Mgogoro wa Morocco 🇲🇦 na Sahara Magharibi, kisa na mkasa

Mgogoro wa Morocco 🇲🇦 na Sahara Magharibi, kisa na mkasa

JumaKilumbi

JF-Expert Member
Joined
Sep 7, 2022
Posts
432
Reaction score
507
Na Jumaa Kilumbi
10.11.2022

KaskazIni Magharibi mwa Afrika kuna mzozo kati ya nchi ya Morocco na nchi ya Jamhuri ya Waarabu ya Kidemokrasia ya Sahara (Sahrawi Arab Democratic Republic, SADR, Sahara Magharibi).

Morocco inadai kuwa Jamhuri ya Sahara Magharibi ni sehemu ya nchi yake huku Jamhuri ya Sahara Magharibi inadai kuwa yenyewe ni nchi huru inayojitegemea. Mzozo huu ni wa miongo mingi na andiko hili linalenga kutazama historia ya mzozo huu na kupendekeza suluhu itakayoleta amani ya kudumu.

02n3g1j65NZFMSr-_sPtEO__vhuWWQJq10LjiqIfuf4xGeEwCyCmR8lmY5OJL57aUy4rOovK3zP8fnCxeNNrIgoxRYPNAlH4XzUfO2cexeGKC09PzPobSviJaTBnl0brnJYoxAVbHlflAmjvHQ8L_oQB61uxq8cAM110vNahCqaDZQ-ayeOqefevbwEAbA


Jiografia ya nchi hizi
Morocco ni nchi inayopatikana kwenye pembe ya kaskazini-Magharibi mwa Afrika na upande wa Kusini imepakana na Sahara Magharibi na upande wa mashariki imepakana na Algeria, huku upande wa Magharibi ikipakana na bahari ya Atlantiki.

Jiografia ya Morocco inajumuisha safu zisizopungua nne za milima, pamoja na mabonde ya mito, pwani nzuri za mchanga, na maeneo mapana ya jangwa.

Jamhuri ya Waarabu ya Kidemokrasia ya Sahara (Sahrawi Arab Democratic Republic, SADR) ama Sahara Magharibi ni eneo lililo kaskazini-magharibi mwa Afrika, likiwa kusini mwa Morocco na upande wa mashariki imepakana na Mauritania na Magharibi imepakana na bahari ya Atlantiki. Uwepo wake katika kingo za Bahari ya Atlantiki unaipa
umuhimu wa kimkakati kwa mataifa ya Ulaya na Afrika kaskazini.


Historia ya nchi hizi enzi za Ukoloni

Uwepo wa Morocco katika eneo lililo lango linalozikutanisha bahari ya Mediterranea na Bahari ya Atlantiki liliyavutia madola ya Ulaya kutaka kuitawala.
Mnamo 1912 baada ya kusainiwa kwa Mkataba wa Fez, Morocco ilitangazwa kuwa chini ya ulinzi wa Ufaransa (Protectorate), mwaka huo huo baada ya makubaliano kati ya Ufaransa na Uhispania Sahara Magharibi ikatangazwa kuwa chini ya ulinzi wa Uhispania (Protectorate) na ikaitwa ‘Spanish Sahara’ ama Sahara ya Uhispania.

Uhispania ilivutiwa na uwepo wa Sahara katika kingo za bahari ya Atlantiki iliyowapa waHispania eneo kubwa zaidi kwa ajili ya uvuvi. Hivyo Sahara ikatawaliwa na Uhispania huku Morocco ikitawaliwa na Ufaransa.

d7MdUUics2ryp_8ct82U-ipaNcCHAVM4ZalYv_5gMJ0vQ--JqAedR5UbrG310b0s7x00HQl94dmhJm1U6oSSb2ss7NE_tdx311A6OIeLNfDDbbjSGYpjBUnbtsd4ZME6Rxak9poaVGKreAEZFVlx2NKcvaEKIoWWBFQ0rSe-HNDhC2KX0irVrzP6PHOzxg



Ukoloni katika nchi ya Morocco ulifika ukomo Mnamo Machi 1956 ambapo Morocco ilijipatia Uhuru wake toka kwa Ufaransa baada ya machafuko na hisia kali za utaifa (nationalism).

Katika Vyuo Vikuu vya Morocco wanafunzi wenye asili ya Sahrawi pamoja na wenzao waliokuwa nchini Algeria na Mauritania waliunda kile kilichokuja kuitwa ‘The Embryonic Movement for the Liberation of Saguia el-Hamra na Rio de Oro’ kwa lengo la kuikomboa Sahara ambayo bado ilikuwa chini ya utawala wa kikoloni wa Uhispania.

Mnamo Mei 1973 vuguvugu lililopewa jina la Polisario Front liliundwa ambalo lilijumuisha hasa watu wenye asili ya Sahrawi toka Morocco, Algeria na Mauritania huku lengo kuu likiwa ni kuikomboa Sahara Magharibi (SADR) kwa gharama yoyote ile.


Vuguvugu hilo lilipata kuungwa mkono na Algeria na Libya na Mauritania.

Wakati Uhispania ikijiandaa kuondoka Sahara Magharibi, Novemba Mwaka 1975 Morocco ilituma raia 350,000 waliovuka mpaka na kuingia Sahara katika kile kinachojulikana kama maandamano ya ‘Green march’ kwa lengo la kuishinikiza Uhispania kuikabidhi Morocco koloni hilo.

Rhy_vk1-aVuLOGP_OOZtB5zi6vlp_w330a0e6Hf2u-F1Ahvw9o0XsXqxs69PQouwi6UfC_-J6euP2UhWmuI_bMUHIoJHr_8FpOGsDFJqoF8iyOCioCXCt4Emn2ypoET8dss5e1xTDparZLYv6j7anNelUNhPp5Lhl0OyKtqo36HHL1UlLh6ek8K9ZWBJXA


Uhispania haikuweza kukabiliana na vuguvugu hilo hivyo ikalazimika kutafuta suluhu kwa njia ya amani na siku chache baadaye ndani ya mwezi huohuo mwaka 1975 nchi za Morocco, Mauritania na Uhispania zilisaini Mkataba wa Madrid, katika mkataba huu Uhispania ilizikabidhi Mauritania na Morocco eneo la Sahara Magharibi kwa sharti la kuwa Uhispania itachukua 35% za migodi yote ya Fosfeti (Phosphate) iliyopo Sahara Magharibi na haki za uvuvi ( Fishing rights) katika maji ya Sahara Magharibi kwa muda wa miaka kumi.

Algeria haikukubaliana kabisa na suluhu hilo kwakuwa iliona kuwa watu wa Sahara Magharibi waliowakilishwa na Polisario Front hawakushirikishwa wakati wa majadiliano hayo na ikatishia kupigana dhidi ya Morocco kuitetea Sahara Magharibi.

Toka mwaka huo Polisario Front walipewa hifadhi nchini Algeria pia walipewa vituo vya kijeshi, misaada ya silaha na uungwaji mkono wa kisiasa. Polisario Front ilianzisha mashambulizi ya kupigana na Mauritania na Morocco ili kuwa nchi huru.

Kwa kuanza tu, ilipotimu Februari 27, 1976 Polisario Front ilitangaza kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Sahrawi kuwa ni nchi huru na mipaka yake ni eneo lote la Sahara Magharibi.
Awali Jamhuri hiyo ilitambuliwa na idadi ndogo ya nchi, mojawapo ikiwa ni Algeria.

Mapigano yalipamba moto baina ya Polisario Front ikiungwa mkono na Algeria dhidi ya Mauritania na Morocco ambazo ziliiona Polisario Front kama kikundi cha waasi.

Mwaka 1979 Mauritania ilitupilia mbali madai yake kuwa eneo la Sahara Magharibi ni lake kwa mujibu wa mkataba wa Madrid hivyo Morocco ikabaki peke yake kuendelea na madai hayo na ilifanikiwa kutwaa sehemu kubwa ya eneo la Sahara Magharibi.

Mapigano kati ya Polisario Front na vikosi vya Morocco yaliendelea hadi 1991 wakati ambao Umoja wa Mataifa uliishinikiza kusitishwa kwa mapigano, wakati huo Polisario Front ilidhibiti 20% tu ya eneo lote inalodai kuwa ni la kwake.

Mwaka 1984 Organization of African Union (OAU) iliitambua nchi ya Sahara Magharibi na kuipa uanachama wa Umoja wa Afrika, Morocco iligomea uamuzi huo kwa kuamua kujitoa kwenye OAU Mwaka.

Mgogoro huu umekuwa ukiendelea mpaka hivi karibuni kati ya Polisario Front na majeshi ya kifalme ya Morocco kitu ambacho kinatishia maisha ya watu wanaoishi katika eneo hilo na kuchochea mgawanyiko zaidi katika Umoja wa Afrika.


Sababu na Chanzo cha mgogoro huu
02A342DA-8F9A-4773-8BE9-F5AB5FF7D18A.jpeg

Mkataba wa Madrid wa Novemba 14 1975, yalikuwa ni makubaliano yaliyofikiwa kati ya Morocco, Mauritania na Uhispania kwa lengo la kumaliza ukoloni wa Uhispania katika eneo la Sahara Magharibi.
Mkataba huu ndiyo chanzo kikuu cha mzozo huu kwani makubaliano hayo ambayo hayakuwashirikisha wakazi wa Sahara Magharibi wala wawakilishi wao Polisario Front yalichochea mapigano kati ya Polisario Front iliyodai uhuru wake toka kwa Uhispania, Morocco na Mauritania ambao walidai kuwa maeneo ya sahara ni ya kwao.

Mapigano hayo yanaendelea mpaka leo, Polisario Front wanadai kuwa wakoloni (Morocco) bado hawajaondoka katika eneo hilo.

Kwa sasa Morocco inadhibiti takriban 80% ya Sahara Magharibi. Polisario Front inadhibiti 20% pekee.

Kukosa msimamo kwa Umoja wa Mataifa, kwa upande mmoja, Umoja wa Mataifa ulisisitiza kuwa suala hilo lilikuwa ni la ‘Self determination’, jambo ambalo lilimaanisha kuwa masuala mengine ya mzozo huo yatapuuzwa kabisa (haswa pingamizi la Algeria dhidi ya Morocco kukiuka kanuni ya ‘uti possidetis’, isemayo kwamba mipaka iliyorithiwa kutoka enzi ya ukoloni inaweza kubadilishwa kwa njia ya mazungumzo pekee), na kwamba mzozo huo ungeweza kutatuliwa kwa kura ya maoni (Referendum) tu ambapo suala la aidha Sahara Magharibi itakuwa huru au itakuwa sehemu ya Morocco litakuwa ni chaguo la wapiga kura.

Kwa upande mwingine, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshughulikia suala hili chini ya Sura ya VI ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa (Chapter VI, UN Charter), ambayo inataka migogoro kutatuliwa kwa mazungumzo (badala ya chini ya Sura ya VII, ambayo inaidhinisha kuwekwa kwa usuluhishi unaofunga (binding) au hata kulazimisha (coercion)), na hivyo kuipa Morocco kura ya turufu ambayo imeitumia mara kwa mara tena kikamilifu kuhujumu kila jaribio la kuandaa kura ya maoni (Referendum).
International Crisis Group (ICG) ilisema kuwa Umoja wa Mataifa hauwezi kusuluhisha mzozo wa Sahara Magharibi, na kwamba inapaswa kuruhusu pande zinazohusika kusuluhisha mgogoro huu wao wenyewe kupitia mazungumzo baina ya nchi mbili bila uangalizi wa Umoja wa Mataifa au masharti yoyote.

Nchi za kigeni kama vile Marekani, EU na Algeria, nchi na jumuiya tajwa zinachochea mgogoro huu kuendelea.
Algeria inatoa msaada kikamilifu kwa Polisario Front tangu kuanzishwa kwake kwa kutoa mafunzo ya kijeshi, misaada ya silaha, na hata askari wa kujitolea ili kuimarisha zaidi harakati zao.

Marekani kwa upande mwingine imekuwa ikiunga mkono madai ya Morocco juu ya Sahara Magharibi na kukubaliana na pendekezo la Morocco la kuichukua Sahara Magharibi na kuifanya kuwa jimbo linalojitawala (Semi-Autonomous region) hatua ambayo haikupokewa vizuri na Algeria na Polisario Front. Mfano tarehe 10 Disemba 2020, Rais Donald Trump alitangaza kwamba Marekani itatambua rasmi madai ya Morocco kuhusu Sahara Magharibi endapo Morocco itakubali kurejesha uhusiano na Israeli, ambayo ilifanya.

Na EU mwaka wa 2019 bunge lao lilipitisha Makubaliano ya Ushirikiano wa Uvuvi Endelevu (SFPA) makubaliano haya yaliruhusu meli za Uvuvi za Ulaya kufanya uvuvi katika eneo la Morocco, ingawa Polisario Front haikuhusika katika mazungumzo makubaliano hayo yanaruhusu meli hizo kuvua hata katika maji yenye migogoro yanayodaiwa na Polisario Front kama sehemu ya nchi yao ya Sahrawi Arab Democratic Republic (SADR), makubaliano haya yanaonyesha wazi kuwa EU inatambua na kukubali madai ya Morocco juu ya eneo la Sahara Magharibi, jambo ambalo linaikasisha Polisario Front na Algeria.

Migodi tajiri ya Fosfeti (Phosphate) iliyopo Sahara Magharibi, Kufikia 2020, kulikuwa na hifadhi ya takriban tani bilioni 50 za miamba ya fosfeti (phosphate) huko Morocco na Sahara Magharibi, na kuifanya kuwa nchi yenye akiba kubwa zaidi ya bidhaa hii ulimwenguni. Licha ya bei ya fosfeti kushuka lakini mamlaka ya Morocco haiko tayari kuacha migodi hiyo maaana kuna uwezekano wa kupanda tena, na kwa kuikalia Sahara Magharibi inaondoa mshindani katika uzalishaji huo maana itakuwa ndiye nchi pekee yenye akiba hiyo kubwa ya fosfeti Duniani.

Katika eneo la uchimbaji madini ya Fosfeti la Bou Craa limetoa mapato makubwa na ajira kwa WaSahrawi, sekta ya madini hayo Inaajiri karibu watu 1,900 sasa.
Mwaka 1968, kulikuwa na wafanyikazi 1,600 wa Sahrawi, na kushuka mpaka 567 mwaka mmoja baada ya Morocco kuitwaa.

Wanaharakati wa Sahrawi wanasema sasa kuna wafanyikazi takriban 200 pekee na wengi wao wako katika kazi za daraja la chini.

Ajira katika sekta hiyo zinatolewa nchini Morocco hali hii inaikasirisha Polisario Front ambao wanaona watu wa nchi yao wanateswa na haki zao hazisingatiwi.

Morocco inataka kutwaa maeneo zaidi ya bahari kwa ajili ya uvuvi,
Eneo-bahari la Sahara Magharibi limeongeza uchumi wa Morocco kwa ujumla. Hii ni kutokana na mambo kadhaa.

Kwanza: Maendeleo ya sekta ya uvuvi ya Morocco kama njia ya mapato na ajira.

Pili: kuongezeka kwa mahitaji ya kimataifa ya dagaa. Kutoka tani 200,000 kwa mwaka katika miaka ya 1960, Morocco iliuza zaidi ya tani milioni moja mwaka wa 2001. Zaidi ya WaMorocco 400,000 wameajiriwa kwenye sekta ya uvuvi na mauzo yake ya nje yana thamani ya karibu $1bilioni kwa mwaka.

Kwa mujibu na Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na Kilimo na chakula linaeleza kuwa samaki waliopo Morocco wamepungua kwa 80% na hiyo ni kutokana na uvuvi holela na uhamaji wa samaki wengi. Ni katika Eneo-bahari la kusini mwa Sahara Magharibi pekee ndipo Samaki na viumbe bahari wanapatikana kwa wingi.

Cephalopods (ngisi na pweza) hujumuisha asilimia 80-90 ya mapato ya nje ya sekta hii kwa Morocco na hupatikana katika maji ya Sahara pekee.

Hali hii ya upatikanaji wa samaki inaipa Morocco sababu nyingine ya kuhakikisha Sahara Magharibi inakuwa sehemu ya ufalme wa Morocco.

Tafiti za mafuta na madini ya kimkakati kama kichocheo cha uvamizi wa Morocco katika eneo la Sahara Magharibi,
Morocco haina mafuta katika ardhi yake, huku bei ya mafuta ikiongezeka katika soko la dunia mfano tu mwaka 2022 imeweza kufikia dola za Kimarekani 80 kwa pipa. Mafuta ni muhimu katika kuwezesha uzalishaji Viwandani. Kuendeshea mashine na magari.

Ugunduzi wa kisima cha mafuta cha chinguetti nchini Mauritania mwaka wa 2001 unampa matumaini Mfalme wa Morocco kutoa leseni kwa kampuni ya mafuta ya Ufaransa ya Total kuanza utafiti wa mafuta katika maji ya Sahara Magharibi kwa kuwa jiografia yake ni sawa na ile ya Mauritania.

Licha ya kuwa na akiba kubwa ya Fosfeti Sahara Magharibi ina kiasi kikubwa cha madini ya kimkakati kama vile Titanium na vanidiamu (strategic metals) ambayo inatabiriwa kuwa miongoni mwa rasilimali zinazoshindaniwa katika siku za usoni.

Jitihada za kuleta amani

Umoja wa mataifa, ulipitisha ‘resolution’ waka 1965 ikiitaka Uhispania kuitisha kura ya maoni kwa watu wa Sahara Magharibi kujiamulia hatma yao.

OAU, nao walikuja na mpango wa kuitisha kura ya maoni lakini jitihada zao ziligonga mwamba maana walionesha wazo kuiunga mkono Sahara Magharibi. Kitendo ambacho kilitafsiriwa na Morocco kuwa OAU iliipendelea Sahara Magharibi.

Miaka ya 1980 Umoja wa Mataifa ulikuja na mpango mpya, mpango huo ulijumuisha Kusitisha mapigano, kura ya maoni, Utawala wa mpito na mazungumzo ya moja kwa moja baina ya Morocco na Polisario Front.
Mpango huu ulikubaliwa mwaka 1990, na ilipotimu mwaka 1991 palikubaliwa kusitishwa kwa mapigano huku mchakato wa kuandaa kura ya maoni ukiendelea.

Umoja wa mataifa ukatuma vikosi kwa kazi maalum kinachofahamika kama ‘United Nations Mission for the Referendum in Western Sahara’ kwa lengo la kusimamia usitishwaji wa mapigano (ceasefire) na kusimamia kura ya maoni (referendum).

Hatua hiyo ilikuwa ni muhimu katika kuamua hatma ya Sahara Magharibi lakini mzozo mpya ukaibuka katika kutambua vigezo vya wapiga kura na machaguo (options) kwenye karatasi ya kura.

Polisario Front walitaka kuwe na machaguo mawili tu
  1. Uhuru kamili
  2. Kujiunga na Morocco

Morocco walipendekeza machaguo mawili pia
  1. Kujiunga na Morocco
  2. Kujitawala chini ya Morocco (Semi-Autonomous status)

Polisario Front waligomea chaguo la Kujitawala ndani ya Morocco (semi-autonomous status) kwakuwa waliona kuwa hiyo haina tofauti na kutawaliwa na Morocco.

Morocco nao waligomea chaguo la Uhuru kamili kwa Sahara Magharibi, kwakuwa waliona kuwa hiyo ni sawa na kujinyima haki ya wao kuitawala ardhi wanayoiona kama ya kwao.

Na mchakato mzima wa nani anafaa kupiga kura na nani hafai ulizozaniwa na pande zote. Morocco wakitaka makabila matatu yaliyo kusini mwa nchi yao kuongezwa katika orodha ya wapiga kura na Polisario Front wakiligomea hilo.

Morocco walihujumu jitihada za Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) lililopewa kazi na UN kuhamisha watu waliotambuliwa kama wapiga kura toka kwenye makambi ya wakimbizi kwenda sehemu za kupigia kura.

Pande zote zimeonesha jitihada kutaka kutatua mgogoro huu ila aina ya suluhu ndiyo imekuwa kikwazo.
Morocco wanataka Sahara Magharibi kuwa jimbo linalojitawala lakini ndani ya ufalme wa Morocco.

Sahara Magharibi wenyewe wanataka kuwa nchi yenye uhuru kamili na si sehemu ya nchi nyingine.

Mapendekezo
Afrika leo hii inafanya jitihada kuungana na wapigania uhuru wa bara letu Mwalimu Nyerere na Nkwameh Nkrumah walipigia sana chapuo sualala Afrika kuungana japo walitofautiana njia ya kufikia muungano huo.

Leo hii mchakato huo unaendelea japo ni wa taratibu na unaanza katika ngazi za kikanda mathalan tuna ECOWAS, SADC na EAC hivyo ni muhimu kwa Sahara Magharibi kukubali kuwa ndani ya Ufalme wa Morocco kwa sharti la kupewa hadhi ya Kujitawala kama ilivyo Zanzibar kwa Tanzania au Ogaden kwa Ethiopia ili walau kuashiria umoja wa Afrika.

Ila kama Sahara Magharibi itaruhusiwa kuwa nchi huru, inayotambuliwa kimataifa basi Afrika itakuwa katika hatari ya kuendelea kugawanyika maana vuguvugu la kujitenga katika kila nchi yenye mzozo italiona suala la Sahara Magharibi kama mfano wa kuigwa na hamasa kwa wao kutimiza azma yao kujitenga, Vuguvugu ya kujitenga yaliyopo Afrika ni kama vile:

NchiVuguvugu
Kenya 🇰🇪Jamhuri ya Mombasa
Zambia 🇿🇲Barotseland
Afrika Kusini 🇿🇦• Jamhuri ya Cape town
• KwaZulu Natal
• Volkstaat
Somalia 🇸🇴• Puntland
• Somaliland
• Jubaland
Nigeria 🇳🇬• Biafra
• Niger Delta
• Jamhuri ya Oduduwa
Uganda 🇺🇬Falme ya Buganda
Zimbabwe 🇿🇼Matebeleland
Cameroon 🇨🇲Ambazonia
Sudan 🇸🇩Darfur

Eneo la Sahara Magharibi halina amani tangu kujiondoa kwa Uhispania mwaka 1975 kutokana na sababu zilizojadiliwa hapo juu.

Watu wa Sahara Magharibi wanateseka zaidi kutokana na kutotatuliwa mgogoro huu. Sasa ni wakati wa Umoja wa Mataifa na wajumbe wa baraza la usalama kuendelea kujitolea katika kufanya uzengezi (Lobbying) kwa Polisario Front kukubali kuwa jimbo linalojitawala ndani ya nchi ya Morocco ili kupata amani ya kudumu katika eneo hilo.
Mungu ibariki Afrika.

1668162925120.png
1668162925309.png
1668162925438.png
 

Attachments

  • 33C61D13-62E9-46D8-A71C-6FC4FF4A7F45.jpeg
    33C61D13-62E9-46D8-A71C-6FC4FF4A7F45.jpeg
    29.7 KB · Views: 23
  • C37114DF-8B6D-4142-AEE2-39D6AAB3BF80.jpeg
    C37114DF-8B6D-4142-AEE2-39D6AAB3BF80.jpeg
    24.3 KB · Views: 22
  • 77F840AA-5048-4A18-81E9-D754259CC0CF.jpeg
    77F840AA-5048-4A18-81E9-D754259CC0CF.jpeg
    66.8 KB · Views: 30
Kule Ukraine vs Russia
Huku Rwanda vs DRC
Pale China vs Taiwan

Ww3 inanukia[emoji848]
 
Linalonivutia kuhusu Morocco ni kuwa ni taifa pekee la Afrika lililoitawala Ulaya karibu yote kuanzia Ureno mpaka Ufaransa tena kwa miaka mingi.Hii uliyoandika ni historia ya karibuni sana.Kuna wakati pia mabedui wa kutoka Mali nao walitawala Ulaya chini ya mwavuli wa dola ya kiislamu kama walivyofanya Morocco.kabla kugombanishwa wenyewe kwa wenyewe na wakristo..
Historia nyengine kuhusu Morocco ni kuwa ndilo lango la ustaarabu na elimu zote kuingia Ulaya kupitia Uhispania wakati huo ilipokuwa dola ya Andalusia.Ulaya ingeendelea kuwa gizani iwapo elimu zilizoasisiwa na dola ya kiislamu ya Abbasiya na Ummawiya zisingeingizwa Ulaya kupitia Morocco.
 
Linalonivutia kuhusu Morocco ni kuwa ni taifa pekee la Afrika lililoitawala Ulaya karibu yote kuanzia Ureno mpaka Ufaransa tena kwa miaka mingi.Hii uliyoandika ni historia ya karibuni sana.Kuna wakati pia mabedui wa kutoka Mali nao walitawala Ulaya chini ya mwavuli wa dola ya kiislamu kama walivyofanya Morocco.kabla kugombanishwa wenyewe kwa wenyewe na wakristo..
Historia nyengine kuhusu Morocco ni kuwa ndilo lango la ustaarabu na elimu zote kuingia Ulaya kupitia Uhispania wakati huo ilipokuwa dola ya Andalusia.Ulaya ingeendelea kuwa gizani iwapo elimu zilizoasisiwa na dola ya kiislamu ya Abbasiya na Ummawiya zisingeingizwa Ulaya kupitia Morocco.
Hadi Physcs??😂😂😂😂
 
Tetemeko la Ardhi kwenye mji wa Marrakech nchini Morocco imenikumbusha kulikuwa na vita kati ya Morocco na Popular Front for the Liberation of Saguia el-Hamra and Río de Oro (Polisario Front), nikaingia google kuitafuta Polisario.

Hawa Polisario kumbe bado wapo.
 
Back
Top Bottom