshinda," amehoji Mchafu.
Mei 8, 2021 mchezo kati ya miamba hiyo ya soka nchini uliahirishwa baada ya kutokea mkanganyiko uliosababishwa na ratiba kubadilishwa kutoka saa 11 jioni na kusogezwa mbele hadi saa 1 usiku jambo lililozua sintofahamu huku kila shabiki wa soka nchini akizungumza lake.