Ubalozi wa Tanzania nchini Nigeria kwa kushirikiana na Jimbo Katoliki la Minna nchini humo na Serikali ya Nigeria zilihangaika usiku na mchana kuhakikisha wanaachiwa huru kwa kutumia mbinu zote.
Pia Watanzania hasa katika jimbo la Kigoma alikotoka Melkiori, walikuwa wakimwombea kijana huyo pamoja na Padri Sanogo ili wapatikane wakiwa hai na sasa maombi hayo yamejibiwa, wako huru.
Anasimulia ilivyokuwa
Melkiori anasema Agosti 2, Saa 5 usiku (saa 7 usiku kwa saa za Tanzania), alikuwa akizungumza kwa simu na rafiki yake Mtanzania aliyopo nchini humo, baada ya kumaliza mazungumzo akasikia milio ya risasi.
Akajiuliza inatokea wapi, lakini akajipa matumaini huenda ni wawindaji kwa kuwa eneo wanaloishi limejitenga kidogo.
Baada ya dakika chache, anasema alisikia tena milio hiyo ya risasi, hivyo ikabidi achungulie dirishani aone kuna nini.
“Bahati nzuri chumba changu kiko ghorofani, nikafungua dirisha nikawaona magaidi wawili wanaingia, wakaanza kuingia chumba kimoja baada ya kingine. Walipofika kwenye chumba changu nikaruka dirishani,” anasimulia Melkiori.
Anasema baada ya kuruka alivunjika vidole vya miguuni, hata hivyo hakuhisi maumivu wakati huo kwa sababu alikuwa ameghadhabika akipambana kujiokoa kutoka kwa wavamizi hao wenye silaha.
Melkiori anasema alikimbilia kwenye bustani iliyopo pembeni mwa nyumba wanayoishi ambako huko alikutana na watekaji wengine wawili waliomkamata na kumwambia watamuua.
“Wale watu wakaniuliza kwa lugha ya Hausa, oga yuko wapi, yaani bosi wako yuko wapi? Basi kwa kuwa na mimi najua kidogo lugha hiyo nikawaambia sijui alipo. Wakanibeba wakasema nikawaonyeshe chumba chake,” anaeleza.
Melkiori anasema aliondoka nao na kuwapeleka hadi kwenye chumba chake, akawaambia hicho ndiyo chumba cha bosi wake. Humo alikuwa na fedha takribani Sh400,000 za kitanzania, kadi ya benki (ATM) ikiwa na kama Sh500,000, vyote vilichukuliwa na watekaji hao pamoja na nguo zake.
Hata hivyo, wakamwambia fedha hizo hazitoshi, hivyo wakamchukua na kushuka naye chini, huko akakutana na wengine wakiwa wamemkamata Padri Sanogo. Wakawaambia waonyeshe walipo wenzao, hawakufanya hivyo wakasema wanataka kulipua nyumba.
“Hawa jamaa walikuwa zaidi ya 12 na wote walikuwa na bunduki na mabomu. Hatukutaka kusema sisi ni watu wa dini kwa kuwa wangeweka msukumo zaidi na kutaka pesa nyingi,” anasema Melkiori.
Hivyo, anasema wote wawili walichukuliwa na kupelekwa kwenye msitu mnene wanakojificha watekaji hao.
Anasema walisafirishwa usiku huohuo hadi katika msitu huo ambao ukiingia kutoka siyo rahisi.
Walipofika wakaanza kuhojiwa lakini wakawaambia wao si Wanigeria, walikwenda huko kujifunza lugha na aliwaeleza yeye ni mkulima na mwenzake (Padri Sanogo) ni mpishi na wazazi wake wamestaafu
“Wakasema tumpigie bosi wetu simu, walikuwa wakitaka Naira 100 milioni. Tukawapa namba zake wakaongea naye, akawaambia yuko tayari kuwapa pesa hizo. Aliwaambia hivyo ili wasitudhuru, wakaendelea kusubiri,” anaendelea kusimulia.
Walivyokuwa wakiishi
“Tulikuwa tunaishi ndani ya pori nene. Hakuna nyumba wala tenti. Tulikuwa tunalala kwenye mawe au nyasi. Hakuna kujifunika.
“Tulikuwa tunalala tumefungwa mikono na uso tunafungwa kitambaa. Mvua, jua ilikuwa ni sehemu ya maisha yetu, chakula tulikuwa tunapika wenyewe ila kwa kiasi kidogo kwa siku, wakati mwingine hakuna msosi. Kuoga haikuwa inaruhusiwa,” anasimulia Frateli huyo.
Anasema baada ya siku kadhaa kupita, watekaji hao wakaanza kupoteza matumaini ya kupata fedha hizo, hivyo wakawa wanatishia kuwa watawaua kama hawatapewa Naira 80 milioni na si 100 tena.
Anasema waliendelea kufunga kwa sala huku wakimwomba Mungu awaokoe kutoka mikononi mwa watekaji hao. Baada ya muda, anasema walianza kuona nguvu ya Mungu kwa sababu watu hao walianza kudhoofika, wakaanza kugombana wao wenyewe. Anasema waliendelea na maombi na kwamba alikuwa akisali kila siku sala ya Mtakatifu Rita wa Kashia pamoja na sala ya Bikira Maria.
“Mtu wao aliyekuwa akiwasiliana na viongozi wetu akawaambia (viongozi wetu) wana kiasi kidogo cha fedha wawapatie ili watuachie huru. Kilikuwa kiasi gani, sijui lakini kwa kuwa walikuwa wamechoka, wakakubali kupokea.”
Hivyo, waliwaachia huru Jumatano Agosti 23, Saa 5 asubuhi.
Baada ya kuachiwa huru
Melkiori anasema baada ya kuachiwa huru, changamoto ikawa ni namna ya kutoka nje ya msitu huo kwa sababu uko mbali takribani kilomita 100 kutoka yalipo makazi ya watu. Hivyo, anasema walianza kutembea kwa miguu kwenda wasikokujua.
Walipokuwa wakitembea walikuwa wakipishana na malori yaliyokuwa yamebeba mbao. Waliendelea na safari kwa mguu na ilipofika saa 3 au 4 usiku, walikuwa kwenye kijiji cha kwanza, wakasikia wanakwaya wanaimba sofa, wakajua ni wenzao.
“Nikamwambia mwenzangu ‘ngoja niende nikazungumze nao’, nikaenda tukaongea kwa lugha ya Hausa, nikawaambia mimi ni Frateri, tunakwenda Abuja, wakatuelekeza njia na kutupa msaada,” anasema.
Usiku huohuo wakachukua pikipiki kuwapeleka kwenye parokia ya jirani, wakapokelewa na kupewa huduma ya kwanza. Anasema walikuwa wamechoka na miguu ilikuwa imevimba kwa kuwa walitembea umbali mrefu.
Wakiwa parokiani hapo, simu ikapigwa kule walipokuwa wakiishi, wakaja kuchukuliwa na gari na kupelekwa hospitali ambako mpaka sasa anapatiwa matibabu. Anasema wanamshukuru Mungu kwa kujibu maombi ya watu waliokuwa wakiwaombea kila siku walipokuwa mikononi mwa watekaji hao.
Kuhusu kurejea Tanzania, Melkiori anasema hajajua ni lini. Hata hivyo anasisitiza hawezi kuikimbia Nigeria kwa sababu ya tukio hilo, ataendelea na utume wake kadiri ya Mungu alivyompangia.
“Nigeria ni nchi nzuri isipokuwa kuna watu wachache hawataki kufanya kazi, wanateka watu ili wapate pesa,” anasema Melkiori.
Sifa ziende kwa Serikali ya Tanzania, Nigeria na makanisa ya RC Duniani