akihojiwa kiongozi ambae nae alijeruhiwa amedai kabla ya Ajali kuna land cruiser ilipita mbele yao kwa spidi na ndio chanzo cha wao kupt Ajali
chanzo. ch10
my take: polisi msipuuzie kwan kwenye mitandao kuna kauli isemao huna haja kujiua taja ugonjwa wa mh it will happen.
[h=2]Familia yafunguka kifo cha Mtikila.[/h]
Hatimaye, familia ya Mchungaji Christopher Mtikila, imeibuka na kuelezea hisia zao kuhusiana na uvumi uliozagaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii juu ya chanzo cha kifo cha mpendwa wao huyo aliyefariki dunia juzi alfajiri baada ya gari alilokuwa akisafiria kupinduka akiwa njiani kutokea Njombe kuelekea jijini Dar es Salaam.
Mchungaji Mtikila ambaye hadi umauti unamfika alikuwa Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), alifariki dunia katika ajali iliyohusisha gari alilokuwa amekodi aina ya Toyota Corolla, lenye namba za usajili T 189 AGM, kuacha njia na kupinduka katika kijiji cha Msolwa, Chalinze mkoani Pwani. Taarifa ya Polisi ilieleza kuwa ajali hiyo iliyotokana na mwendokasi mkubwa, ilimkuta Mtikila wakati akirejea kutoka katika mikutano ya kampeni ya wagombea ubunge na udiwani wa chama chake mkoani Njombe.
Hata hivyo, taarifa mbalimbali zilizagaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa kifo cha Mtikila kimejaa utata na baadhi yao kwenda mbali zaidi kwa kukihusisha na baadhi ya wanasiasa wakiwamo wanaogombea uraisi; kwa madai kuwa msimamo wa Mtikila kuhusiana na baadhi yao ndiyo chanzo cha ajali iliyomuua.
Baadhi ya mitandao ya kijamii imekuwa ikieleza kuwa marehemu Mtikila alifikwa na mauti hayo kwa kunyongwa, jambo lililoibua mkanganyiko kwa baadhi ya wananchi kuhusiana na kifo cha mwanasiasa huyo aliyekuwa mmoja wa wapambanaji wasiosahaulika katika harakati za kurejesha mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992.
Hata hivyo, kwa kutambua hilo, familia ya Mtikila iliibuka jana na kuamua kuelezea kwa kina juu ya suala hilo kwa kile ilichodai kuwa ni kuwawezesha Watanzania wafahamu undani wake na pia kujua juu ya msimamo wao.
Msemaji wa familia hiyo, Victor Manyahi, akizungumza na Nipashe jana jijini Dar es Salaam, alisema Mchungaji Mtikila alifariki dunia kwa ajali ya kawaida tofauti na inavyoelezwa na baadhi ya watu, baadhi ya vyombo vya habari na pia kwenye mitandao ya kijamii.
"Mchungaji alikufa kwenye ajali ya gari ambayo kimsingi ilikuwa kwenye mwendo wa kasi wa takriban kilomita 120 kwa saa na bahati mbaya hakufunga mkanda, hivyo gari lilipopoteza mwelekeo na kupinduka, akatoka na kukandamizwa nalo,"alisema.
Akieleza zaidi, alisema wakiwa safarini, kuna gari lilitanua upande wao na dereva wa gari alilokuwa amepanda Mchungaji Mtikila, kwa kujihami akaamua kupeleka gari porini na kusababisha gari hilo kupasuka matairi ya mbele kabla ya kupinduka.
Manyahi alisema baada ya ajali hiyo kutokea, Mchungaji Mtikila alipata majeraha kichwani na gari lilimkandamiza kabla ya wasamaria wema kufika eneo la tukio na kumtoa.
"Mchungaji alibanwa na gari na kusababisha akose hewa... na kama angepatiwa huduma ya kwanza vizuri, pengine maisha yake yangeokolewa,"alisema na kuongeza:
"Inasikitisha sana kuona watu wanazusha mambo ya ajabu wakati ajali ile ilikuwa ni ya kawaida, licha ya kwanba imeleta maafa."
Akieleza zaidi, alisema wakati kunatokea ajali hiyo, hakukuwa na mtu yeyote mahali pa tukio na kwamba, hata waliokuwamo katika ajali hiyo wamethibitisha kwamba hakukuwa na mkono wa mtu.
"Nadhani wanaosambaza taarifa hizo za uongo wana sababu zao binafsi... huwezi kuhusisha watu katika tukio kama hilo hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi," alisema Manyahi.
RATIBA MAZISHI
Katika hatua nyingine, Manyahi alitoa muhtasari wa ratiba ya mazishi ya Mchungaji Mtikila kwa kueleza kuwa kesho (Jumatano), wakazi wa jiji la Dar es Salaam watapata fursa ya kuuaga mwili wake kabla ya kuusafirisha kwenda kwao wilayani Ludewa, mkoa wa Njombe.
Alisema mazishi yatafanyika kati ya Alhamisi au Ijumaa wiki hii katika Kijiji cha Milo wilayani humo (Ludewa).
POLISI WAFAFANUA
Kufuatia kuzagaa kwa taarifa potofu kuhusu ajali ya Mtikila, Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani chini ya Kamanda wake Jaffary Ibrahim, jana lilitoa taarifa kuelezea ajali hiyo na kusema kuwa uchunguzi wao umethibitisha kuwa ilisababishwa na mwendo kasi mkubwa na kwamba hata baada ya ajali, ilirushwa umbali wa mita 125 kutoka barabarani.
Kadhalika, taarifa hiyo ileleza sababu nyingine za ajali hiyo ni uchovu wa dereva kutokana na safari ndefu kwa kuendesha gari mchana na usiku kucha; kutofunga mikanda ya usalama kwa marehemu Mtikila ambaye baada ya ajali alirushwa nje kupitia kioo cha mbele na pia ubovu wa gari, hasa mfumo wa usukani (steering system).
Taarifa zaidi ya Polisi imeeleza kuwa uchunguzi wa daktari unaonyesha Mchungaji Mtikila alipoteza maisha baada ya kuvunjika kwa mbavu nane upande wa kushoto na kuingia kwa damu kwenye mfumo wa hewa na kumuondolea uwezo wa kupumua.
Kwa sababu hiyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limewataka wananchi kuacha kutoa taarifa za uongo na uzushi pindi ajali na matukio mbalimbali yanapotokea na kwamba halitasita kuwachukulia hatua waenezaji wa taarifa potofu kwenye mitandao kwa mujibu wa Sheria ya Mtandao.