Mfuko wa Maendeleo wa China na Afrika (CAD-Fund) ulianzishwa kwenye juni mwaka 2007, kwa lengo la kuitikia mahitaji ya ukosefu na fedha na uwekezaji kwenye miradi ya maendeleo katika nchi za Afrika. Katika muda wa miaka 18 tangu kuanzishwa kwake, mfuko huo umetatua changamoto nyingi za kifedha kwenye miradi ya maendeleo ambayo wadau wa magharibi (hasa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF) wanakataa kuifadhili.
Moja ya changamoto kubwa zinazozikabili serikali za nchi za Afrika ni ukosefu wa fedha kwenye miradi mikubwa inayoweza kuchochea maendeleo ya nchi. Na zinapojaribu kukopa fedha toka Benki ya Dunia au Shirika la fedha la kimataifa IMF, masharti yanayowekwa mara nyingi yanakuwa magumu, na wakati mwingine matokeo yake ni kuhatarisha uhuru na hata kuleta umaskini zaidi kwenye nchi za Afrika. Kutokana na kutambua hilo China ilianzisha mfuko huo ambao uko chini ya Benki ya maendeleo ya China, ambao unaendesha shughuli zake kwa misingi ya soko, lakini kwa masharti na gharama nafuu kwa wakopaji wa Afrika.
Moja ya maeneo yaliyokuwa na ukosefu mkubwa wa fedha, na ambayo ilikuwa ni vigumu sana kupata fedha kutoka mashirika la fedha ya kimataifa ni eneo la miundombinu, iwe ni ya barabara au ya huduma za jamii. Lakini kupitia mfuko huu miradi mingi ilianza kujengwa na sasa imekamilika na inawanufaisha wananchi. Mfano ya miradi iliyofadhiliwa na mfuko huu, ni pamoja na ile ya umeme wa maji nchini Kenya na ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini Ghana. Pia viwanda vingi vipya vilivyojengwa nchini Ethiopia na Afrika Kusini, ambavyo vimetoa maelfu ya fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, vimejengwa kupitia ufadhili wa mfuko huu. Nchini Tanzania, kituo cha kisasa kabisa cha upasuaji wa moyo kwenye Hospitali ya Muhimbili, kimejengwa kupitia utaratibu wa mfuko huu.
Pengine jambo la kutia moyo zaidi kuhusu mfuko huu ni kuwa unalenga kuhimiza maendeleo ya Afrika katika maeneo yote. Kupitia mfuko huu serikali ya China imekuwa ikiyahimiza makampuni yake yenye uwezo bila kujali yapo kwenye sekta gani, kuwekeza na kuchochea maendeleo barani Afrika. Miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ya kuzalisha umeme, ujenzi wa reli, bandari, na kongani za viwanda, ambayo inaweza kuboresha muunganisho na kuweka mazingira bora ya maendeleo ya kiuchumi, pia imekuwa inafadhiliwa kupitia utaratibu wa mfuko huu.
Hata hivyo mfuko huu umekuwa unakosolewa na baadhi ya wadau wa maendeleo wa nchi za magharibi, kwa madai kuwa unakiuka baadhi ya kanuni za kifedha za kimataifa. Lakini uhalisi wa mfuko wa CAD-Fund ni kuwa unafanya kazi zake kibiashara, na kwamba kati ya machaguo yote yaliyopo kwa nchi za Afrika kufadhili miradi yake, mfuko huu ni rahisi, wenye gharama nafuu, na ambao matokeo yake yanaonekana kwa haraka zaidi. Kwa nchi za Afrika ni chaguo linalofaa. Kwa hiyo ukosoaji huo kimsingi unatoka kwa wale ambao wamekosa fursa za kujipatia fedha kutoka kwa serikali za Afrika kwa njia za kinyonyaji.
Jambo lingine la muhimu ni kuwa chaguo hili linaendana na nadharia ya China. Kwamba ukitaka kumsaidia mtu mwenye njaa, usimpatie samaki tu, bali mfundishe pia kuvua samaki. Miradi mingi inayotekelezwa kupitia mfumo huu, ina kipengele cha “kuhamisha teknolojia na ujuzi”. Tukiangalia mfano wa ujenzi wa reli ya SGR ya Kenya, kwenye hatua za awali za ujenzi wa reli hiyo, kulikuwa na idadi kubwa ya wataalam wa China, lakini polepole kupitia mafunzo ya wakenya waliopatiwa mafunzo nchini China, na wale waliopata uzoefu kwenye maeneo ya kazi wakati wa ujenzi wa reli hiyo, hatua kwa hatua sehemu kubwa ya watu wanaendesha mradi huo kwa sasa ni wenyeji.