MAHAKAMA ya Rufani Tanzania imetoa angalizo kwamba uamuzi wa Makamama Kuu uliotolewa kuhusu mgombea binafsi kusimama katika uchaguzi mkuu uko pale pale, ingawa umekatiwa rufaa.
Angalizo hilo lilitolewa jana na majaji saba wanaosikiliza rufani inayopinga uamuzi uliotolewa na waliokuwa majaji wa Mahakama Kuu; Amir Manento, Salum Massati na Thomas Mihayo, ambao walikubaliana na ombi la Mchungaji Christopher Mtikila na kuruhusu kuwapo mgombea binafsi katika uchaguzi.
Majaji hao walitoa angalizo hilo baada ya Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, kuomba mahakama iahirishe usikilizwaji wa rufani hiyo na impe miezi minne apitie jalada kwa kuwa hajajiandaa na pia mwanasheria mwenzake anauguliwa na baba yake, hivyo hajapata muda wa kutosha, ombi ambalo lilipingwa na walalamikiwa ambao ni mawakili wa Mtikila, wakidai wiki moja itatosha.
Masaju pia alihoji kuwapo majaji saba katika rufaa hiyo badala ya watatu kwa mujibu wa ibara ya 122 ya Katiba.
Hata hivyo, Jaji Mkuu Augustino Ramadhani, alihoji ni wakati gani jopo kama hilo huwa linakaa na kusema kama ni makosa, basi yalishafanyika tangu mwaka 1984 ambapo jopo la namna hiyo lililohusisha majaji watano lilitumika Zanzibar.
Alisema aliamua kuunda jopo hilo kulingana na unyeti wa suala lililoko mbele yao. Baada ya kutoa ufafanuzi huo, rufani hiyo iliahirishwa hadi Aprili 8 mwaka huu.
Rufaa hiyo iliyofunguliwa na Jamhuri namba 45 ya mwaka jana inasikilizwa na majaji wakiongozwa na Jaji Mkuu, Ramadhani. Wengine ni Eusebia Munuo, Januari Msofe, Nathania Kimaro, Mbarouk Salim, Bernard Luanda and Sauda Mjasiri.
Katika rufaa hiyo, Serikali imetoa sababu sita za kukata rufaa, mojawapo ikidai Mahakama Kuu ilikosea kujipa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, ilikosea kutengua vifungu vya Katiba ya nchi, na ilikosea kisheria kupunguza matakwa ya lazima ya Ibara 30 (5) na 13 (2) ya Katiba ya nchi.
Sababu nyingine, ni kujipachika mamlaka ya Bunge ya kutunga sheria, kukosea kisheria kwa kuiweka Katiba ya nchi katika vyombo vya kimataifa na kuitolea uamuzi kesi hiyo bila kuweka suala hilo bayana.
Hukumu ya Mahakama Kuu juu ya kesi iliyofunguliwa na Mtikila ilitolewa Mei 2006, ikiruhusu kuwapo kwa mgombea binafsi katika uchaguzi, kwa sababu Katiba ya nchi inatoa haki hiyo.
Mahakama Kuu ilibainisha kuwa Katiba inatamka wazi kuwa kila mwananchi ana haki ya kuchagua au kuchaguliwa kuwa kiongozi na haiweki masharti kuwa hilo lifanyike kwa mtu kujiunga na chama fulani.
Awali Mchungaji Mtikila alifungua kesi hiyo ya kikatiba mwaka 1993 katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Jaji Kahwa Lugakingira (marehemu), alikubaliana na hoja za Mtikila na kuitaka serikali kuruhusu wagombea binafsi.
Baada ya serikali kuwasilisha rufani hiyo iliyotakiwa kuanza kusikilizwa jana, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, alisema msingi wa rufaa ya Serikali si kupinga mgombea binafsi, bali ni kuiuliza Mahakama ilikopata mamlaka ya kufuta vifungu vya Katiba ya nchi, kama ilivyofanywa na Mahakama Kuu katika uamuzi wa kuruhusu mgombea binafsi.
Alisema msingi wa serikali kupinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu, unatokana na Ibara ya 98 ya Katiba ya nchi, ambayo imelipa Bunge peke yake mamlaka ya kubadili Katiba ya nchi na kwa kufuata mchakato maalumu na kwamba, ibara hiyo haitaji mahali popote mahakama kupewa uwezo huo.
Katika uamuzi wa Mahakama Kuu, iliamriwa kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ifanye marekebisho ya Sheria Namba 34 ya 1994 ambayo inapingana na kifungu cha 21 (1) cha Katiba ambacho kinampa haki ya mtu kugombea na kupiga kura.
Mahakama Kuu ilimpa Mwanasheria Mkuu kati ya Mei 5, 2006 hadi uchaguzi ujao, awe amewasilisha bungeni sheria inayotoa fursa ya kuwapo mgombea binafsi katika uchaguzi bila kutegemea chama chochote